NDOA YA MTUKUFU FATIMAH ZAHRAA (A.S) 3
NDOA YA MTUKUFU FATIMAH ZAHARA AS, KUTOKA NYUMBA YA MTUKUFU MTUME SAWW, NA MTUKUFU IMAMU ALLY BIN ABI TWALIB AS, MZALIWA KATIKA NYUMBA YA MWENYEZI MUNGU MTUKUFU. 01 Dhul Hijja mwaka wa 2 hijiria
SIKU YA NNE BAADA YA HARUSI MTUKUFU MTUME SAWW AENDA KUWASALIMIA MAHARUSI
Imamu Ally as anasema: Mtukufu Mtume saww alikaa siku tatu baada ya harusi pasipo kuingia nyumbani kwetu. Ilipokuwa asubuhi ya siku ya nne alikuja akitaka kuingia chumbani kwetu. Akamkuta Asmaa binti Umais Alkhath'amiyah, chumbani kwetu Mtukufu Mtume saww akawaambia: Kwa nini umesimama hapa kwenye chumba cha mtu?
Asmaa binti Umais Alkhath'amiyah akasema: Natoa fidia babangu na mamangu, hakika Msichana anapokutana na mme wake, anahitaji mwanamke wa kumliwaza na kusimamia haja zake. Nimesimama hapa ili kukidhi haja za Fatimah. Mtukufu Mtume saww akawaambia: Mwenyezi Mungu Mtukufu akukidhie haja zako za duniani na Akhera.
Imamu Ally as anaendelea kusema: ilikuwa ni asubuhi tulivu na mimi na Fatimah tulikuwa bado tumejifunika blanket. Tulipomsikia Mtukufu Mtume saww akiongea na Asmaa, tuliamka. Mtume saww akasema: Haki yangu iwe juu yenu msitawanyike Hadi nitakapoingia. Tukarudia katika hali yetu, akaingia na akakaa upande wa vichwa vyetu, akaingiza miguu yake kati yetu, mimi nikaushika mguu wa kulia nikaukumbatia kifuani mwangu, na Fatimah akaushika mguu wake wa kushoto akaukumbatia kifuani mwake, tukawa tunaitoa miguu yake kutoka kwetu hadi tulipoitoa Mtukufu Mtume saww akasema: Ewe Ally niletee kikombe cha maji. Nikamletea akayapulizia mara tatu na akayasomea Aya kutoka kwenye Qur-ani Tukufu.
Kisha akasema: Ewe Ally, kunywa haya maji bakisha kidogo. Nikanywa na nikabakisha kidogo. Maji yaliyobaki akayanyunyizia kichwani mwangu na kifuani mwangu na akasema: Mwenyezi Mungu aondoe kwako uchafu (wa makosa na madhambi ya aina yoyote) Ewe baba Hassani na akutoharishe kabisa.
أذهب الله عنك الرجس يا أبا الحسن، وطهرك تطهيرا.
Akasema: Niletee maji mengine mapya. Nikamletea. Akayapulizia mara tatu na akayasomea Aya kutoka kwenye Qur-ani Tukufu.
Kisha akampa mtoto wake na akamwambia: kunywa haya maji bakisha kidogo. Fatimah as akanywa na akabakisha kidogo. Maji yaliyobaki akayanyunyizia kichwani mwa Fatimah na kifuani mwake na akasema: Mwenyezi Mungu aondoe kwako uchafu (wa makosa na madhambi ya aina yoyote) Ewe Fatimah na akutoharishe kabisa.
أذهب الله عنك الرجس يا فاطمة وطهرك تطهيرا.
Baada ya hapo Mtukufu Mtume saww akaniambia toka nje wakawa faragha na mtoto wake akamwambia: ni vipi Ewe mtoto wangu umemuonaje mme wako?
Fatimah as akasema: Ewe baba, ni mme mbora isipokuwa wamekuja wanawake wa Kikuraishi na wakaniambia mimi: Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuoza kwa mwanaume fukara asiye na mali.
Mtukufu Mtume saww akamwambia: Mwanangu! Babako si fukara wala mme wako si fukara hakika nilionyeshwa hazina za ardhini kutokana na Dhahabu na fedha, mimi nikachagua kumtumikia Mola wangu Mtukufu. Ewe mwanangu! Kama ungekuwa unajua yale anayoyajua babako, basi ungeipuuza hii dunia.
Ewe mwanangu Wallaahi! Sikupi nasaha hizi kwa wingi isipokuwa ujue Hakika mme wako ni wa mwanzo wao kusilimu na mwenye elimu nyingi kuliko wengine, na ni mpole mno kuliko wengine wote. Ewe mwanangu! Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ameiangalia hii dunia kwa jicho la rehema na akachagua watu wawili (kuwa ni watukufu na wabora mno) akamfanya mmoja awe babako na mwingine awe mme wako. Ewe mwanangu! Neema ya mme basi ni mme wako. Usimuasi kwa lolote.
Kisha Mtukufu Mtume saww akaniita: Ewe Ally! Nikasema: Nakuitijia na kukutukuza Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu.
لبيك وسعديك يا رسول الله.
Mtukufu Mtume saww akasema: Ingia chumbani kwako, mfanyie upole mke wako na uwe rafiki kwake; Hakika Fatimah ni Sehemu ya mwili wangu kinachomuumiza yeye huniumiza mimi kile ambacho huendeleza ufanisi wake wa kiroho huendeleza ufanisi wangu wa kiroho na kinachomfurahisha yeye hunifurahisha mimi. Kwa heri na kukabidhini kwa Mwenyezi Mungu.
Ally as akasema: Wallaahi sijawahi kumuudhi Fatimah wala sijawahi kumkera kwa lolote hadi alipofariki dunia. Hajawahi kuniudhi wala kuniasi kwa lolote. Nilikuwa nikimuona Fatimah huzuni, machungu na shida zangu zote zinaniishia.
Imamu Ally as akasema: Mtukufu Mtume saww akasimama ili aondoke. Fatimah as akamwambia: Ewe baba! Mimi siwezi kufanya kazi za nyumbani, nitafutie mtumishi awe ananitumikia yaani awe ananisaidia shughuli za nyumbani.
Mtukufu Mtume saww akamwambia Ewe Fatimah, hivi unapenda kheri au mtumishi?
Imamu Ally as akamwambia Fatimah sema napenda kheri. Fatimah as akasema: Ewe baba! Napenda kheri kuliko mtumishi.
Mtukufu Mtume saww akamwambia: Basi utakuwa unafanya Tasbihi kila siku mara 33 na Tahmidi 33, naTakibir 34 hizo zitakuwa jumla ni 100 umetamka kwa ulimi na katika mizani yako ya mema utalipwa mema 1000. Ewe Fatimah hakika wewe ukiyasema haya maneno asubuhi ya kila siku, Basi Mwenyezi Mungu atakutosheleza yale unayo yatamani katika dunia na Akhera.
Na hii ndiyo inatwa Tasbihi Zahraa.
سبحان الله 33 الحمد لله 33 الله اكبر 34.
Fanya iwe ndiyo uradi wako kila baada ya swala ya wajibu, ndugu yangu muislam. [1]
Fuatana nami Sehemu ya kumi na sita historia ya Ma'asumah Fatimah Zahraa as
[1]. Rejea Biharul Anwar Jz 43 UK 132-134; Kashful Ghummah Jz 1 UK 363.