MAZAZI YA IMAMU WA KWANZA ALIYU BIN ABI TWALIB
USIKU WA KUZALIWA AMIRUL MUUMININA ALIY BIN ABI TALIB AS.
Amefaulu mwenye kumtakia rehema Muhammad, Ally na Batuli.
Enyi wasomaji watukufu wa makala hii mtakieni rehema na amani Mwanga uliotimia Muhammad saww!!!
Hakika Viongozi wenu hasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walioamini ambao husimamisha swala na hutoa zaka hali ya kuwa wamerukuu 5:55 Qur-an.
Mara usiku ule wenye baraka ulipowadia na kupita theluthi ya usiku wakati huo Fatimah bint Asadi aliijiwa na amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na akasikia akiambiwa :. Ewe Fatimah! Nenda Baitul Haraam. Kisha Fatimah bint Asadi akaanza kuumwa uchungu na akafikwa na yanayowafika wanawake wakati wa kujifungua. Abu Talib as akasema ; nilipoona mahangaiko hayo nilimsomea majina ambayo huwa yanamuokoa mwenye maumivu, maumivu ya Fatimah bint Asadi yakatulia kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Abu Talib as akamwambia : Je, nikuletee wakunga katika watu wako? Na wasichana wa ami zako wakusaidie suala lako hili? Fatimah bint Asadi as akajibu, hilo ni juu yako. Abu Talib as alituma ujumbe kwa wanawake wa Bani Hashim na wanawake hao walipofika walisikia msemaji kwa nyuma ya Nyumba akisema :. Ewe Abu Talib! Warudishe hao wanawake kutoka kwa Fatimah bint Asadi, hakika atakaye zaliwa ni tohara katoharishwa asimgusi yeyote isipokuwa mikono tohara, hayakutimia maneno ya yule msemaji, isipokuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu akawa amefika na kuwarudisha wale wanawake. Fatimah akatoka kuelekea nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu, akasimama karibu na Alkaaba na akaangalia juu mbinguni akawa anamuomba Mola wake, kisha akaanza kuimba mashairi akisema nakuomba ewe Mola wangu mwenye huruma nihurumie ewe mwenye kuondoa madhara shida na taabu.
Ewe Mwenye kuumba viumbe, ewe Mola wa wenye kuabudu, ewe Mola mwenye upaji, mwenye fadhila, mwenye kufanya mema na mwenye kuneemesha. Akajibiwa na msemaji toka mbinguni akisema :. Furahi ewe msichana mzuri! Kwa ukweli, kwa kumleta Imamu (kiongozi) mwenye kutoharisha miji, yeye ni msaidizi wa viumbe kuwaepusha na vitisho vyote, na atawafedhehesha wafanya maasi siku ya kiyama. Mwenyezi Mungu amemuhusisha na utawala hadi kapata kutoka kwa Mola wake cheo kikubwa kabisa. Amerehemewa katika maisha yake na baada ya kufa kwake na kwa muda wote uliopo na ujao. Yule msemaji alipomaliza mashairi yake Alkaaba ilipasuka na mwanga ulitokeza mkali sana Jibrilu as akaja akamwingiza Fatimah bint Asadi Ndani ya Alkaaba na Akapotea kuepukana na macho, na sehemu aliyotumia Jibrilu as kumuingiza ikaziba ilivyo kuwa mwanzo. (Swalawat)!?
Abu Talib as akasema :. Tukamuonea huruma kutokana na hali aliyokuwa nayo, tukataka kufungua milango ili kumfikia na kumsaidia, milango haikufunguka, tukajua hiyo ilikuwa amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mara tukarudi majumbani mwetu.
Fatimah bint Asadi akasema : Nilipoingia ndani ya Alkaaba iliyotukuzwa ni Mwenyezi Mungu mtukufu nilikaa juu ya Tandiko jekundu kwa muda, Mwenyezi Mungu akaondoa kizuizi katika macho yangu, mara nikamuona Jibrilu as ameteremka mbele yangu ndani ya Alkaaba tukufu waliofuatana naye ni mistari mingi ya Malaika, Alkaaba ikafunikwa kwa mapazia elfu moja na bendera za nuru elfu moja kati ya mbingu na Ardhi, kisha Jibrilu as akapanda mbinguni akiwa pamoja na Jibrilu Mikael na Malaika wengi kabisa na wakaizunguka nyumba tukufu, kisha wakaelekea kuja kwangu pamoja nao alikuwa mtoto wangu Muhammad saww anawaongoza wao kama mwezi ung'ao katikati yao, nao wakiwa kulia na kushoto kwake nikamsikia Jibrilu as akumwambia Muhammad mpokee Ally wakati wa kutoka kwake tumboni kwa mama yake.
Fatimah bint Asadi akasema: Kisha Nabii Muhammad saww akakaa nami kwa muda na sikujisikia kuumwa wala maumivu, mara nikajikuta nimejifungua. (swalawat)!!!?
Fatimah bint Asadi anasema: Wakati nikiwa nimechanganyikiwa kwa jambo langu la kujifungua mara tena nikamuona mtoto wangu Muhammad mbele yangu pamoja na wazee watano Adam, Nuhu, Ibrahim, Musa na Issa alayhim salamu, hali wote wananiambia mlinde na kumtunza kuepukana na macho mabaya ya wanaoangalia. Hakika yeye ni kipenzi cha mlezi wa viumbe. Ni furaha iliyoje na malipo mazuri yaliyoje kwa yule anayemfuata, Ole wake kwa yule atakaye tofautiana naye na kumkhalifu.!
Nilibaki ndani ya Alkaaba siku tatu mara nikamsikia mtoto wangu (Ally) akiniambia hakuna ubaya wowote ewe mama ukuta utaachia pale pale ulipoingilia na utatokea hapo hapo mara ya pili ile hali umembeba mtoto wako na wasii wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Swalawat!!!?
Baada ya siku tatu ukuta ulipasuka na Fatimah bint Asadi akatoka kwenye Alkaaba na huku kambeba Ally uso wake uking'aa kama mwezi kumi na nne. Swalawat!!!?
Fatimah bint Asadi as akasema: Nilipotoka kwenye Alkaaba ami zake wakawa wanampokea mmoja baada ya mwingine na wakimsalimia kama kiongozi wa waumini (Amirul Muuminina) naye akirudisha salamu,. Kisha Muhammad saww akamchukua Ally bin Abi Twalib as akatabasam, mara nuru ikaangaza Mashariki na Magharibi kutoka mdomoni mwake. Fatimah bint Asadi akasema :. Nilipotaka kumchukua mtoto wangu Ally as alirudisha mikono yake na kumkumbatia Mtume wa Mwenyezi Mungu saww. Fatimah bint Asadi anasema: Kila Nilipotaka kumbeba mtoto wangu Ally na kumfunga kwa mbeleko aliichana na huku akisema! Ewe mama usinifunge mikono yangu hakika mimi nahitaji kupeana mikono na Malaika, naona aibu kuwa mikono yangu imefungwa.
Hayo yote yalimfurahisha Abu Talib as na akafurahi sana akasema: Namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kanineemesha mimi kwa kumdhihirisha mtoto wangu Ally bin Abi Twalib as. Swalawat!!!?
Ni kwa ajili ya kuzaliwa Ally bin Abi Twalib as ndani ya Nyumba tukufu Alkaaba alipoulizwa na mtu mmoja aitwaye Sa'asa'a sahaba wa Imam Ali mkubwa na ametajwa kama mkweli mwaminifu na wanazuoni wa ahlisuna wakubwa wakubwa na wanazuoni wa Shi'ah ;. Sa'asa'a alimuuliza Imamu Aliy as kuwa ni nani mbora, wewe au Issa bin Mariamu? Ally bin Abi Twalib as akasema :. Mimi ni mbora, kwani wakati Mariamu alipokuwa mjamzito kwa rehema za Mwenyezi Mungu na wakati wake wa kujifungua ukakaribia ulishushwa wahyi kwake Ondoka katika hii nyumba tukufu (Baitul Muqqadas ya pili kwa utukufu baada ya Alkaaba) kwani nyumba hii ni nyumba ya ibada siyo mahala pa kuzalia watoto. Matokeo yake aliondoka kwenye nyumba tukufu (Baitul Muqqadas) na kwenda kwenye kichaka ambako alijifungua mtoto Issa Nabii wa Mwenyezi Mungu. Lakini wakati mama yangu mimi Fatimah bint Asadi alipojisikia uchungu wa uzazi ndani ya eneo la nyumba tukufu Alkaaba (nyumba ya kwanza kwa utukufu duniani), Mama aling'ang'ania kwenye ukuta na akamuomba Mwenyezi Mungu kwa jina na cheo cha nyumba ile (Alkaaba) na kwa cheo cha mjenzi wa Nyumba ile (Nabii Ibrahim as), ili apunguziwe maumivu yake. Mara Ufa ukajitokeza katika ukuta huo wa Alkaaba na mama yangu akasikia sauti ya kimiujiza ikimwambia, ; ewe Fatimah! Ingia ndani ya Nyumba Alkaaba, yeye akaingia ndani na mimi nikazaliwa ndani ya Alkaaba tukufu. Swalawat!!!?
Imamu Aliy as Alizaliwa mwezi kumi na tatu Rajabu mwaka wa thalathini A'amul fiyli sawa na miaka ishirini na tatu kabla ya hijiria na 25:05:600 AD.
Amirul Muuminina Aliy bin Abi Talib as katika Ahlul Bayt halinganishwi na yeyote.
Kutoka kwa Abdullah bin Umar bin khatabi anasema :. Tulipokuwa tunahesabu maswahaba wa Nabii saww tulikuwa Tunasema Abu Bakr, Umar na Uthmani mtu mmoja akasema ewe Aba Abdurrahmaan Ally bin Abi Twalib as yeye ni nani? (siyo sahaba?) Ibn Umar akasema :. Ally bin Abi Twalib as ni Ahlul Bayt wa Mtume saww halinganishwi na sahaba yeyote (kwa utukufu). Yeye yupo Daraja moja na Mtume wa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema :. Na walioamini na watoto wakafuata kwa imani tutawakutanisha na watoto wao. 52:21 Qur-an.
Fatimah yu pamoja na Mtume saww katika Daraja lake, Ally yu pamoja nao.
ANAYEMPENDA ALLY (A.S) ATAKUWA DARAJA MOJA NA MANABII.
Umar Khattab anasema :. Mtume saww amesema :. Anayekupenda ewe Ally atakuwa pamoja na Manabii katika Daraja lao. Na atakaye kufa hali ana chuki juu yako atakufa akiwa Yahudi au nasara (mkirsto).
Mtukufu Mtume Muhammad saww alisema mtu mbora anayetembea katika ardhi hii baada yangu ni Ally bin Abi Twalib as.
Tukutane katika Sehemu ya ishirini na moja ya historia ya Maasumu Ally bin Abi Twalib as.
Rejea:
1.Mustadrakul Hakim, Fusulu al Muhimma ya Nuru d dini bin Sabbagh Malik. Faslu ya 1 UK 14.
2.Yanabiul Mawaddah.
3.Kawaakib Durii UK 125 chapa ya Pakistan mtunzi Salehe Hanafiyat.