Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

TAWASSULI (SEHEMU YA KWANZA)

1 Voti 03.0 / 5

TAWASSULI (SEHEMU YA KWANZA)

UTANGULIZI
Hakika Tawassul uhalisi wake umeelezwa na Qura’ni tukufu pindi Mwenyezi Mungu alipowaambia waumini:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَابْتَغُوا إِلَيْهِ الْوَسِيلَةَ وَجَاهِدُوا فِي سَبِيلِهِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ {35}
“Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu na tafuteni njia ya kum- fikia. Na piganeni kwa ajili ya dini yake ili mpate kufaulu.” Al-Maida: 35.
Hakika Aya hii tukufu imehesabu Uchamungu na Jihadi kuwa ni miongo- ni mwa njia za kisheria ambazo mwanadamu anaweza kuzifanya sababu ya kumfikia Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na je, kuna njia nyingine ambazo zimehimizwa na Sheria? Au jambo hili ameachiwa mwanadamu na kwa uwezo wake agundue njia nyingine za kumkurubisha kwa Mwenyezi Mungu?
Ni wazi kuwa njia ambazo mja anaweza kujikurubisha kwazo kwa Mwenyezi Mungu hazitokani na Juhudi za kielimu, kwani kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na njia za kupatikana ukuruba huo zinahitaji mwongozo wa Mwenyezi Mungu.
Na hapo ndipo Sheria ilipochukua jukumu la kuzibainisha, ikazitolea maelezo na kuziwekea mipaka ndani ya Kitabu na Sunna tukufu. Kila njia isiyokuwa ile iliyoelezwa na Sheria kwa namna ya pekee au ya mjumuisho, basi yenyewe ni aina moja ya bidaa na upotovu.
Imam Ali bin Abu Twalib amegusia njia ambazo kwazo mja atajikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, akasema: “Hakika njia bora ya kupita wenye kwenda kwa Mwenyezi Mungu ni: Kumwamini Yeye na Mtume wake na Jihadi katika njia yake, hakika yenyewe ndio heshima ya Uislamu.
Na Tamko la dhati, hakika lenyewe ndio silika. Na kusimamisha Swala, haki- ka yenyewe ndio dini. Na kutoa Zaka, hakika yenyewe ni faradhi.
Na Funga ya Ramadhani, hakika yenyewe ni ngome dhidi ya adhabu. Na Kuhiji Nyumba tukufu na kufanyia Umra, hakika hivyo viwili vinaondoa ufakiri na kuondoa dhambi. Na kuunga undugu wa damu, hakika kwenyewe ni ongezeko la utajiri katika mali.
Na Sadaka ya wazi, hakika yenyewe inaepusha kifo kibaya. Na kutenda wema, hakika wenyewe unazuia kushindwa kwa udhalili.”1
Qur’an tukufu imeelekeza mwenendo wa kusifika unaohitajika kwa waislamu, Mwenyezi Mungu akasema:
وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّهَ تَوَّابًا رَحِيمًا {64}
“Na lau wangelikujia walipojidhulumu nafsi zao wakaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na Mtume akawaombea msamaha, bila shaka wangemkuta Mwenyezi Mungu Mwenye kupokea toba, Mwenye kure- hemu.” An-Nisai: 64.
Kwa waislamu utaratibu huu uliosifiwa haukomei kipindi cha uhai wa Mtukufu Mtume tu, hilo ni baada ya Mwenyezi Mungu kusema:
وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ عِنْدَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ {169}
“Wala usidhani wale waliouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni wafu, bali wako hai wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi.”Al-Imrani: 169.
Hivyo yenyewe ni Ibada endelevu inayofanywa hata baada ya kifo cha Mtukufu Mtume, na waislamu waliifahamu ruhusa hiyo na wakaitenda baada ya kifo chake kama walivyosema baadhi ya wafasiri.2
Hivyo hakuna kizuizi cha mahusiano na Mwenyezi Mungu na kuomba msamaha kutoka kwake au kuomba kupata haja za kiakhera na kidunia kwa njia ya kupitia njia ya Mtukufu Mtume ili awaombee kwa kuzingatia ukuruba wake kwa Mwenyezi Mungu na nafasi yake maalumu kwake. Njia hii imehimizwa na Sheria na kuainishwa na Qur’ani tukufu. Kwa ufafanuzi zaidi tutafuatilia utafiti katika nukta zifuatazo:
Kwanza: Maana ya Tawassuli kilugha na kiistilahi.
Pili: Rai mbalimbali kuhusu hukumu ya Tawassuli.
Tatu: Ruhusa ya Tawassuli ndani ya Qur’ani.
Nne: Tawassuli ndani ya Hadithi za Mtume.
Tano: Mwenendo wa Waislamu katika Tawassuli. Sita: Tawassuli kwa mujibu wa Ahlul-Baiti.
Saba: Mjadala dhidi ya wanaokanusha ruhusa ya kisheria juu ya Tawassuli
KWANZA: MAANA YA TAWASSULI KILUGHA NA KIISTILAHI
Ndani ya kamusi ya Lisanul-Arabi imeelezwa kuwa: Al-Wasilatu Indal- Malaki: Al-Wasilatu ni: Ngazi na ukuruba. (Husemwa): fulani ametumia Wasila kwa Mwenyezi Mungu: Pindi anapotenda amali itakayomkurubisha Kwake.
Al-wasilu: Mwenye raghba na Mwenyezi Mungu. Labidu amesema: “Nawaona watu hawajui thamani ya jambo lao. Ndio; kila mwenye rai ana raghba ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu.”
Ametawasali Kwake kwa Wasila: Pindi anapojikurubisha Kwake kwa amali fulani.
Na ametawasali Kwake kwa kadha: Amejikurubisha Kwake kwa utukufu wenye huruma utakaomhurumia.
Na Al-Wasilatu ni: Fungamano na ukuruba, na wingi wake ni Al-Wasailu. Mwenyezi Mungu amesema: “Hao wanaowaomba, wao wenyewe wanatafuta njia (Al-Wasilatu) iliyo karibu sana miongoni mwao ya kwenda kwa Mola Wao Mlezi” (17: 57) 3
Na kamusi nyingine za lugha ya kiarabu zimetoa baadhi ya mifano halisi ya neno Al-Wasilatu, kwa sababu maana yake ni miongoni mwa ufahamu wa wazi na uhalisi wake si zaidi ya kukifanya kitu njia ya kufikia jambo jingine ambalo ndilo makusudio na shabaha. Na njia hiyo hutofautiana kulingana na tofauti za makusudio.
Yule anayetafuta radhi za Mwenyezi Mungu njia yake ya kupitia huwa ni matendo mema ambayo kwayo hupata ridhaa zake, na anayetaka kuizuru Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu hutumia kile kitakachomfikisha huko.4
Ibnu Kathir amesema kuhusu Tawassuli kuwa: “Ni mwanadamu afanye kiungo kati yake na Mwenyezi Mungu ili akidhiwe haja yake kwa sababu ya kiungo hicho.”5
PILI: RAI MBALIMBALI KUHUSU HUKMU YA TAWASSULI.
Kabla hatujaingia kwenye dalili za Tawassuli na uhalisi wake kisheria na kisha kuzijadili, hatuna budi kwanza tunukuu muhtasari wa rai mbalimbali ambazo zimepatikana kuhusu kuruhusiwa na kukatazwa kwa Tawassuli.
RAI YA KWANZA: KUKATAZWA TAWASSULI:
Al-Baniyu ndani ya kitabu chake ametoa rai hiyo na kuona kuwa ni upotovu. Na katika utangulizi wa Kitabu Sharhu At-Twahawiyatti6 amesema: “Hakika suala la Tawassuli si miongoni mwa maswala ya kiimani.”
Na miongoni mwa wanaokataza Tawassuli ni Muhammad bin Abdul- Wahabi, anasema: “Iwapo baadhi ya Mushirikina (Yaani Waisilamu wasiyokuwa Mawahabi) wakikwambia: Sikilizeni; “Hakika vipenzi vya Mwenyezi Mungu havina khofu wala havihuzuniki.”7
Au shufaa ni haki au Manabii wana jaha kwa Mwenyezi Mungu au akatoa maneno ya Nabii ambayo kwayo anafanya ni dalili juu ya batili yake, na ikawa wewe hufahamu (Yaani huna uwezo wa kumjibu), basi jibu lake ni kumwambia: Hakika Mwenyezi Mungu ndani ya Kitabu chake ametaja kuwa ambao ndani ya nyoyo zao mna upotovu huacha Aya zilizo waziwazi na hufuata yaliyofichikana.”8
Na miongoni mwa wanaozuia ni Abdul-Aziz bin Bazi, kwani anasema: “Atakayemwomba Nabii na kumwomba shufaa, basi ametengua Uislamu wake.”9
RAI YA PILI: KAULI YA KURUHUSU:
As-Shawkani Az-Zaydiyu ameona hivyo ndani ya kitabu chake (Tuhfatudh-Dhakirina) kwa kusema: “Na anatawasali kwa Mwenyezi Mungu kupitia Manabii wake na watu wema.”10
As-Samuhudiyu Ash-Shafiiyyu ameruhusu kwa kusema: “Kutawasali kupitia Mtume inawezekana kukawa kwa kuomba jambo hilo kutoka kwake, ikimaanisha kuwa (s.a.w.w.) ana uwezo wa kusababisha jambo hilo kwa yeye (s.a.w.w.) kuomba na kukuombea kwa Mola wake Mlezi, hivyo inarudi kwenye kumwomba dua yake; japokuwa ibara zinatofautiana.
Na miongoni mwa Tawassuli ni mtu kumwambia: Nakuomba kuingia pamoja na wewe Peponi Hakuna kinachokusudiwa hapa ila ni Mtume (s.a.w.w.) kuwa sababu na mwombezi”11
Ibnu At-Taymiyya ndani ya kitabu (Mansakul-Marawiziyu) amenukuu kutoka kwa Ahmad bin Hanbali kuwa Mtume (s.a.w.w.) ana Tawassuli na Dua. Pia amenukuu hilo kutoka kwa Ibnu Abid-Duniya na Al-Bayhaqi na At-Tabarani kwa njia mbalimbali akithibitisha usahihi wake.12
Na miongoni mwa wanaosema kuwa inaruhusiwa ni Imam Shafi, amesema: “Mimi hutafuta baraka kupitia Abu Hanifa na huja kwenye kaburi lake kila siku, na ninapopatwa na haja huswali rakaa mbili kisha huja kwenye kaburi lake na kumwomba Mwenyezi Mungu haja kwake na huwa haichelewi kukidhiwa.”13
Na miongoni mwa wanaosema kuwa inaruhusiwa ni Abu Ali Al-Khalali Sheikh wa kihambali kwani anasema:
“Sikuhuzunishwa na jambo lolote kisha nikaja kwenye kaburi la Musa bin Jafar na kutawasali kupitia kwake ila Mwenyezi Mungu alinirahisishia lile nilipendalo.”14
Ama Shia Imamiya wao wamesema: “Katika kukidhiwa haja na kuondolewa matatizo inaruhusiwa kutawasali kupitia Nabii na Maimamu baada ya kifo chao, kama inavyoruhusiwa katika hali ya uhai wao, kwakuwa kufanya hivyo; kwanza si kumsemeza asiyekuwepo, na pili si shirki.”15
RAI YA TATU: KUTENGANISHA KATI YA AINA ZA TAWASSULI:
Rai hii ni ya Ibnu At-Taymiyya, lakini tunamkuta katika suala la Tawassuli anatapatapa kirai, mara anakanusha na mara nyingine anaruhusu, na tatu anatenganisha. Na alipoonyesha vigawanyo vyake vya sura za Tawassuli, aliruhusu viwili na kuharamisha cha tatu, amesema: “Neno Tawassuli, linakusudiwa maana tatu: Mojawapo ni: Kutawasali kwa kumtii Mtume na kumwamini, na hili ndio asili ya Imani na Uislamu, na atakayelikanusha basi ukafiri wake ni dhahiri kwa watu maalumu na wa kawaida.
Pili: Kutawasali kwa dua yake na shufaa yake - Yaani Mtume hapa ndiye anayeomba na kumwombea moja kwa moja - hili lilifanyika zama za uhai wake na litafanyika siku ya Kiyama, watatawasali kupitia shufaa yake. Na atakayekanusha hili basi yeye ni kafiri murtadi anayetakiwa kutubu, basi akitubu sawa na kama sivyo huuwawa akiwa murtadi.
Tatu: Kutawasali kupitia shufaa yake baada ya kifo chake na kuapa kwa Mwenyezi Mungu kupitia dhati yake, hili ni miongoni mwa Bidaa iliyozushwa.”16
•    1. Nahjul-Balagha, uhakiki wa Subhiyu Asw-Saleh: Hotuba ya 110/ 163.
•    2. Tafsiri Ibnu Kathir 1:532.
•    3. Lisanul-Arabi cha Ibnu Mandhuri, Juzuu ya 11, kitomeo: Wasala.
•    4. At-Tawassul fi Ash-Shariati Al-Islamiya, Jafar Subhani: 17.
•    5. Tafsir ya Ibnu Kathir 1: 532.
•    6. Al-Bisharatu Wal-Ittihafi cha As-Saqafi: 52. Amenukuu toka kwenye Sharhu At-Twahawiya: 60.
•    7. Yunus: 62.
•    8. Kashfu -Shubuhati cha Muhammad bin Abdul-Wahabi: 60.12 Mukhalafatul-Wahabiyati Lil-Qur’ani Was-Sunnati cha Umar Abdus-Salami:
•    9. Amenukuu toka kwenye Al-Aqidatus-Swahihatu Wanawakidhul-Islami cha Abdul-Aziz bin Abdullah bin Bazi.
•    10. Tuhfatudh-Dhakirina cha Ash-Shawkani: 37.
•    11. Wafaul-Wafa Biakhbari Daril-Mustwafa cha As-Samuhudiyu 2: 1374.
•    12. At-Tawassulu Wal-Wasilatu cha Ibnu At-Taymiyya: 144-145, chapa ya Darul- Afaki mwaka 1399 A.H. Na itakujia rai yake yeye mwenyewe.
•    13. Tarikhu Baghdadi 1: 123, mlango wa yaliyoelezwa kuhusu makaburi ya Baghdadi.
•    14. Tarikhu Baghdadi 1: 120, mlango wa yaliyoelezwa kuhusu makaburi ya Baghdadi.
•    15. Al-Barahinu Al-Jaliyatu fi Daf ’i Tashikikatil-Wahabiyya, cha As-Sayyidu Muhammad Hasani Al-Kazawiniyu Al-Hairiyu: 30.
•    16. Tazama: At-Tawassulu Wal-Wasila: 13, 20, 50.

ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini