KUFUNGUA SAFARINI KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNA
KUFUNGUA SAFARINI KWA MUJIBU WA KITABU NA SUNNAH
Sehemu ya kumi na mbili
KUFUNGA SAUMU YA RAMADHANI SAFARINI KWA MUJIBU WA SUNNAH/HADITHI SAHIHI ZA MTUKUFU MTUME (S.A.W.W).
VIGEZO WALIVYOCHUKUA ILI KURUHUSU SAUMU SAFARINI
Kuna baadhi ya riwaya wanazoshikilia kuthibitisha kuwa kufungua ni ruhusa ya hiyari na kuwa mukallafu ana hiyari ya kufungua au kufunga.
Kabla hatujazama ndani ya uchumbuzi huu tunapenda kumkumbusha msomaji aweze kuangalia mambo matatu kwa makini sana na mwisho itamdhihirikia hali halisi ya riwaya hizo walizozitaja.
Hakika uchambuzi unahusu hukumu ya funga ya mwezi wa Ramadhani safarini, je, kufunga ni lazima au ni ruhusa ya hiyari. Hivyo Saumu nyingine isiyo ya Ramadhani si maudhui ya uchumbuzi wetu, na iko mbali na uchambuzi wetu.
Hakika Mtume saww aliamrisha kufungua ndani ya mwaka wa ukombozi wa Makkah mwaka wa nane hijiria kabla ya hapo hukumu ya Saumu safarini ilikuwa ni ruhusa ya hiyari. Hivyo kama kuna hadithi inayoonyesha ruhusa ya hiyari basi ili isihi inatakiwa iwe ni ya baada ya mwaka wa ukombozi wa Makkah. Ama kinyume na hivyo Itakuwa hadithi hiyo iko nje ya maudhui yetu kwani ruhusa ya kabla ya mwaka wa ukombozi si maudhui ya uchumbuzi wetu.
Na iwapo tukijaalia kuwa riwaya hizo zinaonyesha ruhusa ya hiyari basi kutakuwa na mgongano kati ya zile zinazoamrisha kufungua na hizo zinazoonyesha hiyari. Hivyo ni lazima turejee kwenye vigezo vya ziada, na hapo zitakazoafikiana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu ndipo zitakuwa hoja na dalili na kuwa sio zile zinazopingana na Kitabu.
Hivyo baada ya haya mambo matatu, sasa tunasoma riwaya zinazotoa ruhusa ya hiyari. Tunasema: Hakika riwaya hizo ziko katika makundi.
Kundi (a) Ni riwaya ambazo hazitamki wazi kuhusu mwezi wa Ramadhani.
Bukhari amepokea toka kwa Aisha kuwa Hamza Bin Amru Al Aslamiy alimwambia Mtume saww: Je, nifunge safarini- na alikuwa mwingi wa Saumu - Mtume saww akasema: "Ukitaka funga ukitaka fungua."
Hakika kauli yake: "Na alikuwa mwingi wa Saumu," inafaa kuwa dalili na alama ya kuwa swali lake lilikuwa kuhusu Saumu ya Sunnah.
Na hata kama neno hilo si alama lakini bado hadithi haitamki wazi ni Saumu ya mwezi wa Ramadhani. Na kama hali ndiyo hiyo basi Hadithi hiyo haiwi hoja.
Bukhari amepokea kwa njia yake toka kwa Abdur'dau kuwa amesema: "Tulitoka na Mtume saww katika baadhi ya safari zake, ilikuwa siku ya joto kali mpaka ilifikia mtu anaweka mikono yake juu ya kichwa chake kwa ajili ya ukali wa joto, na hakukuwa na yeyote aliyefunga isipokuwa Saumu ya Mtume saww na Ibn Rawahati.
Anajibiwa kwa jibu lile lililotangulia, nalo ni kuwa riwaya haijadhihirisha kuwa ni Saumu ya Ramadhani, hivyo nayo si hoja. Japokuwa inawezekana Saumu hii ilikuwa kabla ya mwaka wa ukombozi wa Makkah.
Bukhari amepokea toka kwa Anas bin Maalik amesema: "Tulikuwa tukisafiri na Mtume saww, na wala mwenye kufunga hakumkosoa mwenye kufungua wala mwenye kufungua hakumkosoa mwenye kufunga.
Anajibiwa kuwa: Hadithi hii haitamki kuwa ni Saumu ya Ramadhani, kisha kitendo cha Maswahaba kunyamaza si hoja ya kisheria, kwani baada ya Utume wa Mtukufu Mtume Muhammad saww hakuna Utume mwingine mpaka iwe kunyamaza kwao ni hoja. Na pia inawezekana hilo lilitokea kabla ya mwaka wa ukombozi wa Makkah, na tayari umeshaona jinsi Mtume saww alivyowakhalifu waliofunga siku hiyo ya ukombozi wa Makkah na akasema: "Hao ni waasi hao ni waasi.
Muslim amepokea kwa njia yake toka kwa Tausi toka kwa Ibn Abbasi kuwa amesema: "Msimkosoe anayefunga wala anayefungua, kwani hakika Mtukufu Mtume wa Mwenyezi Mungu alifunga safarini na alifungua."
Hadithi hii haitamki wazi mwezi wa Ramadhani wala haionyeshi mwezi huo, japokuwa inawezekana ilikuwa ni kabla ya mwaka wa ukombozi wa Makkah. Na ndiyo hali ya riwaya alizozinukuu Muslim ndani ya Sahihi yake.
Na ni riwaya alizozitaja Ibn Hazmi Andlusiy ndani ya "Al Mahaliy" toka kwa Ally.
Tumeshaona ambazo hazitamki wazi kuhusu mwezi wa Ramadhani na majibu yake
Fuatana nami kwenye uchumbuzi wa riwaya zinazotamka wazi mwezi wa Ramadhani lakini hazitamki kuwa ni baada ya mwaka wa ukombozi wa Makkah.
REJEA:
Sahihi Bukhari Jz 3 UK 43
Sahihi Bukhari Jz 3 UK 43
Sahihi Bukhari Jz 3 UK 44
Sherhu Sahihi Muslim ya An Nawawiy Jz 7 UK 232
Sahihi Muslim Jz 3 UK 143
Sahihi Muslim Jz 3 UK 143
Al Mahaliy ya Ibn Hazmi Andlusiy Jz 6 UK 247.