Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 4

0 Voti 00.0 / 5

IMAMU HUSSEIN (A.S)

Sehemu ya nne

JIHADI YA IMAMU HUSSEIN (a.s).1

MAANA YA JIHADI

Jihadi maana yake ni kutetea na kulinda heshima, mali na uhuru wa raia. Na kulinda yote hayo yataka kujitolea kinafsi, kimali, kifamilia na hata heshima.

Imamu Hussein (a.s) Sayyid Shuhadaa mwana wa Ally bin Abi Twalib (a.s) aliamua kuulinda Uislamu kwa kutoa muhanga nafsi yake, familia yake, mali zake na vingine vinavyohusiana naye kwa ajili ya Uislamu, hivyo kuna umuhimu kwa Waislamu kujua mwamko huu Mtukufu kwanza, pili wamuunge mkono kwa aina zote za msaada na tatu wachukue kigezo kwa Imamu wao katika kujitoa muhanga kwa ajili ya Uislamu. Na muislamu ajue kwamba kujitoa muhanga ni katika vitu vinne, na Imamu Hussein (a.s) alijitoa muhanga kwa mambo haya manne katika mapambano ya Karbala:-

Kujitoa muhanga katika nafsi.

Kujitoa muhanga katika familia.

Kujitoa muhanga katika mali.

Kujitoa muhanga katika umaarufu wake.

Imamu Hussein (a.s) alijitoa muhanga katika nafsi yake akauliwa. Alijitoa muhanga katika familia yake mpaka likauliwa kundi miongoni mwao, na wengine wakatekwa. Alijitoa muhanga katika mali zake ambapo nyingi alitumia katika maandalizi ya kivita na nyingine aliporwa. Alijitoa muhanga katika umaarufu wake mpaka wakamwita Khawariji na wakamlaani juu ya majukwaa (mimbari). Ni kweli ilikuwa hivyo kwa muda mchache kama ambavyo ni kawaida katika udanganyifu na tuhuma, hivyo ni lazima kwa mwanajihadi asiogope kuvunjika kwa umaarufu wake kama atapigana kwa ajili ya kutengeneza. Kwani Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuafiki na kutakwa msaada.

KUFARIKI KWA MUAWIYYAH L.a

Alipokufa Muawiyyah huko Damascus katika nusu ya mwezi wa Rajabu mwaka wa sitini 60 hijiria, mtoto wake Yazeed alikuwa Hauran, ndipo Dhahaka bin Qais akachukua Sanda zake na akapanda jukwaani, baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumshukuru akasema :. Muawiyyah alikuwa ni uzio wa waarabu, msaada wao na utukufu wao, kwake Mwenyezi Mungu amekata fitina na akamtawalisha kwa waja wake na akafungua nchi, lakini ameshakufa na hizi ni Sanda zake, hivyo sisi tutamvika na tutamzika katika kaburi lake na tutamwacha baina ya amali zake, kisha ni maisha ya barzakhi hadi siku ya kiyama. Hivyo anayetaka miongoni mwenu kushuhudia basi ahudhurie.

Kisha Dhahaka akamsalia na kumzika katika makaburi ya mlango mdogo, na akatuma barua kwa Yazeed kwa kumpa Rambirambi kwa kifo cha baba yake na kumtaka aje haraka ili achukue kiapo cha utii kwa watu, na aliandika chini ya barua:-

Ameondoka Ibn Sufiyan mpweke kwa kifo chake, na umeachwa tazama utafanyaje baada yake. Tuongoze katika njia na Fuata mwendo wa sawa, kwani wewe wakati wa fazaa ni mwenye kutegemewa.

Yazeed l.a akaondoka kuelekea Damascus na kuwasili baada ya siku tatu kuzikwa kwa Muawiyyah l.a. Dhahaka akatoka pamoja na kundi kwa ajili ya kumpokea, Yazeed alipowasili kwao, Dhahaka kwanza alimpeleka kwenye kaburi la baba yake, akasali kaburini kisha akaingia mjini na akawaandikia magavana katika miji akiwaeleza kifo cha baba yake na kuwathibitisha katika kazi zao, na akaunganisha miji miwili ya Iraq ikawa chini ya uongozi wa Ubaydullah bin Ziyad baada ya kushauriwa hilo na Sarjon aliyekuwa Mtumwa wa Muawiyyah l.a, na akamwandikia Walid bin U'tbah ambaye alikuwa gavana wa Madina:

Ama baad:. Hakika Muawiyyah alikuwa mja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu, alimtukuza, akamteua kisha akampa uwezo kisha akamchukua kwenda kwenye makazi yake, pepo yake, rehema yake na adhabu yake. Aliishi kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na amekufa kwa mauti. Na alikuwa ameniahidi na kuniusia kujihadhari na watu wa Abu Turaab (Ally bin Abi Twalib (a.s) kwa wepesi wao wa kumwaga damu, na umeshajua ushujaa ewe Walid kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu kupitia kwa watu wa Abu Sufiyan atalipiza kisasi kwa Uthmani aliyedhulumiwa. Kwa sababu wao ni wafuasi wa haki na wanaotafuta uadilifu. Hivyo itakapokufikia barua yangu hii chukua kiapo cha utii kwa watu wote wa Madina.

Kisha akaambatanisha barua yake na karatasi ndogo akasema ndani yake: Chukua kiapo cha utii kwa Hussein, Abdullah bin Umar, Abdurrahmaan bin Abi Bakr na Abdullah bin Zuber kwa ukali zaidi, na atakaye kataa kata shingo yake na tuma kichwa chake kwangu.

Gavana Walid alifanya kazi hii, alituma ujumbe kwa Hussein (a.s) na Ibn Zuber katika nusu ya usiku kwa kutaka kutumia fursa ya kutoa kwao kiapo cha utii kabla ya watu wengine. Mjumbe wake Abdurrahmaan bin Uthmani bin Afan aliwakuta katika msikiti wa Nabii saww, Ibn Zuber akaogopa kutokana na wito huu ambao haukuwa katika wakati ambao ni wa kawaida Gavana kukutana na watu, lakini Imamu (Khalifa) wa zamani hizo Imamu Hussein (a.s) mwanamapinduzi alimweleza juu ya Jambo la ghaibu, nalo ni kufa kwa Muawiyyah l.a, na kwamba yeye anataka kiapo cha utii kwao, na akatilia nguvu hilo Hussein (a.s) kwa kile alichokiona katika ndoto ya kuwaka moto katika nyumba ya Muawiyyah na kwamba mimbari yake imepinduka.

Na akamweleza Ibn Zuber ambayo Hussein (a.s) ameazimia, nayo ni kukutana na Gavana katika wakati huu, ndipo Ibn Zuber akamshauri kuchukua tahadhari ya ujanja, lakini Hussein (a.s) akamjulisha uwezo wake wa kumzuia.

Hussein (a.s) alimwendea Gavana na watu thalathini miongoni mwao walikuwa ni watumwa wake, familia yake na wafuasi wake wakiwa wamebeba silaha ili wawe mlangoni wamnusuru atakapopaza sauti yake. Na mkononi mwake alikuwa na fimbo ya Mtume (s.a.w.w).

Abu Abdillahi alipoingia kwenye baraza, Walid alimpa Rambirambi kwa kifo cha Muawiyyah, kisha akamwambia ampe kiapo cha utii Yazeed. Imamu Hussein (a.s) akajibu kwa kusema :. Aliye mfano wangu mimi hatoi kiapo cha utii kwa siri. Utakapowaita watu kuja kutoa kiapo cha utii basi utatuita pamoja nao na jambo letu litakuwa ni moja tu.

Walid akatosheka, lakini Marwan bin Hakam alikwenda mbali kwa kusema :. Akiponyoka sasa na hakutoa kiapo cha utii hutamuweza baadaye hadi mauaji yawe mengi baina yenu, lakini mzuie mpaka atoe kiapo cha utii au mkate shingo.

Hussein (a.s) akasema: Ewe Ibn Zaraqau! Wewe utaniuwa au yeye? Umesema uongo na umepata dhambi. Kisha akamwelekea Walid na kumwambia :. Ewe Amiri, sisi ni watu wa Nyumba ya Utume na hazina ya ujumbe, wenye kuteremkiwa na Malaika, kwetu Mwenyezi Mungu amefungua (Raho zilizoumbwa mwanzo) na kwetu amehitimisha. Na Yazeed ni mtu mnywa pombe, muuwaji wa nafsi isiyo na hatia, mwenye kutangaza ufisadi. Mtu aliye mfano wangu hampi kiapo cha utii aliye mfano wa Yazeed. Lakini tutaamka nanyi mtaamka na tutaona nanyi mtaona ni yupi kati yetu ana haki zaidi ya Ukhalifa.

Walid akawa mkali katika mazungumzo yake, na sauti ikasikika, wanaume kumi na tisa wakavamia wakibeba panga zao na wakamtoa Hussein (a.s) kwa nguvu hadi kwenye nyumba yake. Marwan akamwambia Walid: Umeniasi, Wallahi hatutamuweza aliye mfano wake. Walid akasema: Mlaumu mwingine, ewe Marwan umenichagulia yaliyo na maangamio ya dini yangu, nimuuwe Hussein kwa kusema sitoi kiapo cha utii, Wallahi mtu atakaye hukumiwa kwa damu ya Hussein (a.s) ni lazima atakuwa na Mizan (ya wema) nyepesi siku ya kiyama na wala hatotukuzwa, na atakuwa na adhabu iumizayo.

Fuatana nami sehemu ya tano historia ya Maasum Hussein (a.s).

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini