ADHANA: SHERIA NA VIPENGELE VYAKE KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA (SEHEMU YA TATU)
ADHANA: SHERIA NA VIPENGELE VYAKE KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA (SEHEMU YA TATU)
UCHAMBUZI WA MADHUMUNI YA RIWAYA
Riwaya hizi hazifai kuwa dalili kwa sababu mbalimbali:
Kwanza: Zinapingana na hadhi ya unabii Hakika Allah alimtuma Mtume ili yeye na waumini wasimamishe Sala ndani ya nyakati tofauti, hivyo asili ya suala hili inalazimu Mwenyezi Mungu amfunze Mtume jinsi ya kutimiza matakwa haya. Hivyo hamna maana yoyote Mtume kubakia hajui chochote kipindi chote hiki muda wa siku ishirini kama alivyopokea Abu Daudi katika riwaya ya mwanzo, eti abakie huku hajui ni jinsi gani atatimiza jukumu alilopewa huku akihangaika mara atumie njia hii mara njia ile mpaka akapata njia na sababu zitakazompa matumaini ya kufikia kusudio lake ilihali Mwenyezi Mungu anasema kuhusu Mtume kuwa:
وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكَ وَرَحْمَتُهُ
Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyeezi Mungu juu yako na rehema. (4:113)..
Na makusudio ya fadhila hapa ni elimu, hiyo ni kutokana na mazungumzo ya sentensi ya kabla yake: Na amekufundisha yale uliyokuwa huyajui..
Hakika Sala na Swaumu ni kati ya mambo ya kiibada na wala si kama vita na mapigano ambayo huenda Mtume akashauriana na maswahaba wake. Na wala kushauriana kwake na maswahaba katika vita na mapigano si kwa kuwa alikuwa hajui ni lipi linalofaa, bali alishauriana nao kwa ajili ya kuta ka kuvuta nyoyo zao kama anavyosema Mwenyezi Mungu:
فَبِمَا رَحْمَةٍ مِنَ اللَّهِ لِنْتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنْتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانْفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ ۖ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ ۖ فَإِذَا عَزَمْتَ فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُتَوَكِّلِينَ
Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyeezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, Mwenye moyo mgumu, bila shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriane nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyeezi Mungu.. ( 3: 159)
Hivi huoni kuwa ni kuidharau dini kwa ndoto za watu wa kawaida kuwa chanzo cha amri ya kiibada iliyo muhimu sana kama vile adhana na iqama. Jambo hili linatupelekea kusema kuwa: Ndoto kuwa chanzo cha adhana ni uongo mtupu dhidi ya sheria na ni rahisi sana kusema kuwa ami zake Abdallah bin Zaid ndiyo waliyoeneza ndoto hiyo na kuipamba ili familia zao na makabila yao yapate ubora, hivyo ndiyo maana tunaona katika baadhi ya sanadi kuwa watoto wa ami zake ndio wapokezi wa hadithi hii, na yule aliyewategemea katika kunukuu basi alifanya hivyo kwa kuwadhania vizuri.
Pili: riwaya hizi kiundani zinapingana. Hakika riwaya zilizopita zinazohusu mwanzo wa adhana na jinsi sheria ya adhana ilivyoletwa kiundani zinapingana kwa sababu zifuatazo:
1. Kulingana na riwaya ya kwanza ya Abi Daud ni kuwa Umar aliiona adhana kabla ya Abdallah siku ishirini zilizopita. Lakini kwa mujibu wa riwaya ya nne ya Ibnu Majah ni kuwa aliiona usiku huo huo aliyoiona Abdallah bin Zaid.
2. Ndoto ya Abdallah ndio chanzo cha sheria ya adhana na Umar aliposikia adhana akaja kwa Mtume na kudai kuwa hata yeye aliota ndoto mfano wa hiyo hata hivyo hakuinukuu kwa Mtume kwa kuona aibu.
3. Hakika chanzo cha sheria ya adhana ni yeye mwenyewe Umar wala si ndoto yake kwa sababu yeye ndiye aliyetoa wazo la kupatikana wito kwa ajili ya Sala, wito ambao kwa ibara nyingine ndio adhana. Tirmidhi kapokea ndani ya kitabu chake (Sunan) kuwa: Waislamu walipofika Madina ...mpaka akasema: Baadhi yao wakasema: Tengenezeni tarumbeta kama tarumbeta la mayahudi. Akasema: Hapo Umar akasema: Hamumteui mtu anadi kwa ajili ya Sala? Amesema: Hapo Mtume akasema: Ewe Bilal simama na unadi kwa ajili ya Sala, yaani adhana 1 Pia hadithi hii kaipokea An-Nasaiy2 na Al-Bayhaqiy 3 ndani ya Sunan zao (vitabu vyao). Ibnu Hajari kafasiri kuwa makusudio ya wito kwa ajili ya Sala ni tamko (Salati jamia ) Wala hakuna dalili yoyote juu ya tafsiri hiyo.
4. Hakika chanzo cha sheria ya adhana ni Mtume mwenyewe. Amepokea Bayhaqiy. Wakasema wapige kengele au wawashe moto, hapo akaamrishwa Bilal aadhini mara mbili mbili na aqimu mara moja moja. Akasema: Ameipokea Bukhari toka kwa Muhammad toka kwa Abdul- Wahabi At-Thaqafy. Na ameipokea Muslim toka kwa Ishaqa bin Ibrahim 4
Je? Itakuwaje tutegemee nukuu hizi zenye kupingana kwa kiasi hiki.
5. Hakika kwa mujibu wa riwaya, kwanza ni kuwa Omar alikuwepo kwa Mtume pindi Abdallah akisimulia ndoto lakini kwa mujibu wa riwaya ya pili hakuwepo kiasi kwamba alitoka nyumbani kwake pindi aliposikia adhana ya Bilal baada ya kuwa Abdallah tayari amekwisha simulia ndoto yake.
Tatu: waotaji wa ndoto hiyo walikuwa ni watu kumi na nne, si mtu mmoja.
Kwa mujibu wa yale aliyopokea Al-Halabiy inaonekana kuwa aliyeota ndoto ya adhana si Ibnu Zaid na Ibnu Al-Khatabi peke yao bali amedai kuwa hata Abubakari aliota kwani aliona mfano wa yale waliyoyaona hao wawili. Na inasemekana kuwa na wengine saba kati ya Answari. Na inasemekana ni watu kumi na nne5 wote walidai kuwa waliiona adhana ndotoni. Sheria si matakwa ya kila mtu, hivyo ikiwa sheria na hukumu zinafuata ndoto ya kila mtu basi Uislamu umekwisha.
NNE: mgongano kati ya riwaya za Bukhari na nyinginezo
Hakika tamko la wazi la Sahihi Bukhari ni kuwa Mtume alimuamrisha Bilal atoe wito kwa ajili ya Sala wakiwa katika kikao cha ushauri. Umar alikuwepo wakati amri hiyo inatoka. Amepokea kutoka kwa mtoto wa Umar kuwa: Walipofika Madina Waislamu walikuwa wakikusanyika na wakiitana kwa ajili ya sala bila ya kuwepo wito mahususi kwa ajili ya Sala.
Hivyo siku moja wakajadiliana kuhusu suala hilo. Baadhi yao wakasema: Fanyeni kengele kama kengele ya wakristo, wengine wakasema: Fanyeni tarumbeta kama za mayahudi, hapo Umar akasema: Hivi hamumteui mtu anadi kwa ajili ya Sala? Hapo Mtume akasema: Ewe Bilal simama, hapo akanadi kwa ajili ya sala6.
Uwazi wa hadithi ya ndoto ni kuwa Mtume alimuamuru Bilal kunadi baada ya kuwa amesimuliwa ndoto na Ibnu Zaid wala Umar hakuwepo bali alisikia adhana akiwa nyumbani kwake akatoka huku akiburuza nguo yake akisema: Naapa kwa yule aliyekutuma kwa haki ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika niliona mfano wa aliyoyaona.7.
Hatuwezi kufasiri neno wito lililopokewa na Bukhari kuwa ni tamko: (salat jamia ) na neno wito lilomo ndani ya hadithi za ndoto kuwa ni adhana, kwa sababu kufanya hivyo kwanza ni kuoanisha bila dalili. Pili laiti kama Mtume angemuamrisha Bilal ainue sauti kwa kutamka: (Salat jamia) basi tatizo lingekwisha na utata ungeondoka hasa hasa kama sentesi salat jamia ingekaririwa mara kwa mara na wala isingebakia tena sehemu ya utata. Na hii ni dalili kuwa kunadi huku alikoamrisha Mtume kulikuwa ni kwa kutumia adhana hii ya kisheria. (Adhana ya kawaida )8
MJADALA JUU YA NJIA ZA UPOKEZI (SANADI)
Sababu tano zote tulizozitaja zinahusu madhumuni ya hadithi huku zikitosha kabisa kuvunja utegemezi juu ya hadithi hizo. Na sasa ni uchambuzi wa njia za upokezi moja baada ya nyingine. Njia ambazo baadhi ya mtiririko wake haujafika kwa Mtume (s.a.w.w.) na nyingine zina watu wasiojulikana au wasio waaminifu au madhaifu wasiyokubalika, Ufuatao ni uchambuzi kwa kufuata utaratibu uliopita:
RIWAYA YA KWANZA
Ambayo kaipokea Abu Daudi nayo ni riwaya dhaifu: Kwa sababu mwisho imekomea kwa mtu au watu wasiojulikana pale anaposema: toka kwa ami zake wa kianswari. Abu Umayri bin Anas naye kapokea toka kwa ami zake. Ibnu Hajari katoa wasifu wake kwa kusema: Amepokea riwaya kuhusu kuuona mwezi mwandamo na adhana toka kwa ami zake wa kianswari miongoni mwa swahaba wa Mtume. Na Ibnu Saadi kasema: Alikuwa mkweli mchache wa hadithi. Ibnu Abdul-Bari amesema: Hajulikani, huyu si hoja9.
Jamalud-dini amesema: Haya aliyosimulia katika hizi maudhui mbili: Kuona mwezi mwandamo adhana ndiyo yote aliyonayo kwao10.
RIWAYA YA PILI
Katika sanadi ya riwaya hii kuna watu wasiosihi kuwa hoja, mfano wa:
1. Muhammad Ibrahim Al-Harithi bin Khalidi At-Taymiy Abu Abdallah aliyefariki mwishoni mwa miaka ya 120. Amesema Abu Jafar Al-Aqiliy toka kwa Abdallah bin Ahmadi bin Hambali: Nilimsikia baba yangu akimtaja Muhammad bin Ibrahim At-Taymiy Al-Madaniy nakusema: Katika simulizi zake kuna shaka kwani hupokea hadithi zisizokubalika au isiyokubalika11
2. Muhammad bin Ishaqa bin Yasari bin Khiyari. Hakika riwaya zake huwa si hoja kwa masunni. Japokuwa yeye ndiyo msingi wa Sira ya Ibnu Hisham.-Iliyochapishwa . Amesema Ahmadi bin Abi Khaythamat. Na Yahya bin Muini aliulizwa kuhusu yeye (Ibnu Is.haqa) akajibu: Yule si chochote ni dhaifu. Akasema: Na nikamsikia Yahya bin Muini mara nyingine akisema: Kwangu mimi Muhammad bin Ishaqa ni dhaifu mwenye dosari. Amesema Abul-Hasani Al-Maymuni: Nilimsikia Yahya bin Muini akisema: Muhammad bin Is.haqa ni dhaifu. Al-Nasai naye kasema: Sio tegemeo12
3. Abdallah bin Zaidi: Mpokezi wa hadithi moja tu. Inakutosha ufahamu kuhusiana na yeye kuwa ni mchache sana wa hadithi. Amesema Tirmidhiy: Hatufahamu chochote kilicho sahihi alichokipokea toka kwa Mtume isipokuwa hadithi moja tu kuhusu adhana. Al-Hakim amesema: Ni sahihi na yeye aliuwawa katika vita vya Uhud na riwaya zote zilizopokewa toka kwake ni pungufu..
Ibnu Adii amesema: Hakuna tunachikifahamu kuhusu yeye kinachosihi kutoka kwa Mtume isipokuwa hadithi hii ya adhana.13
Tirmidhiy kapokea toka kwa Bukhari kuwa hatuna chochote tunachokijua toka kwake isipokuwa hadithi ya adhana14. Al-Hakim amesema: Abdallah bin Zaidi ni yule aliyeoteshwa adhana ambayo wanazuoni wa Kiisilamu wameikubali na wala haijatoka ndani ya sahihi mbili kwa sababu ya kutofautiana wapokezi katika njia za upokezi wake.15
RIWAYA YA TATU
Mtiririko wa sanadi yake umemjumuisha Muhammad bin Is.haqa bin Yasari na Muhammad bin Ibrahim At-Taymiy. Tayari umeshaujua wasifu wao kama ulivyojua kuwa Abdallah bin Zaidi alikuwa mchache zaidi wa
RIWAYA YA NNE
Katika mtiririko wa sanadi yumo Abdur-Rahmani bin Is.haqa bin Abdallah Al-Madaniy. Amesema Yahya bin Said Al-Qataniy: Niliuliza watu wa Madina kuhusu yeye. Sikumuona yeyote akimsifia. Na hivyo ndivyo alivyosema Ali Al-Madayniy. Pia Ali amesema: Sufiyani aliulizwa kuhusu Abdur-Rahmani nikamsikia akijibu: Alikuwa ni qadiriya, hivyo watu wa Madina wakamkanusha akaja hapa wakati wa kifo cha Al-Walidi wala hatukukaa naye.
Abu Twalibu Amesema: Nilimuuliza Ahmadi bin Hambali kuhusu yeye. Akajibu: Alipokea hadithi zisizokubalika kwa Abi Al-Zanadi. Amesema Ahmadi bin Abdallah Al-Ajaly: Hadithi zake huandikwa lakini si tegemeo.
Abu Hatimu amesema: Hadithi zake huandikwa lakini si hoja. Bukhari amesema: Si mtu anayetegemewa kwa yale aliyohifadhi..Hana mwanafunzi anayejulikana Madina isipokuwa Musa Az-Zamiiyu, Amepokea vitu kutoka kwake, vitu ambavyo vingi kati ya hivyo ni utata mtupu..
Ad-Daruqutniy amesema: Ni dhaifu wa kutupiliwa mbali. Amesema Ahmadi Adii: Katika baadhi ya hadithi zake kuna mambo yasiyokubalika wala hayafuatwi16.
2- Muhammad bin Khalidi bin Abdallah Al-Wasitwiy (150- 240 A.H. ) Jamalul-Dini Al-Maziy ametaja wasifu kwa kusema: Amesema Ibnu Muiniy: Huyu si chochote, na amekanusha riwaya zake alizipokea toka kwa baba yake. Abu Hatimu amesema: Nilimuuliza Yahya bin Muiniy kuhusu yeye akajibu: Huyo ni mtu mbaya, muongo sana. Kisha akatoa mambo yasiyokubalika. Abu Uthman Saidi bin Amru Al-Baradaiy amesema: Nilimuuliza (Yaani Aba Zariat) kuhusu Muhammad bin Khalid akajibu: Ni mtu mbaya. Ibnu Habani kataja wasifu wake ndani ya kitabu chake kiitwacho Thuqati akasema: Hukosea na huenda kinyume17. Na As- Shaukaniy baada ya kunukuu riwaya akasema: Ni dhaifu sana katika upokezi wake18
RIWAYA YA TANO
Kaitika mtiririko wa njia hii yumo:
1. Muhammad bin Is.haqa bin Yasari
2. Muhammad bin Al-Harithi At-Taymiy
3. Abdallah bin Zaid. Tayari umeshajua dosari za wawili wa mwanzo na jinsi zisivyo timilifu kila riwaya anazipokea wa tatu. Kwa ajili hiyo inadhihirika wazi hali ya sanadi ya riwaya ya sita.
Haya ndiyo yaliyopokewa ndani ya Sunan. Ama yaliyomo ndani ya vitabu vingine tutayataja baadhi kama yalivyopokewa na Imam Ahmadi na Al- Daramiy na Ad-Dariqatwaniy katika vitabu vyao vya hadithi.
Pia Imam Maliki katika kitabu chake Al-Muwatwau. Na Ibnu Saadi katika Twabaqati yake. Na Bayhaqiy katika Sunan. Na ufuatao ni uchambuzi.
RIWAYA ZA ADHANA KATIKA VITABU VINGINE MBALI NA SAHIH SITA
Kutokana na maelezo ya Al-Hakim umefahamu kuwa mashekhe wawili (Bukhari na Muslim) hawakuitoa hadithi ya Abdallah bin Zaid kwa sababu ya kutofautiana wapokezi katika njia zao hao wawili. Isipokuwa mtu aliyeitoa hadithi hiyo kati ya waandishi wa vitabu sita ni Abu Daud, Tirmidhiy, na Ibnu Majah. Na tayari umeshajua jinsi madhumuni ya riwaya hizo yanavyopingana, huku sanad (njia zake) zikiwa dhaifu. Hivyo twende pamoja ili tusome yale yaliyoandikwa na waandishi wa hadithi na wengine kati ya watu ambao vitabu vyao huhesabika ni makini na sahihi baada ya vitabu sita.
A: ALIYOPOKEA IMAM AHMADI NDANI YA MUSNADI YAKE:
Imam Ahmad amepokea ndoto ya adhana ndani ya Musnad yake toka kwa Ibnu Zaid kwa njia tatu:19
1-Katika njia ya kwanza yumo Zaidi bin Al-Hababi bin Al-Rayani At- Tamimiy (Aliyefariki mwaka 203 A.H. ). Yeye kasifika sana kwa kukosea na amepokea toka kwa Sufian At-Thauriy hadithi zenye kushangaza jinsi anavyozipokea.
Ibnu Muini amesema: Riwaya zake toka kwa Al-Thauriy zimegeuzwa20.
Pia imemjumuisha Abdallah bin Muhammad bin Abdallah bin Zaid bin Abdurabah ambaye ndani ya sahihi sita na vitabu vya hadithi hana riwaya isipokuwa moja tu, nayo ndiyo hii ambayo ndani yake mna ubora kwa familia yake, na kwa ajili hiyo hatuitegemei sana riwaya hii.
Njia ya pili yumo Muhammad bin Is’haqa bin Yasari ambaye tayari umeshamfahamu. Njia ya tatu yumo Muhammad bin Ibrahimu Al-Harithi At-Taymiy, ukiongeza na Muhammad Ishaqa na mwisho inakomea kwa Abdallah bin Zaid na yeye ndiye yule mchache sana wa hadithi.
Katika riwaya ya pili ni kuwa baada ya kutaja kisa cha ndoto na Bilal kujifunza adhana amesema: Hakika Bilal alikuja kwa Mtume akamkuta kalala hapo. Bilal akanadi kwa sauti ya juu: .Sala ni bora kuliko usingizi,. basi ndipo tamko hili likaingizwa katika adhana ya asubuhi.. Yaliyopo mwishoni mwa hadithi hii yanatosha kuthibitisha kuwa ni hadithi dhaifu.
B: ALIYOPOKEA AD-DARAMIY KATIKA MUSNADI YAKE
Ad-Daramiy kapokea kwa njia nyingi ndani ya kitabu chake kisa cha ndoto na njia zote ni dhaifu. Na hapa tunakuonyesha baadhi ya njia hizo: Alitupa habari Muhammad Hamid kuwa: Alitusimulia Salamat kuwa: Alinisimulia Muhammad Is’haqa kuwa: Mtume alipofika Madina alikuwa.
Njia hiyo hiyo baada ya Muhammad Ishaqa imekuja: Amenisimulia hadithi hii Muhammad bin Ibrahim Al-Harithi At-Taymiy toka kwa Muhammad bin Abdallah bin Zaidi bin Abdurabah toka kwa baba yake, akataja hadithi hii.
Ametupa habari Muhammad bin Yahya kuwa ametusimulia Yaaqubu Ibrahim bin Saadi kuwa ametusimulia baba yangu toka kwa Is’haqa . Maelezo yaliyobaki ni kama yale ya njia ya pili21 .
Njia ya kwanza si kamilifu. Njia ya pili yumo Muhammad bin Ibrahim Al-Harithi At-Taymiy ambaye tayari umeshaujua wasifu wake. Njia ya tatu yumo Ibnu Is’haqa naye tayari umeshaujua wasifu wake.
C: ALIYOPOKEA IMAM MALIK KATIKA KITABU CHAKE AL-MUWATWAU
Imam Maliki kapokea kisa cha ndoto ya adhana ndani ya Muwatwau toka kwa Yahya toka kwa Maliki toka kwa Yahya bin Saidi kuwa alisema: Mtume alitaka kutengeneza kengele ya mbao ili iwe inagongwa22.
Njia yake ni pungufu na makusudio ya Yahya hapa ni Yahya bin Saidi bin Qaysi aliyezaliwa kabla ya mwaka 70 akafariki eneo la Hashimiyat mwaka 143.23
D: ALIYOPOKEA IBNU SAADI KATIKA TWABAQATI YAKE.
Ibnu Saadi kapokea ndani ya kitabu chake kwa njia pungufu24 zisizokuwa hoja.
Kwanza: Inakomea kwa Nafi.u Jubayrii ambaye alifariki ndani ya kumi la tisini na inasemekana mwaka 99 A.H.
Pili: Inakomea kwa Urwatu bin Al-Zubairiy ambaye alizaliwa mwaka 29 na kufariki mwaka 93 A.H.
Tatu: Inakomea kwa Zaidi bin Aslamu ambaye alifariki mwaka 136 A.H.
Nne: Inakomea kwa Saidi bin Al-Musayyab ambaye alifariki mwaka 94 A.H. na pia inakomea kwa Abdurahmani bin Abi Layli ambaye alifariki mwaka 82 A.H. au 83. A.H.
Katika kutoa wasifu wa Abdallah bin Zaidi amesema Ad-Dhahabi kuwa: Wamesimulia toka kwake Saidi bin Al-Musayibu na Abdu-Rahman bin Abi Layli ili hali hawakukutana nae25.
Pia amepokea kwa njia ifuatayo: Ametujulisha Ahmadi bin Muhammadi bin Al-Wahidi Al-Azraqiy kuwa: Ametusimulia Abdurahmani bin Umar toka kwa Abdallah bin Umar kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alitaka Uchambuzi wake utakuijia sehemu ya pili. kuweka kitu kitakachomsaidia kuwakusanya watu mpaka mtu katika Answari alipooteshwa, Mtu huyo anaitwa Abdallah bin Zaid. Ndani ya usiku huo huo Umar naye akaoteshwa. Akaendelea mpaka akasema: Bilal akaongeza katika Sala ya asubuhi (Sala ni bora kuliko usingizi); Mtume akaipitisha.
Njia hii imemjumuisha :
1. Muslimu bin Khalidi bin Qarqurat, pia huitwa Ibnu Jarhat ambaye kadhoofishwa na Yahya bin Muini.
Amesema Ali Al-Madayniy kuwa: Huyo si chochote. Bukhari amesema: .Hadithi yake haikubaliki.. An-Nasai amesema: .Ni dhaifu.. Abi Hatimu amesema:26. .Huyo ni dhaifu hadithi yake haikubaliki, hadithi yake huandikwa lakini si hoja, hadithi zake hujulikana na hukanushwa..
2. Muhammad bin Muslim bin Ubaydullah bin Abdallah bin Shahabu Az- Zahariy (51 . 123 A.H.) Anas bin Iyadhi amenukuu toka kwa Abdallah bin Umar kuwa: nilikuwa nikimuona Az-Zahariy akitoa kitabu lakini hakuna anayekisoma wala anayesoma kwake, mwisho huambiwa tupokee haya toka kwako? Naye hujibu ndiyo.
Amesema Ibrahim Abu Sufiyani Al-Qaysaraniy toka kwa Al-Faryabiy kuwa: Nilimsikia Sufyani At-Thauriy akisema: .Nilimuendea Az-Zahriy yakanizidia mambo. Nikamwambia: Ni vizuri kama ungewaendea mashekhe zetu wakutengenezee mfano wa hili. Akajibu: Kama wewe? Akaingia ndani na kuniletea kitabu na kusema: Chukua hiki na upokee toka kwangu; lakini sikupokea hata herufi moja toka kwake.27
E- ALIYOPOKEA AL-BAYHAQIY KATIKA KITABU CHAKE
Bayhaqiy kapokea kisa cha adhana kwa njia ambazo zote hazikosi dosari moja au nyingi, na yafuatayo ni ishara tu ya wale dhaifu waliyopatikana ndani ya njia zake:
Kwanza: Imemjumuisha Abu Umayri bin Anas toka kwa ami zake wa kianswari. Tayari umeshamjua Abu Umayr bin Anas, yeye kazungumziwa na Ibnu Abdul-Bari kuwa: Hakika yeye hajulikani na wala si hoja28, hupokea kwa jina la ami zake toka kwa watu wasiojulikana29. Wala hakuna dalili yoyote inayothibitisha kuwa hawa walikuwa ni swahaba. Hata tukikadiria kuwa maswahaba wote ni waadilifu na tukasema kuwa ami zake walikuwa ni maswahaba lakini bado hadithi zikomeazo kwa swahaba si hoja kwani hatuna yakini kama kweli kapokea toka kwa nabii.
Pili: Imejumuisha watu ambao huwa si hoja: Muhammad bin Ishaqa bin Yasari Muhammad bin Ibrahim Al-Harithi At-Taymiy 3-Abdallah bin Zaid. Na hawa wote tayari umeshajua wasifu wao.
Tatu: Imemjumuisha Ibnu Shihabi Az-Zahariy ambaye anapokea toka kwa Saidi bin Al-Musayyab aliyefariki mwaka 94 A.H. toka kwa Abdallah bin Zaidi30 . Tayari umeshajua kuwa wote wawili hawakuwepo zama za uhai wa Abdallah bin Zaidi
F: ALIYOPOKEA AD-DARQUTNIY KATIKA KITABU CHAKE
Ad-Darqutniy kapokea kisa cha ndoto ya adhana kwa njia nyingi na ufuatao ni uchambuzi wake: Katusimulia Muhammad bin Yahya bin Murdasi kuwa: Katusimulia Abu Daudi kuwa: Katusimulia Uthuman bin Abi Shaybat kuwa: Katusimulia Hamadi bin Khalid kuwa: Katusimulia Muhammad bin Amru toka kwa Muhammad bin Abdallah toka kwa ami yake Abdallah bin Zaidi.
Katusimulia Muhammad bin Yahya Katusimulia Abi Daudi kuwa: Katusimulia Ubaydullah bin Omar kuwa: Katusimulia Abdul-Rahmani bin Mahdi kuwa: Katusimulia Muhammad bin Amru amesema: Nilimsikia Abdallah bin Muhammad akisema: Babu yangu Abdallah bin Zaidi alikuwa akisimulia habari hii31.
Njia zote mbili zimemjumuisha Muhammad bin Amru huku yeye hajulikani ni yupi kati ya answari, ambaye ndani ya sahihi na vitabu vya hadithi hana riwaya isipokuwa hii tu. Ad-Dhahabiy amesema: Hajulikani. Yupo pia Muhammad bin Amru ambaye ni Abu Sahlu Al-Answari ambaye Yahya bin Al-Qitaniyna Ibnu Muini na Ibnu Adiy wamemdhoofisha32.
Ametusimulia Muhammad bin Sa’id kuwa: Alitusimulia Al-Hasan bin Yunus kuwa: Alitusimulia Al-As.wadi bin Amiri kuwa: Alitusimulia Abubakar bin Iyashi toka kwa Al-Aamashi toka kwa Amru bin Marati toka kwa Al-Rahman bin Abi Layli toka kwa Maadhi bin Jabali kuwa amesema: Alisimama mtu toka kwa answari Abdallah bin Zaid akaenda kwa Mtume na kusema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika mimi nimeona usingizini33.
Njia hii ni pungufu kwa sababu Maadhi alifariki mwaka wa ishirini au kumi na nane. Na Abdul-Rahmani bin Abi Layli kazaliwa mwaka wa kumi na saba. Zaidi ya hapo ni kuwa Ad-Darqutniy kamdhoofisha Abdurahmani kwa kusema: Ni dhaifu wa hadithi mwenye kumbukumbu mbaya. Huku Ibnu Abi Layli haujathibitika usikivu wake toka kwa Abdallah bin Zaid34
Mpaka hapa mazungumzo kuhusu sehemu ya kwanza yamekamilika na imedhihiri kuwa: Sheria ya adhana ililetwa kwa njia ya ufunuo wa Mwenyezi Mungu na wala si kwa ndoto ya Abdallah bin Zaid wala si kwa ndoto ya Umar bin Al-Khattabi wala si kwa ndoto ya mtu yoyote. Na ni kwamba hizi hadithi zinapingana, na hazina njia timilifu kimapokezi wala hazithibitishi chochote. Zaidi ya hapo ni kama tulivyosema mwanzo wa uchambuzi kuwa akili salama haikubaliani na hilo.
Sasa umefika wakati wa kuchambua jinsi kilivyoingizwa kipengele cha ziada ndani ya adhana ya alfajiri. Na hii ni sehemu ya pili tutakayokuletea hivyo tunasema:
• 1. (1, 2, 3) At-Tirmidhiy; As-Sunan:1/362 namba 190 na An-Nasai: As-Sunani
• 2. 2/3. Al-Bayhaqiy: As-Sunani: 1/389 mlango: Kuanza kwa adhana. Hadithi ya kwanza
• 3. As-Sirat Al-Halabiyat: 2/297
• 4. Al-Bayhaqiy: As-Sunan: 1/390, hadithi 1
• 5. As-Sirat Al-Halabiyat: 2/300
• 6. Al-Bukhari: Al-Swahihi:1/120 mlango: Mwanzo wa adhana
• 7. Angalia hadithi namba 2
• 8. Sharafu dini: An-Nasu wal-ijtihadi: 137
• 9. Ibnu Hajar: Tahdhibul-Tahdhibi:12/188 namba. 867
• 10. Jamaludini Al-Maziy: Tahadhibul-Kamali:34/142 namba 7545
• 11. Tahdhibul-Kamali:24/304
• 12. Chanzo cha mwanzo 24/423-424, Angalia Tarikhu Baghdadi: 1/221-224.
• 13. As-Sunan: Al-Tirmidhiy:1/361, Ibnu Hajar: Tahdhibul-Tahadhibi: 5/224
• 14. Tahdhibul-Kamali: 14/541
• 15. Al-Hakimu: Al-Mustadarak, 3/336 riwaya na riwaya zote zilizotoka kwake ni pungufu kwasababu aliuwawa vita vya Uhud
• 16. Tahdhibul-Kamali:16/ 519 namba 3755
• 17. Tahdhibul-Kamali 25/139 namba 5178
• 18. Al Shaukaniy: Naylul-Atuwar:2/37-38
• 19. Al-Imam Ahmadi: Al-Musnadi: 4/42-43
• 20. Al-Dhahabiy: Mizanul-Itidali: 2/100 namba 2997
• 21. Al-Daramiy: As-Sunan:1/268-269 mlango: mwanzo wa adhana
• 22. Maliki: Al-Muwatwau:15 mlango: yanayohusu wito wa sala namba 1
• 23. Siratul-Aalamu Al-Nubalau: 5/468 namba 213
• 24. Kitab Tabakatil Kubra
• 25. Siratul-Aalamu Al-Nubalau:2/376 namba 79.
• 26. Jamalul-Dini Al-Maziy: Tahdhibul-Kamali:27/508 namba 5925.
• 27. Chimbuko lile lile
• 28. Al-Bayhaqiy: As-Sunan:1/390.
• 29. Ibnu Hajar Tahdhibul-Tahadhibi: 12/188 namba 868
• 30. Al-Bayhaqiy: As-Sunani: 1/390
• 31. Ad-Daruqutniy: As-Sunan: 1/245 namba 56 na 57
• 32. Al-Dhahabiy: Mizanul-Itidali: 3/674 namba 8017 na 8018. Jamalul-Dini Al-Maziy: Tahdhibil-Kamali: 26/220 namba 5516. Ibnu Hajar: Tahdhibul-Tahadhibi: 9/378 namba 620
• 33. Ad-Daruqutniy: As-Sunan:1/242 namba 31 Abdallah bin Zaid
• 34. Ad-Daruqutniy: As-Sunan:1/241
ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO