ADHANA: SHERIA NA VIPENGELE VYAKE KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA (SEHEMU YA NNE)
ADHANA: SHERIA NA VIPENGELE VYAKE KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA (SEHEMU YA NNE)
UCHAMBUZI KUHUSU HISTORIA YA KUINGIA KIPENGELE CHA KUHIMIZA (TATHUWIBI) KATIKA ADHANA YA ALFAJIRI
At-Tathuwibi ni neno la Kiarabu litokanalo na kitenzi Thaba - Yathubu: Linaweza kuwa na maana ya kurejea, hivyo katika adhana litamaanisha kurejea kwenye amri kwa kuharakisha kuelekea kwenye Sala. Hivyo muadhini akisema: Njooni kwenye Sala atakuwa kawaita waelekee kwenye Sala, hivyo akisema tena: Sala ni bora kuliko usingizi atakuwa karejea katika maneno ambayo maana yake ni kuharakisha kwenda kwenye Sala. Mwandishi wa kamusi iitwayo: Al-Qamusi amefasiri kwa maana mbalimbali kati ya hizo maana ni: Kuomba waelekee kwenye Sala. Na ile hali ya kurudia mara mbili mbili ni ombi. Na pia kusema katika adhana ya alfajiri: Sala ni bora kuliko usingizi mara mbili - ni ombi.
Na amesema ndani ya kitabu Al-Magharibi kuwa: At-Tathuwibi ya zamani ilikuwa ni ile kauli aisemayo muadhini katika adhana ya asubuhi: Sala ni bora kuliko usingizi - mara mbili - Na hivi sasa At- Tathuwibi ni kusema: Sala Sala, imesimama 1
Dhahiri ni kuwa tathuwibi inatumika sana kwa maimam wa hadithi wakimaanisha ile kauli inayotajwa ndani ya adhana. Pia huenda ikatumika kumaanisha wito wowote unaokuja baada ya wito wa mwanzo hivyo hujumuisha wito wowote autoawo muadhini baada ya kumaliza adhana kwa kutamka tamko lolote alipendalo lenye maana ya wito wenye kuelekeza kwenye Sala.
As-Sanadiy amesema katika maelezo yake ya ziada ndani ya kitabu Sunanin-Nasai kuwa: Tathuwibi maana yake ni kurudia tangazo baada ya tangazo, Hivyo kauli ya muadhini: Sala ni bora kuliko usingizi ni sawa na hali hiyo hiyo, hivyo ikaitwa tathuwibi.2
Makusudio ya sehemu hii ni kutaka kudhihirisha hukumu ya kauli ya muadhini ndani ya adhana ya Sala ya alfajiri: Sala ni bora kuliko usingizi. Je ni kauli ya kisheria au ni bidaa iliyozushwa baada ya Mtume kutokana na pendekezo la baadhi ya watu walioona kuwa ni vizuri iwekwe kwenye adhana. Hiyo ni sawa iwe ndani ya adhana au hata baada ya adhana kwa wito wowote unaoelekeza kwenye Sala. Sawa iwe kwa tamko hili au lingine.
Hivyo tunasema kuwa tathuwibi kwa maana hii (Sala ni bora kuliko usingizi) imepatikana ndani ya hadithi za kisa cha ndoto ya adhana, na imepatikana tena katika hadithi nyingine. Ama katika fungu la kwanza imepatikana katika riwaya zifuatazo:
1. Riwaya aliyoipokea Ibnu Majah (Riwaya ya nne) na tayari umeshasikia maelezo ya As-Shaukaniy jinsi ilivyodhoofika3
2. Riwaya aliyoipokea Imam Ahmad nayo umeshajua udhaifu wa njia yake kwani yumo Muhammad bin Is’haqa na Abdallah bin Zaid bin Abdurabah4 . Riwaya aliyoipokea Saad katika kitabu chake At-Twabaqat. Katika njia yake yumo Muslim bin Khalid bin Qarqarat. Udhaifu wake tayari umeshaujua5.
Ama katika fungu la pili yaani tathuwibi katika hadithi zisizo za kisa cha ndoto ya adhana ni kwamba hadithi hizo zimenukuliwa na waandishi wa vitabu sita, na yafuatayo ni maelezo yao:
ALIYONUKUU IBNU MAJAH: NI KWA NJIA IFUATAYO:
Alitusimulia Abu Bakr bin Shaybati kuwa: Alitusimulia Muhammad bin Abdallah Al-Asadiy toka kwa Abi Izraili toka kwa Al-Hakamu toka kwa Abdurahmani bin Layli toka kwa Bilal amesema kuwa: Mtume aliniamrisha nihimize (Sala ni bora kuliko usingizi ) katika Sala ya Asubuhi na akanikataza katika Sala ya Isha6.
Katika riwaya hii kuna dalili inayoonyesha kuwa katika kuhimiza unaweza kutumia wito wowote unaoelekeza kwenye Sala hata kama si tamko la: Sala ni bora kuliko usingizi. Dalili juu ya hilo ni kile kitendo cha kukataza kuhimiza katika Sala ya isha kwa sababu huwezi kuhimiza katika Sala hii isipokuwa kwa tamko lingine, mfano wa: Salat jamia, au imesimama Sala, au tamko lingine.
5-Ametusimulia Umar bin Rafi kuwa: Ametusimulia Abdallah bin Al- Mubarak toka kwa Maamari toka kwa Az-Zahariy toka kwa Saidi bin Al- Musayab toka kwa Bilal kuwa: Alikuja kumuadhinia Mtume kwa ajili ya sala ya asubuhi akaambiwa amelala, hapo akasema: Sala ni bora kuliko usingizi, Sala ni bora kuliko usingizi, basi ikaidhinishwa iwekwe kwenye adhana ya Sala ya alfajiri. Basi kwa namna hiyo jambo hilo likathibiti7. Njia zote mbili za upokezi ni pungufu.
Kwanza: Ibnu Abi Layli amezaliwa mwaka wa 7 na Bilal kafariki mwaka wa 20 au 21 huko Sham. Na Bilal alikuwa huko Sham tangu Shamu ilipofunguliwa hivyo Bilal ni mkazi wa Sham na Ibnu Abi Layli ni mkazi wa Kufa, hivyo itakuwaje asikie toka kwa Bilal ilhali kiumri yeye ni mdogo sana kwa Bilal na kimakazi yuko mbali na Bilal8.
Na Tirmidhi kapokea kama hivyo lakini kwa tofauti katika njia (sanad) asema: Hadithi ya Bilal hatuijui isipokuwa kupitia hadithi ya Abi Israii Al- Mlai, na huyu Abi Israili hajaisikia hadithi hii toka kwa Al-Hakamu (Ibnu Utayba).
Akasema: Hakika yeye aliipokea toka kwa Al-Hasani bin Amarat toka kwa Al-Hakam. Na Abu Israili jina lake ni Ismail bin Abi Is.haqa, na yeye kwa watu wa hadithi ni dhaifu8
Pili: ni kuwa Ibnu Majah amenukuu maneno toka kwa Az-zawaidi kwa kusema: Wapokezi wake ni wakweli isipokuwa njia yake ni pungufu kwa sababu Said bin Al-Musayabu hakuisikia toka kwa Bilal9 .
6. ALIYOPOKEA AN-NASAIY
Alitupa habari Suwayd bin Nasri kuwa: Alitupa habari Abdallah toka kwa Sufiani toka kwa Jafari toka kwa Abi Salmani toka kwa Abi Mahdhurat amesema kuwa: Nilikuwa nikimuadhinia Mtume wa Mwenyezi Mungu na nilikuwa nikisema katika adhana ya Alfajiri ya mwanzo: (Njooni kwenye ushindi, Sala ni bora kuliko usingizi, Sala ni bora kuliko usingizi, Allah mkubwa Allah mkubwa, hapana mola wa haki isipokuwa Allah)10 .
Katika Sunan ya Al-Bayhaqiy11 na Subulu Salama12 sehemu ya jina Abi Salmani lipo jina Abi Sulaymani. Al-Bayhaqiy amesema: Na Abu Sulaymani jina lake ni Hamamul-muadhin, wala katika vitabu vyote tulivyonavyo vya wasifu wa wapokezi hakuna wasifu wa Hamamul- Muadhini hivyo Adh-Dhahabiy hakumtaja ndani ya kitabu chake (Mwenendo wa wasomi wema). Wala Al-Mazriy hakumtaja ndani ya Tahdhibil-Kimal na huyu Hamamu ni mtu asiyefahamika.
Ama Abu Mahdhurat yeye ni kati ya swahaba lakini mchache wa riwaya kwani riwaya alizopokea hazizidi kumi na alikuwa muadhini wa Mtume mwaka wa nane wakati wa vita vya Hunayni13 .
7. ALIYOPOKEA AL-BAYHAQIY
Katika kitabu chake (Sunan) kuna njia inayokomea kwa Abi Qadamat toka kwa Muhammad bin Abdul-Malik bin Abi Mahdhurat toka kwa baba yake toka kwa babu yake kuwa amesema: Nilisema: Ewe Mtume wa Allah, nifundishe sunna ya adhana. Akasimulia hadithi husika, na katika maelezo yake Mtume akasema:
حي علي الصلاة حي علي الصلاة
(Njooni kwenye Sala njooni kwenye Sala), ikiwa ni sala ya Asubuhi sema:
الصلاة خيرمن النوم
(Sala ni bora kuliko usingizi, Sala ni bora kuliko usingizi).
8. Pia kapokea kwa njia inayokomea kwa Uthman bin Al-Saibu: Alinipa habari baba yangu na mama wa Abdul-Maliki bin Abi Mahdhurat toka kwa Abi Mahdhurat toka kwa Mtume. Mfano wa riwaya iliyopita14. Umeshajua hali ya Muhammad bin Abdul-Malik. Na Uthman bin Al-Saibu ni mtoto na mzazi wasiyojulikana hawana riwaya isipokuwa hiyo moja tu15
9-ALIYOPOKEA ABU DAUD
Amepokea kwa njia inayokomea kwa Al-Harith bin Ubaydi toka kwa Muhammad bin Abdul-Malik toka kwa baba yake toka kwa babu yake amesema kuwa: Nilisema: Ewe Mtume wa Allah nifundishe sunna ya adhana. Akaendelea mpaka akasema: Kama ni Sala ya asubuhi utasema: (Sala ni bora kuliko usingizi Sala ni bora kuliko usingizi)16.
Njia hii imemjumuisha Muhammad bin Abdul-Malik. Amesema Ibnu Hajari kuwa: Amesema Abdul-haqi kuwa: Njia hii si hoja. Na Ibnu Qaytani akasema: Huyu hajulikani, hatumjui aliyopokea toka kwake isipokuwa Al- Harith17. Na Amesema Al-Shaukani kuhusu Muhammad bin Abdul-Malik bin Abi Mahdhurat kuwa wasifu wake haujulikani. Na Al-Harith bin Ubaydi na yeye ana maelezo yake 18.
10-Pia amepokea kwa njia inayokomea kwa Uthman bin Saibu: Alinijulisha baba yangu na mama wa Muhammad binAbdul-Malik bin Abi Mahdhurat toka kwa baba Mahdhurat toka kwa Mtume Mfano wa habari hii19. Tayari umeshajua udhaifu wa njia hii.
11. Pia amepokea kwa njia inayokomea kwa Ibrahim bin Ismail bin Muhammad bin Abdul-Malik bin Abi Mahdhurat amesema kuwa: Nilimsikia babu yangu Abdul-Malik bin Abi Mahdhurat akisema kuwa alimsikia Abi Mahdhurat akisema kuwa: Mtume alinifundisha adhana herufi baada ya herufi - mpaka akasema: Alikuwa akisema katika Sala ya Alfajiri:
الصلاة خيرمن النوم
(Sala ni bora kuliko usingizi).20
Na Ibrahim bin Ismail ana riwaya moja tu na ukweli wake haujathibitishwa 21. Zaidi ya hapo huenda njia hii ni pungufu.
ALIYOPOKEA AD-DARQUTNIY
Nayo yamegawanyika:
12. Zipo riwaya zinazoonyesha kuwa ni sunna ndani ya adhana, amezipokea toka kwa Anas na Umar bila kuzinasibisha kwa Mtume nazo ni hadithi tatu:22
13. Zinazoonyesha kuwa Mtume alimuamrisha Bilal kufanya hivyo, lakini njia hiyo ni pungufu. Amepokea Abdul-Rahman bin Abi Layli toka kwa Bilal 23 huku njia yake ni dhaifu kwa kuwemo Abdur-rahmani bin Al- Hasan ambaye huitwa Abu Mas.udi Az-Zajaju.Na Abu Hatim kamuelezea kwa kusema: Yeye si hoja hata kama wengine wakimlainisha 24.
14. Zipo zinazoonyesha tangazo kabla ya adhana kwa namna yoyote ile. Na hilo liko nje ya mada. Na baadhi ya waliyomo katika mtiririko wa njia hii wameidhoofisha25.
ALIYOPOKEA AL-DARAMIY
15. Ad-Daramiy kapokea kwa njia inayokomea kwa Az-Zahariy toka kwa Hafsa bin Umar bin Suad Muadhini.Hafsa amesema: .Walinisimulia ndugu zangu kuwa Bilal alikwenda kumuadhinia Mtume kwa ajili ya Sala ya Asubuhi, wakamwambia Mtume amelala, hapo Bilal akanadi kwa sauti ya juu:
الصلاة خيرمن النوم
(Sala ni bora kuliko usingizi:, ndipo ikapitishwa na kuwekwa ndani ya adhana ya Sala ya Alfajiri 26. Riwaya hii si hoja: Kwanza kwa kuwemo Az-Zahriy na Hafsa ambaye hana riwaya isipokuwa moja tu nayo ni hii 27.
Zaidi ya hapo ni kuwa hajulikani ni nani asili aliyenukuu riwaya hii.
16. ALIYOPOKEA IMAM MALIK
Ni kuwa muadhini alikwenda kumuadhinia Umar bin Al-Khatab kwa ajili ya Sala ya Asubuhi hivyo akamkuta amelala, muadhini akasema:
الصلاة خيرمن النوم
(Sala ni bora kuliko usingizi), ndipo Umar akaamrisha kipengele hicho kiwekwe ndani ya wito wa Sala ya Asubuhi 28.
MATOKEO YA RIWAYA
Hakika riwaya zinazoelezea kipengele cha kuhimiza (Sala ni bora kuliko usingizi) zinapingana sana huwezi kuzioanisha katika maana moja. Na vifuatavyo ni vifungu vyake:
1. Zipo zinazoonyesha kuwa Abdallah bin Zaid aliota usingizini kipengele cha (Sala ni bora kuliko usingizi) katika ndoto yake na ilikuwa ni sehemu ya adhana tangu mwanzo wa adhana.
2. Zipo zinazoonyesha kuwa Bilal aliongeza kipengele hicho ndani ya adhana, na Mtume akakipitisha na kumtaka Bilal akiweke kiwe sehemu ya adhana, na hilo ni kama ilivyo kwenye riwaya ya Ad-Daramiy.
3. Zipo zinazoonyesha kuwa Umar bin Al-Khatabi alimuamrisha muadhini akiweke ndani ya wito wa asubuhi, hilo ni kama alivyopokea Imam Malik.
4. Zipo zinazoonyesha kuwa Mtume wa Allah alimfundisha Abi Mahdhurat, hilo ni kama ilivyo katika riwaya ya Al-Bayhaqiy katika kitabu chake.
5. Dhahiri ni kuwa Bilal alikuwa akinadi asubuhi akisema: حي علي خيرالعمل (Njooni kwenye amali bora), hivyo Mtume akamwamrisha atoe kipengele hicho na sehemu yake aweke kipengele:
الصلاة خيرمن النوم
(Sala ni bora kuliko usingizi), na aache حي علي خيرالعمل (njooni kwenye amali bora.
Haya ni kama alivyopokea Al-Muttaqiy Al-Hindiy ndani ya kitabu chake Kanzu 8 / 345 namba 23188 ).
Kutokana na mgongano huu wa wazi hatuwezi kutegemea riwaya hizo. Na kwa kuwa jambo lenyewe lipo kati ya hali mbili: ima liwe ni sunna au bidaa basi tunapasa kuliacha kwa kuwa hatutoadhibiwa iwapo tutaliacha kinyume na litakapokuwa ni bidaa.
• 1. Al-Baharaniy: Al-Hadaiqu: 7/419 Angalia An-Nihayati mlango wa hadithi ya kustaabasha 1/226. (2)Lisanul-Arabi: kitenzi: Thawaba. Na Al-Qamusi kitenzi: Thawaba
• 2. As-Sunan: 2/14 Upande wa nyongeza
• 3. Angalia riwaya ya nne uk. 25 na maneno ya Ash-Shaukani katika kitabu hiki uk.39
• 4. Angalia tuliyonukuu toka kwa Imam Ahmadi baada ya hadithi toka vitabu sita uk.41
• 5. Angalia uk. 47 ndani ya kitabu hiki.
• 6. Ibnu Majah: As-Sunan: 1/237 namba 715
• 7. Ibnu Majah: As-Sunan: 1/237 namba 716
• 8. Ash-Shaukaniy: Naylil-Awtari: 2/38
• 9. At-Tirmidhiy : As-Sunan1/378 namba 198
• 10. Ibnu Majah: As-Sunani:1/237 namba 716. Saidi Al-Musayabu amezaliwa mwaka 13 na kufariki mwaka 94
• 11. An-Nasaiy: As-Sunan: 2/13 Mlango: kuhimiza katika adhana (Tathuwibi) 34
• 12. Al-Bayhaqiy: As-Sunan: 1/422.
• 13. Al-Swinaiy: Subulul-Salami: 1/221
• 14. Ibnu Hazmi Muhispania: Majina ya maswahaba wapokezi:161 namba 188
• 15. Al-Bayhaqiy: As-Sunan: 1/421- 422 Mlango: kuhimiza katika adhana ya Subhi
• 16. .Al-Dhahabiy: Mizanul-Itidali: 2/114 namba 3075. (Al-Saibu), Ibnu Hajar: Tahdhibul-tahdhibi: 7/117 namba 252 (Uthman bin Al-Saibu)
• 17. Abu-Daudi: As-Sunan: 1/136 namba 500
• 18. Ibnu Hajar: Tahdhibul-Tahdhibi: 9/317
• 19. Al-Shaukaniy: Naylul-Awtwari: 2/38
• 20. Abu Daudi: As-Sunan: 1/136-137 Mlango: Muundo wa adhana namba 501
• 21. Abu Daudi: As-Sunan:1/136-137 Mlango: Muundo wa adhana namba 504 36
• 22. Jamalud-Dini Al-Maziy: Tahdhibul-Kamali: 2/44 namba 147
• 23. Ad-Darqutniy: As-Sunan: 1/243 namba 38-39-40
• 24. Ad-Darqutniy: As-Sunan:1/243 namba 41
• 25. Angalia Mizanul-Itidali:2/556 namba 4851
• 26. Ad-Darqutniy: As-Sunan:1/244-245 namba 48, 51, 52, 53
• 27. Ad-Darqutniy: As-Sunan:1/270 Mlango: Kuhimiza katika adhana ya Al-fajiri 37
• 28. Jamalul-Din Al-Maziy: Tahdhibul-Kamali: 7/30 namba 1399. Na Al-Dhahabiy amesema katika Mizanul-Itidali: 1/560 namba 2129 kuwa: Al-zaharii peke yake ndiye kapokea riwaya toka kwa Hafsu
ITAENDLEA KATIKA MAKALA IJAYO