Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA MTUKUFU MTUME (S.A.W.W) 5

0 Voti 00.0 / 5

MTUKUFU MTUME MUHAMMAD SAWW BAADA YA KUFUNGA NDOA NA BAADA YA KARAMU YA HARUSI

SAFARI YA BI HARUSI (KHADIJA BINT KHUWAILID) YAANZA KWENDA KWA BWANA HARUSI (MTUKUFU MTUME MUHAMMAD SAWW)

Watumishi wake walimsaidia Bibi harusi kupanda kwenye kibanda cha harusi.

وقال اركبوا فيها بسم الله مجراها ومرساها إن ربي لغفوررحيم.

"Na akasema: Pandeni humo kwa jina la Mwenyezi Mungu, kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu mlezi ni mwenye kusamehe, mwenye kurehemu."11:41

Mmojawapo wa watumishi wa kike aliketi kwenye kibanda na Bibi harusi. Kwenye kichwa chake, alivalia tiara la maua na nywele zake zilisokotwa kwa utepe wa buluu na ncha zenye lulu za kifahari. Alivalia bangili zenye nakshi ya vito vigumu na zenye kung'ara, na alishika kipepeo kilicho pambwa na vito.

Kikundi cha watumwa wa Kinubi walibeba miange, walitembea mbele ya Ngamia jike kulia na kushoto.

Bwana harusi naye pia alipanda farasi wake, na yeye, na ami zake, vijana wa Bani Hashim na wageni wao, walirudi nyumbani kwa Abu Twalib katika hali na Mavazi yale yale waliyoenda nayo mapema siku ile nyumbani kwa Bibi harusi.

Wakati msafara huu ulioongozwa kwa miange ya moto ulipofika nyumbani kwa Abu Twalib, mke wake dada zake Abu Twalib walimsaidia Bibi harusi kuteremka kutoka kwenye kipando chake, Ngamia jike. Msimamizi mkuu alimkinga kwa mwamvuli wa hariri nyeupe juu ya kichwa chake na akamuongoza kwenye vyumba vya ndani zaidi kwenye nyumba hiyo.

وقل رب أنزلني منزلاً مباركا وانت خير المزلين.

"Na sema: Mola wangu mlezi! Niteremshe mteremsho wenye baraka, na wewe ni mbora wa wateremshaji."23:29.

Kila kitu kilifanyika kwa usahihi wa kiwango cha juu sana. Mawasiliano yalikuwa mazuri sana toka mwanzo hadi mwisho.

Kuoana kwa Muhammad na Khadija ni tukio lililomfurahisha kila mtu lakini furaha ya Abu Twalib ilivuka mipaka ya kawaida. Alikuwa na dukuduku la kumuoza mpwa mke mzuri. Dukuduku hili liligeuka kuwa furaha kubwa isiyo na kifani baada ya mpwa wake na Khadija kuoana. Haingekuwa rahisi kupata malingano kama hayo. Abu Twalib alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa furaha mpya aliyoipata, na furaha yake iliwapata pia ndugu zake, Abbas na Hamza na watu wengine wote wa ukoo wa Hashim.

Siku tatu baada ya harusi, Abu Twalib alifanya Karamu ya chakula kusherehekea tukio ambalo tangu hapo mpaka sasa linaitwa "karamu ya walima." Jiji lote liling'aa kwa ukarimu wake. Kila mkazi wa Makkah alikuwa mgeni mwalikwa wa karamu hiyo . Muhammad ambaye alikuwa Bwana harusi, alikuwa anawakaribisha wageni. Yeye mwenyewe, ami zake, Binamu zake na vijana wote wa ukoo wa Banu Hashim, walijivunia kuwa wenyenji wa Sherehe hiyo.

Karamu hiyo ilidumu kwa muda wa siku tatu. Miaka mingi baadae, Uislamu uliifanya karamu ya walima kuwa kumbukumbu ya karamu ya Abu Twalib alioifanya kwenye harusi ya Muhammad na Khadija, na kuiweka kama desturi ya ndoa zote za waislamu. Abu Twalib alikuwa mtu wa kwanza kuitekeleza. Karamu ya walima haikujulikana katika bara lote la Arabu kabla ya harusi ya Muhammad na Khadija.

Abu Twalib alilazimika kufikiri kama ingewezekana ndugu yake mpendwa Abdullah na mkewe Amina, Mwenyezi Mungu awateremshia rehema zake, wao pia kama wangekuwepo kushuhudia na kuibariki ndoa ya mtoto wao, na kushiriki pamoja katika ile furaha yake (Abu Twalib). Lakini hata kama Abdullah na Amina wangekuwepo, harusi ya mtoto wao haingesherehekewa kwa fahari na tamasha kuzidi alivyofanya Abu Twalib kama mlezi wa Muhammad saww.

Fuatana nami Sehemu ifuatayo Sherehe bado inaendelea Bibi Khadija naye aandaa siku tatu zingine za Karamu ya chakula

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini