HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 6
IMAMU HUSSEIN (A.S)
Sehemu ya Sita
JIHADI YA IMAMU HUSSEN BIN ALIY (A.S). 3
NDUGU JAMAA NA MARAFIKI WAMSHAURI IMAMU HUSSEIN (A.S).
Umar al At raf akamwambia Imamu Hussein (a.s) : Amenisimulia Abu Muhammad Hassan (a.s) kutoka kwa baba yake Amirul Muuminina Aliy (a.s) kuwa hakika wewe utauliwa, hivyo kama utatoa kiapo cha utii itakuwa Kheir kwako. Hussein (a.s) akasema :. Ameniusia baba yangu Ally (a.s) kwamba Mtume (s.a.w.w) amempa habari za kuuliwa kwake na kuuliwa kwangu, na kwamba kaburi lake litakuwa karibu na kaburi langu, je unadhani umejua nisiyoyajua? Na mimi sionyeshi udhaifu katika nafsi yangu kamwe. Fatimah atakutana na baba yake akilalamika kutokana na yaliyokipata kizazi chake kutoka katika ummah wake, na wala hataingia peponi atakaye muudhi kupitia kizazi chake.
Na Muhammad bin Hanafiyyah akasema :. Ewe ndugu yangu wewe ni Mtukufu mno kwangu, na sitatoa nasaha kwa yeyote katika viumbe isipokuwa kwako, na wewe una haki zaidi kwayo, jinasue kwa kiapo cha utii, watu kama watakupa kiapo cha utii utamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hilo, na kama watakusanyika kwa mwingine Mwenyezi Mungu hatapunguza kwa hilo dini yako wala akili yako, utu wako hautaondoka wala fadhila yako. Hakika mimi naogopa kwako usije ukaingia mji miongoni mwa miji hii na watu wakahitilafiana baina yao, kundi likawa pamoja nawe na jingine dhidi yako, wakauwana na ukawa mlengwa wa kwanza kwa mapanga.
Hivyo mbora wa ummah huu wote kwa nafsi, kwa baba na mama akawa ni mwenye kupoteza damu na ni mtu dhalili zaidi.
Hussein (a.s) akasema :. Basi nitakwenda wapi? Akasema :. Nenda Makkah kama kuna mji utakaokupokea, vinginevyo utakwenda jangwani, mabondeni na milimani na utatoka mji hadi mji mpaka uangalie jambo la watu litakuwaje, hakika wewe ni mwenye rai ya sawa na msimamo madhubuti mpaka uyakabili mambo sawa sawa na kamwe hayatakuwa na mushkeli kwako utakapoyaacha yazunguke.
Hussein (a.s) akasema: Ewe ndugu yangu kama pasingekuwa na hifadhi wala makazi nisingempa Yazeed bin Muawiyyah l.a kiapo cha utii. Muhammad akakata maneno yake kwa kilio. Hussein (a.s) akasema :. Ewe ndugu yangu, Mwenyezi Mungu akulipe Kheir, hakika umeshatoa nasaha na umeshauri sawa sawa, mimi nimeazimia kutoka kwenda Makkah na nimejiandaa kwa hilo mimi na ndugu zangu, watoto wa ndugu yangu na wafuasi wangu, jambo lao ni jambo langu na rai yao ni rai yangu. Ama wewe usijali kuishi Madina na utakuwa jicho langu kwao na hakifichikani kwangu kitu katika mambo yao. Akaondoka kwa Ibn Hanafiyyah na akaingia msikitini huku akisoma beti za shairi:
Siogopi vita katika mapambazuko ya asubuhi, Kwa kuleta mageuzi na wala sitamwacha Yazeed.
Hata siku moja, sikubali Dhulma kwa kuogopa mauti, Hali nimeandamwa na kuwindwa na mauti.
Abu said Al Maqbari akamsikia na akajua kuwa yeye anataka jambo kubwa.
HUSSEIN (A.S) AKUTANA NA UMMU SALAMA.
Ummu salama (mke wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w)) akasema: Usinihuzunishe kwa kutoka kwako kwenda Iraq, hakika mimi nimemsikia babu yako Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) anasema: Atauliwa mtoto wako Hussein (a.s) katika ardhi ya Iraq katika sehemu inayoitwa Karbala. Na nina udongo wake kwenye chupa aliyonipa Nabii (s.a.w.w).
Hussein (a.s) akasema: Ewe mama yangu na mimi najua kwamba mimi ni mwenye kuuliwa, Mwenye kuchinjwa, kwa Dhulma na kwa uadui, na ameshataka Mwenyezi Mungu Mtukufu kuona familia yangu na wafuasi wangu wanafukuzwa, na watoto wangu ni wenye kuchinjwa, wenye kutekwa, wamefungwa pingu hali wao wanataka msaada na wala hawapati mwenye kuwanusuru.
Ummu salama akasema: Ni ajabu ilioje, lini utakwenda na wewe ni mwenye kuuliwa? Hussein (a.s) Akasema: Ewe mama yangu! Kama sitakwenda leo nitakwenda kesho, nitakwenda baada ya kesho na Wallahi katika mauti hakuna budi, na hakika mimi najua siku ambayo nitauliwa, saa nitakayouliwa na shimo ambalo nitazikwa humo kama ninavyokujua wewe, nalitazama kama ninavyokutazama, na ukitaka ewe mama yangu nitakuonyesha kaburi langu na makaburi ya wafuasi wangu.
Ummu salama akaomba hilo kwake, ndipo akamuonyesha udongo unaotokana na udongo huo na akamwamuru auhifadhi kwenye chupa, na atakapouona umetoka damu basi atakuwa na yakini ya kifo chake. Na ilipofika siku ya Ashura alizitazama chupa zote mbili baada ya Adhuhuri, alipomuona Mtume (s.a.w.w) kwenye ndoto amevumbika huku akikusanya damu kwenye chupa, Ummu salama alipozinduka usingizini alikimbilia zile chupa basi akaona zinatoka damu.
Jambo la kutoka Hussein (a.s) likawa kubwa kwa wanawake wa Bani Abdul Mutwalibi, wakakusanyika kwa kilio, Hussein (a.s) akawaendea na akawanyamazisha na akasema :. Nawashauri msidhihirishe jambo hili kwa kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wakasema :. Tutambakizia nani kilio? Kuombeleza kwetu leo ni kama siku aliyokufa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Ally, Fatimah, Hassan, Zainabu na Ummu Kuluthumu (a.s) hivyo tunakushauri usiende. Tunakusihi kwa haki ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ajaalie tuwe fidia kwako kutokana na mauti ewe kipenzi cha wema miongoni mwa watu wafu.
Na mmoja katika shangazi zake akampa habari kwamba amesikia sauti inasema :. Hakika muuliwa wa Twaffu ni katika Bani Hashim, amedhalilisha shingo za Makurayshi nazo zikawa dhalili. Ndipo Hussein (a.s) akamtaka awe na subira na akamjulisha kwamba hili ni jambo lenye kuwa, na ni hukumu iliyohukumiwa.
HUSSEIN (A.S) AKUTANA NA ABDULLAH BIN UMAR BIN KHATABI r.a
Abdullah bin Umar akamtaka Hussein (a.s) abaki Madina, Hussein (a.s) akakataa na akasema :. Ewe Abdillahi hakika miongoni mwa fedheha ya kidunia kwa Mwenyezi Mungu ni kwamba kichwa cha Yahaya bin Zakaria kilitolewa zawadi kwa Muovu katika waovu wa Bani Israeli, na kichwa changu kitatolewa zawadi kwa waovu wa Bani Umayyah. Je, hukujua kwamba Bani Israeli walikuwa wanawauwa Manabii Sabini baina ya kuchomoza jua na kuzama kwake, kisha wanauza na kununua kana kwamba hawakufanya kitu, na Mwenyezi Mungu hakuwaadhibu upesi bali baadaye aliwaadhibu adhabu kubwa yenye kuangamiza.
Ibun Umar alipojua kutoka kwa Hussein (a.s) azma ya kutoka Madina, akamwambia :. Ewe Aba Abdillahi, nifunulie sehemu ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuacha kuibusu kwako. Basi akamfunulia kitovu chake, Abdullah akakibusu mara tatu na akalia sana. Hussein (a.s) akamwambia :. Muogope Mwenyezi Mungu ewe Aba Abdulrahman na wala usiache kuninusuru.
Fuatana nami sehemu ya saba historia ya Maasumu Hussein bin Aliy (a.s).