Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MILADU ANNABI (S.A.W.W)

0 Voti 00.0 / 5

 

Miladun Nabi: Assalaamu Alaykum Warahmatullaahi Wabarakaatuh.

Hii ni makala maalumu ya kuadhimisha Maulidi ya Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) nuru ya muongozo na rehma kwa walimwengu. Kila zama zinavyopita, fikra zake zinazidi kuenea na kuwavutia wanaadamu wengi zaidi.

Sisi hapa katika Idhaa ya Kiswahili tunachukua fursa hii kuwatumia Waislamu wote ulimwenguni salamu zetu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa siku kuu hii ya kuadhimisha uzawa wa Mtume wa Mwisho katika mitume wa Mwenyezi Mungu, Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Tunaweza kusema kuwa mafanikio muhimu zaidi ya Mtume wa Uislamu ni kuasisi jamii kwa msingi wa umoja na mapenzi. Umoja ni johari ya jamii. Ili kuibua umoja huu, Mtume (s.a.w.w) alitoa wito kwa jamii ya wanaadamu na jamii za Kiislamu kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu katika kivuli cha ucha Mungu. Mtume Mtukufu aliwaambia Waislamu kuwa ustawi na nguvu za mataifa hutokana na umoja na mshikamano. Waislamu kwa karne kadhaa walipitia kipindi cha dhahabu cha kuongoza wanaadamu katika uga wa sayansi na ustaarabu kutokana na kuwa walitekeleza nasaha za Bwana Mtume (s.a.w.w).

Baada ya kuja Uislamu, shakhsia adhimu na ya kipekee ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ilikuwa chanzo cha ukarimu miongoni mwa watu na mhimili mkuu wa jamii ya Kiislamu. Kutokana na jitihada zake kubwa, aliibua umoja wa kudumu katika ulimwengu.

 

Mtume Mtukufu (s.a.w.w) alitumia mbinu mbali mbali kuondoa vizingiti vya umoja kama vile ubaguzi wa rangi, kujitakia ukubwa na ukabila. Mtume wa Mwenyezi Mungu hata alitoa wito wa amani kwa wafuasi wa dini nyingine za mbinguni kwa kusema "Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu."

Jamii ya kijahili ya bara Arabu kutokana na ukosefu wa sheria za utawala na mfumo wa kisiasa ilikumbwa na ghasia na machafuko. Vita, ujahili, ukafiri na taasubi za kikabila ni kati ya sifa za kimsingi zilizotawala kaumu za Waarabu wakati wa kudhihiri Uislamu. Kama alivyosema Ibn Khaldun mwanahistoria maarufu Muislamu, ‘Kaumu za Waarabu zilikuwa ni magenge ya uporaji. Zilipora kila zilichokiona.' Kuna wanaosema kuwa katika historia ya Waarabu kabla ya Uislamu kulijiri vita 1,700.

Baadhi ya vita hivyo vilidumu kwa miaka mingi na kuendelea katika vizazi kadhaa. Hisia ya kupenda vita ilikuwa imekita mizizi miongoni mwa watu kiasi kwamba wakati Mtume alipozungumza kuhusu amani na utulivu wa peponi mmoja kati ya Waarabu alumuuliza: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, huko peponi kuna vita." Mtume akamjibu kwa kusema, "la," Mwarabu akasema: "Iwapo hakuna vita basi pepo ina faida gani."

Ni katika mazingira haya magumu ndio Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akieneza ujumbe wa rehma na muongozo wa Mwenyezi Mungu na kuyaleta pamoja makundi yaliyokuwa Madina.

Kuibua umoja wa kisiasa na kijamii kupitia utiwaji saini mikataba ilikuwa moja kati ya harakati muhimu zaidi za Mtume SAW katika kuleta utulivu na maelewano katika jamii iliyokuwa imetawanyika katika zama hizo. Mikataba hii ni kati ya ushahidi wa wazi zaidi wa kutumiwa stratijia ya umoja wa wa Kiislamu katika zama hizo.

Mikataba baina ya Mtume na makabila ya Yathrib ni kati ya mikataba muhimu zaidi iliyotiwa saini na pande mbili katika zama hizo. Baadhi ya wataalamu wameitaja mikataba hiyo kuwa "sheria ya kwanza ya maandishi duniani." Katika vipengee vya mikataba hiyo ilitajwa wazi kuwa Waislamu wanajumuisha ummah mmoja. Baadhi ya ibara katika mikataba hiyo zinaonyesha umaridadi wa umoja.

Baadhi ya ibara hizo ni kama vile
-Waislamu wataungana katika kupambana na dhulma, uvamizi na njama.
-Iwapo kutaibuka hitilafu miongoni mwa Waislamu, marejeo ya utatuzi yatakuwa ni Mwenyezi Mungu na Mtume.
Katika sehemu nyingine ya mikataba hiyo ya kihistoria uhusiano wa Waislamu na Mayahudi umeashiriwa ifuatavyo:
-Waislamu na Mayahudi wataishi Madina kama taifa moja na kila mmoja atakuwa na dini yake.
-Waislamu na Mayahudi watasaidiana katika kukabiliana na wanaovamia Yathrib.

Tunaweza kusema juhudi za kuibua nukta za pamoja katika dini ni moja kati ya mbinu za wazi kabisa zilizotumiwa na Mtume katika kufikia umoja wa Kiislamu. Mtukufu huyo katika mkataba wa Aqabah aliotia saini na watu wa Yathrib aliyaambia makundi tafauti kuwa:

"Chagueni miongoni mwenu wawakilishi 12 ili waweze kuwajibika kuhusu yatakayojiri katika kaumu zenu."

Hatua hii ya busara ya Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu iliwafurahisha sana watu kiasi kwamba wakati wajumbe wa watu wa Yathrib walipokutana na Mtukufu huyo katika eneo la Aqaba karibu na Makaa na kusikiliza hotuba yake kuhusu umoja na kusameheana walisema: "Kuna shari, ufisadi na hitilafu miongoni mwa kaumu za Aus na Khazraj - makabli mawili ya Madina- na hatujawahi kushuhudia moto wa hitilafu kama hizo miongoni mwa makabila yoyote. Ni matumaini yetu kuwa Mwenyezi Mungu atakufanya kuwa chanzo cha watu wetu kuelewana na kuleta umoja na huruma miongoni mwao."

Ili kuleta mfungamano wa kijamii katika mhimili Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW alieneza mapenzi na rehma katika jamii. Mtukufu huyo alimini kuwa jamii bora ni jamii ambayo watu wote wana mfungamano wa kidugu na wote wawajibike kulinda udugu huo ili Mwenyezi Mungu mwenyewe awaandalie mazingira ya umoja endelevu. Ni kwa sababu hii ndio Mtume Muhammad SAW akaleta udugu kati ya Waislamu 300 na kumtaja Imam Ali (AS) kuwa ndugu na mrithi wake.

Kwa mkataba wa jumla na wa umma kati ya watu wa Madina, Mtume alieneza urafiki na mashikamano katika jamii ya Kiislamu. Mtume SA aliwafahamisha watu kuwa "Jamaa ni rehma na mifarakano ni adhabu". Vile vile alisema: ‘Watu wenye imani ni kama mwili mmoja katika mshikamano urafiki na ukarimu. Iwapo sehemu moja ya mwili itaumwa viungo vingine vinakuwa macho usiku kuonyesha ufungamano.'

Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW alikuwa na wasi wasi kuhusu kuzuka hitilafu katika ummah wa Kiislamu na kuibuliwa ghasia miongoni mwa Waislamu. Mtu mmoja aliyejulikana kama Sheith bin Qeiys alimchochea Yahudi mmoja ili kukumbusha kuhusu hitilafu kati ya makabila ya Aus na Khazraj katika zama za ujahiliya na hivyo kuamsha hisia za kale.

Kufuatia uchochezi huo makabila yote mawili yalichomoa silaha na mapigano makali yakajiri. Baada ya kupata habari hizi, Mtume alielekea sehemu iliyokuwa na mapigano na kusema: "Enyi Waislamu, je mumemsahau Mwenyezi Mungu? Mnatoa nara za kijahiliya pamoja na kuwa niko miongoni mwenu na baada ya Mwenyezi Mungu kuwaongoza katika nuru ya Uislamu na kuwapa thamani na kuwaondoa katika ukafiri."

Katika nyakati tofauti Bwana Mtume alikuwa akisoma aya yenye kutuliza nyoyo ya 103 katika Sural Ale Imran katika Quran Tukufu isemayo: "Na shikamaneni na kamba ya Mwenyeezi Mungu nyote wala msifarakiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyeezi Mungu iliyo juu yenu, mlipokuwa maadui na akaziunganisha nyoyo zenu, hivyo kwa neema yake mkawa ndugu na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto naye akawaokoeni nalo. Hivyo ndivyo Mwenyeezi Mungu anakubainishieni dalili zake ili mpate kuongoka."

Wakati nyota ya Uislamu ilipokuwa inachomoza kwa kasi huko Hijaz wanafiki baada ya kuona Mtume hayuko karibu walijenga Msikiti mkabala wa Msikiti wa Qubaa ili kwa njia hiyo wapunguze nguvu za kimaanawi za Waislamu na kwa kisingizio cha kusimamisha faradhi ya Sala wafanya mazungumzo kuhusu namna ya kutekeleza njama dhidi ya Waislamu na kuuangusha Uislamu.

Wakati Mtume aliporejea Madina kutoka Vita vya Tabouk, aliombwa aswali katika eneo hilo ambalo kidhahiri ni la ibada ili kwa njia hiyo lifunguliwe rasmi. Katika wakati huo Malaika wa Wahyi alimfahamishe Mtume kuhusu njama za watu hao na hapo eneo hilo likaitwa Masjid Dhirar.

Mtume wa Mwenyezi Mungu aliamurisha Msikiti huo uharabiwe. Hatua ya Mtume SAW ya kuharibu Msikiti wa Dhirar ilichukuliwa kwa ajili ya kuzuia hitilafu katika Jamii ya Kiislamu ili maelewano ya kitaifa yasivurugike na nguzo za mfungamano zibaki kuwa imara.

Kwa hivyo kama alivyosema Imam Ali AS: "Nyoyo za watenda mema zilivutiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu kwa baraka za kuwepo Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW alizika chuki na moto wa maadui. Kupitia kuwepo kwake, Waislamu walielewana na kupata izza na kufungua njia za saada."

Kwa mara nyingine tena tunatoa salamu zetu kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume wa rehma na ukarimu, Mohammad al Mustafa SAW.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini