ADHANA: SHERIA NA VIPENGELE VYAKE KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA (SEHEMU YA KWANZA)
ADHANA: SHERIA NA VIPENGELE VYAKE KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA (SEHEMU YA KWANZA)
Kila sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu mlezi wa ulimwengu.
Rehma na Amani zimfikie mbora wa viumbe na hitimisho la mitume wake, pia kizazi chake kitakatifu ambacho ndicho kasha la elimu yake na hazina ya mafunzo yake. Hakika Uislamu ni imani na sheria. Imani ni kuamini Mwenyezi Mungu, mitume wake na siku ya mwisho.
Na sheria ni hukumu za Mwenyezi Mungu ambazo zinajukumu la kumpa mwanadamu maisha bora na kumhakikishia wema wa dunia na Akhera.
Sheria ya Kiislamu ni ya kipekee kwa kuwa inahusika na kila jambo huku ikiweka utatuzi wa matatizo yote yanayompata mwanadamu katika sekta zote za maisha yake, hivyo Mwenyezi Mungu akasema:
الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا
“Leo nimewakamilishieni dini yenu na kuwatimizieni neema yangu na nimewapendeleeni Uisilamu uwe dini yenu.. ( 5:3 ).
Isipokuwa kuna masuala madogo madogo ambayo wanazuoni wa sheria wameikhtilafiana kwa sababu ya kutofautiana kwao kuhusu riwaya ambazo zimenasibishwa kwa Mtume. Jambo ambalo limepelekea kutofautiana kuhusu masuala madodo madogo ya sheria.
Kwa kuwa ukweli hutokana na utafiti, basi hakika katika mtiririko wa masomo haya tumejaribu kuliweka sala hili juu ya meza ya utafiti, kwani huenda ikawa ndio njia ya kuunganisha mtazamo na kusogeza hatua katika uwanja huu. Kwani tofauti iliyopo si katika asili na misingi ya dini hata ipelekee kuwa na uadui na chuki, bali tofauti iliyopo ni kuhusu riwaya zilizonasibishwa na Mtume, nalo ni jambo dogo ukilinganisha na mambo mengi ambayo tunaafikiana kati ya madhehebu za kiisilamu. Na muongozo wetu katika njia hii ni kauli ya Mwenyezi Mungu:
وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ۚ وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنْتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُمْ بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا
Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msifarakiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, mlipokuwa maadui na akaziunganisha nyoyo zenu, hivyo kwa neema zake mkawa ndugu.” (3:103).
Imam Ja’far Sadiq (a.s.) aliambiwa: ”Wanadai kuwa kuna mtu kati yaAnswari aliona adhana usingizini.” Imam akajibu: Wamesema uongo, hakika dini ya Mwenyezi Mungu ni takatifu zaidi ya
kuonekana usingizini.”
Muhammad Al-Hanafiya amesema: ”Mmelizushia uongo jambo ambalo lina asili ndani ya sheria ya Uislamu na mafunzo ya dini yenu, hivyo mkadai eti lilitokana na ndoto aliyoiona mtu kati ya Answari usingizini mwake. Ndoto ambayo huenda ikawa ni uongo au kweli, na huenda ikawa si chochote.”
ADHANA KILUGHA NA KISHERIA
Na nafasi ya muadhuni mbele ya Allah
Adhana kilugha: Ni tangazo. Mwenyezi Mungu amesema:
وَأَذَانٌ مِنَ اللَّهِ وَرَسُولِهِ إِلَى النَّاسِ يَوْمَ الْحَجِّ الْأَكْبَرِ
“Na ni tangazo litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa watu siku ya Hijja kubwa.”(9:3).
Maana yake ni tangazo kwa watu kutoka kwa wao wawili.
Kisheria: Ni tangazo la kuingia wakati wa Sala ya faradhi kwa kutumia maneno maalumu yaliyopokewa kwa sifa mahususi. Nayo ni kati ya amali bora ambazo humkurubisha mtu kwa Mwenyezi Mungu, na ni yenye fadhila nyingi na ujira mkubwa.
Amepokea Sheikh Tusi katika (Tahdhib) kutoka kwa Muawiya bin Wahabi, toka kwa Abu Abdillah (a.s.) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: “Atakayeadhini muda wa mwaka mmoja ndani ya mji kati ya miji ya Waisilamu basi atawajibika kupata pepo.”1
Pia amepokea toka kwa Saadil-askafu kuwa: “Nimemsikia Aba Abdillah akisema: Atakayeadhini muda wa miaka saba kwa ajili ya kupata radhi za Allah basi atakuja siku ya Kiyama akiwa hana dhambi yoyote.”2
Amepokea Swaduq toka kwa Al-Urzumiy toka kwa Aba Abdillah kuwa: “Watakaokuwa na shingo ndefu sana siku ya Kiyama zaidi ya watu wote niwaadhini.”3
Ameandika Ahmadi Muhammad Al-Barqiy katika kitabu Al-Mahasini toka kwa Jafar Al-Jaafy toka kwa Muhammad bin Ali Al-Baaqir kuwa: “Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Muadhini mwenye kutaka radhi za Allah ni sawa na mpiganaji katika njia ya Allah, mwenye kupigana kati ya makundi mawili.”4
Na nyingine nyingi riwaya kama hizi zenye kuhimiza kutoa adhana huku zikiwataka watu wa tabaka zote kuitangaza, na kukerwa na kitendo cha madhaifu kuificha adhana kwa udhaifu wao.
Tumeleta uchambuzi huu kwa ajili ya kubainisha mambo mawili:
Kwanza: Hakika sheria ya adhana ni sheria ya Mwenyezi Mungu haina uingiliano wowote na mwanadamu.
Pili: Kusoma historia ya tamko la الصلاةخيرمن النوم Sala ni bora kuliko usingizi (Tathwib) katika Sala ya asubuhi. Huku tukithibitisha kuwa tamko hili si sehemu ya adhana bali liliongezwa kwa kuungwa mkono na baadhi ya watu.
Hivyo mazungumzo yatahusu sehemu mbili.
REJEA:
• 1. At-Tahdhibu: 2 /283 ?1126
• 2. At-Tahdhibu: 2 /283 ?1128
• 3. Thawabul-Amali: 52
• 4. Al-Mahasin: 48 Namba: 68
ITAENDELEA KATIKA MAKALA IAJAYO