Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

SWALA NI NGUZO YA DINI (SEHEMU YA NNE) A

0 Voti 00.0 / 5

SWALA NI NGUZO YA DINI (SEHEMU YA NNE) A
SWALA

i. Swala za wajibu

ii. Swala za kila siku

iii. Swala ya kutufu Al-Kaaba

iv. Swala ya misukosuko, nayo husaliwa pale panapotokea matukio ya kiasili, kama vile, kupatwa kwa mwezi, kupatwa kwa jua, na tetemeko la ardhi.

v. Swala ya kulipa anayoisali mtoto mkubwa baada ya kifo cha baba ambaye hakutekeleza Swala za wajibu.

vi. Swala ambayo huwa wajibu kwa sababu ya nadhiri au mfano wake au kukodishwa.(ijara)

vii. Swala ya maiti.
SWALA ZA KILA SIKU NA IDADI YA RAKAA ZAKE

Nazo ni sala za faradhi ambazo ni wajibu kuzisali kila siku.

i. Swala ya Subhi, ina rakaa mbili.

ii. Adhuhuri, ina rakaa nne.

iii. Alasiri, ina rakaa nne.

iv. Magharibi, ina rakaa tatu.

v. Isha, ina rakaa nne.
MAVAZI YA MWENYE KUSALI

Mwanamume: Ni linalositiri tupu mbili, yaani kwa kiwango cha kuweza kusitiri utupu wa mbele na wa nyuma.

Mwanamke: Lazima kwa mwanamke kusitiri mwili wake wote wakati wa Swala isipokuwa uso na vitanga vya mikono pamoja na nyayo mbili, kama inavyoonekana katika picha nambari 20.
SHARTI ZA VAZI LA MWENYE KUSALI:

i. Liwe tohara.

ii. Liwe la halali (yaani lisiwe la unyang’anyi).

iii. Vazi la mwanamume lisiwe limetengenezwa kutokana na Hariri.

iv. Lisiwe linatokana na viungo vya mzoga, ambavyo vinafikiwa na uhai, kama vile nyama ya mnyama ambaye hakuchinjwa kisharia.

v. Lisiwe linatokana na viungo vya wanyama ambao ni haramu kuliwa, hata kama watakuwa wamechinjwa kwa taratibu za kisharia, bali pia hairuhusiwi kuchukua kiasi kidogo cha viungo hivyo katika Swala.
MAS’ALA KUHUSU VAZI

i. Katika hijabu ya kisharia isiyokuwa ya ndani ya Swala ni lazima kusitiri miguu, na hairuhusiwi kuvaa vazi lenye kubana wala kuonyesha mapambo.

ii. Mwanamke awapo ndani ya Sala anaruhusiwa kisharia kuvaa vazi lenye kubana au lenye kuukamata mwili na kudhihirisha mapambo iwapo tu hakuna mwanamume ajnabi anayemuona.

iii. Ni sunna kwa mwanamume katika Swala kuvaa vazi kamili kama heshima kwa sababu anasimama mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
TOHARA YA MWILI

Ni sharti mwili wa mwenye kusali uwe tohara dhidi ya najisi, hata kucha na nywele, vilevile ni sharti kwa mwenye kutaka kusali awe ametawadha, na kama anatakiwa kuoga kisharia basi itamlazimu kufanya hivyo ili aweze kusali.
NAJISI ZINAZOSAMEHEKA KATIKA SWALA

i. Kuwapo damu ya jeraha na majipu kwenye nguo na mwili wa mwenye kusali hakudhuru Swala; mpaka litakapopona, iwapo tu haiwezekani kuiondoa au kuna ugumu wa kufanya hivyo.

ii. Pia imesamehewa kisharia damu ya jeraha na majipu iwapo kwenye mwili au nguo kama itakuwa si zaidi ya kiasi cha fundo la kidole cha shahada, madamu tu si damu ya mnyama aliye najsi, kama vile mbwa na nguruwe na kafiri, na madamu tu si damu ya mzoga, hedhi au nifasi au istihadha.

iii. Inaruhusiwa kisharia kusali na soksi, kofia, mkanda na mfano wake vilivyo najisika, miongoni mwa vitu ambavyo havitoshelezi kusitiri tupu iwapo tukitaka kusitiri tupu mbili kwa wenyewe tu.
MASHARTI YA MAHALI PA KUSALIA

i. Mahali pa kusalia pawe pa halali, yaani pasiwe pa unyang’anyi.

ii. Sehemu ya kusalia iwe tulivu, yaani isiwe na mtikisiko. Sharti hili litazingatiwa katika mazingira yasiyokuwa na udhuru, ama katika hali ya udhuru kama vile msafiri wa melini au ndege, sio lazima kuzingatia sharti hili iwapo haitawezekana kuiahirisha Swala kwa kuhofia kupitwa na wakati.

iii. Sehemu ya kusalia isiwe na najisi isiyosameheka, ambayo inaweza kuhamia kwenye mwili au nguo yake.1

iv. Siyo sharti kwa mwanamume kumtangulia mwanamke, hasa inapokuwa kuna umbali wa kiasi cha shibri kati yao.

v. Ni lazima mahali pa kufanyia sijda pawe tohara.2

vi. Mahali pa kufanyia sajda pasiwe juu au chini sana kuliko sehemu ya nyayo kwa zaidi ya kiasi cha vidole vinne vilivyobebana.
NYAKATI ZA SWALA

Mwenyezi Mungu asema: “Simamisha Swala jua linapopinduka mpaka giza la usiku na kusoma Qur’an ya alfajri (Swala ya alfajri).”3 Na akasema: “Hakika Swala kwa wenye kuamini imekuwa ni faradhi yenye kuwekewa wakati maalumu.”4

Imepokewa kutoka kwa Imam As-Sadiq (a.s.) kuwa: “Hakika Mtume (s.a.w.w.) alisali Adhuhuri na Alasiri kwa adhana moja na ikama mbili, na akasali Magharib na Isha pasipokuwa na safari wala ugonjwa kwa adhana moja na ikama mbili.”5

Wakati wa Sala ya Subhi: Huanzia kuchomoza kwa alfajiri na hukomea wakati wa kuchomoza jua.

Wakati wa Swala ya Adhuhuri: Huanzia wakati jua linapopinduka wakati wa mchana mpaka kabla ya jua kuzama kwa kiasi cha muda utoshao kutimiza Swala ya Alasiri.

Wakati wa Sala ya Alasiri: Huanzia baada ya kupinduka jua baada tu ya kiasi cha kuweza kutimiza Sala ya Adhuhuri, na hukomea wakati wa kuzama jua kisharia.

Wakati wa Swala ya Magharibi: Huanza baada ya kuzama jua kisharia mpaka kabla ya nusu ya usiku kabla haujaisha muda utoshao kusali Sala ya Isha.

Wakati wa Swala ya Isha: Huanzia tangu kuzama jua kisharia pale unapopita muda utoshao kusali Sala ya Magharib, na hukomea nusu ya usiku, na iliyo bora kwa yule ambaye alichelewa kusali sala za Magharib na Isha mpaka nusu ya usiku, azisali mpaka wakati wa kuingia alfajiri kwa lengo la kutekeleza wajibu.
KIBLA

Mwenyezi Mungu asema: “Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtukufu. Na popote mtapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo.”6

Ni lazima kwa mwenye kusali aelekee Kibla wakati wa Sala zote. Kibla ni upande wa Kaaba Tukufu kulingana na miji yote, hivyo Kibla hutofautiana kati ya mji na mji kulingana na tofauti za maeneo.

Wakati huo tunaelekea upande wa nyumba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuzielekeza nyuso zetu upande wa Al-Kaaba Tukufu iliyojengwa na Nabii Ibrahim (a.s) na mwanaye Ismail (a.s).
ADHANA

Imepokewa kuwa: “Malaika wasikiapo adhana kutoka duniani husema: “Hizi ni sauti za umma wa Muhammad (s.a.w.w.) wakimpwekesha Mwenyezi Mungu”, hivyo huwaombea maghfira mpaka mwisho wa Swala hiyo.”7

Kuingia wakati wa Swala hutambulishwa kwa Adhana.8 Nayo ni katika sunna zilizotiliwa mkazo wakati wa sala tano, nayo ni:

اللهُ أكْبَرُ

Allahu Akbar (mara nne)

Allah ni mkubwa (zaidi ya kusifiwa).

أشْهَدُ أنْ الاَ اِلهَ اِلّا الله

As-Sh’hadu an’lailaha illa llah (mara mbili)

Nashuhudia kuwa hakuna Mungu ila Allah tu

أشْهَدُ أنَّّّّ مُحَمَّدا رَسُوْلُ ا لله

As-Sh’hadu anna Muhammada Rasulullah (mara mbili)

Nashuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah.

حَيَّ عَلَي الصَلَاة

Hayya a’las-Swalah (mara mbili)

Njooni kwenye Swala

حَيَّ عَلَي الفَالاَح

Hayya alal-Falah (mara mbili)

Njooni kwenye njia ya salama na mafanikio.

حَيَّ عَلَي خَيْر العَمَل

Hayya ala khayril-A’mal (mara mbili)

Njooni kwenye amali bora zaidi

اللهُ أكْبَرُ

Allahu Akbar (mara mbili)

Allah ni mkubwa (zaidi ya kusifiwa)

لاَ اِله اِ لاَّ ا لله

La Ilaha Ila llah (mara mbili)

Hakuna Mungu ila Allah tu.
KUKIMU

Baada ya kusikia sauti ya adhana, mwenye kusali hujiandaa kwa ajili ya Swala na kuelekea msikitini au mahali pengine palipoandaliwa kwa ajili ya sala ya jamaa au ya mtu mmoja mmoja ili apate kusali, na wakati huo, wakati wa kutaka kusali, huanza kukimu Swala. Nako ni katika sunna zilizotiliwa mkazo wakati wa Swala tano, atasema:

اللهُ أكْبَرُ

Allahu Akbar (mara mbili)

Allah ni mkubwa (zaidi ya kusifiwa)

أشْهَدُ أنْ الاَ اِلهَ اِلّا الله

As-Sh’hadu an’lailaha illa llah (mara mbili)

Nashuhudia kuwa hakuna Mugu ila Allah tu.

أشْهَدُ أنَّّّّ مُحَمَّدا رَسُوْلُ ا لله

As-Sh’hadu anna Muhammada Rasulullah (mara mbili)

Nashuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah.

حَيَّ عَلَي الصَلَ ة

Hayya alas-Swalah (mara mbili)

Njooni kwenye Swala.

حَيَّ عَلَي الفَالاَح

Hayya alal-Falah (mara mbili)

Njooni kwenyenjia ya salama na mafanikio.

حَيَّ عَلَي خَيْر العَمَل

Hayya ala khayril-Amal (mara mbili)

Njooni kwenye amali bora zaidi.

قدْ قاَ مَتْ ا الصَلَاة

Qad qamatis-Swalah (mara mbili)

Hakika Swala imesimama.

اللهُ أكْبَرُ

Allahu Akbar (mara mbili)

Allah ni mkubwa (zaidi ya kusifiwa)

لاَ اِله اِ لاَّ ا لله

La Ilaha Ilallaha (mara mbili)

Hakuna Mungu ila Allah tu.
MAS’ALA KUHUSU ADHANA NA IQAMA

i. Ni sunna katika adhana na ikama baada ya kipengele cha tatu kuongeza kipengele “As-Sh’hadu anna Aliyyan waliyullah.” Kipengele hiki si sehemu ya adhana lakini ni sunna ya adhana.

ii. Adhana huachwa katika sala ya pili pale mwenye kusali anapoamuwa kukusanya kati ya Sala mbili.

iii. Adhana na ikama vyote viwili huachwa pale mwenye kusali anapoingia kwenye Sala ya jamaa ambayo tayari adhana yake imeshaadhiniwa na ikama kukimiwa. Na pia pale mwenye kusali atakapomsikia mwingine kaadhini na kukimu, kwa sharti tu kati ya adhana na Sala au ikama na sala kusiwe na muda mrefu, na pia awe amesikia vipengele vyote vya adhana na iqama.

REJEA:

    1. Najsi huhama iwapo tu kimoja kati ya najsi au kitu husika kina unyevunyevu unaohama -Mhariri.
    2. Hapa ni hata kama najsi hiyo haihami, kinyume na sharti la tatu ambalo linakomea iwapo tu najsi inahama. Kwa ufafanuzi rejea vitabu vya matendo ya kisharia -Mhariri.
    3. Sura Al-Israil: 78.
    4. Sura An-Nisai: 103
    5. Al-Faqihi, Juz. 1.
    6. Sura Al-Bqarah: 144.
    7. Al-Faqihi, Juz. 1.
    8. Lazima ifahamike kuwa kisharia wajibu wa kutambua uingiaji wa muda wa sala ni wa mtu binafsi, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kujua je wakati wa Sala fulani umeingia au la. Na wala si wajibu wa mwadhini peke yake, kama ambavyo ni wajibu wa kila mmoja kujua ni upi upande wa Kibla ili aweze kuelekea huko wakati wasala yake.

ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini