Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA IMAMU HUSSEIN (A.S) 16

0 Voti 00.0 / 5

IMAMU HUSSEIN A S

Sehemu ya Thelathini

Jihadi ya Imamu Hussein Bin Ally as 27

SIKU YA ASHURA.

BWANA WA MASHAHIDI.

Imamu Hussein a.s alisema siku ya Ashura :

ألا وإن الدعي إبن الدعي قد ركز بين إثنتين بين السلة والذلة يأبى الله ذلك ورسوله والمؤمنين و حجور طابت وطهور وأنوف حمية ونفوس أبية من أن توثر طاعة اللئام على مصارع الكرام.

Ehe! Hakika mtoto wa zina (Yazeed bin Muawiyyah l.a) ameniweka kati ya mambo mawili, kati ya makali ya upanga na udhalili, na kamwe hatutachagua udhalili. Mwenyezi Mungu, Mtume wake waumini, mapaja mema na yaliyo safi, pua zenye uzalendo na nafsi zenye kujiheshimu, wote wamekataa hilo kwa ajili yetu kuchagua kumtii Muovu kabla ya kifo cha heshima.

Imamu Hussein a.s alisema siku hiyo ya Ashura :.

لا والله لاأعطيكم بيدي إعطاء الذليل ولا أفر فرار العبيد

Hapana! Wallahi sintatoa mkono wangu kwenu utoaji wa mtu dhalili na wala sintakimbia ukimbiaji wa Mtumwa.

Na ikiwa dini ya babu yangu haitakuwa imara isipokuwa ni kwa kuuawa kwangu basi enyi mapanga njooni mnichukue.

Hussein a.s akasonga mbele kuelekea kaumu na hali amechomoa upanga wake na ameyapa nyongo maisha, na akawataka watu wajitokeze na hakuacha kumuuwa kila aliyejitokeza hadi akauwa kundi kubwa, kisha akashambulia huku akisema :.

القتل أولى من ركوب العار والعار أولى من ركوب النار.

Mauti ni bora kuliko fedheha,na fedheha ni bora kuliko kuingia Motoni.

Mimi ni Hussein bin Aliy a.s, nimependa kutopuuzwa,Nahami watoto wa baba yangu, napita katika dini ya Nabii.

Abdullah bin Ammar bin Yaghuth amesema :

Katu Sijaona shujaa aliyezidiwa kwa idadi ambaye mtoto wake ameuliwa, watu wa Nyumba Yake na masahaba wake wameuwawa lakini akaendelea kuwa shujaa kama alivyokuwa Hussein a.s. Hakika askari wa adui walikuwa wakimshambulia naye akiwashambulia kwa upanga wake, alikuwa akishambuli kikosi cha askari elfu thalathini walio pamoja, lakini yeye peke yake wanashindwa na kukimbia kama nzige waliotawanywa, kisha anarejea kwenye kituo huku akisema :

لاحول ولا قوة الا بالله العلي العظيم.

Hakuna ujanja wala nguvu isipokuwa ni kwa msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu aliyetukuka.

Umar bin Saad l.a akalipigia kelele kundi :. Huyu ni mtoto mwenye kipara mwenye tumbo kubwa, huyu ni mtoto wa muuwaji wa (mushirikina) waarabu, mshambulieni kwa kila upande. Basi ikamjia mishale elfu nne na wanaume wakamzunguka baina yake na hema lake. Imamu Hussein a.s akapiga kelele :. Enyi wafuasi wa (Banu umayyah) Abu Sufiyan, kama hamna dini na ikiwa hamuogopi siku ya kiyama, basi kuweni huru katika dunia yenu na rejeeni katika koo zenu kama nyinyi ni waarabu kama mnavyodai.

Shimr I.a akamwita: Unasemaje ewe mtoto wa Fatimah? Imamu Hussein a.s akasema :. Mimi ndio ninaowapiga vita na wanawake hawana hatia, wazuieni waovu wenu kushambulia familia yangu maadamu ningali hai.

Shimr I.a akasema :. Umekubaliwa hilo. Watu wakamwelekea na mapigano yakawa makali hali ameshazidiwa na kiu, akashambulia upande wa mto Furat kwa Amru bin al Hajjaj na alikuwa na watu wapatao elfu nne, akawasogeza mbali na maji, Farasi wake akaingia ndani ya maji, alipotaka kunywa Hussein a.s akasema :. Wewe una kiu na mimi nina kiu, hivyo sinywi hadi wewe unywe. Basi Farasi akanyanyua kichwa chake kana kwamba amefahamu maneno, Hussein a.s aliponyoosha mkono ili anywe mtu akamwita :. Unaburudika kwa maji na familia yako inavunjiwa heshima? Akatupa maji na hakunywa na akaelekea kwenye hema.

KUAGA

Kisha Imamu Hussein a.s aliaga familia yake na akawaamuru kusubiri na akavaa shuka na akasema :. Jiandaeni kwa balaa na Jueni kwamba Mwenyezi Mungu atawalinda na atawahifadhi na atawaokoeni na Shari ya maadui, na atajaalia mwisho wenu kuwa ni Kheir na atawaadhibu maadui wenu kwa aina za adhabu, na kuwabadilishia balaa hii kwa aina ya neema na utukufu, hivyo msiwe na shaka wala msiseme yanayopunguza hadhi yenu.

Umar bin Saad l.a akasema :. Ole wenu, mshambulieni maadamu anajishughulisha na nafsi yake na familia yake. Wallahi akimaliza hamtafanya vizuri kuliani kwenu wala kushotoni kwenu, basi wakamshambulia kwa mishale hadi mishale ikapishana katika ncha za Mahema, na mishale ikapenya katika pazia la wanawake, wakashangaa na wakaogopa wakapiga kelele na wakaingia ndani ya Mahema huku wakimwangalia Hussein a.s atafanya nini? Akawashambulia kama simba aliyekasirika, hamkuti mtu isipokuwa anampasua kwa panga lake na kumuuwa, mishale ikamjia toka kila pande huku akiizuia kwa kifua chake na shingo lake. Akarejea kwenye kituo chake hali akisema kwa wingi :.

لا حول ولا قوه الا بالله العلي العظيم.

Hakuna ujanja wala nguvu isipokuwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu aliye juu.

Akiwa katika hali hii aliomba maji. Shimr I.a akasema :. Hutoyaonja hadi uingie motoni. Mtu mmoja akamwita: Ewe Hussein! Je, huoni Furat kana kwamba ni Matumbo ya nyoka? Hutoyanywa hadi ufe kwa kiu. Hussein a.s akasema: Ewe Mwenyezi Mungu, muuwe hali ya kuwa ana kiu. Hivyo mtu huyo alikuwa anaomba maji na anapewa na anayanywa hadi yanatoka katika kinywa chake lakini hayakati kiu, na hakuacha kuwa hivyo hadi akafa hali ya kuwa na kiu kali.

Hussein a.s aliwauwa idadi kubwa ya askari wa adui yapata elfu nne 4000, hadi upanga ukawa butu, alichoka akataka kupumzika kidogo. Mara Abu al Hatuf al Ja'fiy akamtupia mshale katika uso wake, na Hussein a.s akautoa na damu ikatoka nyingi katika uso wake, Hussein a.s akasema: Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika wewe unaona yaliyonifika kutoka kwa waja wako hawa waovu, eee Mwenyezi Mungu, punguza idadi yao na waangamize kabisa na wala usiache katika ardhi yeyote kati yao aslani, na wala usiwasamehe abadani.

Kisha akapaza sauti: Enyi umma Muovu, ni mabaya yaliyoje mliomtendea Muhammad saww katika kizazi chake? Hakika nyinyi hamtamuuwa mtu baada yangu huku mkiogopa kumuuwa, bali kitendo hicho mtakipenda sana baada ya kuniuwa mimi. Eee Wallahi hakika mimi nataraji Mwenyezi Mungu atanikirimu kwa kupata shahada, kisha atanilipizia kisasi kwenu bila nyinyi kuhisi. Al Hasiyn akasema: Na ni kwa kitu gani atakulipizia kisasi kwetu ewe mtoto wa Fatimah? Hussein a.s akasema: Atatupia uovu wenu baina yenu na atamwaga damu yenu kisha atawaletea adhabu baada ya adhabu.

Imamu Hussein a.s alipodhoofika na kushindwa kupigana alisimama ili ampumzike, ndipo mtu mmoja akamtupia jiwe usoni mwake, damu ikatiririka usoni mwake, akachukua nguo ili kufuta damu machoni mwake, mtu mwingine akamtupia mshale mkali wenye ncha tatu ukampiga moyoni mwake, Hussein a.s akasema :. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, na kwa mujibu wa mila ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akanyanyua kichwa chake mbinguni na akasema :. Ewe Mola wangu hakika wewe unajua kwamba wao wanamuuwa mtu ambaye hakuna tena katika uso wa ardhi mtoto wa Nabii zaidi yake yeye.

Kisha akatoa mshale shisogoni mwake na damu ikabubujika kama mfereji, akaweka mkono wake chini ya jeraha, ulipojaa damu akaitupa juu mbinguni na akasema :. Ni mepesi yaliyoniteremkia, hakika ni katika uangalizi wa Mwenyezi Mungu. Na halikudondoka katika damu hiyo hata tone moja ardhini, kisha akaweka mara ya pili, ulipojaa akapaka kichwa chake, uso wake na ndevu zake na akasema :. Hivi ndivyo nitakavyokuwa hadi nikutane na Mwenyezi Mungu na babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu nami nikiwa nimetapakaa damu yangu, na nitasema: Eee babu yangu ameniuwa fulani na fulani.

Akatokea mwanaume mwingine akampiga kiunoni akaanguka kutoka juu ya Farasi na hakufika chini kwa jinsi mishale ilivyokuwa mingi mwilini mwake akawa juu ya mishale hiyo.

Fuatana nami Sehemu ya thelathini na moja ya historia ya Imamu Hussein as , mapambano ya Bwana wa Mashahidi 2

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini