WAAFRIKA WALIOJITOA MUHANGA KARBALA
WAAFRIKA WALIOJITOA MUHANGA KARBALA
Ni mara nyingine tena imewadia Siku ya Ashura mwezi 10 Muharram, pia ni wakati mwingine Uislamu unapata nguvu kutokana na msukumo wa tukio la masaibu ya Karbala; na hii ni indhari na ni kumbukumbu kwa matendo ya kishujaa yaliyofanywa na Wana wa Afrika ambao waliandika ujumbe wa (Haki) kweli kwa damu yao katika ardhi ya Karbala.
Uislamu, pamoja na Ujumbe wake kwa Walimwengu wote, tangu hapo awali ulimpa Uhuru mwanadamu kutoka katika himaya ya Wadhalimu. Ilikuwa suala lisilozuilika kwamba kilio cha “Hapana apasaye kuabudiwa isipokuwa Allah” kingeunganisha watu wa Mataifa yote na wa Imani mbalimbali. Pamoja na ujumbe wake wa kujikomboa mwanadamu kiroho, Qur’an Tukufu imewalingania binadamu kuungana pamoja bila ya kujali rangi wala utaifa wao.
“Hapana shaka mbora wenu mbele ya Allah (s.w.t.) ni yule mwenye kumcha Mwenyezi Mungu" (Qur’an, 49:13). Ni kwa aya hii Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu Haki ya Uhuru wake. Wenye kufuzu na kulipwa mema (Pepo) ni wale tu watakaotii amri zake bila kujali utaifa wao wala utukufu na ubora wa makabila yao.
Kabla ya kuorodhesha majina ya Waafrika waliojitoa muhanga nafsi zao huko katika ardhi ya Karbala ningependa kueleza kuwa hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa damu ya Waafrika kumwagika katika maidani ya kutetea Haki. Ni ukweli usiopingika kuwa Mashahidi wa kwanza walikuwa Mwanamke Mwafrika, Sumaiyya na mumewe, Yasir. Wao walikuwa watu wa kwanza kufa mashahidi kwa kujitoa muhanga pale makafiri walipoishambulia Makka na kuwaua kikatili.
Mtoto wao Ammar, alikuwa miongoni mwa maswahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), mtu ambaye aliaminiwa sana na Mtume. Siku moja Mtume (s.a.w.w.) alisema:
“Ammar, utauliwa na kikundi cha Makafiri. Wewe utakuwa unawaita wao kwenye Pepo (Janah) na wao watakuwa wanakuita kuingia katika moto wa Jahanamu. Ujumbe huu ulikamilika katika vita vya Siffini, wakati Ammar alipopigana bega kwa bega upande wa Imamu Ali (a.s.) na kuuliwa na jeshi la Moawiyya. Khabbab bin Al-Arrat alikuwa sahaba mwingine maarufu zama za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kusilimu. Naye pia alitokea katika bara la Afrika, na aliuliwa na makafiri walipoishambulia Makka wakati akipigania Haki.
Huko katika ardhi ya Karbala pia, ili kuendeleza jadi ya kujitoa Muhanga, Afrika ilitoa mchango mkubwa kuutetea Uislamu. Tunapowakumbuka Mashahidi waliouliwa Kerbaba wapatao 72, na 12 kati yao ni kutoka katika Bara letu, kwa kweli tunafarjika kuona Afrika ilivyokuwa mstari wa mbele kuinusuru Dini ya Allah (s.w.t.).
Katika siku hiyo ya msiba jeshi la maadui liliwashambulia Waislamu alfajiri mapema. Jeshi la maadui lilikusudia kuwakanyaga kanyaga kwa kwato za farasi maswahaba wote wa Imam Husein (a.s.), pamoja na familia yake na watoto wadogo. (Idadi ya Wanaume, wanawake na watoto katika msafara wa Imam Husein (a.s.) haikuwa zaidi ya watu 100). Lakini maswahaba watiifu wa Imamu walijipanga vema na kusonga mbele. Jeshi la Moawiyya lilikuwa na watu (makafiri) wapatao 4,000. Mapigano makali yalianza na baada ya muda maadui walirudi nyuma. Kwa Imamu Husein (a.s.) haukuwa ushindi mzuri, kwa kuwa aliwapoteza miongoni mwa marafiki zake watiifu wapatao 50.
Miongoni mwa hao Mashujaa 50 walikuwepo Waafrika saba: Salim, Zahir, Quarib bin Abdulla, Munjeh bin Salim, Saad bin al-Harth, Nasr bin Abi Naizer na Harth bin Nab-han. Majina yao hawa mashahidi (Mashujaa) yamewekwa katika kumbukumbu sio tu na Wanahistoria mashuhuri, bali pia na Maimamu wetu walioandika Ziyarah wakiwataja Mashahidi wote mmoja baada ya mwingine.
Shaudhab, Mwafrika mwingine alikuwa Mwanazuoni maarufu wa Shariah za Kiislamu na Hadith wa wakati huo. Watu walikuwa wakisafiri masafa marefu kuja kusikiliza hekima na nasaha zake. Baada ya kusikia ukweli wa Imamu Husein (a.s.), Shaudhab pamoja na rafiki yake, Abis Shakiri, waliungana na Imamu Husein (a.s.) na wakafa Mashahidi katika ardhi ya Karbala kwa ajili ya kuunusuru Uislamu.
John; ambaye bila shaka alikuwa Mkristo aliyesilimu alikuwa Mtumwa wa Kihabeshi ambaye baada ya kufariki “Bwana” wake; alichukuliwa na familia ya Mtume ili aishi nao kama mgeni wao. Alibakia hapo kwa furaha na amani kwa muda wa miaka 30 hivi. Aliungana na Imamu Husein kwenda Karbala, ingawa alikuwa tayari ni mzee wakati huo lakini alipigana kwa nguvu zake zote kabla ya kuuawa. Alipoanguka chini, Imam Husein alimwendea, na akakinyanyua kichwa chake na kukilaza juu ya paja lake na kumuombea. Hadith za Kishia zinaelezea kuwa watu wa kabila la Asad waliokuja kuwazika Mashahidi (Mashujaa) baada ya siku tatu walishangaa kuona mwili wa marehemu unang’ara na unanukia kwa manukato mazuri ya peponi. Ulikuwa mwili wa Shujaa, John.
Aquaba, pia kutoka Bara la Afrika alikuwa miongoni mwa maswahaba waaminifu wa Imam Husein (a.s.). Imam aliacha nyaraka zake zote muhimu chini ya uangalizi wa Aquaba. Alijeruhiwa katika vita vya Karbala, na alichukuliwa mateka pamoja na familia ya Imam. Akiwa miongoni mwa watu walioshuhudia mauwaji ya Karbala, amebaki kuwa kumbukumbu na kielelezo muhimu katika Historia.
Miongoni mwa watu waliokuwa pamoja na Imamu Husein (a.s.) Karbala ni mwanamke Mwafrika, Fizza (s.a.); ambaye atakumbukwa milele kutokana na Imani yake na huduma zake kwa familia ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Nchi yake ya asili ilikuwa Nuba, ambayo hivi sasa ni Sudani. Kwanza alitoa huduma kwa Bi. Fatima bint yake Mtume. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipanga utaratibu kwamba siku moja Bi Fatima (a.s.) afanye kazi za nyumbani zote na Fizza apumzike na siku ifuatayo Fizza afanye kazi hizo na Bi. Fatima (a.s.) apumzike.
Baada ya kufariki dunia Bi. Fatima (a.s.), Fizza (s.a.) aliolewa na Muislamu mcha Mungu na akaweza kuitunza familia yake, lakini uwajibikaji wake kwenye nyumba ya Imamu Ali (a.s.) uliendelea kama kawaida. Aliungana na Imam Husain kwenda Karbala na kuwa pamoja nao katika madhila, maafa na masaibu yaliyowapata wanawake na watoto wa Imam katika ardhiya Karbala.
Elimu ya Qur’an ya Fizza (s.a.), imeelezewa na Mwanazuoni maarufu Abul Qasim Qushairi. Mwanazuoni huyu ameandika katika wasifu wa Fizza kwamba, kwenye miaka 20 ya mwisho ya uhai wake Fizza hakuweza kutamka neno lake mwenyewe, wakati wote alizungumza au kusoma aya kutoka katika Kitabu Kitakatifu Qur`an.
Uislamu unajivunia watoto wa ardhi ya Afrika ambao kwa mapenzi yao walijitolea muhanga kuinusuru Dini ya Allah (s.w.t.). Kizazi cha Imam Husain (a.s.) wakati wote walitoa heshima zao kwa Mashahidi wa Karbala kwa maneno yafuatayo:-
“Heshima juu yenu Enyi mlioridhiwa na Allah pamoja na Waja Wake. Heshima juu yenu Enyi Wasaidizi wa Imani. Naomba Wazazi wangu wapate Heshima ya kuyaweka Maisha yao kwa ajili yenu. Mlikuwa Watakatifu na Watoharifu na mpo watakatifu na Watoharifu hapo mlipo milele. Kwa hali ya juu mmefuzu, Ninamuomba Allah aniweke pamoja nanyi ili niwe miongoni mwa wenye kufuzu.”
MWISHO