Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE 4

0 Voti 00.0 / 5

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE

Sehemu ya Nne

TUKIO MUHIMU NDANI YA MSIKITI WA MTUME (S.A.W.W.)

Siku moja Bibi Fatimah (a.s.) alitaka kutoa mhadhara ndani ya msikiti wa Mtume (s.a.w.w). Kabla ya kuanza kuhadhiri alitengenezewa sitara humo Msikitini, akakaa yeye na Waumini wengine wakike upande mmoja na Waumini wanaume wa Kiansari na Muhajirina nao wakakaa upande wa pili. Sitara hii aliyotengenezewa Bibi Fatimah (a.s) ilikuwa ina maana nyingi ndani yake.

Kwanza ilikuwa ni kutekeleza sheria inayohusu Hijabu katika sura ya kuweka kizuizi, ambapo pande mbili hizo zilitenganishwa. Pili, hali hiyo ilikuwa ni kuonesha kutokuukubali kwa vitendo mchanganyiko wa wanaume na wanawake, jambo ambalo maadui wa Uislamu wanatumia kila mbinu kulihalalisha kwa kulitolea hoja batili.

Sasa nakutazama ewe dada yangu wa kiislamu, nikitarajia umeiona mifano hii mitatu inayohusu maisha ya Bibi Fatimah (a.s.) ambaye ni mwanamke bora kuliko wanawake wote duniani, na ni mwanamke anayestahiki kuigwa katika Uislamu. Inafaa uige na ujifunze kwake ili upate kupambika kwa umbile la kike ( yaani kuwa na haya) na utukufu, kadhalika ifanye nafsi yako iwe ya mwanamke Mchamungu mwenye kushika mafunzo ya kiislamu na hukmu za Qur'an. Ewe dada wa kiislamu hebu shikamana na mafunzo ya kiislamu ambayo Mwenyezi Mungu amekupa ili ufanikiwe duniani na akhera. Mafunzo haya yatakupandisha kwenye daraja tukufu la wenye imani na mafanikio. Fahamu kwamba hutafanikiwa isipokuwa uwe umeshikamana na kuyatumia mafunzo hayo kwa kuyatekeleza maishani mwako.

KUJIHESHIMU NDIYO PAMBO LA MWANAMKE

Bwana Mtume (s.a.w.w) amesema, "Kujiheshimu ndiyo pambo la Mwanamke[1]." 

Hapana shaka kwamba pambo limegawanyika sehemu mbili: Pambo lisilo halisi na pambo halisi. Ama pambo lisilo halisi ni lile ambalo linaloonekana wazi, na ni lenye kubakia kwa muda maalum, kisha hutoweka bila hata ya kumuongezea kitu muhusika katika utu wake. Ama lile pambo halisi, ni lile ambalo hubakia muda wote na pia humfanya mwanamke aupate ule utu wake kamili na kumfikisha kwenye daraja ya ukamilifu. Ukweli usiokuwa na shaka ni kuwa, pambo halisi ndilo lenye umuhimu mno kuliko lile jingine, bali ndilo lengo analopaswa kulishughulikia kila mtu. Endapo mtu atakosa kuwa na fungu fulani katika pambo hili halisi, basi pia huwa hana faida yoyote ndani ya lile pambo la dhahiri.

Hapana shaka kwamba kujiheshimu ndilo pambo pekee linalomfaa mwanamke kama alivyosema Bwana Mtume (s.a.w.w). Pambo hilo humjengea mwanamke utu, heshima na utukufu hapa duniani na kesho akhera. Ama madawa ya kujirembesha, manukato na mengineyo miongoni mwa mapambo, yote hayo ni mapambo ya nje tu na hayana maana yoyote khususan mwanamke mwenyewe atakapokuwa si Mchajimungu: Mwenyezi Mungu apishe mbali.

Hijabu ndiyo alama pekee inayoweza kutambulisha Uchaji Mungu wa mwanamke na pia heshima yake na utu wake. Wakati huo huo tabia ya kutokuwa na Hijabu huchafua heshima ya mwanamke na kuacha maswali chungu nzima kuhusu Uchaji Mungu wake na kujiheshimu kwake kwa jumla.

Yote haya yanakuja kwa sababu yeye mwenyewe kauweka mwili wake kuwa maonesho mbele ya maelfu ya watu siku zote. Kutokana na hali kama hiyo, hata huwezi kutambua ni mikono mingapi iliyowahi kuushika mwili wake kwa kuuacha wazi na kutokujisitiri kwa mujibu wa sheria!!

Hivi unadhani watu wa kale na hata wa leo hii, nyoyo zao zitasal imika vipi katika mazingira hayo ya wanawake kuicha wazi miili yao? Kamwe hawatasalimika kabisa, kwani wanawake wanapoiacha wazi miili yao ni jambo linalopelekea tuhuma mbaya kwa wanawake. Imam Ali (a.s.) anasema : "Yeyote mwenye kuiweka nafsi yake mahala penye tuhuma mbaya, basi asimlaumu mtu atakaye mdhania vibaya[2]."

Hapana shaka kwamba, mwanamke asiyekuwa na Hijabu huwa anaidhuru nafsi yake mwenyewe kwa sababu. Kwanza, huwa anapata hasara mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Pili, heshima yake ndani ya jamii huwa inaporomoka.

Hasara anayoipata mwanamke huyo mbele ya Mwenyezi Mungu inakuja kwa sababu mwanamke huyo huwa amekwenda kinyume na kanuni za mbinguni na kukosa utiifu kwa Mwenyezi Mungu. Baadaye tutaeleza adhabu za huko akhera atakazozipata mwanamke asiyejali kujisitiri kwa mujibu wa sheria ya KiIslamu.

Ama hasara atakayoipata mwanamke kutoka na na heshima yake kuporomoka ndani ya jamii, hali hiyo inasababishwa na yeye mwenyewe kutokana na tabia yake ya kuyaacha wazi maungo yake yaonekane kwa kila mtu, hali ambayo humuingiza ndani ya kila aina ya uovu na ufisadi na hatimaye akadhalilika vibaya.

Na tukirejea kwa mwanamke mwenye kujisitiri kwa mujibu wa sheria ya kiislamu, huyu hupata faida za aina mbili kwa pamoja:

Faida aipatayo mbele ya Mwenyezi Mungu ni kwamba, yeye huwa ni mwanamke mtukufu mbele ya Mwenyezi Mungu na Malaika wake pamoja na Mawalii wa Mwenyezi Mungu. Utukufu huu anaupata kwa kuwa amemtii Mola wake, ametekeleza maamrisho yake na ameyasitri maungo ambayo Mwenyezi Mungu ameamrishsa yasitiriwe. Na kwa ajili hii basi, mwanamke kama huyu kamwe hatonyanyua unyayo wake bali rehma za Mwenyezi Mungu huwa ziko pamoja naye, pia radhi za Mwenyezi Mungu humbatana naye, na wakati huo huo Malaika wa Mwenyezi Mungu wanamuombea msamaha. Mwenyezi Mungu anasema: "Kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora na ni chenye kubakia[3]." 

Ama faida atakayoipata ndani ya jamii, ni pale mwanamke huyo anapokuwa ni mwenye kuheshimiwa na kutukuzwa, yote haya anayapata kwa kuwa yeye amejipamba kwa pambo la kujiheshimu na kuuhifadhi utu wake, kisha akausitiri uzuri huo aliopewa na Mwenyezi Mungu.

 

 


[1]. Kalimatur-Rasuli uk 110 cha Sayyid Shirazi.

[2]. Al-kafi juz uk 152. Miongoni mwa dhana mbaya atakayodhaniwa mwanamke asiyejali sitara ya kisheria ni kuwa, wakati wote huonekana yuko tayari kufanya ufisadi. Kama si hivyo, amtazamaye hushawishika kumtendea uovu. Mtarjumi.

[3]. Qur'an 42:36.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini