Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 7)

0 Voti 00.0 / 5

DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 7)

اللّهُمَّ رُدَّ كُلَّ غَرِيبٍ

Ewe Mola Mrudishe Kila Alie Mgeni

MAANA YA ‘GHARIIB’

Kutokana na ujuzi mdogo wa baadhi ya tamaduni na lugha, baadhi yetu tunadhani kwamba neno ‘Ghariib’ lina maana ya ‘maskini’. Kwa mfano neno hili kwa ki-Urdu lina tumiwa kuonyesha umasikini wa mtu, lakini linapo tumiwa kwa maana makhsusi, kama vile ‘Gharibul watan’ lina kuwa na maana nyingine.
Kwa kiarabu ambayo ndio lugha ya asili ya neno lenyewe, ‘lina maana ya kitu kilicho mbali’. Kwa hivyo kitu chochote kilicho ghariib, kiko mbali.
Seyyid Ali al-Madani al Husayni katika ufafanuzi wake wa Sahifatul Sajjādiyya anasema:
الْغُرْبَةُ بالضمّ البَّعْدُ و الَنَّوَى
“Ghurba (yenye irabu ya dhumma juu ya ghayn) ina maana ya ‘mbali’ na masafa”.1
Kwa hiyo, Ghariib ni kitu chochote ambacho kiko mbali [katika kuhusiana na kitu kingine cho chote].
Katika lugha ya kiarabu, maneno yasiyojulikana vile vile hujulikana kama ghariib.
UFAFANUZI
Uchungu unaompata mtu alie mgeni unajulikana vizuri kwa yule ambaye amepitia hali hii au yuko katika hali hii.Yeyote anayekwenda nchi ya kigeni ana matarajio ya kurejea nyumbani akiwa salama na mzima. Na bila ya shaka hangelipenda kutengana na watu wake wa karibu au kuviacha vitu vyake anavyo vihitajia katika maisha.Wale ambao wameacha miji yao na wakakumbwa na misukosuko wakiwa njiani au wamekwama katika nchi nyingine, wanafahamu shida iliyoko ya kuwa mbali na nyumbani.
Historia ya miaka ya hivi karibuni imejaa mifano inayo vunja moyo ya kila msikilizaji mwenye kuhusika. Mazayuni kama walivyo kuwa katika miaka iliyoipita, wanaendelea kuzitesa sehemu mbali mbali za mataifa dhaifu ulimwenguni kwa kuzifanyia ugaidi na kuzihamisha, na hivyo basi kuwatoa wengi wasio na hatia wakiwemo wanawake na watoto katika miji yao, ili wapate uchungu wa mateso katika makambi ya wakimbizi.
Watu kama hawa ambao hawana hatia, wanahitajia msaada wetu. Na kama tulivyo taja pale mwanzo, tuna wajibika kuziangalia sehemu ambazo tunaweza kutoa michango yetu ipasavyo kuhusiana na jambo hili na tuwasaidia kwa vyovyote vile iwezekanavyo. Kwa mfano, ikiwa kuna michango inayotolewa kupitia kwa vyama vya kutoa misaada vinavyo aminika, tujaribu tutoe michango yetu kwa wingi iwezakanvyo. Na ikiwa tunaweza tumsaidie ili aweze kuyazoea maisha mapya ambayo amelazimika kuwa ndani yake. Na ikiwa hatuna uwezo wa kuyafanya haya yote, basi tusisahau kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awasahilishie yanayo wakabili na awape utulivu.
Kwa hivyo tunapo muomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) awarudishe walio mbali na kwao ambao hawawezi kurudi kutokana na shida mbali mbali, tusisahau tunayo yaona katika historia ya hivi karibuni yanayo husiana na watu kama hawa. Tuna wajibika kuwakumbuka wote ambao wanateseka kutokana na matatizo wanayo yapata ya kutolewa katika miji yao, kama vile wapalestina, wa- afghanistani na wengineo.
NYONGEZA ZA GHURBA
Ina wezekana mtu kuwa mgeni mahali fulani lakini akawa anafaidi sana maisha ya anasa. Matokeo yake mtu anaweza akawa hapatwi na uchungu wa kutengwa [mbali na jamaa zake]. Wale ambao Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewapa utajiri huwa hawapatwi na uchungu wa kutengwa [na watu wao]. Kwa wepesi wakati wowote wanaweza kurudi kwao bila ya shida yeyote. hadithi zifuatazo zinazungumzia jambo hili:
Imepokewa kutoka kwa Imam ‘Ali (a.s.) akisema kwamba:
الْغَنيُّ في الْغُرْبَةُ وَطِنٌ
“Utajiri ugenini ni uwenyeji.”2
Na kinyume chake ni kwamba, umaskini humfanya mtu akawa mgeni.
Imepokewa tena kutoka kwa Imam ‘Ali (a.s.)akisema kwamba:
الْفَقْرُ في الْوَطَنِ غُرْبَةٌ
“Umasikini (wa mtu) katika nchi (yake) ni ugeni.”
Vile vile imepokewa kutoka kwa Imam ‘Ali (a.s.):
اَلْمُقِلُّ غَرِيْبٌ فِى بَلْدَتِهْ
“Asiye na mali ni mgeni katika mji wake.”3
Huenda hii ni moja ya sababu ya neno Ghariib katika lugha ya ki-Urdu ikiwa linatumika kuonyesha umasikini.
NYONGEZA NYINGINE ZA GHURBA NI KAMA ZIFUATAVYO
1. Imam ‘Ali (a.s.) amesema:
اَلْغَرِيِبُ مَنْ لَيْسَ لَهُ حَبِيْبٌ
“Mgeni ni mtu yule ambaye hana rafiki.”
2. Imepokewa kutoka kwa Imam ‘Ali (a.s.) kwamba:
اَلأَحْمَقُ غَرِيْبٌ فِى بَلْدَتِهِ, مُهَانٌ بَيْنَ أَعِزَّتِهِ
“Mtu mpumbavu ni mgeni katika mji wake na kutwezwa baina ya rafiki zake.”
UWIANO WA KIPENGELE CHA NENO ‘GHARIIB’
Hadithi iliyotajwa hapo juu inaonyesha kwamba yeyote aliye mpumbavu ni ghariib (mgeni). Hata hivyo, hii isije ikachukuliwa katika hali yake halisi. Neno ghariib ni kiwakilishi. Kwa mfano, mtu ambaye ni mpumbavu japo kuwa ni ghariib (mbali) na kikundi cha wasomi, yuko nyumbani akiwa katika kikundi chake. Na hivyo hivyo kuhusiana na wasomi, wako mbali wakiwa katika kikundi cha wajinga, lakini ni wenyeji katika kikundi cha wasomi. Na hali nyingine ni wakati ikiwa wengi wa watu ni wajinga. Hapa tena wasomi ni wageni.
Imam ‘Ali (a.s.) amesema: -
الْعُلَمَآءُ غُرَبآء لِكثْرَةِ الْجُهَّالِ
“Wasomi ni wageni kutokana na idadi kubwa ya wajinga”.
Wakati mwingine wasomi huwa wageni katika kikundi cha wasomi wenzao. Kwa mfano, mtu ambaye amesomea kemia (madawa) na hana ujuzi wa filosofia ya mashariki, atakuwa ni mgeni katika kikundi cha wanafilosofia wa kiislamu na kinyume chake.
Pia kuna uwezekano vile vile wa mtu kuwa mgeni na mwenyeji kwa wakati mmoja. Kwa mfano, msomi anaweza kuwa mbali na mji wake lakini akawa karibu na wasomi wenzake, hivyo basi akawa ni mgeni na mwenyeji kwa wakati huo huo. Wakati mwingine msomi japokuwa yuko katika mji wake ambao wakazi wake ni wasomi kama yeye bado anaitwa mgeni kwa kuwa mbali na ujirani wa Allah (s.w.t.).
Ahlulbeit (a.s.) ni nyongeza ya Ghariib.
Waislamu wengi walikuwa hawayajui matokeo ya baadaye ya uamuzi uliochukuliwa kuhusu Ukhalifa baada ya kufariki Mtume (s.a.w.w.). Suala la Ukhalifa lilikuwa sio jambo la kufaidi utawala wa kidunia kwa muda fulani, bali ni jambo la kulinda mafunzo halisi ya Uislamu na uongozi wa wabebaji wa dini ya mwisho pamoja na vizazi vyao vya baadae. Huzuni kubwa aliyokuwa nayo Fatimah (a.s.) inaonyesha umbali uliokuwepo baina ya Umma na uwezo mpana wa kuona mambo aliokuwa nao Bibi Fatimah (a.s.). Yeye alikuwa akiwaza kuhusu siku za usoni, hali ya kuwa wengine walikuwa na lengo la kuuharibu uislamu na kuchukuwa kwa nguvu utawala wa kidunia. Moyo wake ulikuwa kwa ajili ya wanadamu wote, ambapo wengine waliwaza kuhusu mipango yao. Bibi Fatimah na Kizazi chake Kitukufu (a.s.) na maswahaba wachache waaminifu walikuwa ghariib kwa kuwa walikuwa mbali na wale ambao walikuwa wakimuasi Mungu na hawakuweza kutabiri misiba ambayo ingelifika taifa la ki-Islamu. Mtu anapojaribu kuwaza nyongeza hii ya ghurba, moyo huuma na ulimi ukashindwa kutamka na chozi likatiririka. Maneno yafuatayo ya Bibi Fatimah (a.s.) yanatupa picha ya hali hii:
Ummu salama alimuuliza bibi Fatimah (a.s.): “ Ewe Binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) umeamkaje?” bibi Fatimah (a.s.) alimjibu:
أصْبَحْتُ بَيْنَ كَمَدِ وَ كَرْبِ فَقْدِ النَّبِيِّ وَ ظُلْمِ الْوَصِيِّ
“Nimeamka nikiwa kati ya majonzi na huzuni ya kumkosa Mtume (s.a.w.w.) na kudhulumiwa kwa wasii wake.”4
Baada ya pigo hili kubwa juu ya msingi wa Ummah wa ki-islamu, Ahlul-Bayt (a.s.) na wafuasi wao halisi, daima wamekuwa ghariib miongoni mwa idadi kubwa ya umma wa ki-islamu.
GHURBA YA KILA MWANADAMU YA TABIA YENYE DOA
Ewe [Jina la asili ya (kila kitu) lililo na sifa zote zenye ukamilifu Mungu], warudishe ghurabā wote (walio mbali) [ambao wako mbali kiroho, ambao ina maana kwamba hawafaidi Sifa za Mungu].
Hafidh, mshairi mkubwa wa irfani anasema:
Man az diyāre habibam na az bilāde gharib
Muhayminā be rafiqāne khud rasān bāzam.5
“Mimi ninatoka katika mji wa wapendwa,
Siyo katika mji wa wageni,
Ewe Mola niunganishe tena na marafiki Zako.”
Mabwana katika njia ya kumfikisha mtu katika ukamilifu, wanaamini ya kwamba mwanaadamu ni msafiri hapa duniani. Ana njia ya kupita ambayo ni ‘dini’ au kwa maneno ya ki-Qur’an “sirat al mustaqim” na ‘kituo’ anachoelekea, ambacho ni kwa Allah (s.w.t.) Mwenyewe. Akidokezea hili, Allah (s.w.t.) anasema:
1. (Mwanadamu ni msafiri: Qur’an, 84: 6).
يَا أَيُّهَا الْإِنْسَانُ إِنَّكَ كَادِحٌ إِلَىٰ رَبِّكَ كَدْحًا فَمُلَاقِيه
“Ewe mwanadamu hakika wewe unajitahidi ukielekea kwa Mola wako kwa juhudi na bidii, basi utakutana nae”
2. (Njia: Qur’an Tukufu, Al-Fatiha-1: 5)
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
“Tuongoze kwenye njia iliyo nyooka.”
3. (Maelekeo, Qur’an Tukufu, al Fatir-35:18)
وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۚ وَإِنْ تَدْعُ مُثْقَلَةٌ إِلَىٰ حِمْلِهَا لَا يُحْمَلْ مِنْهُ شَيْءٌ وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۗ
إِنَّمَا تُنْذِرُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ بِالْغَيْبِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ ۚ وَمَنْ تَزَكَّىٰ فَإِنَّمَا يَتَزَكَّىٰ لِنَفْسِهِ ۚ
وَإِلَى اللَّهِ الْمَصِيرُ
“…na maelekeo ni kwa Mwenyezi Mungu.”
Dini kama ikitekelezwa vilivyo, inaweza kumuinua mwanadamu juu sana kiasi kwamba anaweza kuwavuka Malaika katika ukamilifu. Mtu mwenye kuvutiwa na hili anaweza kuuliza, ni dhikri gani au kitendo gani cha kufanya kama mtu angetaka kuanza safari ya kiroho kwenda kwa Allah. Jambo ambalo Tariqa (njia ya kiroho) ni lingine lisilokuwa Shari’a (sheria ya ki-Islamu) ni kikwazo kikubwa kilichokaziwa na shetani. Ni kwa kusoma tu Qur’an na Sunnah kwa usahihi na kufuata Tawdhiu’l-Masa’il (kitabu cha sheria za ki-islamu) ndipo mtu anaweza kupata ukamilifu wa juu.
Wengi wetu tuna mazoea ya kuwaza kwamba ‘ārif (mwanachuoni wa mambo ya dini na maarifa) ndiye ambaye lazima ajitenge wakati wote na kufanya baadhi ya dhikri na kungojea kufunuliwa kiroho (Mukāshafāt). Wanazuoni wetu wa Kishia hawakubaliani na dhana hii. Wanaamini kwamba vyote viwili, Sharia na Tariqa viko pamoja, vimeungana. Na ni kwa kutekeleza sheria za kiislamu na kuchunga sehemu zake zote za ndani, na halikadhalika taratibu zake za nje ndipo mwanadamu anaweza kupata ujirani wa Allah na kuwapita Malaika.
Upaaji wa mwanadamu kwenda kwa Mungu hakupaswi kufananishwa na safari ya kimwili. Safari ya leo ni nje ya mipaka ya muda wa sehemu. Kwa kweli amejitia rangi ya sifa za Mungu na hivyo kukaribia Hadhara Tukufu. Maimamu wetu (a.s.) ambao wamefikia vilele vya ukamilifu walikuwa ni udhihirisho wa Sifa za Mungu. Tazama hadithi ifuatayo:
Imam Ja’far al-Sadiq (a.s.) amenukuliwa akisema:
نَحْنُ اَلاسْمَاءُ الْحُسْنَى
“Sisi ni Majina Mazuri (ya Allah).6”
Hivyo, ili kurudi mjini kwetu, ambako ni wa jirani na Allah, lazima tujaribu kuchukuwa njia sahihi iliyowekwa na Allah; Qur’an Tukufu (35:18) inasema:
وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۚ وَإِنْ تَدْعُ مُثْقَلَةٌ إِلَىٰ حِمْلِهَا لَا يُحْمَلْ مِنْهُ شَيْءٌ وَلَوْ
كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۗ إِنَّمَا تُنْذِرُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ بِالْغَيْبِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ ۚ
وَمَنْ تَزَكَّىٰ فَإِنَّمَا يَتَزَكَّىٰ لِنَفْسِهِ ۚ وَإِلَى اللَّهِ الْمَصِيرُ
“...Na mwenye kujitakasa amejitakasa kwa ajili ya nafsi yake, na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu”.
Hivyo njia hii ni utakaso wa nafsi, ambao kuna tofauti na kufuata sheria za ki-islamu.
Hata hivyo, lazima tuelewe kwamba safari hii sio rahisi kama inavyoonekana kuwa. Kwani ili kufikia vituo mbali mbali vya safari, kiongozi aliyehitimu vizuri elimu ya dini, anahitajika sana, kwa vile njia imejaa vikwazo na shetani mlaaniwa, siku zote anaichunga njia hiyo. Siku zote anajitahidi kuweka kikwazo kwenye njia ya mtu ambaye amefanya uamuzi imara kufuata njia hii ya kiroho.
Hata hivyo, hii isije ikawavunja moyo wale ambao wako mbali na sehemu ambako viongozi kama hao hupatikana, kwani kuna mifano, ambayo huonyesha kwamba mtu anaweza kufikia vituo hivyo vitukufu bila uhusiano wa moja kwa moja na viongozi hao.
(Jukumu la msingi la Ahlul-Bayt (a.s.) siku zote linabakia. Tutaelezea hili katika majadiliano yetu ya baadae Insha-Allah.) Marhum Ayatullah Muhammad Husayn Tehrani anasimulia kisa cha kusisimua katika kitabu chake ‘Anwār-e-Malakut’ kama ifuatavyo:7

HESHIMA KWA MAMA HUMGEUZA MTU KUWA RAFIKI WA ALLAH (SWT)
(Ayatullah Tehrani anasimulia kwamba, siku moja alipo kuwa mjini Tehran alikwenda kwenye duka la vitabu la Ishamiyya lililoko mtaa wa Burarjumhari kununua vitabu. Alikuwa rafiki wa mmoja wa washiriika wa duka hilo anayeitwa Haj Sayyid Muhammad Kitab chi, ambaye alikuwa anahusika na bohari la duka hilo. Alikwenda dukani hapo kukutana naye na pia kununua vitabu. Ilikuwa wakati wa asubuhi na takribani saa nne zimebaki kabla ya adhuhuri. Mtu mwingine pia amekuja dukani pale kununua vitabu. Alipokuwa amekwisha nunua vitabu alivyohitaji, aliondoka, ghafla alianza kusema: Mungu wangu, Msaidizi wangu, roho yangu, roho yangu.
Ayatullah anasimulia: Katika kumuangalia, niliona kwamba uso wake umebadilika kuwa mwekundu na jasho linamtoka, alitumbukia katika furaha na raha kubwa isiyo kikomo. Nilimuita na kumuambia: Mpenzi Bwana! Mpenzi Darweshi, usile yote peke yako, hii sio tabia ya adabu; Aligeuka na kuanza kusoma baadhi ya mashairi ya Baba Tahir Uryan, (mwanairfani ajulikanae sana aliyezikwa Hamadan). Baada ya hapo alinyamaza na kisha akalia sana. Kisha alibadilika kuwa mwenye furaha na kucheka. Nilisema; Ahsante! (Baada ya hapo mazungumzo yalifuata. Wakati wa mazungumzo, Ayatullah Muhammad Husayn Tehrani alimuomba Darweshi yule amueleze jinsi anavyoweza kupata kituo kitukufu kama hicho, na Darweshi alielezea kisa chake kama ifuatavyo):
“Nilikuwa na mama mzee. Alikuwa mgonjwa wa kitandani kwa miaka mingi sana. Mimi peke yangu ndiye niliyekuwa ninamhudumia, na nilimsaidia shida zake zote: nilipika chakula kwa ajili yake, kumletea maji kwa ajili ya kufanyia wudhu, na nilikuwa katika huduma yake kwa ajili ya shida zake mbali mbali. Hata hivyo alikuwa mkali sana, wakati mwingine alinitukana, lakini niliyavumilia hayo na kumjibu kwa tabasamu. Kwa ajili ya tabia yake hii sikuoa, ingawa umri wangu ilizidi miaka arobaini. Hii ni kwa sababu, kuwa na familia pamoja na mama yangu mwenye tabia kama hiyo, ilikuwa haiwezekani kwangu nilijua kwamba kama nikioa, ima atasababisha tutengane, au nitalazimika kumuacha. Hata hivyo, kumtelekeza mama pia haikubaliki katika dhamira yangu. Hivyo niliamua kuvumilia na kubakia kapera, na nikajizoesha hali hii. Wakati mwingine kwa ajili ya uvumilivu mkubwa mbele ya ukali wake, nilihisi mwanga wa cheche katika moyo wangu, hali ya furaha na shangwe. Hata hivyo, hii huwa kwa muda tu. Hali hii iliendelea mpaka usiku mmoja wa baridi wa kipupwe. Niliweka kitanda changu karibu na chake ili kwamba asiwe peke yake, na asiwe na haja ya kunyanyua sauti yake kuniita kwa ajili ya haja zake. Siku hiyo nilijaza maji katika jagi na kuliweka karibu na kitanda changu ili wakati wowote mama akihitaji maji, nimpatie mara moja.
Katikati ya usiku huo aliomba maji, niliamka upesi na kujaza maji katika chombo kidogo na kumpa huku nikisema: Chukua mpenzi mama. Kwa vile alikuwa anasinzia sinzia hakujua kwamba nilimtekelezea haja yake mara moja alifikiri kwamba nilichelewesha kuleta maji . Kuona hivyo, alinitukana na matusi ya nguoni na akanipiga na kile chombo kichwani. Kwa haraka sana nilikijaza tena maji kile chombo, na kumuambia: Mpenzi mama chukua na unisamehe; nasikitika! Wakati ninasema hivi, nilipagawa, na sikuelewa kilichotokea baadae. Kwa ufupi, nilipata ukamilifu wangu huu: cheche zile zilibadilika kuwa ulimwengu wa nuru ufananao na miali ya jua, na Mpendwa wangu, Rafiki yangu, Msaidizi wangu na Mganga wangu alinisemesha. Kwa hiyo hali hii kamwe haikusimama. Na ni miaka sasa hali hii nimebaki nayo…”
Wapenzi wasomaji, kuna tofauti kubwa kati ya mtumishi kunong’onezana na Mpendwa wake, na Mpendwa kumnong’oneza Mtumishi wake. Kamwe usidhani kwamba tukio kama hilo haliwezekani kwani tafsiri nyingine ya Imam Ali (a.s.) kuna maelezo yake katika ‘Nahjul Balagha’ kama ifuatavyo:
وَمَا بَرِحَتْ لِلّهِ عَزَّتْ آلاَؤهُ فِي الْبُرْهَةِ بَعْدَ الْبُرْهَةِ، وَفِي أَزْمَانِ الْفَتَرَاتِ،
عِبَادٌ نَاجَاهُمْ فِى فِكْرِهِمْ، وَكَلَّمَهُمْ فِي ذَاتِ عُقُولِهِمْ،
“Katika vipindi na nyakati zote ambapo kulikuwa hakuna Mitume, kulikuwepo na watu ambao walikuwa ni neema kubwa za thamani za Allah, hunong’oneza katika nyoyo zao na kuzungumza katika asili ya akili zao.”8
Maadamu fursa hii ipo, “Shauku yetu ya kupata ubora” lazima iwe ni kupata makazi haya mahususi matukufu kabla ya kuutoka ulimwengu huu na kutokuweza kuufanya kitu chochote. Kuna tukio ika kusisimua sana lililosimuliwa katika Rawdhat al-Kafi na Imamu Muhammad al-Baqir a.s.9
DU’A YA BIBI KIZEE MWENYE AKILI KUBWA
عن أبي جعفر ( عليه السلام ) قال : إن رسول الله ( صلى الله عليه وآله ) كان نزل على
رجل بالطائف قبل الاسلام فأكرمه فلما أن بعث الله محمدا ( صلى الله عليه وآله ) إلى
الناس قيل للرجل : أتدري من الذي أرسله الله عز وجل إلى الناس ؟ قال : لا ، قالوا له :
هو محمد بن عبد الله يتيم أبي طالب وهو الذي كان نزل بك بالطائف يوم كذا وكذا
فأكرمته ، قال: فقدم الرجل على رسول الله ( صلى الله عليه وآله ) فسلم عليه وأسلم ،
ثم قال له : أتعرفني يا رسول الله ؟ قال : ومن أنت ؟ قال : أنا رب المنزل الذي نزلت به
بالطائف في الجاهلية يوم كذا و كذا فأكرمتك فقال له رسول الله (صلى الله عليه وآله):
مرحبا بك سل حاجتك ، فقال : أسألك مأتي شاة برعاتها ، فأمر له رسول الله (صلى
الله عليه وآله ) بما سأل ، ثم قال لأصحابه : ما كان على هذا الرجل أن يسألني سؤال
عجوز بني إسرائيل لموسى ( عليه السلام ) بما سأل ، فقالوا : وما سألت عجوز بني
إسرائيل لموسى ؟ فقال : إن الله عز ذكره أوحى إلى موسى أن أحمل عظام يوسف من
مصر قبل أن تخرج منها إلى الأرض المقدسة بالشام فسأل موسى عن قبر يوسف(ع)
فجاءه شيخ فقال:إن كان أحد يعرف قبره ففلانة ، فأرسل موسى ( عليه السلام ) إليها
فلما جاءته قال:تعلمين موضع قبر يوسف ( عليه السلام ) ؟ قالت : نعم قال: فدليني
عليه ولك ما سألت : قال : لا أدلك عليه إلا بحكمي ، قال : فلك الجنة ، قالت:
لا إلا بحكمي عليك ، فأوحى الله عز وجل إلى موسى لا يكبر عليك أن تجعل لها
حكمها فقال :لها موسى فلك حكمك ،قالت:فإن حكمي أن أكون معك في درجتك
التي تكون فيها يوم القيامة في الجنة فقال رسول الله ( صلى الله عليه وآله ):
ما كان على هذا لو سألني ما سألت عجوز بني إسرائيلز.
Kabla ya kuja kwa Uislamu, wakati mmoja Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alitembelea Ta’if, mtu mmoja alimkaribisha kwa ukarimu sana. Baadae Mtume (s.a.w.w.) alipoteuliwa kuwa Mjumbe wa Allah, yule mtu aliyemkaribisha Mtume aliulizwa: Je, unamjua mtu aliyeteuliwa na Allah kama Mjumbe wake kwa watu? Yule mtu akajibu “Simjui” wakasema: Ni Muhammad bin Abdillah, yatima wa Abi Talib, ambaye siku fulani alikuwa mgeni wako mjini Ta’if na ulimkaribisha kwa ukarimu sana. Aliposikia haya, mtu yule alikwenda katika hadhara ya Mtume (s.a.w.w.) akamsalimu, akasilimu na kisha akasema: Ewe Mjumbe wa Allah, je, unanitambua mimi? Mtume akasema, kwani wewe ni nani? Yule mtu akasema: Mimi ni mwenye nyumba ile ambayo ulifikia kule Ta’if zama za ujahiliyya, mimi ndiye niliyekukaribisha siku hiyo: Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema unakaribishwa sana; omba unalotaka. Yule mtu akasema: Ninataka kondoo 200 pamoja na wachungaji wake? Mtukufu Mtume akaamuru apewe alichotaka. Kisha aliwaambia Masahaba wake, ya kwamba alitamani kwamba yule mtu angeomba alichoomba Bibi kizee wa Bani Israil kutoka kwa Mtume Musa (a.s.); Masahaba wakauliza: ni kitu gani alichoomba Bibi huyo wa Bani Israil kutoka kwa Mtume Musa (a.s.)?
Mtume akasema.. aliuliza ni wapi lilipo kaburi la Mtume Yusufu (a.s.) na Hakika Allah alimfunulia Mtume Musa (a.s.) kubeba mifupa ya Mtume Yusufu (a.s.) kabla ya kuondoka Misri na kuelekea ardhi tukufu ya Sham ambapo hapo mwanaume mmoja mzee alimwendea na kusema: kama kwa kweli kuna mtu yeyote Mtume Musa (a.s.) aliyepata kujua lilipo kaburi la Mtume Yusufu (a.s.) basi ni Bibi kizee fulani. Mtume Musa (a.s.) alitaka aletwe kwake na wakati alipofika katika hadhara yake, alimuuliza Je, unajua sehemu lilipo kaburi la Mtume Yusufu (a.s.)? Yule Bibi akasema: Ndio Mtume Musa akasema: kwa hiyo nielekeze kwenye kaburi hilo na nitakupa chochote utakachoomba.
Yule Bibi akasema: Sitakuelekeza isipokuwa mpaka ukubali ninachotaka kama malipo. Mtume Musa akasema: ‘Utapata pepo.’ Yule Bibi akasema, hapana, isipokuwa ninachotaka. Hapo ndipo Allah (s.w.t.) akamteremshia Mtume Musa wahayi akamuambia kwamba kukubali ombi lake hakuwezi kushindikana kwako. Kwa hiyo Mtume Musa a.s. alisema ‘Vizuri’ utapata unachotaka: Yule Bibi akasema: Ningetaka kuwa na wewe katika kituo kimoja ambacho utapata katika Pepo siku ya Hukumu. Akisimulia hili Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema kwa nini mtu huyu hakuomba kile ambacho Bibi kizee yule wa Bani Israil alichoomba?
Hadithi hii fupi inatoa somo muhimu sana kwetu sisi. Tafakari juu ya hamu kubwa ya Bibi Kizee yule anapewa pepo lakini anaikataa. Anatamani zaidi ya hiyo. Alitamani kituo kile kile ambacho Mtume Musa a.s. atakachofaidi katika Akhera ambacho si kingine bali ni ujirani wa Allah au Jannat al-liqa (Pepo ya kukutana na Allah). Zifuatazo ni aya za Qur’an ambazo hudokeza kwenye kituo hiki kitukufu.
1.Qur’an Tukufu Sura al-Fajr - 89: 27-30
يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ.ارْجِعِي إِلَىٰ رَبِّكِ رَاضِيَةً مَرْضِيَّةً .
فَادْخُلِي فِي عِبَادِي . وَادْخُلِي جَنَّتِي
“Ewe nafsi iliyo tua! Rudi kwa Mola wako ukiwa umeridhia, mwenye kuridhiwa (na Mwenyezi Mungu). Basi ingia katika waja wangu (wazuri) na uingie Pepo Yangu.”
2. Qur’an Tukufu Sura al-Qamar - 54:54-55
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَهَرٍ .فِي مَقْعَدِ صِدْقٍ عِنْدَ مَلِيكٍ مُقْتَدِرٍ
“Bila shaka wachamungu watakuwa katika mabustani na mito. Katika kikao cha haki Kwake Mfalme Mwenye uweza wote.”
Kwa dhahiri hamu kubwa ya Bibi kizee wa Bani Israil hutufanya sisi wote kuelewa haja yetu ya kweli ya asili na kuomba kama inavyopasa. Hivyo basi, tusipoteze fursa ya mausiku ya qadir ambayo yametolewa kwetu. Hamu yetu iwe ni kusamehewa dhambi zetu na ujirani wa Allah (s.w.t.). Naam, kuomba maisha marefu, riziki ya kutosha, n.k kwa vile njia ya kutuwezesha kupata ujirani wa Allah (s.w.t.) vile vile kunapendekezwa sana.
Vitabu vyetu vya du’a maombi vimejaa maelezo ya haja kama hizo. Lakini haja za kidunia lazima siku zote ziombwe kama njia kwa ajili ya malipo makubwa kwa Mwenyezi Mungu. Vinginevyo neema hizo hizo za kiduniya zinaweza sikaufanya mwanya ukawa mkubwa. Hebu natupate somo kutoka kwa Bibi Asia Mke wa Firauni, ambaye pamoja na kufaidi raha zote za kidunia, hakusalimu amri kwa Firauni na akayakabili mateso makubwa kutoka kwake. Allah (s.w.t.) anataja maombi yake kama ifuatavyo:

وَضَرَبَ اللَّهُ مَثَلًا لِلَّذِينَ آمَنُوا امْرَأَتَ فِرْعَوْنَ إِذْ قَالَتْ رَبِّ ابْنِ لِي عِنْدَكَ بَيْتًا


فِي الْجَنَّةِ
وَنَجِّنِي مِنْ فِرْعَوْنَ وَعَمَلِهِ وَنَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ
“Ewe Mola wangu unijengee Karibu Na Wewe nyumba katika pepo”.
Ayatullah al-udhma na mboni ya macho yetu, Sheikh Jawadi Amuli (Allah akirefusha kivuli chake kitukufu) mfasir wa kisasa wa Qur’an na kwa hakika mrithi wa kweli wa mwalimu wake Allama Tabatabai katika fani ya Tafsir anasema:10
“Mwanamke huyu anaomba Pepo karibu na Mwenyezi Mungu, ambapo wengine wanaomba Pepo tu. Hata hivyo Bibi huyu kwanza anaomba kwa ajili ya (kupata radhi ya) Mwenyezi Mungu na kisha kwa ajili ya nyumba karibu na Mwenyezi Mungu. Hasemi: Rabbi ibni li baytan fi-Jannat (Ewe Mola wangu, jenga nyumba kwa ajili yangu katika Pepo) Wala hasemi: Rabbi ibni li bayatan indaka fil Jannat (Ewe Mola wangu nijengee Nyumba karibu na Wewe katika pepo). Bali anasema: Rabbi ibni li indaka baytan fil Jannat (Ewe Mola wangu nijengee Karibu na Wewe nyumba katika pepo) kwanza anataja ujirani wa Allah na kisha anazungumza kuhusu Pepo. Yaani kama ni jambo la ‘al-Jaar, thummaddar’ (kwanza ujirani, kisha nyumba), Bibi huyu anasema Allah thumma al-Jannat (kwanza Allah, na kisha Pepo). Kwa hakika pepo ambayo ni, indallah (karibu na Mungu) ni tofauti sana na pepo ambayo chini yake inapita mito…
‘Allāma Tabātabāi anasema:11
الْجَمْعُ بَيْنَ كَوْنِ الْبَيْتِ الْمَبْنِيِّ لَهَا عِنْدَ اللّهِ وَ فِي الْجَنَّةِ لِكَوْنِ الْجَنَّةِ
دَارَ الْقُرْبِ مِنَ اللّهِ...
“Kuomba nyumba ijengwe karibu na Mungu na katika Pepo kwa wakati huo huo, ni kwa ajili ya ukweli kwamba Pepo ni Makazi ya ujirani kwa Mungu.”
WAUMINI WA KWELI NI GHARIIB!
Kuna hadithi mbali mbali ambazo kwa dhahiri huelezea kwamba mu’umini ni mgeni. Kwa mfano:
1. Imam Muhammad Al-Baqir (a.s.) amenukuliwa akisema:
الْمؤمِنُ غَرِيْبٌ وَطُوبَى لِلْغُرَبآءِ
“Mu’umini ni mgeni, na baraka ziwe kwa wageni!”12
2. Kāmil at-Tammār anasema:
سَمِعْتُ أبَا جَعْفَرٍ ( عليه السلام ) يَقُوْلُ : النَّاسُ كُلُّهُمْ بَهَائِم - ثلاثا - إلا قَلِيْل
مِنَ الْمُؤْمِنينَ وَالْمُؤْمِنُ غَرِيْبٌ ثلاث مَرَّاتٍ
“Nimemsikia Abu Ja’far (Imamu Muhammad al-Baqir ambaye juu yake iwe amani) akisema mara tatu: Watu wote ni wanyama, isipokuwa wachache katika waumini; na mara tatu, Mu’umini ni mgeni (ghariib)”13
“Allāma majlisi katika kitabu chake kikubwa, Bahari za Nuru anatoa ufafanuzi juu ya hadithi hii kama ifuatavyo:
بيان كلهم بهائم أي شبيه بها في عدم العقل وإدراك الحق وغلبة
الشهوات النفسانية علي القوي العقلانية كما قال تعالي إِنْ هُمْ
إِلاَّ كَالأنْعامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ سَبِيلا إلا قليل كذا ...المؤمن غريب
لأنه قلما يجد مثله فيسكن إليه فهو بين الناس كالغريب الذي
بعد عن أهله ووطنه...
Ufafanuzi: “Wote ni wanyama” ina maana wanafanana nao katika kutotumia akili zao, na kutokutambua ukweli na katika matamanio yao ya nafsi yanayotawala ustadi wao wa akili, kama Allah (s.w.t.) anavyosema: “Wako kama wanyama; bali, wamepotea zaidi … Mu’umini ni mgeni kwa sababu hata mara chache hapati mfano wake ambaye kwamba anaweza kupata utulivu katika yeye, kwa hiyo yuko miongoni mwa watu kama mgeni, ambaye yuko mbali na familia yake na nyumbani kwake…”14
Hivyo, mambo yafuatayo yanaweza kuwa sababu za mu’umini kuwa “ghariib”:
1. Mu’umini kwa kawaida anatamani usuhuba wa Muumba wake Mpendwa na kujitahidi kufikia kituo hiki kitukufu. Maadamu hajafikia kituo hicho, hujiona mwenyewe kila siku ni mgeni. Imamu ‘Ali (a.s.) amenukuliwa akisema:
الدُّنْيَا دَارُ الْغُرْبَةِ وَ مَوْطِنُ الِّاشْقِيآء
“Dunia ni nyumba ya ugeni na makazi kwa ajili ya wenye huzuni.”
Na habari ifuatayo imeelezwa katika hadithi nyingine.
حُبُّ الْوَطَنِ مِنَ الإِيْمَانِ
“(Mtu) kuipenda nchi yake ni dalili ya Imani.”15
2. Waumini ni wageni katika kusuhubiana na makafiri, Hii ni kwa sababu wakati ambapo wanaishi katika ulimwengu wa imani, upendo wa Mwenyezi Mungu na kujihusisha na ukombozi wa wanadamu, makafiri hawatambui ukweli huu na wamejiambatanisha wenyewe kwenye mambo ya dunia na neema zake.
KWA NINI IMAMU ALI AL-RIDHA (A.S.) ALIKUWA AKIJULIKANA KAMA IMAM AL-GHARIIB
Wakati mwingine tunapomsalimia Imam wetu wa nane (a.s.) tunasema:
السَّلاَمُ عَلَيْكَ يَا غَرِيبَ الْغُرَبَاء
“Amani iwe juu yako, ewe mgeni wa wageni.”
Mwalimu wa Ayatullah Muhammad Husayn Tehrani katika somo la Haddad, wakati mmoja aliuliza sababu ya Imamu al-Ridha kujulikana kama Imam al-Ghariib. Alijibu katika baadhi ya maelezo sababu mbili mtu anaweza kuzitaja ni:16
1. Imamu alikuwa anafaidi daraja ya Wilaya, ambayo ilikuwa tukufu mno, na karibu na ujirani wa Mwenyezi Mungu lakini mbali kutoka kwa wanadamu wengine. Watu wengi walikuwa hawana utambuzi wa sifa za Wilayat na tabia za Wali (ambaye ni udhihirisho wa sifa za Mwenyezi Mungu). Hivyo Imamu alikuwa ni Ghariib miongoni mwa watu wao.
2. Ma’amun alimlazimisha Imamu kwenda Marvi, na Imamu (a.s.) alilazimika kuuwacha mji wake, familia yake na ujirani wa kaburi la Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Hivyo alikuwa Ghariib… na kwa nyongeza, kumuita kwenda Marv ni aina ya ufungwa, uhamisho na kufungwa jela, kwani pamoja na kumpa mamlaka na cheo cha waliyyul ahdi (mrithi wa Khalifa) alimzuia shughuli zake zote. Hakuruhusiwa kutoa hukumu za kisheria wala kusalisha Ijumaa na Iddi.
Katika Ziyarat nyingine17 vile vile tunamuita Imamu Husain (a.s.) kama Ghariib al-Ghuraba. Na katika hadithi iliyosimuliwa katika kitabu cha ‘al-Mashhadi al-Mazar al-Kabir’, Imamu Ja’far al-Sadiq (a.s.) amenukuliwa akiuliza kundi la watu swali lifuatalo:
فَمَا يَمْنَعْهُمْ مِنْ زِيَارَةِ قَبْرِ الْغَريْب....
“Na ni kitu gani kilichowazuia kuzuru kaburi la al-Ghariib (ana maana ya Imamu al-Husain (as.).”18
MJINI KWAKE GHARIIB
Sayyid ‘Ali Khan al-Husayni al-Madani, katika kitabu chake ‘Riyadh al- Salikiina’ ananukuu maelezo yafuatayo:
سئل أبو جعفر الشّاشي : من الغريب ؟ فقال : الذي يطلبه رضوان في الجنّة فلا يجده ويطلبه
مالك في النّار فلا يجده ويطلبه جبرئيل في السّماوات فلا يجده ويطلبه إبليس في الأرض
فلا يجده ، فقال له أهل المجلس وقد تفطّرت قلوبهم : يا أبا جعفر فأين يكون
هذا الغريب ؟ فقال : في مقعد صدق عند مليك مقتدر
“Abu ja’far al-Shashi aliulizwa: ‘Ni nani mgeni (ghariib)? Akasema: ‘Ni mtu ambaye Malaika Ridhwan anamtafuta katika pepo, lakini hamuoni, mtu ambaye Malik (Malaika wa motoni) anamtafuta katika Moto wa Jahannam, lakini hamuoni, mtu ambaye Jibril anamtafuta mbinguni, lakini hamuoni, mtu ambaye iblis anamtafuta katika ardhi, lakini hamuoni.’ Hivyo watu katika hadhara ile wakamuuliza kwa mioyo iliyokata tamaa: ‘Ewe Abu Ja’far, basi mgeni huyu yuko wapi?’ Akasema: ‘Katika makazi ya kweli pamoja na Mfalme Mwenye Nguvu zaidi (54:55).”
Dalili Kubwa Ya Malalamiko Ya Ghurba Katika Du’a Ya Kumeil
Uma’suum wa Imam ‘Ali (a.s.) ni ukweli uliothibitishwa na hivyo tusingelitaka kujishughulisha sana katika kulielezea hilo. Tunajua vile vile msemo wake mashuhuri:
لَوْ كُشِفَي الْغِطَآءُ مَا ازْدَدْتُ يَقِيْنًا
“Lau litaondolewa pazia hakuna kitakacho ongezeka kwenye yakini yangu.”19
Kwa nini basi aonyeshe hofu yake ya kutenganishwa kutokana na Mpendwa? Huu ni utenganisho wa aina gani? Hii ni ghurba ya aina gani isiyovumilika?
Imamu Khomeini katika kitabu chake: ‘Hadithi Arubaini’ wakati anapoelezea viwango vya uvumilivu vya wanachuo wa elimu ya kiroho (Irfan) anasema:
“Kiwango kingine ni kile cha ‘sabr a’nillah’, (subira kutoka kwa Mungu) ambacho hufungana kwenye daraja za wapenzi wa Mwenyezi Mungu na za wale waliobarikiwa na udhihirisho (ahlash-shuhud wal-ayan) wakati mwingi kimaisha na utulivu. Hiki ni cheo kigumu na chenye tabu sana, na cheo hicho kinamuonyesha Bwana wa wasafiri wa kiroho, Amiri wa Waumini, na Kiongozi wa wakamilifu, yaani ‘Ali ibn Abi Talib Talib (a.s.) katika du’a tukufu ya Kumeil.
فَهَبْنِي يَا إِلَهِي وَسَيِّدِي وَمَوْلاي وَرَبِّي صَبَرْتُ عَلَى عَذَابِكَ؛
فَكَيْفَ أَصْبِرُ عَلَى فِرَاقِكَ
“Ewe Mungu wangu, Bwana wangu na Mola wangu! Hata kama ningelikuwa na uwezo wa kuvumilia adhabu yako, vipi nitavumilia utenganisho wako.?”
Pengine msemo ufuatao wa Imamu ‘Ali a.s. vile vile huelezea ukweli wa jambo hili:
نَارُ الْفُرْقَةِ أَحَرُّ مِنْ نَارِ جَهَنَّمِ
“Moto wa utenganisho ni mkali mno kuliko Moto wa Jahannam.”20
اللّهُمَّ رُدَّ كُلَّ غَرِيب
Ewe Allah, mrudishe kila mgeni
Kwa hiyo, wakati tunaomba kurudishwa kwa wageni wote, lazima tuombe kutoka kwa Allah:
1. Kurudi kwa wale wote ambao wamefukuzwa kutoka kwenye nyumba zao na kupatwa na maumivu ya utenganisho.
2. Kurudi kwa watu wote wenye dhambi kwenye ujirani wa Allah ambapo kwa ukweli ni: (1) kumkamilisha mwanadamu katika masuala ya Sifa za mwenyezi Mungu kama vile elimu, uvumilivu n.k. na (2) kupunguza mwanya wa daraja la juu sana la wageni kama la Maimamu (a.s.) na daraja la watu wa chini kama wenye dhambi na hivyo kuondoa ghurba ya Maimamu kutoka kwa wengine pia. (Nukta hii inafaa tafakari). Vinginevyo, katika hali nyingine, Maimamu (a.s.) kwa kuwa kwao karibu na Allah (s.w.t.) kamwe hawajawa gharib (wageni). Hii ni kwa sababu kamwe hawajawa mbali kutoka kwenye mji wao wa kiroho. Kuna taarifa nzuri sana iliyosimuliwa na al-Zamakhshari katika kitabu chake, ‘Rabi al-Abrar’, yafaa kuitafakari:
لَمَّا أُخْرِجَ يُوْسف (ع) من الجبّ واشتُرِي قَالَ لهم قائل:
استوصوا بِهَذَا الغريب خَيْرًا. فقال لهم يوسف : من كان مع الله
فلَيس في غربة
“Wakati Yusufu (a.s.) alipotolewa kisimani, na kununuliwa, mtu mmoja akawaambia mchungeni mgeni huyu (Ghariib). (Aliposikia hivi) Yusufu (a.s.) akasema kuwaambia: Yeyote yule ambaye yuko pamoja na Allah (s.w.t.) sio mgeni.”21
•    1. Sayyid ‘Ali Khān, Riyādh al-Sālikin, j. 1, uk. 473.
•    2. Marhūm Āmadi, Tasnifu Ghurari’l Hikam, uk. 369.
•    3. Marhūm Āmadi,Mu’jamu Alfāzi Ghurari’l Hikam, uk. 810.
•    4. Allāma Majlisi, Bihār al-Anwār, j. 43, uk.156, tr. 5.
•    5. Hāfidh Shirāzi, Diwāne Khwājah Hāfidh, toleo la Pezhman, uk.150, Ghazal 334.
•    6. Allāma Majlisi, Bihār al-Anwār, j. 25, uk. 4, tr. 7.
•    7. Āyatullah Tehrāni, Anwāre Malakūt, j. 1, uk. 141 – 145.
•    8. Imam ‘Ali (a.s.), Nahju’l Balāgha, hutuba ya 222.
•    9. Thiqatu’l Islām al-Kulayn, Rawdhat al-Kāfi, j. 8, uk. 110 – 111.
•    10. Āyatullah Jawādi Āmuli, Zan dar āineye Jamālo Jalāl, uk. 156 – 157.
•    11. ‘Allāma Tabātabā’I, al-Mizān, j. 19, uk.344.
•    12. Mustadrak Safinat al-Bihār, j. 7, uk. 550.
•    13. Thikat al-Islam al-Kulayni, Al-Kāfi, j. 2, uk. 242.
•    14. ‘Allāma Majlisi, Bihār al-Anwār, j.64, uk.160.
•    15. Shaykh ‘Abbas Qummi, Safinat al-Bihār, j. 8, uk. 525.
•    16. ‘Āyatullah Sayyid Muhammad Husayn Tehrāni, Al-Tawhid Quarterly Jounal, j. xiii, no. 4, uk. 72 – 85.
•    17. ‘Allāma Majlisi, Bihar al-Anwār, j. 98, sura 18, uk. 230.
•    18. Al-Shaykh Abū ‘Abdllāh Muhammad bin Ja’far al-Mashhadi, al-Mazār al-Kabir, uk. 333 toleo la kwanza Qum Iran.
•    19. ‘Allāma Majlisi, Bihāru’l Anwār, j. 40, uk.153, tr. 5.
•    20. Mirāth-e-Hadithe Shi’e, j. 8, uk. 217.
•    21. Abu’l Qasim Mahmud bin ‘Umar al-Zamakhshari, Rabi al-Abrar wa Nusus al-Akhbar, j. 3, uk. 5.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini