Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

NDOA YA MTUKUFU FATIMAH ZAHRAA (A.S) 1

0 Voti 00.0 / 5

NDOA YA MTUKUFU FATIMAH ZAHARA (A.S) KUTOKA NYUMBA YA MTUKUFU MTUME SAWW, NA MTUKUFU IMAMU ALLY BIN ABI TWALIB (A.S) MZALIWA KATIKA NYUMBA YA MWENYEZI MUNGU MTUKUFU. 01 Dhul Hijja mwaka wa 2 hijiria

Katika kitabu cha Biharul Anwar, kutoka A'amaliy ya Sheikh Suduuk kwa isnadi yake kutoka kwa Abi Abdillah Ja'afar Sadiq as anasema:  Mtukufu Mtume saww alipotaka kumuoza Fatimah Zahraa as kws Ally bin Abi Twalib as, Mtukufu Mtume saww aliingia kwa Fatimah Zahraa as akamkuta analia. Mtukufu Mtume saww akamwambia unalia nini mwanangu? Wallaahi kama ingekuwa katika Ahlubaiti wangu kuna mtu mbora kumshinda Ally ningekuoza kwake. Sijakuoza mimi, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenyewe kakuozesha na akakutolea mahari ya vitu Vitano madamu mbingu na ardhi zipo.

Mtukufu Mtume saww alipenda hotuba ya ndoa isomwe msikitini na mbele ya mahudhurio ya watu. Imamu Ally as alikwenda pale msikitini kwa furaha sana, na Mtukufu Mtume saww akaingia msikitini mle. Muhajirina na Ansaari wakajikusanya kumzunguka. Mtukufu Mtume saww akaenda juu ya mimbari na baada ya kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema:

Enyi Watu! Jueni kwamba Jibril amenishukia mimi na akaniletea ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwamba Sherehe ya harusi ya Ally na Fatimah Zahraa as zimefanyika mbele ya Malaika huko Baitul Ma'amur (mbingu ya saba)

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameamuru kwamba mimi nifanye Sherehe hizi hapa duniani na niwafanye nyote kuwa ni Mashahidi. Kufikia hapa Mtukufu Mtume saww akasoma hotuba ya ndoa. Halafu Mtukufu Mtume saww akamwambia Ally: Simama na utoe hotuba. Imamu Ally as alianza hotuba yake na akaonyesha kufurahi na kuridhika kwa ndoa yake na Bibi Fatimah Zahraa as.

Watu wakamuombea Ally na wakasema: "Mwenyezi Mungu Mtukufu aibariki ndoa hii, na aweke mapenzi na usuhuba ndani ya nyoyo zenu.

Ndoa hii ilifungwa baada ya vita vya Badr mwaka wa pili hijiria. Pale Mwenyezi Mungu Mtukufu alipowapa ushindi wa kishindo waislamu katika vita vya Badr. Miezi miwili baada ya vita hivyo, Fatimah Zahraa as, bint yake Mtukufu Mtume Muhammad saww na Ally bin Abi Twalib as walifunga ndoa.

Fatimah Zahraa as alikuwa na miaka mitano tu wakati mama yake, Khadija as, alipofariki, na kuanzia hapo na kuendelea, baba yake, Mtukufu Mtume Muhammad saww alichukua wajibu wa kazi za mama pia kwa ajili yake. Kifo cha mama yake kilileta pengo katika maisha yake lakini baba yake alilijaza kwa upendo na huruma.

Mtukufu Mtume Muhammad saww aliweka uangalifu wa hali ya juu kwenye elimu na malezi ya bint yake. Kama alikuwa ndiye mfano bora kwa watu wote, bint yake alikuwa awe mfano bora kwa wanawake wote, na alikuwa hivyo. Alimfanya yeye kuwa mfano bora wa uwanauke katika Uislamu. Alikuwa ni mfano halisi wa ibada na utii kwa Muumba, na alikuwa ni mfano halisi wa usafi wa ki Ungu na utakatifu. Katika tabia na hulka, alikuwa na mfanano unaovutia sana kwa baba yake. Fatimah, bint huyu, alikuwa ni picha ya Muhammad babake.

Kwa kufanya utii na ibada kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, Fatimah Zahraa as alipanda kufikia cheo kikubwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kama ilivyoshuhudiwa na Qur-ani tukufu. Mwenyezi Mungu Mtukufu alimpa utukufu mkubwa sana juu yake, na Mtukufu Mtume saww, kwa upande wake, alimuonyesha kiwango cha heshima ya juu sana, moja ambayo hakuionyesha kwa mwanaume au mwanamke mwingine yeyote yule katika wakati wowote wa maisha yake.

Fatimah Zahraa as alipokuwa mkubwa, Maswahaba wawili wazee (Abu Bakr na Umar) wa kwanza na kisha baadae mwingine, walimuomba babake wamchumbie. Lakini Mtukufu Mtume saww aligeukia pembeni kwa kuchukia, na akasema:

"Hili suala la ndoa ya Fatimah Zahraa, bint yangu, liko mikononi mwa Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenyewe, na yeye pekee ndiye atamchagulia yeye mchumba."

Mwenyezi Mungu Mtukufu alifanya uchaguzi wake kama ipasavyo. Alimchagua mja wake, Ally bin Abi Twalib as, kuwa ndiye mchumba wa bint ya mja wake mpendwa mno, Mtukufu Mtume Muhammad saww. Alipenda kuwaona Fatimah Zahraa as bint Muhammad na Ally bin Abi Twalib as wakioana.

Miezi miwili baada ya vita vya Badr, yaani, katika mwezi wa Dhilqa'da (mwezi wa 11) wa mwaka wa pili hijiria., Ally alikwenda kwa Mtukufu Mtume Muhammad saww, na akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, umenilea mimi kama mwanao mwenyewe. Ulinijaza na zawadi zako, ukarimu wako na wema wako. Ninawiwa na wewe kila kitu katika maisha yangu. Sasa ninaomba wema mmoja zaidi kutoka kwako."

Mtukufu Mtume saww alielewa wazi nini Ally alichokuwa akijaribu kusema. Uso wake ulichangamka kwa tabasamu pana, na alimwambia Ally subiri kwa muda kidogo mpaka apate Majibu ya bint yake.

Mtukufu Mtume saww, Aliingia ndani, akamwambia Fatimah Zahraa as kwamba Ally alikuwa anaomba uchumba kwake, na akamuuliza ni lipi jibu lake. Fatimah Zahraa as akabakia kimya. Yeye Mtukufu Mtume Muhammad saww akatafsiri kimya chake kama idhini yake, akarudi kwa Ally, akamjulisha kwamba ombi lake limekubaliwa, na akamwambia afanye matayarisho ya harusi.

Fuatana nami Sehemu ya kumi na nne Historia ya Ma'asumah Fatimah Zahraa as, siku ya harusi yenyewe.

REJEA:

Rejea: Biharul Anwar Jz 43 UK 120-129.

Rejea: Biharul Anwar Jz 43 UK 230-131.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini