Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE 5

0 Voti 00.0 / 5

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE

Sehemu ya Tano

KUKOSEKANA SITARA KUNALETA MAOVU

Miongoni mwa maovu na athari mbaya katika jamii, ni wanawake kuacha kuisitiri miili yao ipasavyo, kitu ambacho kimesababisha vijana wetu wa kiume kuteleza na kujikuta wanafanya mambo machafu bila kukusudia. Imam Ali ibn Musa Ar-ridha anasema, "…….Imeharamishwa kuangalia nywele za wanawake, kwani katika kuziangalia nywele hizo kunasababisha kuamsha hisia za wanaume ambazo huwafanya waingie katika maovu na mambo yasiyo halali na yasiyopendeza[1]."11 Hapana shaka kwamba, mwanamke anayetoka nyumbani mwake na kwenda sokoni bila kujali ni vazi gani alilovaa, hajali kama limemsitiri vizuri au hapana, ni wazi kabisa huko njiani ataonekana kwa watu wa aina mbali mbali wakiwemo vijana ambao ndiyo kwanza wanaingia katika rika la ujana na nafsi zao bado hazijaweza kujimiliki kuhusu suala la kijinsiya. Hali kama hii ni lazima itaamsha hisia za kimaumbile za vijana hao kutokana na jinsi mwanamke huyo atakavyokuwa amevaa na umbile lake linavyoonekana kwa jumla pindi atakapopita mbele yao. Hisia hizi za kimaumbile ni lazima ziamke kwa kuwa ndivyo ilivyo hali halisi. Kwa hali hii basi nafsi za vijana hawa kwa tabia ya maumbile ya mwanaadamu huanza kuhangaika kutafuta njia za kuyatosheleza maumbile yao.

Suala la kujiuliza hapa ni je, vijana hawa watafanya nini? Ikiwa wao sio watu walioshikamana na mafunzo ya dini wala hawafuati miongozo ya kiislamu, basi watajaribu kutosheleza hamu zao kwa njia ya siri ambayo ni kujitoa manii jambo ambalo ni hasara na aibu. Ama wengine hufanya baya zaidi ambalo ni kinyume cha utaratibu aliotuwekea Mwenyezi Mungu, hawa hufanya liwati. Kundi jingine wao huamua kuzini na katika huko kuzini huwa wanatumia kila njia kufanikisha azma yao hiyo, ikiwa ni kwa hila au hata kwa nguvu ambayo ni kubaka wanawake mitaani. Matokeo ya ubakaji ni kuvunja heshima za watu na kuwadhalilisha wanawake.

Pamoja na matendo haya kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu, pia yanasababisha maradhi hatari na vifo vya ghafla[2].

Inakadiriwa kwamba idadi ya hospitali zinazo shughulikia maradhi ya uasherati peke yake inafikia hospitali mia sita hamsini.

Hesabu hii ni kwa nchi ya Marekani peke yake. Chanzo cha balaa lote hili ni kwa wale wanawake wasiojali kutenganisha maumbile yao na ya wanaume mpaka wakawa wanaona miili yao haistahiki kulindwa na kupewa hadhi ya pekee. Lakini kila mwanamke asiyezingatia suala la mavazi kisheria ni lazima atambue kwamba, yeye ni mshiriki mkubwa anayesababisha madhambi na misiba hii, na anayo sehemu yake ya adhabu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Yote yaliyotajwa hapa sasa hivi, yanatokana na vijana ambao wao siyo watu wa dini wala hawashikamani na Uislamu. Kwa upande wa pili inawezekana vijana hao wakawa ni watu wa dini na wanaambatana na mafunzo ya kiislamu na sheria zake, basi vijana hao huzuia hisia zao zisivuke mipaka ya Mwenyezi Mungu na hupambana na matamanio ya nafsi zao na kumlaani shetani asije akawahadaa. Vijana hawa huvumilia kero ya maumbile na kubeba mzigo mzito ambao hawakutarajia kuubeba. Kwa mara nyingine tena mwanamke au wanawake wasiojali sheria ya mavazi kama Mwenyezi Mungu alivyoamrisha, wanabeba uzito wa taabu na maudhi yanayowapata watu hawa wa dini.

 


[1]. Biharul Anwaar juz 6 uk 130. Kilichokusudiwa hapa bila shaka ni nywele za mwanamke ambaye si maharim wako wala siyo mkeo. Ikiwa nywele tu zinatosha kumuingiza mwanaume ndani ya madhambi, basi ikoje hali ya watu leo hii kwa namna wanawake wa kileo wanavyovaa.? Je! Ni kwa kiasi gani wanatuingiza katika madhambi? Leo hii siyo nywele tu bali vifua vya wanawake vinaonekana kwa kila mtu na maungo mengi yanakashifiwa na kila mtu. Hivi kweli kwa hali kama hii vijana wetu watasalimika na maovu? Pia hao kina dada nao watamlaumu nani watakapovunjiwa heshima? Mtarjumi.

[2].Asili ya yote hayo ni mwanamke au wanawake ambao kwa makusudi kabisa wanaamua kuvaa nguo ambazo zitahatarisha usalama wao na usalama wa jamii yote. Kuhatarisha usalama wao na wa jamii peke yake haitoshi, bali waelewe kwamba wanasababisha vijana wetu wa kiume kuchuma madhambi makubwa, na wakati mwingine kuwaharibia maisha yao ya baadaye kwa kufungwa jela kutokana na hatia ya kubaka. Madhara mengine yaletwayo na matukio ya zinaa na liwati ni pamoja na kuambukizwa maradhi hatari kama vile kisonono, kaswende, na leo ukimwi. Maradhi haya hatari yameleta huzuni na misiba inayotisha katika ulimwengu. Mtarjumi.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini