Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

SWALA NI NGUZO YA DINI (SEHEMU YA PILI)

0 Voti 00.0 / 5

SWALA NI NGUZO YA DINI (SEHEMU YA PILI)
UDHU
Mwenyezi Mungu amesema: “Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swala, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu na miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba, basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmeingiliana na wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni mchanga ulio safi na mpake nyuso zenu na mikono yenu Mwenyezi Mungu hapendi kukutieni katika taabu, lakini anataka kukutakaseni na kutimiza neema Yake juu yenu ili mpate kushukuru.”1
NI WAKATI GANI TUNAWAJIBIKA KISHARIA KUWA NA UDHU?
i. Ni lazima kuchukua udhu kwa ajili ya kila Swala ya faradhi au ya sunna isipokuwa sala ya kumsalia maiti, kwani si lazima kuchukuwa udhu kwa ajili yake.
ii. Kwa ajili ya kuizunguka Al-Kaaba wakati wa ibada ya Hijja na Umra.
iii. Kwa ajili ya kugusa maandishi ya Qur’an Tukufu.
MASHARTI YA KUSIHI KWA UDHU
i. Nia ya kujikurubisha kwa Allah Mtukufu
ii. Maji yawe tohara
iii. Yawe maji halisia: Yaani yasiwe maji ya matunda au yaliyokamuliwa toka kwenye mmea wowote ule (Kama vile maji ya waridi), au yaliyochanganywa na mada yoyote ile (kama vile maji ya sabuni, maji ya iriki au soda).
iv. Yawe maji ya halali: Yaani yasiwe maji ya wizi, na unyang’anyi au yatokanayo na kipato kisicho cha halali kisharia.
v. Chombo cha udhu kiwe cha halali: Yaani kisiwe cha wizi na unyang’anyi au kitokanacho na kipato kisicho cha halali kisharia.
vi. Chombo cha kufanyia udhu kisiwe cha dhahabu au fedha. vii. Viungo vya udhu viwe tohara.
vii. Kuwepo na muda utoshao kufanya udhu na kusali.
viii. Utaratibu baina ya viungo vya udhu: Yaani aoshe uso kwanza kisha mkono wa kulia na kisha wa kushoto, na baada ya hapo apake kichwa na kisha miguu yake miwili.
ix. Mfululizo baina ya viungo vya udhu: Yaani wakati wa kuchukua udhu asipitishe muda mrefu kabla ya kwenda kiungo kingine kwa kiasi ambacho itapelekea kukauka kwa viungo vya mwanzo kabla ya udhu kukamilika.
x. Atende matendo ya udhu yeye mwenyewe, na wala mtu mwingine asimfanyie udhu, isipokuwa katika hali ya dharura. (Hii ina maana kwamba, kama ukimwambia mtu akuoshe uso na mikono n.k. udhu wako utabatilika; lakini kama huwezi kufanya udhu mwenyewe kwa sababu za ugonjwa unaweza kuomba msaada kwa mtu mwingine).
xi. Lisiwepo tatizo au hatari yoyote ile iwezayo kutokea kutokana na kutumia maji, kama vile maradhi, hofu ya kiu, au kuihofia nafsi yake au nafsi yenye kuheshimika.
xii. Kisiwepo kizuizi chochote katika viungo vya udhu kinachoweza kuzuia maji kugusa ngozi, kama vile mafuta na rangi.
xiii. Kichwa na miguu viwe vikavu kabla ya kupaka maji.
JINSI YA KUTAWADHA
Kwanza: Nia: Nayo ni kukusudia moyoni kuwa: Ninatawadha kwa ajili ya kutafuta radhi ya Allah. Baada ya hapo anza kutenda matendo yafuatayo huku ukiendelea kuwa na nia hiyo moyoni.
 
Pili: Kuosha uso kwa kutumia mkono wa kulia, kuanzia kwenye maoteo ya nywele za kichwa mpaka kwenye ncha ya kidevu. Na ni lazima kuosha kuanzia juu kwenda chini kama inavyoonekana katika picha nambari (1) na (2).
 
WAKATI WA KUOSHA USO NI SUNNA KUSOMA DUA IFUATAYO:
اللهُمَّ بَيَّضْ وَ جْهِيْ يَوْمَ تَسْوَدَّ فِيْهِ الوُجُوْةُ وَ لاَ ثُسَودَّ وَ جْهيْ يَوْمَ تَبْيَضُّ فِيْهِ الوُجُوْةُ
Allahumma! Bayyidh Wajhi yawma tas’waddu fiyhil Wujuuhu walaa tusawwid wajhi yawma tabyaddhu fiyhil wujuuhu
“Ewe Mwenyezi Mungu! ung’arishe uso wangu Siku ambayo nyuso zitafifia, na usiufifize uso wangu Siku ambayo nyuso zitang’ara.”
Tatu: Kuosha mkono wa kulia kuanzia kwenye kifundo mpaka kwenye ncha za vidole. Na ni lazima kuosha kuanzia juu kwenda chini kama inavyoonekana katika picha nambari (3) na (4).
 
WAKATI WA KUOSHA MKONO WA KULIA NI SUNNA KUSOMA DUA IFUATAYO:
اللهُمَّ أعْطِنِي كِتاَ بي بيَمِيْنِيِْ وَ اَلخُلْدَ فِي الجِنَان بيَسَاري وَ حَا سِبْنِي حِسَابًايَسِيْرًا
Allahumma Aatwini kitaabi biyamiyni, walkhulda fil jinaan biyasaari, wahaasibni hisaban Yasiira
“Ewe Mwenyezi Mungu! unipe kitabu cha hesabu ya matendo yangu kwa mkono wangu wa kulia, na kuishi kwa mkono wangu wa kushoto.”
Nne: Kuosha mkono wa kushoto kuanzia kwenye kifundo mpaka kwenye ncha za vidole. Ni lazima kuosha kuanzia juu kwenda chini. kama inavyoonekana katika picha nambari (5) na (6).
 
WAKATI WA KUOSHA MKONO WA KUSHOTO NI SUNNA KUSOMA DUA IFUATAYO:
اللهُمَّ لاَ تُعْطِنِيْ كِتَا بِي بشِمِالِي ولا من ورارء ظهري وَلاَ تَجْعَلْهَا مَغْلُوْلَة اِلَي عُنُقِي
Allahumma la tuutwini kitaabi bishimali, walaa taj’alha maghlulatan ilaa unuqii
“Ewe Mwenyezi Mungu! usinipe kitabu cha matendo yangu kwa mkono wangu wa kushoto na wala nyuma ya Mgongo wangu na usiufanye kuwa wenye kujikunja shingoni mwangu.
Tano: Kupaka kichwa sehemu ya mbele kwa mkono wa kulia kutumia unyevunyevu wa udhu uliobaki kwenye kiganja. Usichukue maji mengine tofauti na unyevunyevu uliyobaki kwenye mkono, kama inavyoonekana katika picha nambari (7) na (8).
 
WAKATI WA KUPAKA MAJI KICHWANI, NI SUNNA KUSOMA DUA IFUATAYO:
اللهُمَّ غَشنِيْ برَ حْمَتِكَ وَ بَرَ كَا تِكَ وَعَفْوِكَ
Allahumma Ghas-Shini birahmatika wa barakaatika wa afwika
“Ewe Mwenyezi Mungu nifunike kwa rehma, baraka na msamaha Wako.”
Sita: Kupaka juu ya unyayo wa kulia kwa kiganja cha mkono wa kulia, kuanzia kwenye ncha za vidole hadi kwenye kifundo cha mguu, ukitumia unyevunyevu wa udhu uliobaki mkononi, kama inavyoonekana katika picha nambari (9) na (10).
 
WAKATI WA KUPAKA MIGUU NI SUNNA KUSOMA DUA IFUATAYO:
اللهُمَّ ثبَّثْنِي عَلَي الصِرَاطِ يَوْمَ تَزُلَّ فِيْهِ الأ قْدَامُ وَاجْعَلْ سَعْيي فِيْمَا يُرْضِيْكَ عّنِي
Allahummah thabbitni ala swiraat yawma tazallu fiyhil aqdaam, waj’al saa’yi fiyma yurdhika anni
“Ewe Mwenyezi Mungu nithabitishe juu ya njia siku ambayo nyayo zitateleza, na ujaalie harakati zangu ziwe katika yale yakuridhishayo.”
Saba: Kupaka juu ya unyayo wa kushoto kwa kiganja cha mkono wa kushoto, kuanzia kwenye ncha za vidole hadi kwenye kifundo cha mguu, ukitumia unyevunyevu wa udhu uliobaki mkononi, kama inavyoonekana katika picha nambari (11) na (12).
 
WAKATI WA KUPAKA MIGUU NI SUNNA KUSOMA DUA IFUATAYO:
اللهُمَّ ثبَّثْنِي عَلَي الصِرَاطِ يَوْمَ تَزُلَّ فِيْهِ الأ قْدَامُ وَاجْعَلْ سَعْيي فِيْمَا يُرْضِيْكَ عّنِي
Allahummah thabbitni ala swiraat yawma tazallu fiyhil aqdaam, waj’al saa’yi fiyma yurdhika anni
“Ewe Mwenyezi Mungu nithabitishe juu ya njia siku ambayo nyayo zitateleza, na ujaalie harakati zangu ziwe katika yale yakuridhishayo.”
VINAVYOTENGUA UDHU
i. Kutokwa na mkojo na kile kilicho chini ya hukumu yake, kama vile unyevunyevu utokao kabla ya kufanya istibraa.2
ii. Kutokwa na haja kubwa.
iii. Kutokwa na upepo katika sehemu ya kawaida.
iv. Usingizi wenye kuvighilibu via vya usikivu na uono.
v. Kila kinachoondoa akili, kama vile ulevi, wendawazimu au kuzimia.
vi. Kila kinachowajibisha kuoga, kama vile janaba, kugusa maiti, ambavyo huitwa hadathi kubwa.
MAMBO YA SUNNA KATIKA UDHU
Ni sunna kabla ya kufanya udhu kutenda yafuatayo:
i. Kuosha mikono mpaka kwenye kiwiko.
ii. Kusukutua maji kinywani mara tatu, au angalau mara moja. iii. Kuingiza maji puani mara tatu, au mara moja kwa uchache.
iii. Kuomba dua zilizopendekezwa kwa kila kiungo cha udhu. Dua hizo zimeshatangulia kwenye maelezo ya jinsi ya kutawadha.
UDHU WA BANDEJI (JABIRA)
Udhu wa Bandeji (Jabira)- Neno Bandeji hapa linamaanisha chochote kile kinachowekwa kwenye jeraha kitabibu, sawa iwe bandeji ya kawaida au plasta au kitambaa au pamba na vinginevyo- Mhariri.
Ikiwa kwenye moja ya viungo vya udhu kuna bandeji iliyosababishwa na jeraha, jipu au kuvunjika, basi kukiwa na uwezekano wa kuiondoa bandeji italazimu kufanya hivyo, na kama haiwezekani basi atapaka juu yake, kama inavyoonekana katika utaratibu wa kisharia ufuatao:
I. IKIWA KIUNGO CHENYE JERAHA NI USO AU MKONO NA KIUNGO HICHO KIKAWA WAZI BILA BANDEJI:
a. Ikiwa maji hayatamletea madhara basi atafanya udhu wake kwa utaratibu wa kawaida.
b. Ikiwa maji yatamletea madhara na inawezekana kuosha pembezoni mwa jeraha basi itatosha kufanya hivyo. Na kama haiwezekani kuosha pembezoni mwa jeraha, basi atafanya udhu wake kwa utaratibu wa udhu wa bandeji.
II. IKIWA KIUNGO CHENYE JERAHA NI USO AU MKONO NA KIUNGO HICHO KIMEWEKWA BANDEJI:
a. Ikiwa inawezekana kuiondoa bandeji hiyo na maji hayatamletea madhara, basi atafanya udhu wake kwa utaratibu wa kawaida.
b. Ikiwa inawezekana kuiondoa bandeji hiyo lakini maji yatamletea mad- hara, basi atafanya udhu wake kwa utaratibu wa udhu wa bandeji.
c. Ikiwa haiwezekani kuiondoa bandeji hiyo, na maji hayamletei madhara lakini jeraha lina najsi, basi atafanya udhu kwa utaratibu wa udhu wa bandeji.
d. Ikiwa haiwezekani kuiondoa bandeji hiyo, na maji hayamletei madhara na jeraha halina najsi, basi atafanya udhu kwa utaratibu wa kawai- da.
e. Ikiwa haiwezekani kuiondoa bandeji hiyo, na maji yatamletea madhara, basi atafanya udhu kwa utaratibu wa udhu wa bandeji.
III. IKIWA KIUNGO CHENYE JERAHA NI KICHWA AU MGUU:
a. Ikiwa inawezekana kupaka sehemu isiyo na jeraha, basi atapaka na udhu wake utakuwa sahihi.
b. Ikiwa haiwezekani kupaka sehemu yoyote ile, na kupaka kutamletea madhara, basi atafanya udhu kwa utaratibu wa udhu wa bandeji.
c. Ikiwa haiwezekani kupaka sehemu yoyote nyingine, na kupaka hakumletei madhara, basi ikiwa jeraha halina bandeji atafanya udhu kwa utaratibu wa kawaida.
d. Ikiwa haiwezekani kupaka sehemu yoyote nyingine, na kupaka hakumletei madhara lakini jeraha lina bandeji, basi atafanya udhu kwa utaratibu wa udhu wa bandeji. Na atafanya ihtiyati kwa kutayammam, hivyo atafanya vyote viwili pamoja.
KUOGA
i. Ni mtu kuoga mwili wake wote kwa maji tohara na ya halali.
ii. Aina za majosho ya wajibu kisharia
iii. Josho la janaba, hedhi, istihadha, nifasi, la kumgusa maiti na la maiti.
MAMBO YANAYOSABABISHA JANABA
i. Kujamiiana, hata kama mtu hatotokwa na manii.
ii. Kutokwa na manii, sawasawa iwe usingizini au katika hali ya kuwa macho, iwe kidogo au mengi, kwa matamanio au bila ya matamanio.
JINSI YA KUOGA KISHARIA
Kwanza: Nia, nayo ni kukusudia moyoni kuwa: Ninaoga kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Pili: Unaweza kuoga kwa njia moja kati ya njia mbili:
i. Kuoga kwa mpangilio maalumu: Nao ni kuanza kuosha kichwa na shin- go, kisha upande wa kulia wa mwili wako, halafu kuoga upande wa kushoto wa mwili wako.
ii. Kuoga kwa kuzama: Nako ni kuzama katika maji mara moja ambapo mwili wako wote uenee maji.
ZINGATIA:
1. Wakati wa kuoga ni lazima kuondoa vizuizi vyote mwilini vinavyoweza kuzuia maji kufika kwenye ngozi.
2. Hakuna tofauti yoyote kati ya mwanaume na mwanamke katika namna ya kuoga.
3. Kuoga kwa ajili ya janaba kunatosheleza udhu.
MAS’ALA MBALIMBALI
Mtu akiwa na janaba, hedhi au mfano wa hayo, ni haramu kwake mambo yafuatayo:
i. Kuswali: Lazima aoge ili Swala yake iwe sahihi, isipokuwa Swala ya maiti.
ii. Kuizunguka Al-Kaaba iliyopo mji mtukufu wa Makka.
iii. Kuyagusa maandishi ya Qur’an Tukufu.
iv. Kusoma Aya zenye sijda ya wajibu zilizopo kwenye sura nne:
1. Sura As-Sajdah: 14.
2. Sura Fusswilat: 36.
3. Sura An-Najmi: 61.
4. Sura Al-Alaq: 18.
v. Kukaa katika misikiti na makaburi ya Maimamu (a.s), na kuingia msik- iti mtukufu wa Makka na msikiti wa Mtume (s.a.w.w.) uliopo Madina.
vi. Kuweka kitu chochote msikitini.
REJEA:
•    1. Sura Al-Maidah: 6.
•    2. Istibrau ni kitendo cha mwanaume kukamua tupu yake baada ya haja ndogo ili kuondoa mabaki ya mkojo katika njia yake. Kwa ufafanuzi zaidi tazama vitabu vikubwa vya hukmu- Mhariri.

ITAENDELEA KATIKA MAKAL IJAYO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini