IMAM MAHDI NDANI YA RIWAYA ZA KISUNNI 1
IMAM MAHDI NDANI YA RIWAYA ZA KISUNNI 1
WANAVYUONI WA MADHEHEBU YA SUNNI WAMEKIRI KUWA IMAM MAHDI (A.S.) AMESHAZALIWA
Kuna matamko mengi ya kukiri kuwa Imam Mahdi (a.s.) ameshazaliwa ambayo Sunni wameyasajili kwa kalamu zao. Na baadhi wamefanya kazi ya kuchunguza kukiri huku katika uchambuzi hasa unaojitegemea, hivyo uchunguzi huu ulikuwa unafuatana zama kwa zama kiasi kwamba haishindikani mwenye kukiri sasa kuhusu kuzaliwa kwa Mahdi kukutana na aliyekiri zama zilizotangulia, na hilo ni kuanzia zama za ghaibu fupi ya Imam Mahdi (a.s.) (260 – 329 A.H.) Na mpaka zama zetu hizi.
Sisi tutafupisha kwa kuwataja baadhi yao, ama atakayetaka kwa urefu na upana ni juu yake kurejea uchunguzi uliotangulia kuhusu kukiri huko,1 na hao baadhi ni:
1. Ibnul-Athir Al-Jazariy Izud-Din aliyefariki mwaka 360 A.H. Amesema ndani ya kitabu chake Al-Kamil fit-Tarikh kwenye mlango wa matukio ya mwaka 260 A.H. kuwa: “Ndani ya mwaka huo alifariki Abu Muhammad Al-Alawi Al-Askari, naye ni mmoja wa Maimamu kumi na wawili wa madhahebu ya Imamiyya, na yeye ndiye mzazi wa Muhammad ambaye wanamwamini kuwa ndiye anayengojewa.”2
2. Ibnu Khallakan aliyefariki mwaka 681 A.H. Amesema ndani ya kitabu Wafayatul-Aayan: “Abu Qasim Muhammad bin Hasan Al-Askari bin Ali Al-Hadiy bin Muhammad Al-Jawwad aliyetajwa kabla ni Imam wa kumi na mbili kwa mujibu wa imani ya Shia Imamiyya maarufu kwa sifa ya Hujah….mazazi yake yalikuwa siku ya Ijumaa nusu ya Shabani mwaka mia mbili hamsini na tano.” Kisha akanukuu kutoka kwa mwanahistoria Ar-Rahalah Ibnul-Azraqu Al-Fariqiy aliyefariki mwaka 577 A.H. kuwa amesema ndani ya kitabu Tarikh Mayyafariqina kuwa: “Hakika Hujjah aliyetajwa amezaliwa Mfunguo sita mwaka mia mbili hamsini na nane, na imesemekana kuwa ni mwezi nane Shabani mwaka hamsini na sita, na ndio kauli sahihi mno.”3
Nasema: Kauli sahihi kuhusu siku ya kuzaliwa kwake (a.s.) ni ile aliyoise- ma mwanzo Ibnu Khallakan, nayo ni siku ya ijumaa nusu ya mwezi wa Shaban mwaka mia mbili hamsini na tano, kauli hiyo wameafikiana Shia wote. Wametoa riwaya nyingi sahihi kuhusu hilo huku wanavyuoni wao waliotangulia wakithibitisha hilo, hakika Sheikh Al-Kulayni aliyeishi zama za ghaibu ndogo ameitoa tarehe hii kwa ukamilifu, kutoa kulikosal- imika na akaitanguliza kabla ya riwaya zinazoikhalifu tarehe hiyo. Amesema kwenye mlango unaohusu kuzaliwa kwake (a.s.): “Amezaliwa (a.s.) nusu ya Shaban mwaka mia mbili hamsini na tano.”4
As-Saduq aliyefariki mwaka 381 A.H. Amepokea kutoka kwa Sheikh wake Muhammad bin Muhammad bin Iswam Al-Kulayniy kutoka kwa Muhammad bin Yaqub Al-Kulayniy kutoka kwa Ali bin Muhammad bin Bandari amesema: “Imam wa zama hizi (a.s.) alizaliwa nusu ya Shaban
mwaka mia mbili hamsini na tano.”5 Na Al-Kulayniy hajanasibisha kauli yake kwa Ali bin Muhammad kwa sababu ya umashuhuri wake na kuwe- po itifaki juu yake.
3. Ad-Dhahabiy aliyefariki mwaka 747 A.H. Amekiri ndani ya vitabu vyake vitatu kuwa Mahdi (a.s.) ameshazaliwa, na hatujafuatilia vitabu vyake vingine. Amesema ndani ya kitabu chake Al-Ibaru: “Na ndani ya mwaka huo (yaani ndani ya mwaka 256 A.H.) alizaliwa Muhammad bin Hasan bin Ali Al-Had bin Muhammad Al-Jawwad bin Ali Ar-Ridha bin Musa Al-Kadhim bin Jafar As-Sadiq Al-Alawi Al-Husayniy, Abu Qasim ambaye Shia walimpa lakabu ya Al-Khalafu Al-Hujjah, wakampa pia lak- abu ya Al-Mahdi na Al-Mantadhar, na wakampa lakabu ya Sahibuz-Zaman na yeye ndiye hitimisho la Maimamu kumi na wawili.”6
Na amesema kwenye kitabu Tarikh Duwalil-Islam katika wasifu wa Hasan Al-Askari kuwa: “Hasan bin Ali bin Muhammad bin Ali Ar-Ridha bin Musa bin Jafar As-Sadiq, Abu Muhammad Al-Hashimiy Al-Husayniy ni mmoja wa Maimamu ambao Shia wanadai utakaso wao, na huitwa Hasani Al-Askari kwa kuwa aliishi Samrau, kwani eneo hilo huitwa Al-Askari, na yeye ndiye mzazi wa yule anayengojewa na Shia. Alifariki huko Samrau mwezi nane mfunguo sita mwaka mia mbili na sitini na akazikwa ubavuni mwa mzazi wake.
Ama mwanaye Muhammad bin Hasan ambaye Shia wanamwita Al-Qaim Al-Khalafu Al-Hujjah yeye alizaliwa mwaka wa hamsini na nane, na inase- mekana ni mwaka hamsini na sita.”7
Na amesema ndani ya kitabu Siru Aalamin-Nubalai: “Sharifu Al- Muntadhar Abu Qasim Muhammad bin Hasan Al-Askari bin Ali Al-Hadiy bin Muhammad Al-Jawwad bin Ali Ar-Ridha bin Musa Al-Kadhim bin Jafar As-Sadiq bin Muhammad Al-Baqir Ibnu Zaynul-Abidina Ali bin Husein As-Shahidu Ibnu Imam Ali bin Abi Talib Al-Alawi Al-Husayni ni hitimisho la mabwana kumi na wawili.”8
Nasema: Kinachotuhusu sisi katika rai ya Ad-Dhahabiy kuhusu kuzaliwa kwa Mahdi tayari tumeshakifafanua. Ama kuhusu imani yake juu ya Mahdi ni kuwa yeye ni kama katika kauli zake zote nyingine bado alikuwa anan- gojea sirabi, kama tulivyoweka wazi hilo kuhusu mtu anayeamini kuwa Mahdi ni Muhammad bin Abdullah.
4. Ibnu Al-Wardiy aliyefariki mwaka 749 A.H. mwishoni mwa muhtasari ujulikanao kwa jina la Tarikh Ibnul-Wardiy: “Muhammad bin Hasan Al- Khalisu alizaliwa mwaka mia mbili hamsini na tano.”9
5. Ahmad bin Hajar Al-Haythamiy Ash-Shafiy aliyefariki mwaka 974 A.H. amesema kwa maelezo haya ndani ya kitabu chake As-Sawaiqul-Muhriqah mwishoni mwa sura ya tatu ya mlango wa kumi na moja: “Abu Muhammad Hasan Al-Khalisu, na Ibnu Khallakani amemfanya huyu kuwa ndio Al-Askari, alizaliwa mwaka mia mbili thelathini na mbili…..alifia huko Samrau na alizikwa karibu na baba yake na ami yake akiwa na umri wa miaka ishirini na minane, na inasemekana kuwa alipewa sumu, na wala hakumwacha ila mwanae wa kiume Abu Qasim Al-Hujah, na alikuwa na umri wa miaka mitano baba yake alipofariki. Lakini Mwenyezi Mungu alimpa hekima na anaitwa Al-Qaim Al-Muntadhar. Imesemekena ni kwa kuwa alifichwa huko Madina na akatoweka na haikujulikana amekwenda wapi.”10
6- As-Shabrawiy Ash-Shafiy aliyefariki mwaka 1171 A.H. ametamka wazi ndani ya kitabu chake Al-Ittihafu kuwa: “Imam Mahdi Muhammad bin Hasan Al-Askari (a.s.) amezaliwa usiku wa nusu ya Shaban mwaka mia mbili hamsini na tano hijiriya.11
7. Muumin bin Hasan As-Shablanjiy aliyefariki mwaka 1308 A.H. Ndani ya kitabu chake Nurul-Absar amekiri ndani ya maneno mengi kuwepo jina Imam Mahdi na nasaba yake tukufu toharifu, na kuniya yake na lakabu zake, mpaka akasema: “Na yeye ndiye Imam wa mwisho katika maimamu kumi na wawili kwa mujibu wa imani ya Shia Imamiyya.”12
8’. Khayrud-Dini Az-Zarkiliy aliyefariki mwaka 1396 A.H. Amesema ndani ya kitabu chake Al-Aalam katika wasifu wa Imam Mahdi Al- Muntadhar: “Muhammad bin Hasan Al-Askari Al-Khalisu bin Ali Al- Hadiy Abu Qasim, Imam wa mwisho kati ya maimamu kumi na mbili wa Shia Imamiyya….alizaliwa Samrau na baba yake alifariki yeye akiwa na umri wa miaka mitano….Na katika tarehe ya kuzaliwa kwake inasemekana kuwa ni nusu ya Shaban mwaka mia mbili hamsini na tano, na katika tare- he ya kwenda ghaibu ni mwaka mia mbili sitini hijiriya.”13
Nasema: Tarehe ya kuanza ghaibu ndogo ni mia mbili na sitini hijiriya, hiyo ni kwa itifaki ya Shia wote pamoja na wengine walioandika kuhusu ghaibu ndogo katika vitabu tulivyoviona, na huenda tarehe iliyomo ndani ya kitabu Al-Aalam inatokana na makosa ya chapa, kwa sababu Az- Zarkiliy hajaandika tarehe ya ghaibu kwa herufi bali kaandika kwa tarakimu, na hivyo uwezekano wa kuwepo makosa katika kuchapa tarakimu ni jambo rahisi mno. Na kuna matamko mengine mengi ya kukiri ambayo uchambuzi hauturuhusu kuyanukuu.14
REJEA:
• 1. kitabu Al-Iman As-Sahih cha As-Sayyid Al-Qazwiniy. Kitabu Al-Imam Al-Mahdi fi Nahjul-Balagha cha Sheikh Mahdi Faqih Imaniy. Kitabu Man huwa Imamul-Mahdi cha At-Tabriziy. Kitabu Ilzamun-Naswib cha Sheikh Ali Al-Yazdiy Al-Hairiy. Kitabu Al-Imam Al-Mahdi cha ustadhi Ali Muhammad Dakhil. Kitabu Difau Anil-Kafiy cha As-Sayyid Thamir Al-Umaydiy. Ndani ya hiki cha mwisho wametajwa watu mia moja na ishirini na nane kutoka Sunni ambao wamekiri kuwa Imam Mahdi (a.s.) ameshazaliwa huku akiwapanga kulingana na karne zao, hivyo wa kwanza wao alikuwa ni Abubakri Muhammad bin Harun Ar-Riwayaniy ndani ya kitabu chake Al-Musnad aliyefariki mwaka 307 A.H. Na wa mwisho wao alikuwa ni ustadhi wa zama zetu Yunus Ahmad As-Samirai ndani ya kitabu chake Samirau fi Adabul-Qurni At-Thalithu Al-Hijiriy, kilichochapwa kwa msaada wa chuo kikuu cha Baghdadi mwaka 1968 A.D. Tazama Difau Anil-Kafiy 1: 568 – 592 chini ya anwani: Dalili ya sita: Matamko ya kukiri kwa Sunni.
• 2. Al-Kamil fit-Tarikh 7: 274 mwishoni mwa matukio ya mwaka 260 A.H.
• 3. Wafayatul-Aayan 4: 176, 562.
• 4. Usulul-Kafiy 1: 514, mlango wa 125.
• 5. Kamalud-Dini 2: 430, mlango wa 42.
• 6. Al-Ibaru fi Khabari Man Ghabara 3: 31.
• 7. Tarikhul-Islam: Juzuu ya kumi na tisa, kwenye matukio na vifo (251 – 260 A.H.): 113.
• 8. Siru Aalamin-Nubalai 13: 119, wasifu namba 60.
• 9. Nurul-Absar: 186. Hatujapata ndani ya Tarikh Ibnu Al-Wardiy ndani ya mwaka uliyotajwa, hatujui je, maelezo yaliondolewa?!!!
• 10. As-Sawaiq Al-Muhriqah cha Ibnu Hajar Al-Haythamiy, chapa ya kwanza: 207 na chapa ya pili: 124 na chapa ya tatu: 313 – 314.
• 11. Al-Ittihafu Bihubil-Ashrafi: 68.
• 12. Nurul-Absar: 186.
• 13. Al-A’alam 6: 80.
• 14. Rejea Al-Mahdi Al-Muntadhar fil-Fikri Al-Islamiy, kilichotolewa na Markazur-Risalah: 123 – 127.
ITAENDELEA..