Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

NDOA YA MTUKUFU FATIMAH ZAHRAA (A.S) 2

0 Voti 00.0 / 5

SIKU YA HARUSI YA MTUKUFU FATIMAH ZAHARA (A.S) NA MTUKUFU ALLY (A.S)

Sherehe za harusi zilifanyika mnamo mwezi mosi Dhul Hijja, mwaka wa pili hijiria, mwezi mmoja baada ya hotuba ya ndoa.[1]

Muda kati ya hotuba ya ndoa na Sherehe za harusi, Imamu Ally as alikuwa ana haya ya kuongea kuhusu Fatimah mke wake kwa Mtukufu Mtume saww. Siku Moja, kaka yake, Aqili, alimuuliza: "Kwa nini huleti mke wako nyumbani ili tuweze kukupongeza na kwa ajili ya shughuli za kufunga ndoa kwako?" Jambo hili lilimfikia Mtukufu Mtume saww, ambaye alimuita Ally as na kumuuliza: "Je, uko tayari kwa ajili ya kufunga ndoa?

Imamu Ally as alitoa jibu la kukubali. Mtukufu Mtume saww akasema: Inshaallah, leo usiku au kesho usiku, mimi nitafanya maandalizi kwa ajili ya harusi." Wakati huo, yeye Mtukufu Mtume saww akawaambia wake zake wamvalishe Bibi Fatimah Zahraa as na kumtia manukato na kuweka mazulia kwenye chumba chake ili kujiandaa kwa ajili ya Sherehe za harusi.[2]

Ally as alisema: Mtukufu Mtume saww aliniambia nenda ukauze lile vazi lako la kivita (Diri'i) Ally as akasema nikaenda nikaliuza na nikachukua thamani yake nikazipeleka kwa Mtukufu Mtume saww nikazimwaga zile Dirham mbele ya Mtukufu Mtume saww na wala hakuniuliza zilikuwa ngapi, hata mimi sikumwambia zilikuwa ngapi. Akachota kwa mkono mmoja, akamwita Bilali bin Rabbaha akampa kisha akamwambia nenda ukamnunulie Fatimah manukato.

Kisha akachota kwa mikono miwili Dirham zingine, akampa Abu Bakr akamwambia nenda ukamnunulie Fatimah nguo na vyombo vya nyumbani. Akamuandaa Ammar bin Yasir na Maswahaba wengine wengi kwenda kumsaidia Abu Bakr.

   Walifika sokoni wakawa wanaonyeshana vitu vinavyofaa kununua na walikuwa hawanunui mpaka wamuonyeshe Abu Bakr. Kama Abu Bakr atasema kinafaa basi walikinunua.

Wakawa wamenunua vitu vingi sana miongoni mwa vitu hivyo ni Gauni la harusi lililogharimu Dirham saba, ushungi Dirham nne kitanda, magodoro mawili mapazia na vyombo vingine vingi vya ndani. Walipomaliza kununua Abu Bakr alibeba baadhi ya vyombo na Maswahaba wa Mtukufu Mtume saww aliokuwa nao wakabeba vilivyobakia.

     Walipovifikisha na kumuonyesha Mtukufu Mtume saww, akawa anavigeuza geuza kwa mikono yake huku akisema Ewe Mwenyezi Mungu wape baraka Ahlubaiti wangu.

Mtukufu Mtume saww akamwambia Ally As: " Hapawezi kuwa na harusi bila ya wageni." Basi Imamu Ally as alipowaalika watu kwa ajili ya harusi yake, Mmoja wa viongozi wa Ansaari aliyekuwa akiitwa Sa'd akasema: Mimi nakuzawadia kondoo mmoja." Na kikundi cha Ansaari nao vilevile wakaleta kiasi cha nafaka Takriban ratili 8 na maji ya maziwa yaliyoganda, mafuta na tende pia vililetwa kutoka masokoni.[3]

   Nyama hiyo ilipikwa na Mtukufu Mtume saww pamoja na usafi wake alichukua jukumu la kupika yeye mwenyewe kwa ajili ya harusi hiyo, na kwa mikono yake iliyobarikiwa, akavichanganya (viungo) na akaanza kutengeneza aina ya chakula cha Kiarabu kinachoitwa Habis.[4]

Hata hivyo, ingawa chakula kilitayarishwa, mwaliko ulikuwa wa jumla. Idadi kubwa ya watu ilishiriki na kwa baraka za mikono ya Mtukufu Mtume saww, kila mmoja alikula na akashiba kutokana na chakula hicho, na kulikuwa na kingine kilichobakia kwa ajili ya masikini na wenye shida; sinia la chakula vilevile liliwekwa kwa ajili ya Bibi harusi na bwana harusi.[5]

Mwezi 12 Dhul Hijja mwaka wa pili hijiria Fatimah Zahraa as ilibidi aiage nyumba yake ya kuzaliwa ili aweze kwenda kwenye nyumba ya mumewe. Baada ya chakula, wanawake walijikusanya karibu na Bibi Fatimah Zahraa as na Mtukufu Mtume saww akamsaidi kumpakia kwenye Ngamia jike wake. Madina ilivuma kwa sauti za Allahu Akbar.

Salman Muajemi (Muiran) alishikilia hatamu za Ngamia jike huyo, na akawa anatembea mbele yake, huku akisoma Qur-ani Tukufu. Mtukufu Mtume saww alitembea upande mmoja wa Ngamia jike huyo, na Hamza Simba wa Mungu, upande mwingine. Wanaume majasiri  na idadi kadhaa ya wanafamilia na maharimu wa Bibi Fatimah Zahraa as wakajikusanya karibu na Ngamia jike huyo wakiwa na panga zilizochomolewa. Wanawake wengi walisuburi nyuma ya Bibi harusi na huku wakisoma Takibira.

Ngamia akaanza kutembea, na wale wanawake wakaanza kusoma Takibira na sifa za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa wakati ule, mmoja baada ya mwingine, walisoma kaswaida nzuri na tamu ambazo zilikuwa zimetungwa kwa utukufu na shangwe, wakampeleka Bibi harusi nyumbani kwa bwana harusi.

         Vijana wote wapanda farasi wa Bani Hashim walipanda kama wasindikizaji wa Bibi harusi huyo, pamoja na panga zinazomeremeta zikiwa zimenyanyuliwa juu kabisa. Nyuma yao walikuwa wanawake Muhajirina na Ansaari, na nyuma yao wakaja Muhajirina na Ansaari wenyewe. Walikuwa wakisoma kaswaida kutoka kwenye Qur-ani Tukufu kumtukuza Mwenyezi Mungu. Usomaji huo wa qaswaida uliwekwa vituo mara kwa Mara na mrindimo wa sauti za Allahu Akbar.

Maandamano haya ya kitukufu yaliuzunguka msikitini mkubwa wa Madina, na kisha yakaishia kwenye ukomo wake nyumbani kwa bwana harusi Ally bin Abi Twalib as. Mtukufu Mtume saww akamsaidi bint yake kushuka toka kwenye Ngamia jike. Akamshika mkono wake, na kwa ishara akauweka kwenye mkono wa mumewe, na kisha, akisimama kwenye kizingiti cha nyumba hiyo, akasoma Du'a ifuatayo:

"Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu! Nanawaweka Ally na Fatimah, waja wako wanyenyekevu, kwenye ulinzi wako. Uwe wewe ndiyo mlinzi wao. Wabariki hawa. Kuwa radhi nao, na uwape neema zako zisizo na mipaka, huruma na fadhila zako bora juu yao. Uifanye ndoa yao kuwa yenye matunda, na uwafanye wote imara katika upendo wako, na ibada zako."

Mtukufu Mtume saww vilevile aliingia chumbani kwa maharusi. Aliitisha karai la maji, na wakati huo lilipoletwa, yeye akanyunyiza kiasi juu ya kifua cha Mtukufu Fatimah Zahraa as na akamwambia atawadhe na kuosha kichwa chake kwa yale maji yaliyobaki. Alinyunyiza kiasi juu ya Imamu Ally as pia akamwambia Ally atawadhe na kuosha kichwa chake.

Kisha Mtukufu Mtume saww akachukua mkono wa Bibi Fatimah Zahraa as na kuuweka kwenye mkono wa Imamu Ally as na akasema: Oh, Ally? Ubarikiwe wewe; Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuweka juu yako bint ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye mbora wa wanawake wa Ulimwengu." Kisha akaongea na Bibi Fatimah Zahraa as na akasema: "Oh, Fatimah! Ally ni kutoka kwa wobora wa wanaume wote." [6]

Kisha Mtukufu Mtume saww akawaombea dua juu yao kwa kusema: "Ewe Mwenyezi Mungu,wafanye wazoeane na kila mmoja wao! Ewe Mwenyezi Mungu, wabariki hawa! Na weka neema kwa ajili yao katika maisha yao.

Wakati alipokaribia kuondoka, yeye akasema: Mwenyezi Mungu Mtukufu amekufanyeni ninyi na kizazi chenu kuwa tohara (Ma'asumin). Mimi ni rafiki wa marafiki zenu, na ni adui wa maadui zenu. Sasa nakupeni mkono wa kwa heri na kukabidhini kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu."[7]

Asubuhi iliyofuata, Mtukufu Mtume saww alikwenda kumuona bint yake. Baada ya kuwatembelea huku, yeye hakwenda tena nyumbani kwao kwa muda wa siku tatu, bali akaenda katika siku ya nne.[8]

Fuatana nami Sehemu ya kumi na tano historia ya Ma'asumah Fatimah Zahraa as

 


[1]. Rejea: Biharul Anwar Jz 43 UK 92.

[2]. Rejea Biharul Anwar Jz 43 UK 230-131.

[3]. Rejea Biharul Anwar Jz 43 UK 137.

[4]. Rejea Biharul Anwar Jz 43 UK 106 na 114.

[5]. Rejea: Manaqibu Ibn Shahr Ashub, Jz 3 UK 354.

[6]. Rejea: Izdawaaj Maktab Insaan Saazi, Jz 2 UK 300.

[7]. Rejea: Manaqibu ya Ibn Shahr Ashub Jz 3 UK 354-355.

[8]. Rejea Manaqibu Ibn Shahr Ashub Jz 3 UK 356.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini