Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA MTUKUFU MTUME (S.A.W.W) 4

0 Voti 00.0 / 5

NDOA YA MTUKUFU MTUME MUHAMMAD SAWW YAFUNGWA , NA ABU TWALIB AS ASOMA KHOTUBA YA NDOA BAINA YA MTUKUFU MTUME MUHAMMAD SAWW NA MTUKUFU KHADIJA BINT KHUWAILID AS, 10 RABI'UL AWWAL MWAKA WA 25 WA NDOVU

Abu Twalib mlezi wa Bwana harusi alisimama na kusoma hotuba ya ndoa ya Muhammad na Khadija, na hotuba yake au waadhi wake unathibitisha bila shaka yoyote kwamba Abu Twalib alikuwa Muislam Muumini muabudu Mungu mmoja. Alianza hotuba yake katika mfumo wa "Kiislamu" kwa kutoa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu, alisema:

"Utukufu na sifa zote ni zake Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na dunia, na shukrani zote ni zake kwa rehema zake zote, riziki na huruma. Ametuleta sisi hapa duniani kutokana na vizazi vya Ibrahim na Ismail. Alitufanya sisi waangalizi wa Msikiti  na kuwa viongozi wa Nyumba yake, Al Ka'aba, ambayo ni kimbilio la viumbe wake wote. Baada ya utangulizi huu Abu Twalib aliendelea:

" Mpwa wangu, Muhammad bin Abdillah Bin Abdu l Mutwalibi, ni mtu mzuri kuliko wote katika jamii ya binadamu kiakili, hekima, uzao ulio safi, utakakatifu wa maisha yake mwenyewe, na kwa heshima ya familia. Anazo dalili zote za mtu ambaye hatimaye atakuwa mtu mkubwa. Anamuoa Khadija bint Khuwaylid kwa mahari ya vipande 400 vya dhahabu. Natangaza kwamba Muhammad na Khadija sasa ni mume na mke. Mwenyezi Mungu na awabariki wote, na awe Mlinzi wao."

Kwa hotuba yake, Abu Twalib alitangaza kwamba ukoo wa Banu Hashim walikuwa warithi wa Ibrahim na Ismail, na walikuwa wabebaji au wachukuaji wa urithi huo. Kwa hiyo, hawakuchafuliwa na ibada ya masanamu.

Abu Twalib alipomaliza hotuba yake, Waraqa bin Naufal alisimama na kusoma hotuba ya ndoa kwa niaba ya Bibi harusi, Khadija. Alisema:

"Sifa zote na utukufu wote anastahiki kupewa Mwenyezi Mungu. Tunashuhudia na kukiri kwamba yale ambayo umeyatamka kuhusu Bani Hashim ni kweli, kweli tupu. Hapana mtu anayeweza kukanusha ubora wao. Kwa sababu ya uzuri wao, tunakubali ndoa ya Khadija na Muhammad. Ndoa yao inaziunganisha familia zetu mbili na kuoana kwao imekuwa chanzo cha furaha kubwa kwetu. Enyi Walezi wa Quraishi! Nawatakeni kuwa Mashahidi kwamba ninaridhia Khadija kuolewa na Muhammad bin Abdillah kwa mahari ya vipande 400 vya dhahabu. Mwenyezi Mungu na ajaalie ndoa yao iwe ya furaha na amani."

M. Shibli, mtaalamu wa historia kutoka India, anasema kwamba mahari ya Hadharat Khadija ilikuwa ni vipande 500 vya dhahabu - Siira

Amri bin Asad, ami yake Khadija mwenye umri mkubwa, naye pia alisema kwenye Sherehe hiyo na aliyaunga mkono, kwa maneno yake mwenyewe, yale aliyoyasema Waraqa bin Naufal. Na alikuwa yeye ambaye kama mlezi, wa Bibi harusi, aliridhia na kumtoa Khadija aolewe na Muhammad bin Abdillah. Abu Twalib alilipa mahari ya mpwa wake Muhammad.

Edward Gibbon anasema:

"Nyumbani na ng'ambo, wakati wa amani na vita, Abu Twalib, Ami wa Muhammad aliyekuwa anaheshimiwa sana, alikuwa ni Kiongozi na mlezi wa kijana wake, wakati alipotimiza miaka 25 alimuona mwanamke tajiri mwenye daraja kubwa na mkazi wa Makkah, ambaye alizawadia uaminifu wake kwa kukubali kuolewa naye pamoja na mali yake. Mkataba wa ndoa, katika jinsi rahisi ya kizamani, unasema kuhusu maelewano ya kimapenzi kati ya Muhammad na Khadija, unamwelezea yeye kama ni mtu hodari sana miongoni mwa kabila la Quraishi na unataja mahari ya wakia kumi na mbili za dhahabu na Ngamia Ishirini, ambayo ilitolewa kwa ukarimu wa ami yake Abu Twalib."

Washington Irving, anasema:

"Khadija alijaa imani ya kusisimua aliyokuwa nayo kwa msimamizi wake bora sana, Muhammad. Kwenye Sherehe ya harusi yake, Halima ambaye alikuwa yaya wa Muhammad wakati alipokuwa mtoto mchanga, aliitwa na kupewa zawadi ya kondoo arobaini."

Wageni wote walimpa hongera Muhammad Mustafa siku ya harusi yake na walimtakia maisha ya furaha. Pia walimpongeza ami yake Abu Twalib, kuhusu hafla yenye heri. Pande zote mbili Bwana na Bibi harusi, waliwashukuru wageni wao kwa uchangamfu.

Baada ya kwisha Sherehe hizo, Mkuu wa Itifaki aliwaagiza watumwa kugawa chakula. Chakula kilikuwa kingi kupita kiasi kwani ilikuwa haijapata kutokea hapo Makkah. Wageni walikula chakula kizuri na kila mlo ulikuwa wa mapishi ya aina yake. Wageni walituliza kiu kwa kinywaji kilichochanganywa na maji matamu yatokanayo na maua.

Baada ya chakula kila mgeni alipewa zawadi ya kanzu ya heshima, ili kuafikiana na mila za kale na uungwana wa Arabuni.

Wakati huo huo mkuu wa Itifaki alitangaza kwamba Bibi harusi alikuwa tayari kuondoka.

Ngamia jike aliyetandikwa mapambo ya kitajiri, alibeba kibanda mgongoni kwake, alikuwa anangoja kwenye lango la nyumba. Wageni wote walikusanyika sebleni kumuona Bibi harusi akisindikizwa kwenye lango.

Fuatana nami Sehemu ifuatayo ya Historia ya Ma'asum Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) kumsindikiza Bibi harusi kwenda kwa Bwana harusi.

Rejea:

  1. The Decline and Fall of Roman Empire.
  2. The life of Muhammad.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini