Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI 2

0 Voti 00.0 / 5

DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 2)

اللّهُمَّ أَغْنِ كُلَّ فَقِير
EWE MOLA MTAJIRISHE KILA ALIYE FAKIRI

KUENEA POTE PAMBAJO LA MOYO LA MUOMBAJI

Allahuma aghni kulla…]: kihusishi kimoja kilichowekwa karibu katika kila aya ya du’a hii ni “kull” ambacho kinamaanisha “kila.” Muombaji siku zote hujaribu kuomba kufanikiwa kwa kila mwanadamu. Huona roho wa Mungu kupitia maombi. Nadharia ya ubinafsi haipatikani tena. Hujifungua kutoka minyororo ya tamaa tu ya kunufaika, na utulivu wa nafsi. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kizazi chake Ma’asum walikuwa na tabia hii. Walitamani mafanikio na uhuru wa wote. Ili kuelewa vizuri moyo huu wa hali ya juu, chunguza nukuu zifuatazo za aya za Qur’an Tukufu na hadithi:
1. Allah (s.w.t.) anasema katika Qur’an Tukufu [Sura al-Ārāf – 7:156]
وَاكْتُبْ لَنَا فِي هَٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ إِنَّا هُدْنَا إِلَيْكَ ۚ قَالَ عَذَابِي أُصِيبُ بِهِ مَنْ أَشَاءُ ۖ وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ ۚ فَسَأَكْتُبُهَا لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَالَّذِينَ هُمْ بِآيَاتِنَا يُؤْمِنُونَ
“…Na rehema Yangu imekienea kila kitu…”
2. Na katika Sura al-Anbiyā’ [21: 107] akimhutubia Mjumbe Wake Mtukufu, anasema:
وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ
“Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu.”
3. Na katika Sura al-Kahf [18: 6] akimhutubia Mpendwa Wake, anasema:
فَلَعَلَّكَ بَاخِعٌ نَفْسَكَ عَلَىٰ آثَارِهِمْ إِنْ لَمْ يُؤْمِنُوا بِهَٰذَا الْحَدِيثِ أَسَفَا
“Huenda ukaingamiza nafsi yako kwa kusikitikia hali yao ya kutoziamini hadithi hizi.”
4. Ifuatayo ni aya yenye nuru ya du’a ya kila siku ya Mwezi Mtukufu wa Rajab:
يَا مَنْ يُعْطي مَنْ لَمْ يَسْأَلْهُ وَمَنْ لَمْ يَعْرِفْهُ تَحَنُّناً مِنْهُ وَرَحْمَةً،
“Ewe ambaye (kila siku) humpa mtu ambaye hajamuomba na ambaye hamjui Yeye, hufanya hivi kwa Upole na Rehema Yake.”
5. Allah (s.w.t.) anasema katika Sura Tāhā [20: 2]:
مَا أَنْزَلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لِتَشْقَىٰ
“Hatukukuteremshia Qur’an ili ujitese [katika njia ya kulingania kwa kujitahidi kuwalazimisha watu kuielekea].”
6. Na katika Sura al-Fātir [35: 8] anasema:
فَإِنَّ اللَّهَ يُضِلُّ مَنْ يَشَاءُ وَيَهْدِي مَنْ يَشَاءُ أَفَمَنْ زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ فَرَآهُ حَسَنًا إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُك عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ
“…Basi nafsi yako isijihiliki kwa kuwasikitikia [ukafiri wao]…”
7. Na katika Sura al-Mumtahana [60: 8] anasema:
لَا يَنْهَاكُمُ اللَّهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُمْ مِنْ دِيَارِكُمْ أَنْ تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ
“Allah hakukatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Allah huwapenda wafanyao uadilifu.”
8. Katika wasia aliomuachia mwanae – Hājj Sayyid Ahmad Khumayni, Marhum Imamu al-Khumayni ansema:
“…Hii ni miujiza ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.)1 …ambaye, kusimama kwake kwenye ncha ya kilele cha ukamilifu wa mwanadamu, kwa uwazi huuona ukweli na bila pazia yoyote. Na wakati huo huo yupo katika vipimo vyote vya ubinadamu hatua za kiumbe, na kuwa ni udhihirisho wa hali ya juu sana wa:
وَمَا يَنْطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ
“Yeye ndiye wa Mwanzo na ndiye Mwisho, naye ndiye wa Dhahiri
na wa Siri…” [53: 3]
hutaka wanadamu wote wafikie ukamilifu huo. Ilikua ni masikitiko kwake kuona kwamba wameshindwa kufikia daraja hilo, na pengine huenda aya:
مَا أَنْزَلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لِتَشْقَىٰ
“Hatukuteremsha Qur’an ili ujitese.” [Tāhā 20: 1-2],
hufanya mtajo usio wazi kwenye ukweli huu, na pengine hadithi hii vile vile hurejelea kwayo:
مَا أُوْذِيَ نَبِيُّ مِثْل مَا اُوْذِيْتُ
“Hakuna Mtume ambaye amefanywa apate shida kama mimi”2
9. Marhum Amin al-Islam Tabrasi katika kitabu chake ‘Majma’ al- Bayān’ anasimulia hadithi ifuatayo:
ولبث في قومه ألف سنة إلا خمسين عاما " ... وكان يدعوهم ليلا " ونهارا "فلا يزيدهم دعاؤه إلا فرارا " ، وكان يضربه قومه حتى يغشى عليه فإذا أفاق قال : اللهم اهد قومي فإنهم لا يعلمون
“Mtume Nuh (a.s.) aliishi miongoni mwa watu wake miaka 950…na aliwalingania mchana na usiku, lakini haikuongeza kitu isipokuwa kinyaa, wakati mwingine watu wake walikuwa wakimpiga kiasi kwamba huanguka na kuzimia, na anapo zindukana husema: “Ewe Allah! Waongoze watu wangu hawa kwani hawana wanachojua.”3
10. Ufuatao ni ubeti wa kwanza wa shairi la kupendeza lililo nasibiwa kwa Imamu ‘Ali (a.s.).4
Wakati alipomuona Ibn Muljim, alisoma kama ifuatavyo karibu na Amr bin Ma’dikarb:
أُرِيْدُ حَيَاتَهُ وَ يُرِيْدُ قَتْلِيْ
“Ninataka uhai wake (uendelee) naye anataka kuniuwa”
11. Imesimuliwa kwamba wakati fulani Mtume Isa (a.s.) alisema:
كُنْ كَا لَشَّمْسِ تَطْلَع عَلى البّرِّ وَ الْفَاجِرْ
“Kuweni kama jua, huwaka juu ya kila mwema na muovu”5
12. Sayyid Radhi al-Din ibn Tāwūs ni mmoja wa wanazuoni wakubwa wa ki-shi’a ambaye kazi zake hufaidi heshima mahususi katika duru la wanazuo. Katika kitabu chake kinachojulikana sana cha du’a ‘Iqbāl al-Ā’māl’, ambacho kwa hakika ni kazi bora ya maombi ya ibada, anasimulia yafuatayo:
كنت في ليلة جليلة من شهر رمضان بعد تصنيف هذا الكتاب بزمان وأنا أدعو في السحر لمن يجب أو يحسن تقديم الدعاء له ولي و...فورد علي خاطري ان الجاحدين لله جل جلاله ولنعمه والمستخفين بحرمته والمبدلين لحكمه
في عباده وخليفته ينبغي أن يبدأ بالدعاء لهم بالهداية من ضلالتهم
فان جنايتهم علي الربوبية والحكمة الالهية والجلالة النبوية أشد من جناية العارفين بالله وبالرسول (ص)
Wakati fulani baada ya kuandika kitabu hiki, katika moja ya mausiku matukufu ya Mwezi wa Ramadhani, wakati nilipokuwa naomba du’a saa za Sahar (daku) kwa ajili ya wale ambao ni lazima au ni vizuri kuwatanguliza katika du’a, na vile vile kwa ajili yangu mwenyewe na… kisha wazo lifuatalo likapita akilini mwangu, inampasa mtu kuomba kwa ajili ya mwongozo wa wale ambao wanamkataa Allah na kupuuza neema Zake, na kwa wale ambao wanaudogesha utukufu Wake na kubadilisha kanuni Zake [juu ya waja na uumbaji Wake], kwani jinai yao na kuhusiana na utawala wa Mungu, hekima ya Mungu, na utukufu wa kiutume ni mkubwa kuliko jinai ya wale ambao wanamjua Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.w.).
Kisha baada ya mistari michache anasema:
فدعوت لكل ضال عن الله بالهداية إليه ، ولكل ضال عن الرسول بالرجوع إليه ، ولكل ضال عن الحق بالاعتراف به والاعتماد عليه .ثم دعوت لأهل التوفيق والتحقيق بالثبوت على توفيقهم ، والزيادة في تحقيقهم ، ودعوت لنفسي ومن..
Hivyo niliomba kwa ajili ya wale ambao wamepotea kutoka njia ya Allah ili wapate kuongozwa kuelekea Kwake, na kwa wale wote ambao wamekengeuka kutoka kwa Mjumbe Wake, ili warudi Kwake, na wale wote ambao wamepotea kutoka kwenye kweli, kuikubali na kuitegemea. Kisha niliomba kwa ajili ya watu wa msaada wa Mungu (ahl al-tawfiq) ili kuthibitishwa juu ya njia zao, na kwa ajili ya watu wa fahamu ili kupata ufahamu zaidi, na [kisha] niliomba kwa ajili yangu mwenyewe na wale ambao…6
Kwa hiyo, wakati wa kusoma beti hizi za maombi za mwezi mtukufu wa Ramadhani, muombaji anapaswa katika maafikiano na Mtume (s.a.w.w.) na kiza chake, afungue moyo wake kwa wote.
Lengo:
Je, haya yaliyotangulia kusemwa yana maana kwamba lazima tuombe kwa ufanisi wa kimwili wa kila mnafiki na kafiri, wakati tunajua kwamba wao ni chanzo cha uharibifu na madhara katika jamii? Je, hatujui hali ya uovu wao katika sehemu mbalimbali za Qur’an? Tutatamani vipi ufanisi wa mwili wa mtu ambaye angesababisha madhara katika ulimwengu.
Majibu:
Allah (s.w.t.) hupendelea vyote , roho na halikadhalika ufanisi wa mwili wa kila mwanadamu. Madhumuni ya kuumbwa mwanadamu kwa mujibu wa Qur’an, kama itakavyojadiliwa hivi punde, haikukusudiwa kwa ajili ya waumini tu, bali kwa msafara wote wa wanadamu. Aya ilioyotajwa hapo juu inaonyesha jinsi Mtume (s.a.w.w.) alivyopata uchungu kwa ajili ya msimamo mgumu wa makafiri. Uchungu huo ulikuwa kwa ajili ya moyo wa kuenea kila kitu aliokuwa nao. Alitaka ukombozi wa kila mwanadamu.
Muombaji ambaye amejisalimisha kwa Allah, vile vile angelitaka hivyo hivyo kufanyika kwa kila mwanadamu. Hata hivyo, itakuwa ni kosa kwake kuwaombea ufanisi wa kimwili kwa ajili ya ufanisi wa kimwili.Wakati unaomba ufanisi wa kila mwanadamu, mtu lazima amuombe Allah kwa ufanisi ule wa mwili ambao utafanikisha, kama lengo la mwanadamu. Mtu lazima atamani, kwa mfano, kwamba kila mwanadamu anapata chakula na nyumba, ili kwamba aweze kumuabudu Allah na kupata ukuruba Wake.
Kuna sababu tofauti ambazo huwafanya wanadamu kunyimwa mahitaji ya muhimu ya maisha. Sababu ya msingi ya unyimwaji mwingi ni ‘kasoro ya chombo cha Neema’.
Vinginevyo Neema za Muumba humiminwa kwa wingi juu ya wote. Qur’an Tukufu kwa uzuri kabisa inaeleza kwa kinaganaga ukweli huu katika sura ya ar-Ra’d (13), aya 17:
أَنْزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَسَالَتْ أَوْدِيَةٌ بِقَدَرِهَا فَاحْتَمَلَ السَّيْلُ زَبَدًا رَابِيًا ۚ وَمِمَّا يُوقِدُونَ عَلَيْهِ فِي النَّارِ ابْتِغَاءَ حِلْيَةٍ أَوْ مَتَاعٍ زَبَدٌ مِثْلُهُ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّهُ الْحَقَّ وَالْبَاطِلَ ۚ فَأَمَّا الزَّبَدُ فَيَذْهَبُ جُفَاءً ۖ وَأَمَّا مَا يَنْفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّهُ الْأَمْثَالَ
“Ameteremsha maji kutoka mbinguni, na mabonde
yakamiminika maji kwa kadri yake…”
Kwa mfano, wale ambao wanakula vyakula ambavyo vingeharibu mfumo wao wa kuyeyusha chakula, wanajitengenezea wenyewe njia ya kujinyima chakula. Wale ambao hujiweka katika dhambi, huzuiya riziki zao wenyewe. Ufanisi wa mwili na halikadhalika wa kiroho hutegemea juu ya chombo. Vinginevyo, Mwingi wa rehema kamwe hawezi kufikiriwa kuwa bahili au mbinafsi. Siku zote ni al-Jawād (Mtoaji) na Mwenye Mikono iliyo Wazi.
Kwa hiyo, maji meupe na safi huteremka kutoka mbinguni, lakini siku zote chombo kichafu hupokea maji machafu, chombo chembamba siku zote hupokea maji kidogo, chombo kilichotoboka siku zote hupoteza maji, n.k. Hii ni kanuni ambayo Qur’an imeielezea vizuri sana kwa kinaganaga.
Inafaa kuangaliwa kwamba neno “Rahim” ambalo kila siku tunalitamka wakati tunaposoma Sura al-Fātiha halionyeshi kikawaida kwamba malipo Yake ya Rehema na Mwongozo yasiyokoma yamewekwa tu kwa ajili ya waumini, bali Rehema hizo humiminwa juu ya wote, lakini ni vyombo vile tu ambavyo vimeamini katika kweli na vina uwezo wa kukubali, vinaweza kunyonya Rehema hiyo. Kwa uwelewaji mzuri wa ukweli huu muhimu, wale ambao wanataka wanaweza kuangalia kitabu cha Ādāb al-Salāt cha marhum Imamu Khumayni.7
Neema Na Baraka Za Maombi Kwa Asiyekuwepo
Muelekeo mwingine muhimu sana katika maombi ni kuomba kwa ajili ya wegine wasiokuwepo. Kuna aya mbali mbali za Qur’an na hadithi ambazo zimeweka msisitizo mkali juu ya hili na kutaja malipo mazuri kwa ajili ya hili. Ifuatayo ni mifano ambayo inafaa kuangaliwa:
1. Mtukufu Mtume amenukuliwa akisema:
لَيْسَ شَيْءٌ أَسْرَعُ إِجَابَةً مِنْ دَعْوَةِ غَآئبٍ لِغَآئبٍ
“Hakuna kinachokubaliwa haraka kama maombi ya mtu kwa ajili ya mwingine wakati kila mmoja akiwa hayupo mbele ya mwenzake.”8
2. Imenukuliwa kutoka kwa Imamu al-Sadiq (a.s.) kwamba alisema:
دُعَآءُ الْمُؤْمِنِ لِلْمُؤْمِنِ يَدْفَعُ عَنْهُ الْبَلآءَ وَ يَدِرُّ عَلَيْهِ الرِّزْقَ
“Du’a ya mu’umini kwa ajili ya mu’umini mwingine humuondolea mabalaa na kummiminia riziki kubwa juu yake.”9
Mahitaji Kamili Ya Mwanadamu
Katika utamaduni wa Qur’an kila mwanadamu, hadhi yoyote awayo katika ulimwengu huu, ni muhitaji. Qur’an Tukufu [35: 15] inasema:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنْتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّهِ ۖ وَاللَّهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ
“Enyi watu ninyi ni masikini mbele ya Allah, na Allah ndiye
tajiri mwenye kuhimidiwa.”
Aya hii inakubaliana kikamilifu na dalili za kiakili ambazo huchukulia kila kiumbe tegemezi kijitegemee juu ya chanzo, ambacho ni Chenye Kujitegemea na kuwepo kwake ni Lazima na muhimu (Wajibul Wujud).
Kwa hiyo, wanadamu wote pamoja na vitu vyao, halikadhalika na vingine vyote tegemezi vinavyoishi, (ambavyo) kabisa huishi na kuruzukiwa kwa mwenendo wa Rehema na Neema za Mungu. Huwa tunasoma mausiku ya Alhamisi:
يَآ دآئِمَ الْفَضْلِ عَلَى الْبَرِيَّة
“Ewe mwenye kuwafadhili viumbe daima”10
Allah (s.w.t.) ni Rabbu’l ‘alamen. Maana ya ‘Rabb’ haipaswi kulinganishwa na neno “Bwana” kama kwa kawaida inavyotafsiriwa. Rabb kama ilivyotajwa katika tafsiri ya Al-mizān ina maana ya “al-Mālik al-Mudabbir” (mwenye kumiliki na msimamizi wa mambo yote) kwa maana ya kwamba Allah ni Mmiliki wa vitu vyote tegemezi vinavyoishi na kabisa ndiye msimamizi na wa vyote kwa kuvifanya vipate riziki na kudhibiti mambo yao ya kila kitu na kila dakika. Hivyo lazima tuondoe fikra mbaya waliyo nayo baadhi ya watu, ya kumtenga Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na umbaji Wake, na kusema ya kwamba hivi sasa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anapumzika. Ametakasika Mwenyezi Mungu na upungufu huu.
Kwa hiyo kama Mmiliki wa roho “katika hali halisi ya maneno” ni Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuna shaka kwamba kila mwanadamu wa hali yoyote ni maskini na muhitaji.
Hatua Ya Kuelekea Kwenye Kuondoa Umaskini
Katika kusoma ubeti huu wa du’a tunayo izungumzia, muombaji siku zote hudhani ya kwamba anawaombea wanaohitajia ambao hawana njia imara ya mapato yakuendeshea maisha hapa ulimwenguni. Tafsiri hii pia ni sawa, lakini kwa mtazamo wa maelezo tuliyo yatoa hapo juu ni lazima tujue ya kwamba umaskini ni mpana kushinda tunavyo dhania kwa kawaida.
Tunapomwomba Mwenyezi Mungu Awatajirishe maskini tunatakiwa kivitendo pia tuchukue hatua katika kuwatajirisha wengine kwa kiasi cha uwezo wetu. Jambo hili ni kwamba ndilo linalo tarajiwa kutoka kwetu kama tulivyo elezea hapo mwanzo.
Tunapoangalia sehemu hii ya du’a kwa makini tunafahamu ya kwamba mwenye kuisoma hawaombei wanaohitajia waondolewe haja zao kwa mda mfupi, kama tufanyavyo wengi wetu tunapowasaidia wanaohitajia kwa kipindi kifupi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuwanunulia mahitaji yao ya nyumbani. Na tukafurahi kwa kuwa tumemfurahisha Mwenyezi Mungu kwa kitendo chetu hiki. Bila ya shaka ni kitendo kizuri, na kina thawabu nyingi, lakini ni tafauti na yale tunayo muomba Mwenyezi Mungu kwenye sehemu hii ya du’a kwa kuwa lengo letu siyo maskini watoshelezewe haja zao muda mfupi, bali tunamuomba Mwenyezi Mungu awasaidie kwa kuwapa njia ya kudumu ya mapato, yaani, “Ewe Mola mtajirishe kila aliye maskini.”
Baada ya kuifahamu du’a hii, basi mwenye kusoma dua hii anatakiwa afikirie namna ya kutoa mchango wake katika kuwatajirisha maskini. Kwa mfano, yule mwenye mali anatakiwa angelifikiria namna ya kuwasaidia maskini ili wajianzishie biashara ndogondogo na kujitajirisha mwenyewe. Na yule mwenye biashara ndogo na anahitaji wafanyikazi angeliwaajiri maskini na awatajirishe kwa kiwango fulani. Na yule ambaye ni mwajiriwa, kutokana na kufahamiana kwake na matajiri angeliwaombea masikini kazi kwao. Wasomaji, linalohitajika hapa ni kufahamu mambo mbali mbali yanayo husiana na jambo hili tukufu. Na lililo muhimu hapa ni kwamba kila mtu achukue hatua kuhusiana na jambo hili.
•    1. Imam Khumayni, Jelwehaye Rahmani, imetafsiriwa na Al-Tawhid Journal, v. xi, no. 3&4 uk.68.
•    2. ‘Ali al-Muttaqi al-Hindi, Kanzu‘l ‘Ummal, j. 11, hadithi na. 32161.
•    3. Ami al-Islam Tabrasi, Tafsir Majma’ al-Bayan, j. 4, uk. 866.
•    4. Min al-Sha’r al-Mansūb ila al Imam al-Wasi ‘Ali bin Abi Talib, uk. 64.
•    5. Mawlā Sayyid Radi al-Din bin Tāwūs, Iqbāl al-Ā’māl, j.1, uk. 385.
•    6. Mawlā Sayyid Radi al-Din bin Tāwūs, Iqbāl al-Ā’māl, j. 1, uk. 384.
•    7. Imām Khumayni, Tafsir Sūrat al-Hamd, uk. 23
•    8. Muhammadi al-Rayy Shahri, Mizān al-Hikma, j. 2, uk. 887, tr. 5730.
•    9. Ibid, uk. 887, tr. 5730.
•    10. Kaf’ami, Misbah al-Kaf’ami, sehemu ya 46, uk.647.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini