Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIYA YA MTUKUFU MTUME (S.A.W.W) 7

0 Voti 00.0 / 5

NDOA YA WATUMISHI WAWILI WA MWENYEZI MUNGU MTUKUFU MTUME MUHAMMAD SAWW NA BI KHADIJA BINT KHUWAILID

Khadija, bint Khuwaylid, alikuwa mkazi wa Makkah. Naye pia alikuwa wa kabila la Quraishi. Aliheshimiwa sana na watu wa Makkah kwa sababu ya tabia yake ya mfano na uwezo wake wa kupanga. Kama vile watu wa Makkah walivyomuita Muhammad "As Sadiq Al Amin', walimuita Khadija "Twahirah", yenye maana ya "Aliye safi." Alikuwa akijulikana pia miongoni mwa Waarabu kama "Malkia wa wafanyabiasha." Wakati wote misafara ilipoondoka Makkah au kurudi Makkah, waliona kwamba mzigo wake ulikuwa mkubwa kwa ujazo kuliko mizigo yote ya wafanyabiasha wa Makkah ikichanganywa pamoja.

Muhammad alipokuwa na umri wa miaka 25 , ami yake na mlezi wake, Abu Twalib, alimshauri Khadija, na kuelewa kwake kwa kimya, kwamba amchague Muhammad kama wakala wake katika mmoja wa misafara yake, uliokuwa uondoke kwenda Syria punde tu.

Khadija kwa kweli alikuwa akihitaji wakala kwa wakati ule hasa. Alikubali kumchagua Muhammad kama wakala wake. Alichukua madaraka ya bidhaa za Khadija, na msafara ukaondoka kwenda Syria. Mtumwa wa Khadija, Maisara, pia alifuatana naye na akamsaidia kama msaidizi wake.

Safari hii ya kibiashara kwenda Syria ilifanikiwa kupita matarajio, Khadija alivutiwa sana na uwezo wa wakala wake na uaminifu wake kiasi kwamba aliamua kumpa madaraka ya shughuli zote za biashara zijazo baadae. Safari hii pia ilithibitisha kuwa mwanzo wa ndoa yao.

Mtarjumi na mfasiri wa Qur-ani tukufu, A. Yusuf Ally, anauliza swali:

"Tunaweza kushangaa jinsi Yakuub alivyokutana na mwanawe Yusuf, au ni jinsi gani Musa alivyokutana na Haruna, au jinsi gani Mtukufu Mtume Muhammad alivyokutana na Bibi Khadija?"

La. Hatuwezi kushangaa. Ilikuwa ni amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba watumishi wake wawili Muhammad na Khadija wangekutana katika ndoa, na walioana.

Katika taarifa isemayo kwamba mmoja wa marafiki wa Khadija alikuwa anatoka kwenye ukoo bora wa Makkah jina lake Nafisa (au Nufaysa) bint Mumyah. Mwanamke huyu alikuwa na habari kwamba Khadija alikwisha kataa posa nyingi za ndoa. Alikuwa anashangaa kama pangetokeza mtu katika Bara Arabu ambaye angekuwa wa kiwango alichoafiki Khadija. Marafiki hawa wawili walizungumzia jambo hili mara nyingi.

Hatimaye, Nafisa alifanya mazungumzo ya mara ya mwisho kuhusu jambo la ndoa yake Khadija na akapata kutambua kwamba rafiki yake Khadija hakujali utajiri, cheo au uwezo wa mume mtarajiwa. Nafisa alijua kwa hakika kwamba rafiki yake Khadija alitaka kuolewa na mtu mweye tabia nzuri, tabia inayokubalika. Khadija alitaka kuolewa na mwanamme mwenye maadili mema na msimamo wa Uadilifu.

Pia Nafisa (au Nufaysa) alijua kwamba alikuwepo mtu wa aina hiyo Makkah na jina lake alikuwa ni Muhammad.

Kuna taarifa isemayo kwamba siku moja Muhammad alikuwa anarudi nyumbani kutoka Al Ka'aba, Nufaysa alimsimamisha na mazungumzo yalifanyika kama ifuatavyo:

Nufaysa: Ewe Muhammad, wewe ni kijana wa kiume na bado hujaoa. Wanaume ambao unawazidi umri, wamekwisha oa na wengine wamezaa watoto. Kwa nini hujaoa?

Muhammad: Bado sina uwezo wa mali; mimi ni fukara.

Nufaysa: Bila kujali ufakiri wako, ungejihisi vipi endapo ungemuoa mwanamke mwenye sura nzuri, tajiri, mashuhuri na mwenye kuheshimika.?

Muhammad: Mwanamke huyu anaweza kuwa nani?

Nufaysa: Mwanamke huyu ni Khadija, bint Khuwaylid.

Muhammad: Khadija?! Inawezekanaje Khadija kukubali kuolewa na mimi? Unajua kwamba wanaume wengi matajiri na wenye uwezo na wakuu wa makabila wamemposa na amewakataa wote.

Nufaysa: Kama wewe upo tayari kumuoa Khadija, sema hivyo, na niachie mambo mengine mimi. Nitapanga kila kitu.

Muhammad alitaka kumwambia ami yake na mlezi wake, Abu Twalib, kuhusu azma ya Nufaysa, na kupata ushauri wake kabla hajatoa jibu.

Abu Twalib alimfahamu Khadija kama alivyokuwa anamfahamu mpwa wake Muhammad. Alikubali ushawishi wa Nafisa. Hakuwa na shaka kwamba Muhammad na Khadija wangekuwa wanandoa makini. Kwa hivyo, alibariki pendekezo la ndoa yao. Hapo hapo Muhammad alimtaarifu Nafisa kwamba pendekezo lake limekubaliwa na hivyo amepata mamlaka ya kuendeleza mazungumzo kuhusu ndoa yake na Khadija.

Mara tu baada ya Abu Twalib kuthibitisha ndoa hiyo, alimtuma dadake, Safiya, kumuona Khadija, na kuzungumza naye kuhusu jambo hilo. Wakati huo huo, Nafisa alikwisha fanya mazungumzo ya awali, na Khadija alikuwa anategemea kupata mgeni kutoka nyumbani kwa wakwe wategemewa. Khadija alimpokea Safiya kwa uchangamfu, alimkirimu, na kumwambia kwamba yeye Khadija alimteua mpwa wake Safiya kuwa mwenzi wake wa maisha bila masharti yoyote. Safiya alifurahishwa sana na mafanikio ya ujumbe wake. Kabla hajaondoka kurudi kwao, Khadija alimpa Safiya kanzu nzuri sana na ambayo aliikubali kwa furaha na shukrani nyingi.

Fuatana nami Sehemu ifuatayo posa lapelekwa na tarehe ya ndoa yapangwa

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini