Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

SWALA NI NGUZO YA DINI (SEHEMU YA TATU)

0 Voti 00.0 / 5

SWALA NI NGUZO YA DINI (SEHEMU YA TATU)
KUTAYAMMAM
Mwenyezi Mungu asema: “Na mkiwa wagonjwa au safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmeingiliana na wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni mchanga ulio safi.”1
WAKATI GANI TUNATAYAMMAM?
    i. Yanapokosekana maji ya kutosha kwa ajili ya udhu, au kuoga josho la kisharia.
    ii. Tunapohofia kuwa kuyafikia maji kutatusababishia madhara juu ya nafsi, au mke na watoto au mali yenye kufungamana nasi.
    iii. Ikiwa kuyapata maji au kuyatumia kutasababisha tabu na mashaka makubwa, ikiwemo madhila na uvunjifu wa heshima.
    iv. Ufinyu wa muda katika kutafuta maji au kuyatumia kwa kiasi kwamba muda wa Swala utatupita.
    v. Iwapo maji yatatosheleza tu kuondosha najisi mwilini na kwenye mavazi.2
TUTATAYAMMAM KWA KUTUMIA VITU GANI?
i. Udongo na mchanga.
ii. Mawe na miamba.
iii. Changarawe, na vinginevyo vinavyoitwa ardhi.
MASHARTI YA KUSIHI KWA TAYAMMAM
i. Nia, anuie moyoni: Ninatayammam badala ya udhu kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
ii. Tayammam ifanyike kwa vitu ambavyo inaruhusiwa kisharia kufanyia tayammam, kama vile udongo na miamba.
iii. Vitu vya kufanyia tayammam viwe tohara. iv. Vitu hivyo viwe vya halali.
iv. Viungo vya tayammam viwe tohara.
v. Kisiwepo kizuizi chochote kwenye viungo vya tayammam kama vile pete na vinginevyo.
vi. Kuzingatia utaratibu baina ya viungo vya tayammam.
vii. Afanye tayammam yeye mwenyewe na asifanyiwe na mtu mwingine isipokuwa katika hali ya dharura.
VITENGUZI VYA TAYAMMAM:
Vitenguzi vya udhu hutumika kama vitenguzi vya tayammam, zaidi ya hapo ni kutoweka kwa udhuru uliyosababisha kufanyika kwa tayammam hiyo.
JINSI YA KUFANYA TAYAMMAM:
Kwanza: Nia, nayo ni kukusudia moyoni kuwa: Ninatayammam badala ya udhu au josho kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Pili: Kupiga mara moja juu ya ardhi kwa vitanga viwili, kama inavyoonekana katika picha nambari 13.
Tatu: Kupaka paji la uso kwa kutumia viganja viwili, kuanzia kwenye maoteo ya nywele mpaka kwenye nyusi pamoja na upande wa juu wa pua, na ni lazima kupaka kuanzia juu kwenda chini, kama inavyoonekana katika picha nambari 14 na 15.
Nne: Kupaka juu ya kitanga cha mkono wa kulia kwa kutumia kitanga cha mkono wa kushoto kuanzia kwenye kiwiko mpaka kwenye ncha za vidole, na lazima kupaka kuanzia juu kwenda chini, kama inavyoonekana katika picha nambari 16 na 17.
Tano: Kupaka juu ya kitanga cha mkono wa kushoto kwa kutumia kitanga cha mkono wa kulia kuanzia kwenye kiwiko mpaka kwenye ncha za vidole, na lazima kupaka kuanzia juu kwenda chini, kama inavyoonekana katika picha nambari 18 na 19.
MAS’ALA MBALIMBALI KUHUSU TAYAMMAM:
i. Ni wajibu kupiga juu ya ardhi, wala haitoshi kuweka tu mkono juu yake.
ii. Haisihi kutayammam kwa ajili ya faradhi ambayo bado wakati wake haujaingia.
iii. Tukitayammam kwa ajili ya Swala ambayo tayari muda wake umeshaingia na ikawa tayammam yetu haijatenguka wala udhuru uliyotusababisha tutayammam haujatoweka; hali hiyo ikaendelea mpaka ukaingia wakati wa sala nyingine, basi hapo tunaruhusiwa kusali Swala hii ya sasa kwa tayammam hiyo, madamu tu tunajua kuwa udhuru hautotoweka mpaka mwisho wa wakati.
Akitayammam badala ya josho, kisha akapatwa na hadathi ndogo, basi kwa mujibu wa ihtiyati atatakiwa kutayammam tena upya badala ya josho kisha achukuwe udhu, kama itawezekana. Kama haiwezekani basi atatayammam mara ya pili badala ya udhu.
REJEA:
•    1. Sura Al-Maidah: 6
•    2. Hizi tulizozitaja ni sababu muhimu na wala si zote, hivyo atakaye ufafanuzi zaidi arejee vitabu vya hukumu za sharia.
ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini