Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S) 3

0 Voti 00.0 / 5

HISTORIA YA MASUMIN (A.S).

MA'ASUMAH WA PILI

2. BIBI FATIMAH ZAHARA (A.S).

Sehemu ya tatu

FATIMAH ZAHARA NDANI YA QURAN

3. Aya ya maapizano

Tarehe ishirini na nane mfunguo wa tatu (Dhul Hijja) mwaka wa tisa hijiria ulikuja ujumbe wa Kikristo wenye watu sitini kutoka Najran katika nchi ya Yemen ukiongozwa na makasisi watatu, Al A'aqib, Al Asqaf na Muhsin. Walikuja Madina kwa ajili ya majadiliano juu ya Issa as, je ni mwana wa Mungu au ni Mungu mwenyewe?

Mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo:

Asqaf:- Ewe Baba Qasim! Yule Musa baba yake alikuwa Anaitwa nani?

Mtukufu Mtume saww akajibu: Imrana.

Asqaf: Na Yusufu nani baba yake?

Mtukufu Mtume saww: Yaaqubu

Asqaf: Natoa fidia kwako baba yangu na mama yangu wewe baba yako ni nani?

Mtukufu Mtume saww: Abdullah bin Abdul Mutwalibi

Asqaf: Na Issa baba yake ni nani?

Mtukufu Mtume saww akanyamaza kidogo, mara akashuka Jibrilu as na kumwambia akasema: Huyu ni Roho kutoka kwa Mwenyezi Mungu na neno lake.

Asqaf: Inawezekana Roho itoke kwa Mwenyezi Mungu bila kiwiliwili?

Mtukufu Mtume saww akanyamaza, Mwenyezi Mungu akamfunulia Mtume wake (s.a.w.w):

إِنَّ مَثَلَ عِيسَىٰ عِندَ اللَّـهِ كَمَثَلِ آدَمَ ۖ خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُن فَيَكُونُ .

Hakika mfano wa Issa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam, alimuumba kwa udongo, kisha akamwambia kuwa, basi akawa. 3:59.

Asqaf akaruka kwa mshangao eti Issa anatokana na udongo!?

Asqaf: Ewe Muhammad haya unayo yasema hatujayaona ndani ya Tawrat Injili wala Zaburi hatujayakuta haya isipokuwa kwako.

Walipotaka kuendelea na majadiliano haya, Mwenyezi Mungu akamfunulia tena Mtume wake (s.a.w.w):

فَمَنْ حَاجَّكَ فِيهِ مِن بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءَنَا وَنِسَاءَكُمْ وَأَنفُسَنَا وَأَنفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَل لَّعْنَتَ اللَّـهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ .

Na atakaye bishana nawe  katika hili (la Issa) baada ya ujuzi uliokuijia, basi waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu, na nafsi zetu na nafsi zenu, kisha tuombe kwa unyenyekevu na tuiweke laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie wenye kusema uongo. 3:61.

Wakristo waliposikia kuna kuapizana ili kupata waongo dhidi ya wakweli, wakawashauri Viongozi wao jambo hili, Askofu Asqaf akajibu akawaambia  ngoja nione atakuja na nani?

Mtukufu Mtume Muhammad saww alipomaliza sala ya asubuhi Alimshika Ally mkono akamtanguliza akamchukua Fatimah as akawawafuata nyuma yao, akamchukua Hassan as kuliani na Hussein kushotoni, akawaambia nikiomba semeni Amina!!!.

Askofu Asqaf, alipowaona tu akawaambia wenzake Enyi Wakristo mimi naziona nyuso hizi (kundi la Muhammad s.a.w.w) kama zitamuomba Mwenyezi Mungu auondoe mlima kutoka mahala pake Wallahi atauondoa. Msiapizane naye mtaangamia, na hatabaki mkirsto yeyote hapa duniani hadi siku ya kiyama.

Naye Askofu Ahtamu akawaambia niacheni nikamuulize Muhammad ; alipomkabili Mtume saww akamuuliza: Ewe Abul Qasim unatoka na akina nani kwa ajili ya maapizano?

Mtukufu Mtume saww akajibu ninaapizana nanyi nikiwa na watu wabora na watukufu hapa duniani na watukufu mno mbele ya Mwenyezi Mungu nao ni hawa (akawaonyesha) Ally bin Abi Twalib as, Fatima bint Muhammad as, Hassan na Hussein (a.s).

Alipoulizwa Askofu Al A'aqib ambaye ndiye mwenyekiti wa ujumbe huo, akawaambia hawa (watano, Muhammad na kikosi chake) ndiyo waliotajwa ndani ya Tawrat, Injili na Zaburi, Enyi Wakristo Wallahi nyinyi mnajua Muhammad ni Nabii aliyeletwa na amekuja na ushahidi uliowazi juu ya jambo la huyu Issa. Wallahi hakuna watu walioapizana na Nabii wakasalimika kama mtaapizana naye mtaangamia.

Kikosi alichoandaa Mtume Muhammad saww Fatumah, mtoto wake aliwakilisha wanawake wote kwa sababu yeye ndiye mwanamke bora na mtukufu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Tukio hili la maapizano wanazuoni wa ahlisuna wakubwa wakubwa wote wamekiri na kuandika vitabuni mwao.

Mtukufu Mtume saww katika kupanga kikosi chake: Mwenyezi Mungu alipoagiza: tuwaite watoto wetu" Mtume saww akamwita Hassan na Hussein, "Na wanawake wetu" Mtume saww akamwita Fatimah. "Na nafsi zetu" Mtume akamwita Ally, Kisha Mtukufu Mtume (s.a.w.w) akasema: Ewe Mola! Hawa ndio watu wangu.

Wakristo walipo waona wakaogopa kuapizana na Mtukufu Mtume Muhammad saww na badala yake wakaomba suluhu kwa kutoa dirham arobaini elfu kama kodi ya kuishi katika utawala wa Kiislamu kwa amani.

Huyo ndiye Fatimah Zahara ndani ya Quran tukufu na kuna aya zisizopungua mia tatu zinazozungumzia ubora na utukufu wa wa bibi Fatimah as na Ahlul Bayt rasuli kwa ujumla.

Rejea:

 Tafsirul Qurtubi Jz 4 UK 104

Tafsirul Ibn Kathir Jz 1 UK 379

Tafsirul Khazin Jz 1 UK 359 - 360

Albaharul Muhiit Jz 3 UK 189

Fat-hul Qadiiri Jz 1 UK 525

Tafsirul Maraghi Jz 3 UK 175

Tafsirul Kabiri Jz 8 UK 81

Zadul Masiir Jz 1 UK 399

Ruhul Maani Jz 3 UK 301

Fuatana nami sehemu ya nne Hisoria ya Maasumah Fatimah bint Muhammad saww katika hadithi za mtukufu Mtume (s.a.w.w).

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini