HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 2
IMAMU HUSSEIN A.S
Sehemu ya pili
KULELEWA KWAKE
Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alikuwa akiwalea wajukuu zake Hassan na Hussein (a.s) na vile vile alikuwa akiulea Uislamu; na Imamu Aliy (a.s) na Bi Fatumah (a.s) walikuwa nao pia wakiwalea watoto hawa ambao Mtukufu Mtume (s.a.w.w) aliwaita wanawe. Alikuwa akiwachukua popote pale aendapo mara nyingi Imamu Hassan (a.s) akikaa bega la kuume na Imamu Hussein a.s alikaa katika bega la kushoto. Kila mara Mtume saww aliwataka Waislamu wawapende hao watoto wake Mtume (s.a.w.w)
Na mapenzi yake kwa Imamu Hussein (a.s) yalikuwa ya kiwango kikubwa. Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akisali, Imamu Hussein (a.s) alikuwa akija na kukaa mgongoni pake. Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alikuwa aliendeleza Sajida yake mpaka Imamu Hussein (a.s) ateremke kwa hiyari yake. Wakati fulani Imamu Hussein (a.s) alikuja kwenye msikiti wa Mtume saww mjini Madina wakati Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akihutubia, Imamu Hussein (a.s) alijikwa na akaanguka chini, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) mara moja aliacha kuhutubia akateremka chini na kumnyanyua mwanawe kwanza. Kisha aliwahutubia watu waliokuwepo hapo akisema: Huyu ni Hussein (a.s); mfahamuni vizuri ".
Siku moja Mtume (s.a.w.w) alikuwa nyumbani kwa mama wa waumini Ummu salama, Mtume (s.a.w.w) akamwambia: Asiingie yeyote mimi nina shughuli, mara Ummu salama akajisahau Hussein (a.s) akajipenyeza akaingia hadi akakaa katika mapaja ya babu yake Mtume (s.a.w.w), Ummu salama aliposhitukia akataka kumtoa, Mtukufu Mtume saww akamkataza asimtoe.
Mara Hussein (a.s) akajisaidia haja ndogo akiwa amepakatwa ni Mtume (s.a.w.w), Ummu salama alipotaka kumpokea ili labda ajisafishe, Mtukufu Mtume saww akamzuia.
Mara Ummu salama akamuona Mtume (s.a.w.w) analia. Ummu salama akamuuliza mbona unalia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Mtukufu Mtume saww akasema amekuja Malaika akanikuta ninambusu Hussein mdomoni na sehemu zingine za mwili wake, Malaika yule akaniuliza :. Je unampenda sana huyu mtoto? Nikamwambia kwa nini nisimpende?
Malaika yule akaniambia kuwa Ummah wako watamuua kisha akanyoosha ubawa wake akachukua udongo wa sehemu atakapo uliwa. Akasema : udongo huu atauliwa mtoto wako ni udongo wa Karbala.
Ewe Ummu salama nakupa udongo huu uutunze siku ukiuona umekuwa mwekundu ujue mwanangu Hussein a.s Ameuawa.
Mtukufu Mtume saww akatoka nje akawakuta maswahaba wake akina Abu Bakr bin Abi Quhafa na Umar bin khatabi na Uthmani Bin Affan na masahaba wengine wengi tu, wakamuona Mtukufu Mtume (s.a.w.w) amembeba Hussein (a.s) huku Akilia. Wakamuuliza mbona walia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?
Mtukufu Mtume (s.a.w.w) akasema: Niacheni nilie hakika Malaika ameniijia akaniambia kuwa huyu mwanangu ummah wangu watamuua. Ehee! Atakaye kuwepo kipindi hicho ni amsaidie. Mtukufu Mtume (s.a.w.w) akaangua kilio na masahaba wote waliokuwepo hapo wakalia hadi ndevu zikaloa kwa machozi.
Na ndio ulikuwa mwanzo wa kumlilia Hussein (a.s). Mtukufu Mtume saww na masahaba wake walilia kwa kupewa taarifa tu kuwa atakuja kuuawa wakalia kiasi hicho na alikuwa bado yuko hai. Je mimi na wewe tunaosoma habari hizi cha mauaji ya kikatili aliyofanyiwa Mjukuu wa Mtume saww, kwa nini tusilie?
Kumlilia Hussein (a.s) ni suna ya Mtukufu Mtume saww na Maswahaba r.a.
Kutoka kwa Hudhaifa bin al Yaman amesema: Nilimuona Mtume (s.a.w.w) akiwa amemshika mkono Hussein bin Ally (a.s) na hali akisema: Enyi watu! Huyu ndiye Hussein bin Aliy (a.s) mtambueni, Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake Hakika yeye ni mtu wa peponi na wapenzi wake ni watu wa peponi na vipenzi vya wapenzi wake ni watu wa peponi.[1]
Mtukufu Mtume saww alikuwa anasema: Hussein (a.s) anatokana na mimi na mimi natokana na Hussein (a.s) ". Akiwa na maana ya kuwa Imamu Hussein (a.s) alikuwa ndio maisha ya Mtukufu Mtume saww na jina la Mtume (sa.w.w) litadumu kupitia kwa Hussein (a.s).
UBORA, UTUKUFU NA FADHILA ZA IMAMU HUSSEIN (A.S).
Mtukufu Mtume (s.a.w.w) amesema:
من أحب أن ينظر الى أحب أهل الأرض إلى أهل السماء فلينظر إلى الحسين.
Apendaye kumtazama kiumbe apendwaye sana na wakazi wa mbinguni kushinda wakazi wa ardhini wote ni amtazame Hussein (a.s).[2]
Imamu Hussein (a.s) amesema: Niliingia kwa Mtukufu Mtume saww akiwa na Ubayyi bin Ka'b, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) akaniambia: Karibu ewe Aba Abdillah, ewe pambo la mbinguni na ardhini ".
Ubayyi akamwambia Mtume (s.a.w.w): Vipi asiyekuwa wewe anakuwa pambo la mbingu na ardhi? Mtukufu Mtume (s.a.w.w) akasema :. Ewe Ubayya! Naapa kwa yule ambaye amenituma kwa haki kuwa Nabii, hakika Hussein bin Aliy ni Mtukufu mno mbinguni kushinda ardhini, na hakika kuliani mwa Arshiy ya Mwenyezi Mungu kumeandikwa: Hussein (a.s) ni Taa ya uongofu jahazi la uokovu, Imamu shupavu, (yeye) ni utukufu, fahari, bendera na hazina.[3]
Fuatana nami sehemu ya tatu historia ya Maasum Hussein a.s