Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

NABII NUUH A.S.

1 Voti 03.0 / 5

NABII NUUH A.S.

Hapo zamani palikuwapo na watu watano walioishi katika nchi ya baina ya mito miwili nayo hivi sasa inaitwa nchi ya Iraq. Hawa watu walikuwa wema wakimuabudu Mwenyezi Mungu mmoja na wakiisimamia mipaka Yake kwa watu; na wakiwafanyia watu wema na ihsani. Ukaendelea vizuri mwendo wao na kujulikana sifa zao nzuri. Watu wakawapenda sana; na ikafika ajali yao wakafa wote. Watu wakawahuzunikia sana baadaye wakaanza kufikiri jinsi ya kuwakumbuka daima, mmoja wao akasema wachoreni ili tupate kuwakumbuka na tukumbuke ile ibada yao ya Mwenyezi Mungu S.W.T. na tutabakia katika hali hiyo. Kisha wakawachora vikapita vizazi wakasahau sababu ya kuwachora wakakumbuka tu ibada na kuzitukuza hizo picha.

Wakachonga masanamu akaja adui Shetani akawafundisha jinsi ya kuyatukuza na kuyaabudu masanamu hayo yaliyotengenezwa kwa mikono yao. Wakapotezwa na Shetani na kuwakhadaa kwamba ati wale watu waliopita kabla yao walikuwa wakiyatumia hayo masanamu kwa kuombea mvua, kheri na wakiyaabudu.

Pole pole ikaanza kuingia ile ibada katika nyoyo zao mpaka ikawaingia barabara na wakabadili kutoka katika ibada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu mpaka ibada ya kuyaabudu masanamu. Ambayo yaliitwa kwa yale majina ya watu watano waliokufa: Waddi, Suwaa, Yaghutha, Ya`uqa na Nasra. Wakaendelea hivyo vizazi na vizazi katika ujinga na kufuru na upotofu. Lakini Mola wa walimwengu wote hawaachi watu wakapotea bila kuwaongoza. Kwa hivyo akawatumia Nabii Nuuh A.S. bin Laamik ambaye aliyezaliwa baada ya kufa Nabii Adam kwa miaka 10,000. Alikuwa Mtume wa kwanza kutumwa ulimwenguni ili awatoe watu wake katika upotofu na awaonye adhabu ya Mola Mtukufu ikiwa watamkanusha. Kama ilivyokuja katika Surat Huud aya ya 25 na ya 26, "

إِنِّي لَكُمْ نَذِيرٌ مُبِينٌ * أَنْ لاَ تَعْبُدُوا إِلاَّ اللَّهَ

Maana yake, "…Mimi kwenu ni Muonyaji anayebainisha (kila kitu). Ya kwamba msimuabudu yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu tu…" Wale watu wake walimjibu "Kwa nini tumuabudu unayetuitia na kuacha tuliorithi kwa baba zetu na tuliyowakuta nayo wakiyaabudu?" Nabii Nuuh akawajibu kama ilivyokuja katika Surat Huud aya ya 26, "

إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ أَلِيمٍ

Maana yake, "…Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya siku chungu." Kama ilivyo desturi ya historia ya binadamu, wale matajiri waliendelea na upotofu wao na wakajivuna kwa kujiona katika nafsi zao kwamba wao ni wenye mali na watoto hivyo wakakataa kumfuata Mtume wao.

Isipokuwa mafakiri waliokuwa wakitaraji Rehema za Mola wao ndio waliokuwa watu wa kwanza kumfuata Nabii Nuuh. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Huud aya ya 27, "

فَقَالَ الْمَلأ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ قَوْمِهِ مَا نَرَاكَ إِلاَّ بَشَرًا مِثْلَنَا وَمَا نَرَاكَ اتَّبَعَكَ إِلاَّ الَّذِينَ هُمْ أَرَاذِلُنَا بَادِي الرَّأْيِ

Maana yake, "Na hapo wakasema wakubwa wa wale waliokufuru katika kaumu yake: "Hatukuoni ila ni mtu sawa na sisi; wala hatukuoni ila wamekufuata wale wanaoonekana dhahiri kuwa ni dhaifu (wanyonge) wetu; (wamekufuata) kwa fikira ya mwanzo tu (bila kupeleleza vizuri)…"

Wale watu matajiri walijitukuza katika nafsi zao wakawadharau Waislamu mafakiri wakasema: "Vipi watakuamini watu walio na mfano kama wewe?" Wakifikiri kwamba Mtume anayetumwa lazima awe na umbo kubwa au tajiri au Malaika kinyume na binadamu wengine. Na awaite matajiri na watu wakubwa tu wala asizungumze na watu mafakiri.

Kwa fikira zao kwamba watu mafakiri hawana thamani katika mikutano yao wala hawastahiki kuheshimiwa, kufadhiliwa na kukirimiwa. Kama ilivyokuja katika Surat Huud aya ya 27, "

وَمَا نَرَى لَكُمْ عَلَيْنَا مِنْ فَضْلٍ بَلْ نَظُنُّكُمْ كَاذِبِينَ

Maana yake, "…Wala hatukuoneni kuwa mna ubora wowote kutushinda sisi. Bali tunahakika nyinyi ni waongo." Nabii Nuuh A.S. akawajibu akasema: "Mbona hamuoni utume na ujumbe niliopewa na Mola wangu? Na kwa nini hamfahamu uwongofu? Au tukulazimisheni na vipi tutakulazimisheni na hali nyinyi wenyewe mnachukia? Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kauli ya Nabii Nuuh katika Surat Huud aya ya 28, "
يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِنْ كُنتُ عَلَى بَيِّنَةٍ مِنْ رَبِّي وَآتَانِي رَحْمَةً مِنْ عِنْدِهِ فَعُمِّيَتْ عَلَيْكُمْ أَنُلْزِمُكُمُوهَا وَأَنْتُمْ لَهَا كَارِهُونَ

Maana yake, "Enyi watu wangu! Hebu fikirini! Ikiwa mimi ninayo hoja wazi iliyotoka kwa Mola wangu, na amenipa rehema kutoka Kwake, nayo ikakufichikieni; jee, tukulazimisheni kuikubali hali nyinyi mnaichukia?"

Nabii Nuuh aliendelea na wito wake wa mara kwa mara bila kuchoka akipita na kuwasisitiza wamuabudu Mola wao na wamtii. Kama ilivyobainishwa katika Surat Nuuh tokea aya ya 3 mpaka aya ya 4, "

أَنْ اعْبُدُوا اللَّهَ وَاتَّقُوهُ وَأَطِيعُونِي * يَغْفِرْ لَكُمْ مِنْ ذُنُوبِكُمْ وَيُؤَخِّرْكُمْ إِلَى أَجَلٍ مُسَمًّى إِنَّ أَجَلَ اللَّهِ إِذَا جَاءَ لا يُؤَخَّرُ لَوْ كُنتُمْ تَعْلَمُون
َ
Maana yake, "Ya kwamba mumuabudu Mwenyezi Mungu na mcheni Yeye na mumtii. Atakusameheni madhambi yenu, na atakuakhirisheni (bila balaa) mpaka muda uliowekwa. Hakika muda wa Mwenyezi Mungu utakapofika haucheleweshwi. Laiti mngejua!" Lakini wapi! Waliukataa wito huo walioitiwa na wakakataa kuamini bila kujali lile onyo la adhabu kali litakalowapata ikiwa hawataamini; pia hawakujali zile kheri walizoahidiwa ikiwa wataamini.

Akawa Nabii Nuuh akirudia wito wake mara kwa mara lakini hata hivyo haikuwazidishia ila kukimbia; ikafikia hadi kuziba masikio yao kwa vidole vyao ili wasimsikie na kupandisha nguo zao ili wazifunike nyuso zao wasimwangalie Nabii Nuuh. Nabii Nuuh alipoona hivyo, akainua kichwa chake mbinguni akimuomba Mola wake amsaidie. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Nuuh aya ya 5 hadi ya 7, "

قَالَ رَبِّ إِنِّي دَعَوْتُ قَوْمِي لَيْلاً وَنَهَارًا * فَلَمْ يَزِدْهُمْ دُعَائِي إِلاَّ فِرَارًا * وَإِنِّي كُلَّمَا دَعَوْتُهُمْ لِتَغْفِرَ لَهُمْ جَعَلُوا أَصَابِعَهُمْ فِي آذَانِهِمْ وَاسْتَغْشَوْا ثِيَابَهُمْ وَأَصَرُّوا وَاسْتَكْبَرُوا اسْتِكْبَارًا

Maana yake, "Akasema (Nabii Nuuh): "Ee Mola wangu! Kwa hakika mimi nimewaita watu wangu usiku na mchana. Lakini wito wangu haukuwazidisha ila kukimbia. Na hakika mimi kila nilipowaita ili upate kuwasamehe, walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na walijifunika nguo zao (gubigubi), na walizidi kuendelea (na kufuru) na wakafanya kiburi kingi."

Ingawa watu wake walimfanyia mabaya Nabii Nuuh lakini yeye hakukata tamaa bali aliendelea na wito wake akawa anasimama kwenye mkusanyiko wao na kwenye nadi zao akiwalingania kwa sauti ya juu halafu akawa akimwita mmoja mmoja kwa siri. Lakini pia haikusaidia kitu wala hawakumuamini, kwani matajiri walikhofia pengine huenda wakiamini watapoteza vyeo vyao na mali yao ikachukuliwa na Waislamu walioamini. Nabii Nuuh akawakumbusha vitu wavipendavyo duniani akasema kuwaambia: "Mwenyezi Mungu S.W.T. atawaletea mvua nyingi, atawazidishieni mali, watoto, mabustani na mito."

Ili labda akiwatajia zile neema za duniani watapata kumuamini. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kauli ya Nabii Nuuh katika Surat Nuuh tangu aya ya 8 hadi ya 12, " B

ثُمَّ إِنِّي دَعَوْتُهُمْ جِهَارًا * ثُمَّ إِنِّي أَعْلَنتُ لَهُمْ وَأَسْرَرْتُ لَهُمْ إِسْرَارًا * فَقُلْتُ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا * يُرْسِلْ السَّمَاءَ عَلَيْكُمْ مِدْرَارًا * وَيُمْدِدْكُمْ بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَيَجْعَلْ لَكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَلْ لَكُمْ أَنْهَارًا

Maana yake, "Tena niliwaita kwa uwazi. Kisha nikawatangazia kwa kelele, tena nikasema nao kwa siri. Nikawaambia: "Ombeni msamaha kwa Mola wenu. Hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe. Atakuleteeni mvua inyeshe mfululizo. Na atakupeni mali na watoto, na atakupeni mabustani na atakufanyieni mito."

Nabii Nuuh hakukata tamaa bali aliendelea na kuwaonesha alama za Mwenyezi Mungu S.W.T. katika nafsi zao na katika ulimwengu na siku ya Kiyama ambayo watahukumiwa. Kama alivyotuambia Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kauli ya Nabii Nuuh katika Surat Nuuh aya ya 13 hadi ya 20, "

مَا لَكُمْ لاَ تَرْجُونَ لِلَّهِ وَقَارًا * وَقَدْ خَلَقَكُمْ أَطْوَارًا * أَلَمْ تَرَوْا كَيْفَ خَلَقَ اللَّهُ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقًا * وَجَعَلَ الْقَمَرَ فِيهِنَّ نُورًا وَجَعَلَ الشَّمْسَ سِرَاجًا * وَاللَّهُ أَنْبَتَكُمْ مِنْ الأَرْضِ نَبَاتًا * ثُمَّ يُعِيدُكُمْ فِيهَا وَيُخْرِجُكُمْ إِخْرَاجًا * وَاللَّهُ جَعَلَ لَكُمْ الأَرْضَ بِسَاطًا * لِتَسْلُكُوا مِنْهَا سُبُلاً فِجَاجًا

Maana yake, "Mna nini hamuweki heshima ya Mwenyezi Mungu? Na hali Yeye kakuumbeni daraja baada ya daraja? Kwani hamuoni jinsi Mwenyezi Mungu alivyoziumba mbingu saba kwa matabaka (moja juu ya moja)? Na akaufanya mwezi ndani yake uwe nuru na akalifanya jua kuwa taa? Na Mwenyezi Mungu amekuotesheni katika ardhi, kama mimea. Kisha atakurudisheni humo na atakutoeni tena. Na Mwenyezi Mungu amekukunjulieni ardhi kuwa kama busati. Ili mtembee humo katika njia zilizo pana."

Akarejea Nabii Nuuh kumuomba Mola wake juu ya watu wake, lakini watu wake kila siku walizidi kuendelea katika maasi na kufuru na wakazidisha ukaidi wao. Kama alivyotuhadithia Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kauli ya Nabii Nuuh katika Surat Nuuh aya ya 21 hadi ya 22, "

قَالَ نُوحٌ رَبِّ إِنَّهُمْ عَصَوْنِي وَاتَّبَعُوا مَنْ لَمْ يَزِدْهُ مَالُهُ وَوَلَدُهُ إِلاَّ خَسَارًا * وَمَكَرُوا مَكْرًا كُبَّارًا

Maana yake, "(Nabii) Nuuh akasema: "Mola wangu! Hakika hao wameniasi na wamemfuata yule ambaye mali yake na watoto wake hawakumzidishia ila khasara. Na wakafanya hila kubwa kubwa (za kubatilisha dini)."

Watu wa Nuuh wakasimama msimamo wa mtu mmoja, wakiyalinda masanamu yao Waddi, na Suwaa, na Yaghutha, na Ya`uqa na Nasra; wakawatisha wale walioamini wasiifuate dini ya Nabii Nuuh bali waabudu miungu yao na miungu ya baba zao. Kama alivyotusimulia Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Nuuh aya ya 23 na ya 24, "

وَقَالُوا لاَ تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلاَ سُوَاعًا وَلاَ يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا * وَقَدْ أَضَلُّوا كَثِيرًا وَلا تَزِدْ الظَّالِمِينَ إِلاَّ ضَلالاً

Maana yake, "(Na ambao waliwaambia wafuasi wao): "Msiwaache miungu yenu, wala msimwache Wadda wala Suwaa wala Yaghutha wala Ya`uqa wala Nasra. (Majina ya waungu wao wa kisanamu). Na hao walikwishawapoteza (watu) wengi, wala usiwazidishie waliodhulumu ila kupotea."

Wale watu matajiri walipokuja kwa Nabii Nuuh wakamuona anazungumza na watu mafakiri, wakaanza kumcheka na huku wakimwambiya: "Wafukuze hawa mafakiri waliokuamini ili sisi matajiri tupate kukuamini." Nabii Nuuh akawajibu: "Ikiwa macho yenu hayaoni uwongofu mimi siwezi kukulazimisheni kuamini. Msifikiri mimi nina tamaa ya mali yenu. Sina ujira wangu isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu; wala mimi sitawafukuza hawa walioamini kama jinsi mnavyotaka nyinyi ili msilimu. Kwani nikifanya hivyo Mola atanisimamisha mbele Yake siku ya Kiyama na atanihukumu na kunihesabu na zaidi ya hivyo hilo jambo si katika njia ya imani." Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T.

kwa kauli ya Nabii Nuuh katika Surat Huud aya ya 29 na ya 30, "

وَيَا قَوْمِ لاَ أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مَالاً إِنْ أَجْرِي إِلاَّ عَلَى اللَّهِ وَمَا أَنَا بِطَارِدِ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّهُمْ مُلاقُو رَبِّهِمْ وَلَكِنِّي أَرَاكُمْ قَوْمًا تَجْهَلُونَ  وَيَاقَوْمِ مَنْ يَنصُرُنِي مِنْ اللَّهِ إِنْ طَرَدْتُهُمْ أَفَلا تَذَكَّرُونَ

Maana yake, "Na enyi watu wangu! Mimi sikuombeni mali kwa ajili ya haya. Mimi sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu; na mimi sitawafukuza walioamini (kama mlivyotaka kwangu niwafukuze hao madhaifu ndipo msilimu nyinyi watukufu. Sitafanya hivyo). Hakika wao watakutana na Mola wao (awalipe kwa mema yao na mabaya), lakini mimi nakuoneni nyinyi ni watu mnaofanya ujinga. (Mnakataa kuifuata haki kwa kuwa imefuatwa na madhaifu)! Na enyi watu wangu! Ni nani atakayenisaidia kwa Mwenyezi Mungu nikiwafukuza hawa? Jee, hamfikiri?"

Watu wake wakamwambiya Nabii Nuuh: Wewe unatuahidi mvua, mito, mali na watoto basi hebu tuletee tuone ikiwa wewe unamiliki hayo uliyotuahidi. Nabii Nuuh akawajibu kama ilivyokuja katika Surat Huud aya ya 31, "

وَلاَ أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَائِنُ اللَّهِ وَلاَ أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلا أَقُولُ إِنِّي مَلَكٌ وَلا أَقُولُ لِلَّذِينَ تَزْدَرِي أَعْيُنُكُمْ لَنْ يُؤْتِيَهُمْ اللَّهُ خَيْرًا اللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا فِي أَنفُسِهِمْ إِنِّي إِذًا لَمِنْ الظَّالِمِينَ

Maana yake, "Wala sikwambieni kuwa nina khazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi najua mambo ya siri; wala sisemi, "Mimi ni Malaika." Wala sisemi wale ambao yanawadharau macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri. Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo katika nafsi zao. (Nikisema hivi) hapo bila shaka ningekuwa miongoni mwa wenye kudhulumu."

Watu wa Nuuh wakadhikika kwa wito wake na wakachokeshwa na maonyo ya ile adhabu aliyowaahidi kisha wakasema: "Wewe kila siku unatuahidi kwa adhabu basi tuletee hiyo adhabu kama wewe ni mkweli." Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Huud aya ya 32, "

قَالُوا يَانُوحُ قَدْ جَادَلْتَنَا فَأَكْثَرْتَ جِدَالَنَا فَأْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِنْ كُنتَ مِنْ الصَّادِقِينَ

Maana yake, "Wakasema (watu wa Nabii Nuuh): "Ewe Nuuh! Umejadiliana nasi na umezidisha kutujadili. Basi tuletee unayotuahidi (kuwa tutaadhibiwa), ukiwa miongoni mwa wasemao kweli."

Lakini Nabii Nuuh akawajibu: "Si mimi ninayekuahidini kuwaadhibu wala si mimi nitakayekuleteeni hiyo adhabu bali Mola wenu Ndiye atakayekuadhibuni." Kama alivyosema katika Surat Huud aya ya 33, "

قَالَ إِنَّمَا يَأْتِيكُمْ بِهِ اللَّهُ إِنْ شَاءَ وَمَا أَنْتُمْ بِمُعْجِزِينَ

Maana yake, "Akasema (Nabii Nuuh): "Mwenyezi Mungu atayaleta kwenu akipenda, na nyinyi hamtaweza kumshinda." Watu wa Nabii Nuuh walimcheka alipowajibu hivyo, wakasema: "Huyu Nuuh ni mtungaji wa maneno haya." Nabii Nuuh akawajibu kama ilivyokuja katika Surat Huud aya ya 35, "

إِنْ افْتَرَيْتُهُ فَعَلَيَّ إِجْرَامِي وَأَنَا بَرِيءٌ مِمَّا تُجْرِمُونَ

Maana yake, "…Ikiwa nimeizua kauli hii, basi kosa hilo ni juu yangu (mwenyewe haikukhusuni kitu), na mimi sikhusiki na makosa myatendayo."

KUAMRISHWA KUTENGENEZA JAHAZI.

Nabii Nuuh akaamrishwa na Mola wake S.W.T. aliunde jahazi; na hilo jahazi atakaloliunda liwe sawa na jinsi alivyoamrishwa (kama vile jinsi alivyomfunulia wahyi). Na hukumu ya Mwenyezi Mungu S.W.T. ikapitishwa ya watu wa Nuuh kugharikishwa. Na inasemekana Mwenyezi Mungu S.W.T. akawajaalia wake zao hawakuzaa hata mtoto mmoja kwa muda wa miaka arubaini. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema kumwamrisha Nabii Nuuh katika Surat Huud aya ya 37, "

وَاصْنَعْ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا

Maana yake, "Na unda jahazi mbele ya macho yetu (yaani katika hifdhi yetu, hawataweza kukudhuru) na (iwe sawa na) amri yetu (wahyi tuliyokuletea)…"

Nabii Nuuh akaanza kuunda jahazi kwa mbao na misumari kama alivyoamrishwa na Mola wake. Wakati watu wake walipomuona Nabii Nuuh akiunda lile jahazi katika nchi kavu walimcheka na kumwambiya: "Ewe Nuuh! Umekuwa fundi seremala baada ya kuwa Mtume." Na wengineo walipomuona akiunda jahazi na hali kabla ya hapo hawajaona jahazi waliuliza wakasema: "Ewe Nuuh! Unaunda kitu gani?" Nabii Nuuh aliwajibu: "Naunda nyumba itakayokwenda kwenye maji." Walishangaa kusikia kauli yake hiyo kisha walimfanyia maskhara wakasema: "Jee, hamumuoni huyu mwehu ati anadai anaunda nyumba ambayo itakwenda kwenye maji?" Lakini Nabii Nuuh alikuwa akiwajibu kama ilivyokuja katika Surat Huud aya ya 38, "

قَالَ إِنْ تَسْخَرُوا مِنَّا فَإِنَّا نَسْخَرُ مِنْكُمْ كَمَا تَس ْخَرُونَ

Maana yake, "…Ikiwa nyinyi mnatucheka (hivi sasa), nasi pia tutakuchekeni (baadaye) kama mnavyotucheka." Nabii Nuuh aliendelea kuwajibu: "Kwa vile sisi tunafahamu na nyinyi hamfahamu chochote basi mtakuja jua kwa nini likaundwa hili jahazi na nani itakayemjia adhabu ya duniani ya kugharikishwa na adhabu ya Akhera ya kuingia Motoni milele."

Kama alivyowaambia Nabii Nuuh kwa kauli ya Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Huud aya ya 39, "

فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ مَنْ يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ وَيَحِلُّ عَلَيْهِ عَذَابٌ مُقِيمٌ

Maana yake, "Karibuni hivi mtajua ni nani itakayemjia adhabu ya kumfedhehesha, na itakayemteremkia adhabu ya kudumu."

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini