Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

25 DHUL HIJJA MWENYEZI MUNGU ASHUSHA SURATU DAHRI

0 Voti 00.0 / 5

25 DHUL HIJJA MWENYEZI MUNGU ASHUSHA SURATU DAHRI (INSANI) KUELEZEA UKARIMU WA ALLY BIN ABI TWALIB AS. NA KIZAZI CHAKE KITUKUFU

هل أتى على الإنسان حين من الدهر لم يكن شيئا مذكورا.

Kutoka kwa Abdullah bin Abbas anasema :Hassan na Hussein a.s walipatwa na maradhi ikawa babu yao Mtume saww anakwenda kuwaona. Imamu Aliy as akaambiwa dawa ya maradhi haya ni nadhiri, Mtukufu Mtume saww akamuamuru aweke nadhiri kwa ajili ya watoto wake, Imamu Aliy as akasema :. Ikiwa watapona atafunga siku tatu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Bibi Fatimah as naye akasema kama alivyo sema mume wake. Mtumishi wao Fedh dhatu akasema :. Ikiwa mabwana zangu watapona basi nitafunga siku tatu kwa kumshukuru Mwenyezi. Muda mfupi Hassan na Hussein a.s wakapona. Nyumbani mwao kulikuwa hakuna chakula. Imamu Aliy as akaenda kwa Sham'un al Khaybary, kuazima pishi tatu za ngano,.

Bibi Fatimah as akachukua pishi moja akaiandaa, akatengeneza mikate kwa ajili ya iftari. Imamu Aliy as alipomaliza kusali pamoja na Mtukufu Mtume saww msikitini, akaingia nyumbani kwake chakula cha kufuturu kikaandaliwa, wakaanza kula mara masikini akafika mlangoni kwao, akagonga mlango akasema: Asalamu Alaykum ya Ahlal Bayt Rasulallah! Mimi ni masikini katika watoto wa kiislam nipeni chakula Mwenyezi Mungu atakupeni chakula cha peponi.

Imamu Aliy as alipomsikia akampa chakula chake, mara familia nzima wakampa siku hiyo wakakaa kutwa kucha hawana walichokula isipokuwa walikunywa maji.

Siku ya pili Bibi Fatimah as akachukua pishi moja akaiandaa, akatengeneza mikate kwa chakula. Imamu Aliy as alipomaliza kuswali pamoja na Mtukufu Mtume saww msikitini, akaingia ndani kikaandaliwa chakula, walipotaka kuanza kula mara Yatima akafika mlangoni kwao, akagonga mlango akasema :. Asalamu Alaykum ya Ahlal Bayt Rasulallah,! Mimi ni Yatima katika watoto wa Muhajirina, mzazi wangu ameuliwa vitani, naomba chakula. Akapewa chakula chote. Wakabaki hiyo siku bila Kutia Chochote vinywani mwao isipokuwa maji.

Siku ya tatu Bibi Fatimah as akachukua pishi iliyobaki katika zile pishi tatu alizoleta mume wake. AKakanda na kutengeneza mikate kwa chakula. Baada ya Imamu Aliy as kumaliza kuswali pamoja na Mtukufu Mtume saww akaingia ndani, chakula kikaandaliwa. Mara mfungwa akafika mlangoni, akagonga mlango akasema :. Asalamu Alaykum ya Ahla Bayt Rasulallah,! Wameniteka na kunifunga na kuninyima chakula! Nipeni chakula, wakampa chakula chote, wakashinda siku ya tatu usiku kucha na mchana kutwa, hawana chakula isipokuwa maji tu.

Historia inasema kuwa :. Mtukufu Mtume saww alipomuona bibi Fatimah as alivyo pinda kama upinde tumbo limekutana na mgongo kwa njaa ya siku tatu alilia kwa kumuonea huruma.

Mwenyezi Mungu akamteremshia Mtume wake Suratu Dahri.

Hakika ulimfikia wakati mtu fulani wa zama ambapo hakuwa kitu kinachotajwa. 76:1

Kwa hakika tulimuumba mtu (huyu) kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika, tunamjaribu, hivyo tukamfanya ni mwenye kusikia, mwenye kuona. 76:2

Hakika watu wema watakunywa katika kikombe kilichochanganyika na kafuri. 76:5 (Itakuwako) chemchem wakakayoinywa waja wa Mwenyezi Mungu, wataitiririsha mtiririko (mzuri). 76:6

Baada ya Imamu Ally na familia yake kupewa mtihani ya kuuguliwa na watoto wao waliweka nadhiri na walipotekeleza nadhiri yao kwa uzuri kabisa Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema:-

Wanatekeleza nadhiri na wanaiogopa siku ambayo shari yake itaenea. 76:7

Na huwalisha chakula masikini na Yatima na mfungwa hali ya kuwa wanakihitaji. 76:8

Huku wakisema :. Tunakulisheni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu hatutaki malipo wala Shukran.76:9

Hakika sisi tunaogopa kutoka kwa Mwenyezi Mungu siku yenye shida na taabu.76:10[1].

Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu Akasema baada ya kusikia kauli ya Imamu Ally as na familia yake:

Basi Mwenyezi Mungu atawalinda katika shari ya siku hiyo na kuwakutanisha na neema na furaha. 76:11

Na atawapa mabustani na hariri kwa sababu ya uvumilivu (wao).76:12

Humo wataegemea viti vya Enzi humo hawataona jua (kali) wala baridi (kali). 76:13

Na vivuli vyake vitafikia karibu yao na matunda yataning'inia chini chini. 76:14

   Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae. 76:15

Vigae vya fedha, wamevifanya kwa vipimo. 76:16

   Na humo watanyweshwa kikombe kilichochanganyika na tangawizi. 76:17

Humo mna chemchem inayoitwa Salsabil. 76:18

      Na watawazungukia wavulana wasiochakaa, utakapowaona utawafikiria ni lulu zilizotawanywa. 76:19

Na utakapoyaona humo utaona (ni) neema na ufalme mkubwa. 7620

      Juu yao watavaa nguo za hariri laini ya kijani kibichi na hariri nzito, na watavikwa bangili za fedha na Mola wao atawanywesha kinywaji safi. 76:21

Ama sisi Shi'ah tunajivunia kuwa tutakuwa pamoja na Imamu Ally as na familia yake kama alivyosema Mtukufu Mtume saww:

Amepokea mwanazuoni wa ki Shafiiyu Ibn Hajar Al Haithami kutoka kwa Tabaraniy kutoka kwa Abi Huraira alisema :. Ally bin Abi Twalib a.s alisema :. Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni nani apendezaye sana kwako ni Mimi au Fatimah?

Mtukufu Mtume saww akasema :. Fatimah a.s anapendeza sana kwangu kuliko wewe. Na wewe ni Mtukufu mno kwangu kuliko Fatimah,(Hapa nilipo) ni kana kwamba nakuona wewe upo katika Haudh unanywesha watu ; na katika Haudh kuna mabirika idadi yake sawa na nyota za mbinguni. Wewe na Hassan na Hussein a.s, Hamza na Ja'far mtakuwa ndugu peponi juu ya viti vya kifalme kwa kuelekeana, na wewe utakuwa pamoja na mimi na Shi'ah (wafuasi) wako.

Kisha Mtukufu Mtume Saww akasoma aya :. Na tutaondoa mafundo yaliyomo vifuani mwao na watakuwa ndugu wakikaa juu ya viti vya kifalme kwa kuelekeana. 15:45-48 Quran tukufu

Rejea Majimau Zawaid Jz 9 UK 173

Fuatana nami sehemu inayofuata tujifunze zaidi kuhusu Uislamu na waislamu

 

 

[1]. Rejea :. Shawahidu Tanzil Jz 2 UK 299. Tafsirul Basair Jz 51 UK 7. Tafsirul Qurtubi Jz 19 UK 130. Usudul Ghaba Jz 5 UK 530. Adurrul Manthur Jz 6 UK 485. Tafsirul Khazin Jz 7 UK 191. Tafsirul Kabiri Jz 30 UK 243. Tafsirul Kashshaf Jz 4 UK 197.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini