Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

TUKIO LA MUBAHALA

0 Voti 00.0 / 5

EIDIL MUBAHALA AU TUKIO LA MUBAHALA

24 Dhul Hijja mwaka wa kumi 10 hijiria

ALLY BIN ABI TWALIB AS NI NAFSI YA MTUKUFU MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W)

YEYE NA FAMILIA YAKE NI WATU WA KIPEKEE KWA MWENYEZI MUNGU MTUKUFU NA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W)

HATA wasiokuwa waislamu wanalijua hilo kutokana na maandiko ya vitabu vya kimbinguni.Taurati Injili Zaburi Qur-ani Tukufu na Suhfu Ibrahim na Musa.

MAAPIZANO KATI YA MTUME MUHAMMAD SAWW NA WAKRISTO WA NAJIRANI

Kabla hatujaingia ndani kuzungumzia suala la Mubahala, kwanza ni vizuri tufahamishe maana ya Mubahla.

Muhabala ni: Kuapizana na kuombeana laana kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu baada ya kila upande wa makundi mawili yanayotafuta ukweli, kung'ang'ania hoja zake kuwa ndiyo za sawa. Maapizano ni hatua ya mwisho kabisa ya kukata mzizi wa fitina.

Tarehe ishirini na nne Dhul Hijja mwaka wa kumi hijiria, Ujumbe wa Kikristo kutoka Najran katika nchi ya Yemen, ukiongozwa na makasisi watatu :. Ahtam, Al A'aqib na Sayyid.

Ulifika kwa Mtume kujadili suala la Nabii Issa (a.s.).

Kwa kuwa Issa as Alizaliwa bila baba, Wakristo wamedhani kuwa baba yake ni Mwenyezi Mungu.

Mtume saww aliwajulisha kwa kusoma aya kuwa: "Hakika mfano wa Issa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam, aliumbwa kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa naye akawa. (3:59).

Kwa kuwa Nabii Issa alizaliwa bila baba, Wakristo wamedhani kuwa baba yake ni Mwenyezi Mungu.

Aya hii inaondoa dhana hiyo ambayo inapingana na utukufu wa Mwenyezi Mungu, na inawapigia mfano wa ajabu zaidi katika kuumbwa Adam bila ya baba wala mama. Aliumbwa kwa udongo kisha akaambiwa: kuwa naye akawa, na kwa neno hilo hilo Nabii Issa (a.s) ndivyo alivyoumbwa.

Ujumbe huo ulipokuwa haukukubaliana na hoja hii, Mwenyezi Mungu akateremsha Aya:-

"Na atakayehojiana nawe (Muhammad) katika hili baada ya ujuzi uliokufikia, waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu, na nafsi zetu na nafsi zenu, kisha tuombe kwa kunyenyekea tuijaalie laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie wenye kusema uongo." 3:61.

Tukio Hili lilikuwa tarehe ishirini na nne mfungo tatu mwaka wa kumi. Mtume akawaita ili waanze kuapizana.

 Wakajibu:- "Ngojea tujadiliane". Walipokwenda faragha, wakamuuliza Askofu Abdul Masih; ana Maoni gani katika suala hili?

Akajibu:- Enyi Wakristo: Wallahi nyinyi mnajua kuwa Muhammad ni Nabii aliyeletwa na amekuja na ushahidi ulio wazi juu ya jambo la Huyu Issa as (Yesu). Wallahi hakuna watu walioapizana na Nabii wakasalimika, ikiwa mtaapizana naye mtaangamia na".

Askofu Peter yeye aliwaambia: "Enyi Wakristo: Mimi naziona nyuso hizi (kundi la Mtume) kama zitamuomba Mwenyezi Mungu auondoe mlima kutoka mahala pake, Wallahi atauondoa. Msiapizane naye mtaangamia, na hatabaki Mkristo ye yote hapa duniani mpaka siku ya Kiama".

Alipoulizwa Ahtam, akawaambia: Niacheni nikamuulize Muhammad, alipomkabili Mtume akamuuliza, "Ewe Abulqasim'! Unatoka na kina nani kwa ajili ya maapizano haya?" Mtume (s.a.w.w ) akamjibu:

 "Ninaapizana nanyi nikiwa na watu bora hapa duniani na watukufu mno mbele ya Mwenyezi Mungu, nao ni hawa (akawaonyesha)

 Aliy, Fatimah, Hassan na Hussein (a.s)

Taarifa ya kikosi hicho cha Mtume (s.a.w.w ) ilipowafikia wakaogopa kuapizana na Mtume, na badala yake wakaomba sulhu kwa Mtume (s.a.w.w .) kwa kutoa dirham arobaini elfu.[1]

Katika Ayatul Mubahala, iliposema:- "Tuwaite watoto wetu" Mtume (s.a.w.w ) alimwita: Hassan na Hussein.

Iliposema: "Na wanawake wetu" Mtume (s.a.w.w .) alimwita: "Fatima bint Muhammad".

 Iliposema: "Na nafsi zetu" mtume akamwita: "Aliy.

Kisha Mtukufu Mtume saww akasema :. Ewe Mola wangu hawa ndio (kikosi cha) watu wangu.

Kwa hivyo Aliy bin Abi Talib as ni nafsi ya Mtume Muhamad (s.a.w.w .).

Tukio hili Ia Mubahala tukilitazama kwa upande wa pili, linatukumbusha lile tukio la "KlSAA" Iliposhuka Ayatut Tat'hir:- Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni (kukukingeni na) uchafu watu wa nyumba (ya Mtume) na (anataka) kukutakaseni sana sana" (33:33).

Iliposhuka Aya hii Mtume alimchukua Aliy as na Fatimah na Hassan na Hussein a.s  akawafunika nguo kisha akasema: "Ee Mola! Hawa ni watu wa nyumba yangu, basi waondolee uchafu na uwatakase sana sana." Mama Ummu Salama (mke wa Mtume) alipotaka kuingia humo, Mtume (s.a.w.w ) akamzuia:

Kama ambavyo kwenye tukio la Mubahala ulipofika wakati wa kuomba maombi maalumu kwa ajili ya maapizano kati yake na Wakristo wa Najran, Mtume alimchukua Aliy as na Fatimah na Hassan na Hussein a.s tu. Ingawa wakati huo Mtume (s.a.w.w .) alikuwa nao wakeze, na Masahaba ambao ni marafiki zake pia, lakini hapa hawakuingia.

Wake za Mtume na Masahaba hawakuingia katika "KISAA" na hawakusimama katika uwanja wa Mubahala, kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwahusisha darja hii Ahlul Bait tu peke yao . Ally bin Abi Twalib as akiiwakilisha nafsi ya Mtukufu Mtume saww, na hakuwakilisha maswahaba.[2]

Mtukufu Mtume saww anasema :. Hakika Ally ana tokana na mimi, na mimi ninatokana naye, pia Ally ni Kiongozi wa kila muumini baada yangu.[3]

Daraja la Amirul Muuminina Aliy bin Abi Talib mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Kutoka kwa Abdullah bin Abbas anasema :. Siku Sita baada ya Kufariki Mtume saww Abu Bakr bin Abi Quhafa aliongozana na Ally bin Abi Twalib as kwenda kufanya Ziyara katika kaburi la Mtume Muhammad saww, walipofika mlango wa kuingia Chumba kilicho na kaburi la Mtume saww, Ally a.s alimwambia Abu Bakr tangulia kuingia, Abu Bakr akasema :. Siwezi kumtangulia mtu ambaye nimemsikia Mtukufu Mtume saww akisema kwa ajili yake :. Ally kwangu mimi ni kama daraja langu kwa Mola wangu.[4]

Fuatana nami sehemu ya ishirini na tano historia ya Maasum Ally bin Abi Twalib (a.s)

 

[1]. Tarikh Ibn Athir J.2 Uk. 200. Tafsirul Qurtubi J.4 Uk. 104. Tafsirul Ibn Kathir J.1 Uk. 376-379. Tafsirul Khazin J.1 Uk. 359-360. Tafsirul Maragh J.3 Uk. 175. Tafsirul Kabir J.8 Uk. 81. Zadul Masir J.1 UK. 399.

[2]. Tafsirul Khazin J.3 Uk. 259. Tafsirul Ibn Kathir J.3 Uk. 494.  Tafsirul Qurtubi J.14 Uk. 183. Zadul Masir J.6 Uk. 381.

[3]. Musnad Ahmad ibn Hambali Jz 4 UK 439. Sunan Tirmidhi Jz 5 UK 632 hadithi 3712.

[4]. Sawaiqul Muhriqa ya Ibn Hajar UK 108. Riyadhn Nadharah ya Muhibu Tabariy Jz 2 UK 162.: Dhakhairul Uqba UK 64.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini