UDHUU KWA MTAZAMO WA QUR’ANI NA SUNNA 5
UDHUU KWA MTAZAMO WA QUR’ANI NA SUNNA 5
MWENDELEZO WA MAKALA ILIYOPITA
KUPAKA JUU YA MIGUU: KATIKA HADITH SAHIHI
Kwa hakika umetambua - kutokana na dalili ya Aya - kuwa faradhi maha- la pa miguu ni kupaka, na kwa sababu Aya iliteremka mwisho mwisho wa maisha ya Mtume na hazijaondolewa hukumu bado, kwa hiyo zenyewe binafsi ni dalili tosha juu ya lililokusudiwa.
Isipokuwa kwa ajili ya kutilia nguvu makusudi, sisi tutataja yaliyoelezwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) na kutoka kwa maswahaba wake kuwa yalazimu kupaka juu ya miguu, na kwa hilo twafupisha kwa kuonyesha yaliyo kwenye matni peke yake pamoja na kujiepusha na sanadi, kwa sababu risala hii haina nafasi ya kuzitaja (sanad).
YALIYOELEZWA KUTOKA KWA MJUMBE WA MWENYEZI MUNGU KUHUSU KUPAKA MIGUU
1. Kutoka kwa Bisru bin Sa’id alisema: Alimpelekea Uthmani kigoda akaomba maji, alisukutua na kuvuta maji puani kisha aliosha uso wake mara tatu na mikono yake mara tatu tatu na alipaka sehemu ya kichwa chake na miguu yake mara tatu tatu, hatimaye alisema:
(Ra’aytu Rasulallahi (s.a.w.w.) hakadha tawadhwa’a yaa haaulai’a kadhalika? Qaaluu: Na’am, linafarin min as’haabi Rasuulillahi (s.a.w.w.)26
“Nilimuona Mtume wa Mungu akitawadha kama hivi, oh ninyi, ndivyo? Walisema: Na’am, kwa watu miongoni mwa maswahaba wa Mtume wa Mungu (s.a.w.w.).”
2. Kutoka kwa Hamrani alisema: Uthmani aliomba maji akatawadha kisha alicheka, hatimaye alisema: “Hamuniulizi nacheka nini?” Wakasema: “Ewe Amiirul’muuminna kitu gani kimekuchekesha?”Akasema: “Nimemuona Mtume wa Mungu akitawadha kama nilivyotawadha, alisukutua na kupandisha maji puani na aliosha uso wake mara tatu na mikono yake mara tatu na alipaka sehemu ya kichwa chake na juu ya unyayo wake.”27
3. Na katika Musnad ya Abdullahi bin Zaid Al-Maazniy kuwa Mtume (s.a.w.w.) alitawadha na aliosha uso wake mara tatu na mikono yake mara mbili na alipaka kichwa chake na miguu yake mara mbili.28
4. Kutoka kwa Abu Matar alisema: Wakati sisi tumeketi pamoja na Ali msikitini, alikuja mtu kwa Ali na alisema: “Nionyeshe wudhu wa Mtume (s.a.w.w.).” Alimwita Qambar, na alisema: Niletee kimtungi cha maji, akaosha mikono yake na uso wake mara tatu, aliingiza baadhi ya vidole vyake kinywani na alipandisha maji puani mara tatu, na aliosha dhiraa zake mbili mara tatu na alipaka kichwa chake mara moja na miguu yake miwili mpaka ka’abu mbili hali ndevu zake zinatona kifuani mwake hatimaye alikunywa funda moja baada ya wudhu kisha akasema:
Muulizaji wa wudhu wa Mtume wa Mungu (s.a.w.w.) yu wapi? Ni kama hivi ulivyokuwa wudhu wa Mtume wa Mungu (s.a.w.w.).”29
5. Kutoka kwa Ubbadu bin Tamim, kutoka kwa baba yake, amesema: “Nimemuona Mtume wa Mungu (s.a.w.w.) alitawadha na alipaka kwa maji juu ya ndevu zake na miguu yake.”30
6. Kutoka kwa Ali bin Abi Talib (a.s.) alisema: “Nilikuwa naonelea kuwa chini ya nyayo mbili ndiko kunastahiki kupakwa kuliko juu yake mpaka nilipomuona Mjumbe wa Mungu anazipaka juu yake.”31
Kutoka kwa Rufa’ata bin Raafi’i kuwa yeye alimsikia Mjumbe wa Mungu (s.a.w.w.) akisema:
(Annahu la yajuzu swalatu ahadikum hata yasbaghal’wudhua kama ama- rahu llahu azza wajalla,thumma yagh’silu wajhahu wayadayhi ilal’mir- faqayni, wayamsaha ra’asahu warijlayhi ilalka’abayni)32
(Kwamba Swala ya mmoja wenu haitojuzu mpaka akamilishe wudhu kama Mungu Mtukufu alivyomuamrisha, kisha aoshe uso wake na dhiraa zake mbili pamoja na mirfaqi mbili - viwiko viwili na apake kichwa chake na miguu yake miwili mpaka ka’ab mbili.”
7. Yaliyoelezwa kutoka kwa Abdullahi bin Amrin, alisema: “Alichelewa mbali na sisi Mtume wa Mungu (s.a.w.w.) katika safari tulioisafiri, alitudiriki hali Swala imetupita nasi twatawadha tukawa tunapaka juu ya miguu yetu, akanadi kwa sauti yake ya juu kabisa:
(way’lu lil’a’aqabi minannari)(ole wa nyayo na moto) mara mbili au tatu.33
8. Kutoka kwa Abu Maaliki Al’Ash’ariy kuwa aliiambia kaumu yake: “Jikusanyeni niwaswalisheni Swala ya Mtume wa Mungu (s.a.w.w.).”
Walipojikusanya, alisema: “Je kati yenu kuna ambaye si katika ninyi?” Wakasema: “Laa, isipokuwa mtoto wa dada yetu.” Akasema: “Mtoto wa dada wa kaumu ni miongoni mwao.” Akaagiza bakuli ndani yake muna maji, akatawadha na akasukutuwa na kupandisha maji puani, akaosha uso wake mara tatu na dhiraa zake mbili mara tatu, na alipaka sehemu ya kichwa chake na juu ya nyayo zake mbili, hatimaye aliwaswalisha, alifanya takbir nao ishirini na mbili.”34
9. Kutoka kwa Ubaadu bin Tamim Al-Maazniy, kutoka kwa baba yake kuwa yeye alisema: “Nilimwona Mjumbe wa Mungu akitawadha na ana- paka maji juu ya miguu yake miwili.”35
10. Kutoka kwa Ausi bin Abiy Ausi Athaqafiy kuwa yeye alimuona Mtume wa Mungu (s.a.w.w.) alikuja kwenye mfereji wa kaumu huko Twaifu, alitawadha na alipaka juu ya nyayo zake.36
11. Kutoka kwa Rufa’ata bin Raafi’u alisema: Nilikuwa nimeketi kwa Mtume wa Mungu (s.a.w.w.) punde mtu mmoja alimjia aliingia msikitini akaswali na alipomaliza swala akaja na kumsalimu Mjumbe wa Mungu (s.a.w.w.) na kaumu ya waliokuwa na Mjumbe wa Mungu, hapo akasema Mtume wa Mungu ( s.a.w.w.): (Irja’a fa swali fa innaka lam tuswal) Rejea ukaswali kwa kuwa haujaswali) yule mtu akawa anaswali, nasi tukawa tunaiangalia Swala yake hatujui kinachoitia dosari, na alipokuja na kumtolea salamu Mtume (s.a.w.w.) na ile kaumu ya watu Mtume (s.a.w.w.) alimwambia: (wa alayka irji’i fa swali fainnaka lam tuswali) (yakupasa urejee ukaswali kwa kuwa haujaswali).
Hammaam alisema: “Hatujui kama alimwamuru kufanya hivyo mara mbili au tatu.” Yule mtu alisema: “Sijui kilichoitia dosari swala yangu?”Akasema mjumbe wa Mungu (s.a.w.w.): “Kuwa Swala ya mmoja wenu haitimii mpaka akamilishe wudhuu kama Mungu alivyomuamuru, aoshe uso wake na mikono yake miwili mpaka viwiko vyake viwili na apake sehemu ya kichwa chake na miguu yake na ka’ab zake mbili, hatimaye asome tak’biiratul’iharam na amsifu Mungu, kisha asome Sura ya Al-fatihah na anayoijuwa na kuwa rahisi, kisha asome takbiira na afanye rukuu, aweke vitanga vya mikono yake juu ya magoti yake kiasi cha kutulia viungo vyake na vitulie kisha aseme: Samia llahu liman hamidah, na asimame sawasawa mpaka ausimamishe mgongo wake na kila mfupa uchukuwe nafasi yake, halafu asome takbiira na asujudu aumakinishe uso wake.”
Hammamu alisema: “Huenda alisema paji lake la uso ardhini mpaka maun- gio yake yatulie na kupumua kisha asome takbiira na akae sawasawa kwa makalio yake na kuusimamisha uti wa mgongo wake.
Aliielezea Swala kama hivi mpaka alimalizia rakaa nne, halafu alisema: “Swala ya mmoja wenu haitotimia mpaka awe amefanya hivyo.”37
12. Kutoka kwa Ibn Abbas yeye alisema: “Kulielezwa kupaka juu ya nyayo mbili mbele ya Umar na Sa’ad na Abdullah bin Umar. Umar bin Al- Khattab alisema: “Sa’d ni mwanachuoni zaidi kuliko wewe.” Umar alisema: “Ewe Sa’d kwa kweli sisi hatupingi kuwa Mtume wa Mungu (s.a.w.w.) alipaka – yaani juu ya nyayo mbili-lakini je, alipaka tokea ilipoteremshwa Suratul-Maaidah, kwa kuwa (hiyo) imeimarisha kila kitu na imekuwa Sura ya mwisho katika Qur’an isipokuwa Baraa’ah.”38
13. Kutoka kwa Urwa bin Zubair kuwa Jibraiyl (a.s.) alipoteremka kwa Mtume (s.a.w.w.) mwanzo wa bi’itha alizibua chemchem ya maji huko al’Ijaazi alitawadha na Muhammad (s.a.w.w.) yuamwangalia; aliosha uso wake, na mikono yake mpaka viwiko viwili na alipaka baahi ya kichwa chake na miguu yake mpaka kaabu mbili. Na Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alifanya kama alivyomuona Jibrail anafanya.39
14. Abdur Rah’man bin Jubair bin Nufair alieleza kutoka kwa baba yake kuwa babe Jubairi alikuja kwa Mtume (s.a.w.w.) akiwa na binti yake ambaye alimuoa Mjumbe wa Mungu, Mtume wa Mungu aliagiza chombo cha maji akaosha mikono yake miwili aliinadhifisha, kisha alisukutua mdomo wake na kupandisha maji puani, halafu aliosha uso wake na mikono yake miwili mpaka viwiko viwili mara tatu, kisha alipaka kichwa chake na miguu yake.40
Mpaka hapa yametimia tuliyogundua katika riwaya kutoka kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) kwa sura ya mpito, nazo zaonyesha kuwa kauli ya Mtume na kitendo chake ilikuwa ni kupaka sio kuosha.
YALIYOELEZWA KUTOKA KWA MASWAHABA NA TAABI’INA KUHUSU KUOSHA MIGUU
15. Sufian alituhadithia alisema: “Nilimuona Ali (a.s.) alitawadha akapa- ka juu (ya nyayo) mbili.”41
16. Kutoka kwa Hamrani kuwa yeye alisema: “Nilimuona Uthman akiagiza maji ya kutawadha, akaosha vitanga vyake mara tatu na alisukutua na kupandisha maji puani na aliosha uso wake mara tatu na dhiraa zake mbili mara tatu na alipaka baadhi ya kichwa chake na juu ya nyayo zake.”42
17. Aaswimu’al-Ah’walu kutoka kwa Anasi alisema: “Qur’an ilishuka na kupaka na Sunna (ilishuka) na kuosha. Na isnadi hii ni sahihi.”43
18. Ikrimah, kutoka kwa Ibn Abbas alisema: “Wudhu ni (sehemu) mbili za kuosha na mbili za kupaka.”
19. Abdullah al-Aatkiy, kutoka kwa Ikrimah alisema: Si wajibu kuiosha miguu miwili imeteremka kuihusu kuipaka.”
20. Kutoka kwa Jaabir kutoka kwa Abii Jafar Al’Baaqir (a.s.) alisema: “Paka juu ya kichwa chako na nyayo zako mbili.”
21. Kutoka kwa Ibn Alyata bin Daudi, kutoka kwa Aamir Asha’abiy kuwa yeye alisema: “Ni kupaka juu ya miguu miwili, huoni (sehemu ambazo) zilikuwa wajibu kuosha zimefanywa wajibu kupaka na ambazo zilikuwa wajibu kupaka zimetelekezwa (katika tayammumu).”
22. Kutoka kwa Aamiru Ash’shaabiy, alisema: “Vimeamriwa vipakwe katika tayammamu ambavyo viliamriwa vioshwe katika udhu, na ame- batilisha alivyoamrisha vipakwe katika wudhu: Kichwa na miguu miwili.”
23. Kutoka kwa Aamiru Ash’shqaabiy alisema: “Vimeamrishwa vipakwe kwa mchanga katika tayammumu (viungo) vilivyoamrishwa vioshwe kwa maji na kutupiliwa mbali vilivyoamrishwa kupakwa kwa maji.”
24. Yunus alisema alinihadithia ambaye aliyefuatana na Ikrima mpaka Waasiti alisema: “Sikumuona akiosha miguu yake, bali alikuwa akiipaka juu yake mpaka aliporudi kutoka huko.”
25. Qutadah katika kutafsiri kauli yake (s.w.t.):
(fagh’silu wujuhakum wa aydiyakum ilalmarafikqi wamsahuu biru’usikum wa arjulakum ilal’kaabayni) na osheni nyuso zenu na dhiraa zenu mpaka viwiko, na pakeni baadhi ya vichwa vyenu na miguu yenu mpaka kwenye ka’ab mbili). Mungu amefaradhisha (sehemu mbili za) kuosha na mbili za kupaka.
26. Musa bin Anas alimwambia Abiy Hamza kuwa Al’Hujaju alituhutubia huko Ah’wazi tukiwa pamoja naye, alitaja atwahuuru akasema:
Igh’silu wujuhakum wa aydiyakum wamsahu biru’usikum wa arjulakum, na kwamba hapana kitu kwa mwanadamu kilicho karibu mno na uchafu wake kuliko nyayo zake, basi osheni chini yake na juu yake na kano zake mbili.” Anas akasema: “Mungu amesema kweli na al-Hujaju amesema uwongo, amesema Mungu (s.w.t.) (wamsahu biru’usikum wa arjulakum).
Alisema: “Na Anas alikuwa aoshapo miguu yake huilowanisha.” Amesema Ibn Kathiir: Isnaadi yake ni sahihi.44
27. Ash’Shaabiy alisema: “Jibril aliteremka na kupaka, kisha Ash’Shaabiy alisema: huoni kuwa mwenye kufanya tayamumu yampasa apake aliyokuwa akiosha na45 aache aliyokuwa akipaka.”46
28. Ismail nilimwambia Aamiru ash’Shaabiy: Kuwa watu wanasema kuwa Jibril aliteremka na kuosha miguu miwili? Akasema: “Jibril aliteremka na kupaka.”47
29. Nizaalu bin Sabrah kuwa Ali aliomba maji akatawadha kisha alipaka juu ya ndara zake na nyayo zake. Hatimaye aliingia msikitini alivua viatu vyake kisha akaswali.48
30. Abiy Dhwabian alisema: “Nilimuona Ali akiwa na shuka ya rangi manjano na kishali na mkononi mwake kuna mkuki alikuja kwenye shamba la Asajin kisha alichepuka alitawadha na alipaka juu ya ndara zake na nyayo zake hatimaye aliingia msikitini, na akavua ndara zake kisha akaswali.49
Hii ni nyembamba kutoka nene na kidogo kutoka kingi, kwa mwenye kupekuwa sanadi nyingi na Sihahi na majaamiu ya Aathaar ataelewa mengi kuliko tulioelewa kwa njia ya mpito.
أُولَٰئِكَ الَّذِينَ هَدَى اللَّهُ ۖ فَبِهُدَاهُمُ اقْتَدِهْ ۗ{90}
“Hao ndio ambao Mungu amewaongoa hivyo fuateni muongozo wao.” (Al-An’aam: 90).
KUPUUZA RIWAYA ZA KUPAKA
Kwa kweli amezipuuza Ibn Kathir na waliomfuata riwaya za kupaka na alisema: Rawafidhu wamekhalifu hilo (kuosha miguu miwili) bila ya egemeo, bali kwa ujahili na upotovu, kwakuwa Aya tukufu yajulisha wajibu wa kuosha miguu miwili pamoja na ilivyothibiti kwa tawatur tendo la Mtume (s.a.w.w.) kwa kuafikiana na ilivyojulisha Aya tukufu, na wao wanakwenda kinyume na hayo yote,
na wala hawana dalili iliyo sahihi katika suala lenyewe.50
Kana kwamba hakuizingatia kwa makini Aya tukufu na uwazi wa dalili yake juu ya kulazimika kupaka, na kana kwamba hakuzielewa hizo Hadith nyingi alipodai kuwa kuna tawatur katika kuosha, au alielewa lakini hakuzizingatia.
Na sheikh Ismail Al-Burusawiy amemfuata akisema: “Rawafidhu wanaitakidi kuwa la wajibu kuihusu miguu ni kupaka, na wamezieleza habari (riwaya) dhaifu zisizo za kawaida kuhusu kupaka.”51
Na hivyo hivyo amedai Al-Alusi, Shia wamejiangika na riwaya moja: alisema wala hawana hoja katika madai ya kupaka ila riwaya walioitoa kwa Ali (Karamallah Taala Wajihahu)
(innahu masaha waj’hahu wa yadayhi, wa masaha ra’asahu warijlayhi, washariba fadhla twahurihi qaiman).52
Hata ikiwa al-Burusawiy na al-Alusiy wamesamehewa kwa udhuru katika dhana hii, na iwe hakuna dalili ya kuwajibisha kupaka isipokuwa riwaya zisizo za kawaida, basi hawatokuwa na udhuru waliozielewa riwaya hizi nyingi ambazo ni zaidi ya riwaya thelathini, hata kama hatutosema kuwa kupaka kumenakiliwa kwa tawatur itakuwa hapana budi tuseme kuwa ni nyingi.
Ongeza juu ya hivyo kuwa Kitabu kinaiunga mkono, hivyo basi sisi hatuna njia isipokua tuchukuwe ambacho Kitabu kinaafiki, na kuifanyia tafsiri ili – riwaya - ambayo iendayo kinyume nacho, yaani inayojulisha kuosha kwa namna fulani, kwa kusema: Alikuwa akiosha muda baada ya bi’itha lakini Aya tukufu ilifuta – hukumu hiyo. Au tuichukulie maana nyingine (wala taqfu ma laysa laka bihi ilmun). (Usifuate ambalo hauna elimu nalo).
ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO