Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KISA CHA MAYAHUDI WALIOVUNJA SABATO

0 Voti 00.0 / 5

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI

KISA CHA MAYAHUDI WALIOVUNJA SABATO

Kisa hiki kimetajwa ndani ya Qurani tukufu. Na watu hawa walikuwa ni Mayahudi ambao walivunja taadhima ya siku hiyo ya Jumamosi. Nao walikuwa wakaazi wa mji ulioitwa Ayla, mji huo ulioko kati ya Madyan na Tuwr ambao uko kando ya bahari. Hawa Mayahudi walikuwa ni wavuvi wa samaki. Ibn Abbaas R.A.A. kasema: "Walikuwa wameshika dini ya Taurati iliyoharamisha kufanya kazi siku hiyo ya Jumamosi katika zama zao.

Na sheria iliyokuwamo ndani ya Taurati iliwaharamishia kuvua samaki siku hiyo ya Jumamosi. Licha ya kuharamishwa kuvua samaki bali ilikuwa hata haramu kufanya kazi yoyote ile ya kujipatia fedha, kwani haikuwa ni siku ya kufanya kazi bali Mola Mtukufu aliifanya iwe ni siku ya ibada yao tu ya kumtukuza Mwenyezi Mungu.

Mola alijalia siku hiyo ya mapumziko wawe samaki wengi sana juu ya bahari, na uwingi wao ulikuwa kuliko siku yoyote ile nyingine. Na hayo hayakutokea isipokuwa ulikuwa ni mtihani na majaribio makubwa uliotoka kwa Mola wao wa kutii na kuasi, na hii haikuwa ila baada ya kuzidi zile kufuru zao walizokuwa wakizifanya.

Kwa hali hiyo baadhi yao wakavutika kuwaona samaki wengi wakiogelea juu ya bahari siku hiyo ya Jumamosi ambayo walikatazwa kuvua samaki, hivyo wakafanya ujanja wa kuweka nyavu zao za kutegea samaki siku ya Ijumaa pamoja na kuchimba mifereji ya maji kutoka baharini mpaka kwenye mitego ya samaki waliyounda wao wenyewe.

Na kila samaki aliyeingia humo mferejini alishindwa kutoka. Nao wakawa wakienda kuwachukuwa samaki hao siku ya Jumapili. Ikawa siku ya Jumamosi haikupita bure bila kazi. Vitendo vyao hivi vilimghadhibisha sana Mola Mtukufu kisha akawalani kwa kule kwenda kinyume na kuvunja amri Yake kwa kufanya hila ambazo zilikuwa wazi kabisa kwa mtu yeyote yule mwenye kuona.

Na walipokwenda kinyume na ile amri ya Mola Mtukufu, baadhi yao ambao hawakuvunja sheria ya Jumamosi waligawanyika makundi mawili. Kundi moja liliwalaumu na kuwakataza wale watu wakosefu waliokwenda kinyume na sheria hiyo ya kuvua samaki. Na kundi la pili hawakufanya hivyo wala hawakukataza bali waliwalaumu wale watu waliokataza kufanya kile kitendo cha uovu cha kuvua smaki wakasema: "Faida gani ya kuwakataza watu ambao tanguwapo Mwenyezi Mungu atawateketeza au atawaadhibu adhabu kali?"

Lakini lile kundi la kwanza lilijibu: "Ili uwe ni udhuru kwa Mola wenu ya kukataza mabaya na kuamrisha mema, kisha sisi kuepukana na adhabu Yake, na huenda nao wakatubu wakamcha Mungu wakaacha kile kitendo kiovu baadaye Mola wao akawasamehe madhambi yao." Na walipoendelea kwa yale waliokatazwa Mola Mtukufu aliwaadhibu wao pamoja na lile kundi la pili ambalo halikukataza mabaya." Kisa hiki kimetolewa kwa urefu katika Suratil A`araaf tangu aya ya 163 hadi 166, "

وَاسْأَلْهُمْ عَنْ الْقَرْيَةِ الَّتِي كَانَتْ حَاضِرَةَ الْبَحْرِ إِذْ يَعْدُونَ فِي السَّبْتِ إِذْ تَأْتِيهِمْ حِيتَانُهُمْ يَوْمَ سَبْتِهِمْ شُرَّعًا وَيَوْمَ لا يَسْبِتُونَ لا تَأْتِيهِمْ كَذَلِكَ نَبْلُوهُمْ بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ * وَإِذْ قَالَتْ أُمَّةٌ مِنْهُمْ لِمَ تَعِظُونَ قَوْمًا اللَّهُ مُهْلِكُهُمْ أَوْ مُعَذِّبُهُمْ عَذَابًا شَدِيدًا قَالُوا مَعْذِرَةً إِلَى رَبِّكُمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ * فَلَمَّا نَسُوا مَا ذُكِّرُوا بِهِ أَنْجَيْنَا الَّذِينَ يَنْهَوْنَ عَنْ السُّوءِ وَأَخَذْنَا الَّذِينَ ظَلَمُوا بِعَذَابٍ بَئِيسٍ بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ * فَلَمَّا عَتَوْا عَنْ مَا نُهُوا عَنْهُ قُلْنَا لَهُمْ كُونُوا قِرَدَةً خَاسِئِينَ

Maana yake, "Na waulize khabari za mji uliokuwa kando ya bahari, wakiivunja Sabato (Jumaamosi ya mapumziko). Samaki walikuwa wakiwajia juu juu siku ya mapumziko yao, na siku zisiokuwa za kupumzika hawakuwa wakiwajia. Kwa namna hiyo tuliwajaribu kwa sababu walikuwa wakifanya upotofu.

Na kikundi kati yao walisema: "Kwa nini mnawawaidhi watu ambao tanguwapo Mwenyezi Mungu atawateketeza au atawaadhibu adhabu kali?" Wakasema: "Ili uwe ni udhuru kwa Mola wenu, na huenda nao wakamcha Mungu." Basi walipoyasahau waliyokumbushwa, tuliwaokoa waliokuwa wakikataza maovu, na tukawatesa waliodhulumu kwa adhabu mbaya kwa vile walivyokuwa wakifanya upotofu. Walipojifakharisha katika waliyo kanywa tuliwaambia: "Kuweni manyani wa kudharauliwa."

Na pia katika Suratil Baqarah aya ya 65 na ya 66, "

وَلَقَدْ عَلِمْتُمْ الَّذِينَ اعْتَدَوْا مِنْكُمْ فِي السَّبْتِ فَقُلْنَا لَهُمْ كُونُوا قِرَدَةً خَاسِئِينَ * فَجَعَلْنَاهَا نَكَالاً لِمَا بَيْنَ يَدَيْهَا وَمَا خَلْفَهَا وَمَوْعِظَةً لِلْمُتَّقِينَ

Maana yake, "Na hakika mlikwisha yajua ya wale miongoni mwenu walioivunja Sabato (ambayo ilikuwa ni siku ya mapumziko, Jumamosi) na tukawaambiya: "Kuweni manyani wadhalilifu." Kwa hivyo tukayafanya hayo kuwa onyo kwa wale waliokuwa katika zama zao na waliokuja baada yao, na mawaidha kwa wachaMungu." Pia kimetolewa katika Suratin Nisaa aya ya 47, "

…أو نَلْعَنَهُمْ كَمَا لَعَنَّا أَصْحَابَ السَّبْتِ وَكَانَ أَمْرُ اللَّهِ مَفْعُولاً

Maana yake, "…Au tukawalaani kama tulivyowalani watu wa Sabato (Jumaamosi). Na amri ya Mwenyezi Mungu ni lazima ifanyike."

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini