SWALA NI NGUZO YA DINI (SEHEMU YA NNE) B
SWALA NI NGUZO YA DINI (SEHEMU YA NNE) B
SWALA
MASHARTI YA DHANA NA IQAMA
i. Nia, nayo ni kunuwia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Ni lazima nia hiyo idumu mpaka mwisho wa adhana
ii. Akili na imani: Mwadhini awe balehe mwenye akili timamu
iii. Adhana ya Sala ya wanaume ni lazima iadhiniwe na mwanamume.
iv. Utaratibu: Ni lazima ianze adhana na kisha ndio ikama. Na pia ni lazima vipengele vyao viwe katika utaratibu uliyotajwa bila kutanguliza wala kuchelewesha.
v. Mfululizo: Ni lazima kusiwe na kitenganishi cha wakati mrefu kati ya kipengele na kipengele.
vi. Iwe kwa kiarabu fasaha.
vii. Iwe baada ya wakati husika kuingia.
MAMBO YA WAJIBU KATIKA SWALA
i. Wajibu uliyo nguzo: Nao ni tendo ambalo huvunja Swala likiongezwa au kupunguzwa kwa makusudi au kwa kusahau.
ii. Wajibu usiyo nguzo: Nao ni tendo ambalo huvunja Sala iwapo likiongezwa au kupunguzwa kwa makusudi.
MAMBO YALIYO WAJIBU YALIYO NGUZO
i. Nia.
ii. Takbira ya kuhirimia.
iii. Kisimamo kwa ajili ya nia na kwa ajili ya takbira ya Ihraam. Na kisi- mamo ambacho huwa tu kabla ya kwenda rukuu.
iv. Rukuu.
v. Sijda mbili kwa pamoja.
MAMBO YALIYO WAJIBU YASIYO NGUZO:
i. Kusoma Alhamdu na sura kamili katika rakaa mbili za mwanzo, na kusoma Alhamdu au kusoma Tasbihi nne katika rakaa ya tatu na ya nne.
ii. Dhikri katika rukuu na sijda.
iii. Tashahhud.
iv. Swalamu.
v. Utaratibu
vi. Mfululizo.
NIA:
Nayonikukusudia kusali, nautasema: ninasali sala ya alfajiri {au adhuhuri au laasir au magharibi au isha} kwahali yakutekeleza waajibu kwakutaka radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu. na wala si lazima katika nia kutamka.bali utashi wa kimoyo unatosha. na vilevile ni sharti nia hiyo iwe ya ikhlasi, na kuainisha iana ya sala (wajibu au sunna, pungufu au timamu).
TAKBIRA YA KUHIRIMIA:
Nayo ni kusema: “Allahu Akbar”
Ambapo ni lazima isomwe katika hali ya kusimama na kunyooka, akiwa ameelekea kibla, vilevile ni lazima kuwa katika hali ya utulivu wa kimwili kabla ya kuitamka.
KISOMO:
i. Ni lazima kusoma Sura Alhamdu pamoja na sura nyingine yoyote kamili katika rakaa mbili za mwanzo, ama katika rakaa ya tatu na ya nne ni hiyari kusoma Alhamdu tu au Tasbihi nne:
سُبْحَانَ الله وَ الحَمْدُ لِلَهِ وَ لاَ اِلهَ اِلّا لله وَا لله أكْبَر
“Utakasifu ni wa Mwenyezi Mungu na kila sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, hapana Mola wa haki ila Allah, na Mwenyezi Mungu ni Mkubwa {zaidi ya kusifiwa}.”
ii. Ni lazima kujifunza namna sahihi ya kusoma katika kutamka herufi na irabu.
iii. Ni lazima kutodhihirisha kisomo katika sala za Adhuhuri na Alasiri, pia ni lazima kudhihirisha sauti katika sala za Asubuhi na Magharibi na Isha kwa wanaume pekee, ama wanawake, sio lazima kwao kudhihirisha.
iv. Swala hubatilika iwapo mtu kwa makusudi ataacha kudhihirisha sauti pale panapotakiwa kudhihirisha au kinyume chake, aidha kama itakuwa ni kwa kusahau, basi hakuna tatizo katika sala yake.
v. Ni lazima kutodhihirisha sauti wakati wa kusoma Tasbihi nne, na wakati wa kusoma Alhamdu badala yake, na vilevile katika sala ya ihtiyaat.
vi. Katika maeneo ya kutodhihirisha sauti ni sunna kudhihirisha Bismillahi isipokuwa katika rakaa ya tatu na ya nne inaposomwa sura Alhamdu badala ya Tasbihi nne.
vii. Sura za Al-Fiil na Quraysh huhesabiwa kama sura moja, halikadhalika sura za Ad-Dhuhaa na Inshiraah huhesabiwa kama sura moja.
ZINGATIA:
a. Kipimo cha kudhihirisha na kutodhihirisha sauti ni kusikika au kutosikika sauti.
b. Ni lazima uwepo mfululizo kati ya herufi za neno. Kama ambavyo ni lazima mfululizo huo uwepo kati ya maneno ya Aya na kati ya Aya za sura, kwa namna ambayo itasadikika kweli kuwa hili ni neno moja au Aya moja au sura maja.
c. Ni karaha kuacha kusoma Sura Ikhlasi ndani ya sala tano za faradhi.
d. Ni lazima kusoma Bismilahi mwanzo wa kila sura isipokuwa sura At-Tawba.
e. Inatosha kusoma Tasbihi nne mara moja, na ni sunna kuzisoma mara tatu katika rakaa ya tatu na ya nne kabla ya kufanya rukuu, nazo ni: “Subhanallah, walhamdulillah, walailaaha illa llah, wallahu akbar”.
f. Na ni wajibu kutodhihirisha sauti wakati wa kusoma Tasbihi nne.
g. Vilevile inawezekana kwa mwenye kusali kusoma sura Alhamdu badala ya Tasbihi nne, na iliyo bora kwa imamu ni kusoma Alhamdu na maamuma asome Tasbihi nne.
RUKUU:
Mwenyezi Mungu asema: “Enyi mlioamini! Rukuuni na sujuduni na mwabuduni Mola wenu na fanyeni mema ili mpate kufaulu.”1
i. Ni lazima kufanya rukuu mara moja katika kila rakaa ya Sala.
ii. Ni lazima kuinama katika rukuu mpaka mikono ifike kwenye magoti. iii. Ni lazima katika rukuu kusoma dhikri ifuatayo: “Sub’hana rabbiyal Adhiim wabihamdihi” mara moja. Au “Sub’hanallah” mara tatu.
iii. Baada ya rukuu na kabla ya kwenda kusujudu ni lazima kusimama kwa unyoofu, ambapo ni lazima kuwa na utulivu ndani yake.
iv. Ni lazima kuwapo na utulivu wakati wa kusoma dhikri za ndani ya sala. vi. Ni sunna wakati wa kuinuka kutoka kwenye rukuu kusema: “Samiallahu liman hamidah”.
SIJDA:
i. Ni lazima kusujudu mara mbili katika kila rakaa ya Sala.
ii. Ni lazima kuegemea viungo saba vya sijda katika hali ya kusujudu, navyo ni paji la uso, viganja viwili, magoti na vidole gumba vya miguu.
iii. Katika kila sijda ni lazima kusoma dhikri ifuatayo: “Sub’hana rabbiyal’ aala wabihamdihi” mara moja. Au “Subhanallah” mara tatu.
iv. Sehemu ya kuweka paji la uso ni lazima ilingane na ile ya kuweka miguu, na sio tatizo iwapo moja wapo itakuwa juu ya nyingine kwa kiasi cha vidole vinne vilivyobebana.
v. Ni lazima kuwa katika hali ya kutulia wakati wa kusoma dhikri ya sijda. vi. Ni lazima kukaa baina ya sajda mbili kwa hali ya utulivu, na ni sunna
vi. Wakati wa kuinuka kutoka kwenye sijda kusema: “AllahuAkbar”.
MASHARTI YA MAHALI PA KUFANYIA SIJDA:
i. Sehemu ya kuwekea paji la uso ni sharti iwe ni sehemu inayoweza kuitwa ardhi, kama vile udongo au jiwe au changarawe, au miongoni mwa viotavyo ardhini, kama vile mimea kwa sharti isiwe inatumiwa kwa chakulana mavazi.
ii. Sehemu ya kuweka paji la uso ni sharti liwe na utulivu wakati wa kufanya sijda.
iii. Ni sharti sehemu hiyo iwe tohara.
KUNUTI:
Ni katika sunna zilizotiliwa mkazo kukunuti katika rakaa ya pili kabla ya kufanya rukuu, nako ni maombi yoyote yanayokusudiwa ndani yake mambo ya kheri hapa duniani na akhera na hasa kuwaombea waumini.
Miongoni mwa dua ambazo ni sunna kuzisoma kama kunuti ni:
“Mola wetu! Usizipotoshe nyoyo zetu baada ya kutuongoza na utupe rehema itokayo Kwako, hakika Wewe ndiye Mpaji Mkuu.”2
“Mola wetu! Utupe wema duniani na wema katika Akhera na utulinde na adhabu ya moto.”3
TASHAHHUD:
Tashahud ni wajibu katika rakaa ya pili baada ya kufanya sijda mbili, na pia katika rakaa ya mwisho ya kila sala, kwa kusema:
أشْهَدُ أنْ لَا إلهَ إلّا الله وَحْدَةُ لَا شَرِيْكَ لَهُ وَأشْهَدُ أنَ مُحَمَّدًا عَبْدُةُ وَرَسُوْلُهُ.
اللهم صَلَّ عَلَي مُحَمَدٍ وَ اَلِ مُحَمَدٍ.
“Ashhadu an lailaha illa llahu wahdahu la shariikalahu, waashhadu anna Muhammadan abduhu warasuuluhu, Allahumma swalli ala Muhammadin waali Muhammadin”.
Dhikri ya tashahhud lazima isomwe katika hali ya kukaa na kunyooka na utulivu.
Kabla ya tashahhud ni sunna kusema: “Alhamdulillah” au “Bismillah wabillah, walhamdulillah, wakhayrul-asmai lillah”.
KUTOA SALAMU:
Swalam ni wajibu katika rakaa ya mwisho baada ya tashahhud, ambapo kwayo, hupata kuhalalika matendo yaliyo nje ya sala, tamko lake ni kama ifuatavyo:
السَلَامُ عَلَيْكَ أيَّهَا النَبِيُ وَرَحْمَهُ الله وَبَرْكَاتُهُُ
As-Salaam Alayka Ayyuhan-Nabiyyu Warahmatullahi Wabarakatuhu.
السَلَامُ عَلَيْنا وَعَلَي عِبَادِ الله الصَالِحِيْنَ
As-Salaam alayna waala ibaadillahi As-Swalihiin.
السَلَامُ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَهُ الله وَبَرْكَاتُهُُ
As-Salaam alaykum warahmatullah wabarakatuhu.
ZINGATIA:
i. Iliyo wajibu ni moja kati ya salam mbili: Ya pili au ya tatu. Ama ya kwanza yenyewe ni sunna.
ii. Ni lazima kusoma salam katika hali ya kukaa, kunyooka na kutulia. iii. Ni sunna kukaa mkao wa tawarruki.4
MFULULIZO:
Nao ni muda kati ya kitendo kimoja na kingine kati ya vitendo vya sala usiwe mrefu sana kiasi cha kuiharibu sala.
UTARATIBU:
Ni wajibu kufuata utaratibu katika vitendo vya sala kwa kuanza takbira ya kuhirimia kabla ya kisomo, na Alhamdu kabla ya sura kamili, na sura kabla ya rukuu, na rukuu kabla ya sijda na kuendelea, hivyo mwenye kutanguliza kitendo kinachofuatia kabla ya kitendo kinachotangulia, au nguzo inayofuatia kabla ya ile inayotangulia, basi sala yake itakuwa batili.
NAMNA YA KUSALI
Baada ya Adhana na kukimu, ambavyo ni sunna zilizotiliwa mkazo kuzifanya kabla ya sala, huanza matendo yafuatayo:
1. Nia: Ni kukusudia moyoni kufanya tendo la sala kama ifuatavyo: Ninasali faradhi ya sala ya Subhi au Dhuhri au Alasiri au Maghrib au Isha kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Si lazima kuitamka bali kusudio la moyoni linatosha.
2. Takbira ya kuhirimia: Yenyewe husomwa mara baada ya nia kwa kusema “Allahu Akbar”. Ambapo ni sunna kuinua mikono mpaka usawa wa masikio, ni lazima uanzaji wa kuinua mikonouende sanjari na uanzaji wa tamko, na umalizike sanjari na tamko hilo,
3. Kisomo: Nako ni kusoma katika rakaa mbili za mwanzo sura Alhamdu kisha sura nyingine kamili kama vile sura Ikhlas au yoyote ile, ukiwa katika hali ya kusimama na mnyoofu,
4. Rukuu: Baada ya kumaliza kisomo, inama kwa ajili ya rukuu na useme: “Sub’hana rabbiyal Adhiim wabihamdihi," kama inavyoonekana katika picha.
5. Baada ya hapo, inua kichwa chako toka kwenye rukuu usimame ukiwa mnyoofu, kisha useme: “Samiallahu liman hamidah” kama inavyoonekana katika picha. Kisha utasubiri kidogo kabla ya kwenda kusujudu.
6. SIJDA MBILI: Baada ya kutoka kwenye rukuu, tunaporomoka kwenda kusujudu kwa kuweka viungo saba vya sijda juu ya ardhi na kusema: “Sub’hana rabiyal-Aala wabihamdihi”, Kisha tunainua kichwa kutoka kwenye sijda ya kwanza na kutulia kidogo, kisha tunasema: “Allahu Akbar”. Kisha tunakwenda kusujudu kwa mara nyingine kwa kufanya kama tulivyofanya katika sijda ya kwanza na kusoma tuliyosoma katika sijda ya kwanza, kama inavyoonekana katika picha.
7. RAKAA YA PILI NA KUNUTI: Baada ya sijda ya pili katika rakaa ya kwanza, tunasimama wima kwa unyoofu kwa ajili ya kuanza rakaa ya pili, kisha tunasoma sura Alhamdu pamoja na sura kamili nyingine yoyote ile, kama tulivyofanya katika rakaa ya kwanza, kisha tunainua mikono na kuomba dua yoyote ile, au zile zilizopendekezwa.
8. TASHAHHUD: Kisha baada ya kunuti tunarukuu kama tulivyorukuu katika rakaa ya kwanza, kisha tunainuka toka kwenye rukuu na kusimama wima kwa unyoofu kama rakaa ya kwanza, ndipo tunafanya sijda mbili kama tulivyofanya katika rakaa ya kwanza, kisha baada ya sijda mbili tunakaa kwa ajili ya tashahhud na kusema:
أشْهَدُ أنْ لَا إلهَ إلّا الله وَحْدَةُ لَا شَرِيْكَ لَهُ وَأشْهَدُ أنَ مُحَمَّدًا عَبْدُةُ وَرَسُوْلُهُ.
اللهم صَلَّ عَلَي مُحَمَدٍ وَ اَلِ مُحَمَدٍ.
“Ashhadu an lailaha illa llaha wahdahu la shariikalahu, waashhadu anna Muhammadan abduhu warasuuluhu, Allahumma swalli ala Muhammadin waali Muhammadin”
Vilevile ni lazima kufanya tashahhud katika rakaa ya mwisho ya kila sala.
9. Tasbihi nne au sura: Baada ya Tashahuud tunasimama wima kama mwanzo kwa ajili ya rakaa ya tatu, na hapo tutasoma sura Alhamdu peke yake au tasbihi nne kwa kusema: “Subhanallah, walhamdulillah, walailaaha illa llah, wallahu akbar” mara moja na vizuri zaidi ni mara tatu
10. Kutoa Salaam: Baada ya kumaliza tasbihi nne au sura Alhamdu, tunafanya rukuu na kisha kusujudu kama tulivyofanya katika rakaa ya kwanza, kisha tutasimama kwa ajili ya rakaa ya nne na kufanya kama tulivyofanya katika rakaa ya tatu kwa kusoma sura Alhamdu au tasbihi nne, na kisha kurukuu na kufanya sijda mbili na kukaa kitako kwa ajili ya tashahhud, na kisha tutatoa salaam kwa kusema:
السَلَامُ عَلَيْكَ أيَّهَا النَبِيُ وَرَحْمَهُ الله وَبَرْكَاتُهُُ
As-Salaam Alayka Ayyuhan-Nabiyyu Warahmatullahi Wabarakatuhu.
السَلَامُ عَلَيْنا وَعَلَي عِبَادِ الله الصَالِحِيْنَ
As-Salaam alayna waala ibaadillahi As-Swalihiin.
السَلَامُ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَهُ الله وَبَرْكَاتُهُُ
As-Salaam alaykum warahmatullah wabarakatuhu.
UFAFANUZI:
Utaratibu tuliouelezea ni wa Sala ya rakaa nne, kama vile Adhuhuri, Alasiri na Isha.
Ama kwa upande wa Sala ya rakaa mbili kama vile Subhi, baada ya kumaliza tashahhud katika rakaa ya pili atasoma salam na kumaliza Sala.
Ama kama Sala itakuwa ya rakaa tatu, kama vile sala ya Maghribi, baada ya kumaliza tashahhud katika rakaa ya pili atasimama wima mnyoofu kwa ajili ya rakaa ya tatu, na baada ya kumaliza rukuu na sijda mbili, atafanya tashahhud na hatimaye atatoa salaam, hapo atamaliza Sala yake.
VIBATILISHI VYA SALA:
i. Chochote kinachotengua udhu miongoni mwa vitenguzi vyake, kama vile kutokwa na mkojo au upepo.
ii. Kula na kunywa.
iii. Kucheka kwa sauti kwa makusudi.
iv. Kila kinachofuta sura ya Sala kwa makusudi au kusahau, kama vile kucheza na kupiga makofi.
v. Kugeuka sana kutoka kwenye uelekeo wa Kibla, kwa makusudi au kusahau.
vi. Kuzungumza kwa makusudi ndani ya sala.
vii. Kufunga mikono makusudi, nako ni kuuweka mmoja juu ya mwingine wakati wa hali ya kisimamo.
viii. Kulia makusudi kwa ajili ya jambo la kidunia, na wala hakuna tatizo kulia kwa jambo la Akhera.
ix. Kubatilika moja ya masharti ya Sala ukiwa tayari ndani ya sala.
x. Kutilia shaka katika idadi ya rakaa za Sala za Subhi na Maghrib, halikadhalika kutilia shaka katika rakaa mbili za mwanzo katika sala yenye rakaa nne.
xi. Kutilia shaka katika idadi ya rakaa ambazo hazina ufumbuzi wa kisharia, kama vile kutilia shaka baina ya nne na sita.
xii. Kuongeza au kupunguza nguzo kwa makusudi au kusahau.
xiii. Kuongeza au kupunguza kwa makusudi wajibu usiyokuwa nguzo ndani ya Sala.
xiv. Kugeuka mwili wote kwa makusudi kwa namna inayomtoa katika Kibla.
xv. Kusema: “Amiin” kwa makusudi baada ya sura Alhamdu.
xvi. Kila kinachobatilisha josho, kama kutokwa na manii kwa mara nyingine.
REJEA:
• 1. Sura Al-Haj: 77
• 2. Sura Al Imran: 8.
• 3. Sura Al-Baqarah: 201.
• 4. Mkao wa tawarrukk ni mkao wakuweka matako chini bila kukalia visigino vya guu-Mhariri
MWISHO WA MSURURU WA MAKALA HIZI ZA: SWALA NI NGUZO YA DINI