Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MUHAMMAD MTUME WA ALLAH 3

0 Voti 00.0 / 5

MUHAMMAD MTUME WA ALLAH 3

KUZALIWA MPAKA KUANZA KWA WAHYI

MWENDELEZO WA MAKALA NO:2

VITA VYA BANI QURAIZAH
Hawa Bani Quraizah walikuwa wamefikia makubaliano ya mkataba na Waislam, lakini waliukiuka mkataba huo kwa kujiunga na watu wa Makkah katika vita vya Ahzab. Hivyo, baada ya vita vya Ahzab, Waislamu walisonga mbele kuwaendea Bani Quraizah ambao mwishowe walisalimu amri kwa Waislamu. Mtume alipendekeza kwao wao kukubali usuluhishi wa Sa’d bin Ma’z. wao walikubali na wakashughulikiwa kwa uamuzi wake: kuwauwa wapiganaji na kutaifisha mali zao.
VITA VYA BANI MUSTALAQ
Katika mwaka wa sita wa hijiria, lile kabila la Mustalaq lilikiuka haki za Waislam. Na matokeo yake, iliwabidi wakabiliane na majeshi ya Waislam mahali panapoitwa Maris’a na walishindwa vita hivyo.
VITA VYA KHAYBAR
Idadi kubwa ya makabila ya kiyahudi yalifanya makazi yao katika ngome za khaybar na maeneo ya karibuni ya Arabia ya kaskazini. Walikuwa na ushirikiano wa karibu sana na watu wa Makkah na walikuwa kila mara wakiwatishia Waislam. Katika mwaka wa saba wa hijiria, Mtume aliamua kumkabili adui.
Waislamu walitoka kijeshi kwenda Khaybar, wakaizingira na hatimae wakapata ushindi baada ya Ali kusonga mbele, akaiteka ile ngome kuu na akamuua yule shujaa jasiri mkuu kuliko wapiganaji wote wa Kiyahudi.
MKATABA WA HUDAYBIA NA KUANGUKA KWA MAKKAH
Katika mwaka wa sita wa wa hijiria, Mtume aliamua kwenda Makkah kuhiji. Watu wa Makkah waliwazuia Waislamu mahali panapoitwa Hudaybia na hawakuwaruhusu kuingia mjini hapo. Makabiliano haya yaliiishia kwenye mkataba wa amani baina ya Mtume na Makuraishi wa Makkah. Mkataba huu wa amani ulijenga mazingira salama kwa kiasi fulani, kwa Mtume kuanza kupanua ule wito wa Uislamu kwa makabila na watu walio mbali na bara Arabu.
Kama matokeo ya shughuli za Mtume na jitihada zisizo na ubinafsi za Waislam katika kipindi kile, Uislam uliendea kote katika peninsula ya Arabia. Zilikuwepo pia barua zilizoandikwa kwa wafalme wa nchi zingine kama vile Persia, Byzantine na Abyssinia zikiwaalika wafalme hao kuukubali Uislamu.
Wakati huu Mtume aliishi katika umasikini na ufukara na alikuwa na fahari nayo hali hiyo. Hakuwahi kutumia muda wake wowote bure bure tu. Bali muda wake wote uligawanywa katika sehemu tatu: moja kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, katika kumuabudu na kumkumbuka Yeye; sehemu nyingine kwa ajili yake binafsi na watu wa nyumbani kwake na mahitaji ya nyumbani; na sehemu kwa ajili ya watu. Katika wakati wa sehemu hii ya muda wake alijishughulisha katika kueneza na kufundisha Uislamu na elimu zake, kusimamia mahitaji ya jamii ya Kiislamu, kuondoa maovu yoyote yaliyokuwepo, kuhudumia mahitaji ya Waislam, kuimarisha mafungamano ya ndani na nje, na mambo mengine kama hayo.
Moja ya masharti ya mkataba huu wa amani lilikuwa ni kwamba Maquraishi wasingeweza kuwadhuru Waislamu au yoyote kati ya washirika wao walioungana nao. Sharti hili, hata hivyo lilikiukwa na Maquraishi pale walipolisaidia kabila la Bani Bakr dhidi ya kabila la Bani Khuza’a-hilo la kwanza ni washirika wa Maquraishi na hili jingine ni washirika wa Waislamu. Mtume aliwaomba Maquraishi kuheshimu mkataba huo, wavunje ushirikiano wao na kabila la Bani Bakr na kuwafidia wale waathirika wa uchokozi wao. Maquraishi walikataa kutii na kufuata masharti ya mkataba wao. Mtume, akiwa na jeshi lililoandaliwa vizuri lenye nidhamu ya hali ya juu, lenye takriban askari 10,000 liliingia Makkah katika mwaka wa nane baada ya hijiria na wakaiteka bila upinzani mkubwa.
Mji huo, ambao ulikuwa umekataa ujumbe wake, na kupanga njama dhidi ya wafuasi wake na wakaungana katika njama ya kumuua yeye, sasa akawa chini ya huruma yake. Mtume aliwauliza watu wa Makkah: “Ni nini mnachoweza kutarajia kutoka kwangu?” Wao wakajibu: “Huruma! Ewe bwana mkarimu na mtukufu!” Kama angependa, angeweza kuwafanya wote kuwa watumwa wake. Lakini Muhammad – “rehma kwa ajili ya ulimwengu” akasema: “Nitaongea nanyi kama Yusuf alivyoongea na ndugu zake. Sitawasuteni leo; Mwenyezi Mungu atakusameheni, kwani Yeye ni Mwingi wa Huruma na Upendo. Nendeni, mko huru kabisa!”
Kwa kuanguka kwa Makkah, kila kizuizi cha mwisho katika njia ya Uislamu kilikuwa kimeondolewa na watu wengi na makabila ya Waarabu katika peninsula ya Arabia yakaanza kuukubali ujumbe wa Uislam. Hivyo ule mwaka wa tisa wa hijiria unajulikana kama “Mwaka wa ujumbe” kwa sababu ya ile idadi ambayo siyo ya kawaida ya wajumbe waliokuwa wakija Madina kuja kutoa heshima zao kwa Mtume hapo Madina.
HIJJA YA MWISHO NA KIFO
Katika mwaka wa kumi wa hijiria, Mtume aliamua kwenda kufanya Hijja. Aliwaalika Waislamu kuungana naye na wajizoeshe kanuni za hija. Zaidi ya Waislam mia moja elfu waliungana naye katika hijja hii. Ingawa hii ni hijja ya mwanzo na ya mwisho ya Mtume, lakini inajulikana kama “al-Hijjatul’wida hija ya muago.” Aliichukua fursa hii ya ule mkusanyiko ambao haujawahi kutokea ili kuwakumbusha Waislamu juu ya mambo mengi muhimu na thamani ya Uislam.
Akiwa njiani akirudi kwenda Madina, alisimama mahali panapoitwa Ghadir Khum na akatoa hotuba ndefu sana ambamo alifanya muhtasari wa yale mafundisho muhimu makuu ya Uislam, akawajulisha kuhusu kifo chake kilichokuwa kina karibia na akamteua Ali bin Abi Talib kuwa mrithi wake.
Baada kuishi kwa miaka kumi ya Madina, Mtume aliugua na kufariki baada ya siku chache tu za maradhi yake. Kwa mujibu wa Riwaya zilizopo, maneno ya mwisho kwenye midomo yake yalikuwa ni ushauri kuhusiana na watumwa na wanawake.
HESHIMA YA LA MARTINE KWA MTUME
Mwanahistoria wa kifaransa wa karne ya kumi na nane, La Martine, anaandika yafuatayo katika kitabu chake “Histoire de la Turquie (1854) kuhusu Mtume wa Uislam:
“Kamwe mwanadamu hajajiwekea mwenyewe, kwa hiari au bila kukusudia, lengo adhimu sana, kwa lengo hili lilikuwa la nje ya uwezo wa kibinadamu: Kuangamiza imani za ushirikina ambazo zilikuwa zimeingilia kati baina ya mwanadamu na muumba wake, kumrudisha Mungu kwa mwanadamu na mwanadamu kwa Mungu; kudumisha lile wazo la kimantiki na tukufu la kimungu katikati ya vurugu za miungu ya kidunia na yenye sura mbaya ya uabudu masanamu uliokuwepo wakati huo…..”
“Kama ukuu wa lengo, ufinyu wa nyenzo, na matokeo ya kushangaza ndivyo kigezo halisi cha kipaji cha kibinadamu, ni nani angeweza kuthubutu kumlinganisha mtu yoyote maarufu katika historia ya kisasa na Muhammad?.......”
“Mwanafalsafa, msemaji mwenye fasaha, nabii, mwanasheria, mpiganaji, mtekaji wa mawazo, mdumishaji wa imani zenye mantiki, mtindo usiokuwa na sura mbali mbali (makundi); mwanzilishi wa dola ishirini za kidunia na ufalme mmoja wa kiroho, huyo ni Muhammad. Na kuhusu vipimo vyote ambavyo kwavyo umaarufu wa kibinadamu unaweza kupimwa navyo, tunaweza kuuliza, hivi kuna binadamu yoyote mashuhuri

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini