HISTORIYA YA MTUKUFU MTUME (S.A.W.W) 3
- Imesambazwa tarehe
-
- Mwandishi:
- Hassani Buss
- Chanzo:
- mailto:buHassani Busssihassan@gmail.com
MWAKA WA THELATHINI WA TEMBO ALIZALIWA MSAIDIZI MKUU, MAKAMU NA KAMANDA MKUU WA JESHI LA UISLAMU, ALLY BIN ABI TWALIB AS
Ally alizaliwa tarehe 13 Rajab ya mwaka wa Tembo sawa na tarehe 25.05.600 AD. Binamu yake, Muhammad, alikuwa na miaka thelathini wakati huo. Wazazi wa Ally walikuwa ni Abu Twalib Bin Abdu l Mutwalibi, na Fatimah, bint Asadi, wote wa ukoo wa Banu Hashim.
Ally alizaliwa ndani ya Al Ka'aba huko Makkah. Yule mwanahistori maarufu, Ma'sud, Herodotus wa Waarabu anaandika kwenye UK wa 76 wa Jz ya 2 ya kitabu chake Muruju Dhahab kwamba moja ya ubora wa Ally alikuwa nao ulikuwa kwamba alizaliwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Baadhi ya mabingwa wengine ambao wanaothibisha kuzaliwa kwa Ally ndani ya Al Ka'aba, ni:-
1. Muhammad Ibn Twalha katika Matalibus Suul UK 11
2. Hakimu katika Mustadrak, Jz 111 UK 483
3. Al Umari katika Sharh Ainia UK 15
4. Halabi katika Sira, Jz 1 UK 165
5. Sibt Ibn Jauzi katika Tadhkiratu Khawasul ummah UK 7
6. Ibn Sabagh Malik katika Fusuulul Muhimma UK 14
7.Muhammad bin Yusuf Ganji Shafii katika Kifayatu Talibi UK 261
8. Shablanji katika Nurul Absar, UK 76
9. Ibn Zahraa katika Ghiyathul Ikhtisar, UK 97
10. Edvi katika Nafahatul Quds UK 41
Miongoni mwa wanahistoria wa kisasa, Abbas Mahmoud Al Akkad wa Misri anaandika katika Kitabu chake Al Abqariyat ul Imamu Ally, (Cairo,1970) kwamba Ally bin Abi Twalib alizaliwa ndani ya Al Ka'aba.
Mwanahistori mwingine wa sasa, Mahmoud Said at Tantawi, wa Supreme council of Islamic Affairs ( Baraza la juu la Mashauri ya Kiislamu), Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, anaandika katika UK wa 286 wa kitabu chake kiitwacho Min Fadha'il al Ashrat al Mubashirina bil Janna, kilichochapishwa mwaka 1976 na Matab'a al Ahram at Tijariyya, Cairo, Misri:-
"Rehema za Mwenyezi Mungu Mtukufu ziwe juu ya Ally bin Abi Twalib. Alizaliwa ndani ya Al Ka'aba. Alishuhudia kuchipuka kwa Uislamu; alishuhudia Da'wa ya Muhammad na alikuwa ni Shahidi wa Wahyi (kushuka kwa Qur-ani Tukufu). Mara moja tu aliukubali Uislamu ingawa alikuwa bado mtoto, na alipigana maisha yake yote ili kwamba neno la Mwenyezi Mungu liwe juu kabisa."
Mshairi wa Kiarabu alitunga ubeti ufuatao juu ya kuzaliwa kwa Ally:
Yeye (Ally) ndiye yule ambaye ile nyumba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iligeuzwa kuwa wod ya wazazi;
Na yeye ndiye aliyeyatupa masanamu nje ya nyumba hiyo;
Ally alikuwa mtoto wa kwanza na wa mwisho,
Daima kuzaliwa ndani ya Al Ka'aba.
Ilikuwa ni desturi ya Waarabu kwamba wakati mtoto anapozaliwa, aliwekwa chini ya miguu ya sanamu au masanamu ya ukoo huo, hivyo kuashiria "kumkabidhi" kwa huyo Mungu wa kipagani. Watoto wote wa Kiarabu "walitolewa" kwa masanamu isipokuwa Ally bin Abi Twalib. Wakati watoto wengine wa Kiarabu walipozaliwa, mmoja wa waabudu masanamu alikuja kuwasalimia na kuwabeba mikononi mwake.
Lakini Ally alipozaliwa, Muhammad, mjumbe wa Mwenyezi Mungu wa baadae alikuja kwenye eneo la Al Ka'aba kumsalimia. Alimbeba mtoto huyo mikononi mwake, na kumtoa kwenye kumtumikia Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mtume huyu wa baadae lazima awe alikwishajua kwamba yule mtoto aliyekuwa mikononi mwake siku moja atakujakuwa adui asiyeshindikana wa wanaoabudu masanamu wote na washirikina na wa miungu yao na miungu ya kike. Wakati Ally alipokuwa mkubwa, aling'oa uabudu masanamu na ushirikina kutoka Arabia kwa upanga wake (Dhulfiqaar)
Kuzaliwa ndani ya Al Ka'aba kulikuwa ni moja kati ya sifa nyingi ambazo Mwenyezi Mungu amezijaalia juu ya Ally. Sifa nyingine aliyokuwa nayo ni kwamba kamwe hakuabudu masanamu. Hii nayo inamfanya awe wa kipekee kwa vile Waarabu wote(isipokuwa baadhi ya Bani Hashim) waliabudu masanamu kwa miaka na miaka kabla ya kukana uabudu masanamu na kuukubali Uislamu.
Ni kwa sababu hii ambapo anaitwa, "Karama llahu waj-hahu كرم الله وجهه ("Ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu ameutukuza uso wake.")
Uso wake ulitukuzwa hasa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwani ulikuwa ndiyo uso pekee katika Maswahaba ambao kamwe haukuinama mbele ya Sanamu lolote.
Ally alikuwa ndiye mtoto mdogo kabisa katika familia hiyo. Katika kaka zake watatu, Twalib na Aqili, walikuwa wakubwa kwa miaka kumi zaidi yake.
Kuzaliwa kwa Ally kuliujaza moyo wa Nabii wa baadae furaha isiyo kifani. Mtoto huyu alikuwa ni mtu mmoja "maalumu" kwake yeye. Ingawaje Muhammad alikuwa na binamu wengi wengine na walikuwa na watoto wao wenyewe, na Ally mwenyewe alikuwa na kaka zake wakubwa watatu; lakini hakuonyesha mvuto wowote juu ya yeyote kati yao. Ally, na Ally peke yake ndiye alikuwa kitovu cha mvuto wake na mapenzi.
Wakati Ally alipokuwa na miaka mitano, Muhammad alimchukua kama mtoto wake wa kupanga, na kuanzia hapo tena hawakutengana daima. Kuna hadithi kwamba wakati mmoja kulitokea njaa huko Makkah, na maeneo yanayoizunguka, na Abu Twalib, akiwa katika dhiki kubwa wakati huo, alikuwa akiona ugumu kutunza kundi kubwa la watu. Ilimjia Muhammad kwamba alipaswa kujaribu kupunguza baadhi ya uzito wa majukumu ya ami yake, na alishawishika kwa hiyo, kumchukua Ally. (Hadithi hii siyo ya kweli ni ya kubuniwa)
Ni kweli kweli kwamba Muhammad alimchukua Ally lakini sio kwa sababu iliyoelezwa hapo juu. Katika nafasi ya kwanza kabisa, Abu Twalib hakuwa kwenye hali ya dhiki kubwa kiasi kwamba hakuweza kumlisha mtoto wa miaka mitano; alikuwa ni mtu mweye hadhi kubwa na uwezo, na misafara yake ilikwenda na kurudi kati ya Hijaz na Syria au kati ya Hijaz na Yemen. Katika nafasi ya pili, kulisha mtoto wa miaka mitano kungekuwa vigumu kuleta tofauti yoyote kwa mtu ambaye aliishi hata wageni kama wangekuwa na njaa.
Muhammad na Khadija walimchukua Ally baada ya kufa watoto wao wenyewe wa kiume. Ally kwa hiyo aliziba uwazi katika maisha yao. Lakini Muhammad, Mtume wa baadae, pia alikuwa na sababu nyingine ya kumchukua Ally. Alimchagua Ally kumlea (kimaadili), kumuelimisha na kumuandaa kwa ajili ya takdir kubwa iliyokuwa ikimngojea katika nyakati zijazo.
Dr. Twaha Hussein wa Misri anasema kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenyewe alikuwa Kiongozi wa Ally, mwalimu na mwelekezaji, na hii ni sifa moja nyingine zaidi ambayo anayo Ally, na ambayo hakuna mwingine yeyote katika Maswahaba anayeshirikiana naye kwayo.
Kuhusu Uislamu inasemekana kwamba kati ya dini zote za duniani, ni hii moja pekee iliyokuwa katika mwanga wa historia, na hakuna Sehemu ya hadithi yake iliyoko gizani.
Bernard Lewis anasema:
"Katika insha juu ya Muhammad na chanzo cha Uislamu, Ernest Renan anazungumzia kwamba, tofauti na dini zingine ambazo zilianzishwa kwa usirisiri, Uislamu ulizaliwa katika mwanga kamili wa historia. "Mizizi yake iko kwenye usawa wa ardhi, na maisha ya Mwanzilishi wake yanafahamika vema kwetu sisi kama ya wale waleta mabadiliko wa karne ya kumi na sita.
Kadhalika, inaweza kusemwa kwamba kati ya marafiki na Maswahaba wote wa Muhammad, Mtume wa Uislamu, Ally ndiye pekee aliyekuwa katika mwanga kamili wa historia. Hakuna Sehemu ya maisha yake, ama katika uchanga wake, utoto wake, uvulana wake, ujana wake, uanaume wake au kupevuka kwake, ambayo imefichikana kutoka kwenye mwangaza wa historia. Alikuwa ndiyo kivutio kikuu cha macho yote tangu kuzaliwa kwake mpaka kufa kwake. Kwa upande mwingine Maswahaba waliobaki wa Mtume saww wanakuja kwenye mvuto wa nadhari ya mwanafunzi wa historia baada tu walivyoukubali Uislamu, na kidogo, kama kipo, kinajulikana mpaka kufikia hapo.
Ally alijaaliwa kuwa mkono wa kuume wa Uislamu, na ngao na kingio la Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Takdira au majaaliwa yake yalikuwa kiungo kisichotenganishwa na takdira ya Uislamu, na maisha ya Mtume wake. Alipokuwa katika kila hali ya mambo katika historia ya harakati hii mpya, na alishika nafasi ya kuwa nyota ndani yake. Ilikuwa, kwa dharura, ni nafasi ambayo yeye pekee ndiye angeweza kuishika. Ally, Aliakisi "taswira" ya Muhammad. Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu chenyewe kimemuita (Ally) "nafsi" au mwandani (nafsi ya pili) ya Muhammad katika Aya ya 61 ya sura ya tatu,
فمن حاجك فيه من بعد ما جاءك من العلم فقل تعالوا ندع أبنآءنا وأبنآءكم ونسآءنا ونسآءكم وأنفسنا وأنفسكم ثم نبتهل فنجعل لعنة الله على الكاذبين.
Na atakayebishana nawe katika hili baada ya ujuzi uliokuijia, basi waambie : Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu, na nafsi zetu na nafsi zenu, kisha tuombe kwa unyenyekevu na tuiweke laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie wenye kusema uongo."3:61
Na alionyesha jina lake maarufu toka upande mmoja hadi mwingine, wa historia.
Katika miaka ijayo, muundo wa ufanyaji kazi pamoja wa Muhammad na Ally- Amir na mfuasi - utakuja kuweka "Ufalme wa mbinguni" katika ramani ya dunia.
Fuatana nami Sehemu ya kumi na nane historia ya Ma'asum Mtukufu Mtume Muhammad saww, kuzaliwa kwa Uislamu.
Rejea:
- The Arabs in History, 1960.
- Uislamu 1969.