Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE 7

0 Voti 00.0 / 5

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE

Sehemu ya Saba

A

KUTOKUVAA HIJABU NA UHARIBIFU WA NDOA

Tangu utamaduni wa kutovaa Hijabu ulipokuwa umeenea baina ya wanawake, yapo matatizo mengi yamezuka katika ndoa, na idadi ya matatizo haya inaongezeka siku hadi siku.

Tatizo hili la ndoa wakati mwingine huwa mume ndiyo sababu kubwa inayochangia uharibifu wa ndoa yake. Hasa pale mume huyu anapochukua fursa ya kutoka yeye na mkewe kwenda kwenye sherehe au mahafali mbali mbali zilizo na mchanganyiko wa wanaume na wanawake au kumpeleka mkewe katika majumba ya starehe na sinema. Wakati mwingine mume huyu hupata akaleta nyumbani kwake wageni wanaume na mkewe akaja kuwapokea kwa tabasamu zuri na kupeana nao mikono na chungu nzima ya makaribisho mengine ambayo mke wa bwana huyu huwafanyia wageni wa mumewe, ikiwa ni pamoja nakuwaletea matunda na vyakula vingine mbali mbali. Yote haya yanafanyika bila ya mume huyu kukumbuka kwamba wageni hao ni wanaume na jinsi yao kimaumbile inatofautiana na maumbile ya mkewe, pia pande mbili hizi hazina uhusiano wa kisheria.

Katika kipindi cha kubakia hapo, wageni hawa huendelea kupata kila aina ya makaribisho yasiyokuwa na mipaka ya kisheria. Kutokana na hali kama hii mara ghafla mume huyu humkuta mkewe amekwishaanzisha uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa marafiki zake hao. Hapa ndipo mume huyu huzusha ugomvi na mkewe na kuwasha moto wa volkano dhidi yake, pamoja na ukweli ulio wazi kwamba, yeye ndiyo sababu iliyoleta huzuni hii kubwa na msiba ndani ya nyumba yao. Mume huyu anasahau kwamba, yeye ndiye aliyekuwa kiongozi na muandalizi wa njia ya mkewe kulifikia giza hili na dhambi hii kubwa.

Baada ya tatizo kama hili baina ya mke na mume, hapo hujitokeza moja katika mambo mawili. Ama mume huyu aendelee kubaki na mkewe huyu muovu katika hali ya maisha ya dhiki yatakayokuwa yakiumiza roho yake na kuiadhibu nafsi yake, na kutokuaminiana tena na mkewe. Au pengine aende mahakamani ili akapate kufungua madai dhidi ya mkewe na kudai fursa ya kutoa talaka. Na mara nyingi talaka ndiyo uamuzi ambao mume huuchagua ili atatue tatizo hili. Lakini uamuzi huu unakuja baada ya kutokea fedheha, aibu na unyonge mkubwa katika familia hii. Na mwisho huu mbaya huleta matokeo ya kusikitisha, kwani familia hii hubomoka na maisha mazuri ya ndoa ya wawili hawa huvunjika.

Zaidi ya hapo msiba mkubwa hubaki kwa watoto ambao huwa bado wanahitajia kuwa na mama yao. Kuishi mbali na mama, watoto hawa hukosa huruma na upole wa mama yao, pia hukosa malezi mazuri na mwelekeo mwema. Hapo ndipo mahali ambapo hujitokeza fundo la moyo kwa watoto hawa na kujihisi kuwa na upungufu katika jamii wanayoishi. Watoto hawa hubadilika taratibu katika tabia zao na hatimaye hutokea wakajiunga katika magenge au makundi yenye mielekeo mibaya na kujikuta wamo miongoni mwa wezi na majambazi[1].

Mengi ya matukio ya aina hii yamekuwa yakitokea katika nchi zisizo za Kiislamu. Katika moja ya makala zake, gazeti la Kisovieti liitwalo Pravda liliandika kama ifuatavyo: "Asilimia themanini ya makosa ya uvunjaji sheria yafanywayo na vijana wenye umri wa kukaribia balehe (miaka kumi mpaka kumi na tano) yanatokana na kuvunjika kwa familia." Pia likaendelea kueleza gazeti hilo kwamba: "Katika kila matatizo tisa yanayohusu ndoa, moja katika matatizo hayo, matokeo yake huwa mume na mke kupeana talaka." Pravda likaendelea kutoa sababu za matatizo hayo kwa kusema: "Sababu za msingi zinazochangia kuleta hali hii, ni kuharibika kwa mwenendo wa jamii kutokana na ulevi wa kupindukia[2].

Sasa basi, ukweli uliopo ni kwamba matokeo ya yote haya yanakuja kutokana na uovu unaosababishwa na kutokujisitiri wanawake kama sheria inavyowataka. Uislamu kwa upande wake haukuharamisha bila mantiki mavazi yasiyowafunika wanawake kwa mujibu wa sheria, isipokuwa ni kwa lengo la kuzuwia maovu haya, na pia haukufaradhisha vazi la Hijabu kwa mwanamke isipokuwa ni kwa nia ya kumuepusha mwanamke asifikwe na maovu haya na mengine mfano wa haya. Kwa hiyo Uislamu unawalazimisha wanawake kuvaa Hijabu ambalo ndilo vazi rasimi kisheria ili kuzuia kuzuka kwa maovu kama yalivyotangulia kuelezwa.

Magazeti na vyombo vingine vya khabari kila mara vinatuarifu habari mbali mbali zinazohusu matatizo ya ndoa na khiyana zinazofanyika baina ya mke na mume, na hali hii husababisha watu kupeana talaka na pengine ikasababisha kutokea mauaji. kila unapofanyika uchunguzi, Sababu za msingi zinarudi kwenye upuuzaji wa Hijabu kwa ile maana yake halisi iliyokusudiwa na Uislamu. Ni mara nyingi tunasoma magazetini au kusikia redioni kwamba mtu kamuacha mkewe na wanawe kwa ajili ya msichana asiye na Hijabu ambaye kakutana naye ofisini au katika mabustani ya mapumziko na au mahali pengine. Au ni mara ngapi tumesikia na pengine kuona mke anamuacha mume wake ili tu akaolewe na kijana aliyekutana naye sinema au pwani wakati wa kuogelea?

Kuna gazeti moja liliandika kama ifuatavyo: "Mtu mmoja alimuua rafiki yake ili amchukue mkewe ambaye alikuwa akijidhihirisha wazi mbele ya bwana huyo bila Hijabu wala aibu. Gazeti liliendelea kueleza kwamba, kuna mwanamke mwingine ambaye yeye alimuua mumewe kwa msaada wa huyo mpenzi wake na kisha wakamkatakata viungo vyake na kuvitupa ndani ya mfereji wa maji machafu. Bibi huyu alifanya madhambi haya ili tu aolewe na huyo bwana mpya." Pia kulitolewa habari na gazeti moja la Kiarabu ambalo liliandika tukio moja miongoni mwa matukio yanayosababisha ndoa za watu kuvunjika, hasa mijini ndiko kwenye matukio mengi ya aina hii. Tukio hilo kwa hakika lilikuwa la kuhuzunisha sana, na cha kuhuzunisha zaidi ni kwa kuwa lilitokea katika moja ya nchi za Kiislamu, lau lingekuwa limetokea katika nchi za magharbi, hali hii ingekuwa ni mahala pake kwa kuwa nchi hizo ndiyo vituo vya kila aina ya maovu, kama vile zinaa na uchafu mwingineo. Lakini ni vipi leo mambo haya yanatokea hata katika nchi takatifu za Kiislamu ambazo hapo kabla zilikuwa zimetakasika kutokana na uchafu huo?

 


[1]. Hapa kwetu Tanzania uko msamiati usemao: "Watoto wa mitaani." Lakini ukifanya uchunguzi utakuta kwamba msamiati huu umeundika kutokana na matatizo ya kuvunjika kwa ndoa bila ya sababu za msingi, pia madhara yatokanayo na? ?kukosekana kwa uaminifu ndani ya ndoa za watu ni sehemu kubwa sana inayozalisha watoto wa mitaani. Pamoja na hali hiyo kuna mambo mengine k.m. umasikini. Kwa hakika kila mtu anapaswa kuwa muaminifu katika ndoa yake si kwa maslahi yake tu bali akiangalie kizazi chake kisije kuishia mitaani na kudhurika kwa mambo mengi yaliyoko huko. Mtarjumi.

Itaendelea katika makala ijayo..

[2]. Gazeti la Al Ahram linalochapishwa mjini Cairo Misri la Tar 26 April 1966 likinukuu kutoka gazeti la Pravda.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini