MTOTO WA NABII NUUH (KAN`AAN).
BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI
MTOTO WA NABII NUUH (KAN`AAN).
Mwenyezi Mungu S.W.T. alimtuma Nabii Nuuh A.S. kuwaonya watu wake kabla ya kujiwa na adhabu iumizayo. Akawalingania kwa muda wa miaka 950 katika ibada ya Mwenyezi Mungu mmoja na kuacha ibada yao ya upotofu ya kuabudu masanamu. Alitumia kila njia ili watu wake wafuate dini ya haki, lakini wapi! Walijivuna na wakaendelea katika upotofu na ukafiri wao bila ya kujali adhabu itakayowapata watu wasiomtii Mola Mtukufu.
Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kauli ya Nabii Nuuh katika Surat Nuuh tangu aya ya 5 mpaka 7, "
…إِنِّي دَعَوْتُ قَوْمِي لَيْلاً وَنَهَارًا * فَلَمْ يَزِدْهُمْ دُعَائِي إِلاَّ فِرَارًا * وَإِنِّي كُلَّمَا دَعَوْتُهُمْ لِتَغْفِرَ لَهُمْ جَعَلُوا أَصَابِعَهُمْ فِي آذَانِهِمْ وَاسْتَغْشَوْا ثِيَابَهُمْ وَأَصَرُّوا وَاسْتَكْبَرُوا اسْتِكْبَارًا
Maana yake, "…Ewe Mola wangu! Kwa hakika nimewalingania, (nimewaita) watu wangu usiku na mchana. Lakini wito wangu haukuwazidishia ila kukimbia. Na kila mara nilipowaita uwasamehe, waliziba masikio yao kwa vidole vyao, na walijifunika nguo zao (gubigubi), na walizidi kuendelea (na kufuru) na wakafanya kiburi kingi."
Nabii Nuuh A.S. alipokata tamaa kwamba watu wake hawatamwamini, hivyo Mwenyezi Mungu S.W.T. akamwamrisha Nabii Nuuh A.S. atengeneze jahazi mbele ya nyumba yake ili kusudi limbebe yeye pamoja na watu waliomwamini tu na ili makafiri wagharikike majini. Mke wa Nabii Nuuh na mwanae aliyeitwa Kan`aan walikuwa miongoni mwa watu makafiri. Na jahazi lilipokuwa tayari limekamilika na hakuna tena tamaa ya watu wake kuamini; Nabii Nuuh alimuomba Mola wake amuokoe na awaangamize makafiri. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa kauli ya Nabii Nuuh katika Suratil Qamar tokeya aya ya 10 hadi ya 14, "
فَدَعَا رَبَّهُ أَنِّي مَغْلُوبٌ فَانْتَصِرْ * فَفَتَحْنَا أَبْوَابَ السَّمَاءِ بِمَاءٍ مُنْهَمِرٍ * وَفَجَّرْنَا الأَرْضَ عُيُونًا فَالْتَقَى الْمَاءُ عَلَى أَمْرٍ قَدْ قُدِرَ * وَحَمَلْنَاهُ عَلَى ذَاتِ أَلْوَاحٍ وَدُسُرٍ * تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا جَزَاءً لِمَنْ كَانَ كُفِرَ
Maana yake, "Ndipo akamuomba Mola wake (akasema) "Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru." Mara tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika (kwa nguvu). Na tukazibubujisha maji chemchemi zilizo katika ardhi; na maji (ya juu na chini) yakakutana kwa jambo lililokadiriwa (na Mungu). Na tukamchukua (Nabii Nuuh) katika ile (jahazi) iliyotengenezwa kwa mbao na misumari. Ikawa inakwenda mbele ya macho, (hifadhi) Yetu. Hii ni tunzo (tuzo) kwa yule aliyekuwa amekataliwa (amekanushwa)."
Nabii Nuuh A.S. aliwaamuru watu wake wapande jahazini. Na walipokwisha panda likawa jahazi linakwenda kwa amri ya Mwenyezi Mungu S.W.T. na mwishowe lilisimama juu ya jabali liitwalo Judi baada ya maji ya mbinguni na maji ya ardhini kukutana na baadaye Mwenyezi Mungu kuiamrisha ardhi imeze maji yote. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Huud aya ya 41, "
وَقَالَ ارْكَبُوا فِيهَا بِاِسْمِ اللَّهِ مَجْرَاهَا وَمُرْسَاهَا إِنَّ رَبِّي لَغَفُورٌ رَحِيمٌ
Maana yake, "Na akasema (Nuuh) "Pandeni humo, kwa jina la Mwenyezi Mungu kuwe kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu." Nabii Nuuh A.S. akawa mlinzi wa Waumini ili apate kuwaokoa katika jahazi lake alilolitengeza kwa amri ya Mola wake. Lakini kabla ya jahazi kuondoka, Nabii Nuuh alimuona mwanae Kan`aan kasimama mbali na jahazi akamwita ili labda aweze kuamini baada ya kuona kwa macho yake mafuriko ya maji na kuwaona makafiri wakigharakika majini. Lakini wapi! Mwanawe alikataa kuwa pamoja na baba yake akapenda awe pamoja na makafiri. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Huud aya ya 42 na ya 43, "
…وَنَادَى نُوحٌ ابْنَهُ وَكَانَ فِي مَعْزِلٍ يَا بُنَيَّ ارْكَبْ مَعَنَا وَلا تَكُنْ مَعَ الْكَافِرِينَ * قَالَ سَآوِي إِلَى جَبَلٍ يَعْصِمُنِي مِنْ الْمَاءِ قَالَ لا عَاصِمَ الْيَوْمَ مِنْ أَمْرِ اللَّهِ إِلاَّ مَنْ رَحِمَ وَحَالَ بَيْنَهُمَا الْمَوْجُ فَكَانَ مِنْ الْمُغْرَقِينَ
Maana yake, "…Na Nuuh akamwita mwanawe aliyekuwa mbali (amekataa kuingia jahazini) "Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi wala usiwe pamoja na makafiri. Akasema (huyo mtoto) "Nitaukimbilia mlima utakaonilinda na maji." Akasema (Nuuh) "Hakuna leo wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu isipokuwa yule atakayemrehemu (Mwenyezi Mungu). Mara mawimbi yakaingia baina yao na akawa miongoni mwa waliogharikishwa."
NABII NUUH KUKATAZWA KUMUOMBEA MWANAWE.
Baada ya jahazi kusimama Nabii Nuuh A.S. akajiwa na hurumu ya baba kwa mwanawe, akatamani mwanawe aokoke na Moto wa Akhera baada ya kugharakishwa duniani. Lakini kipimo kamili cha kuokoka kinatokana na kumwamini Mwenyezi Mungu Mtukufu na si kutokana na ujamaa wa baba yake; yaani kwa vile baba yake ni Mtume basi mtoto ataokoka na adhabu ya Akhera. Huruma ni kitu mbali na kumwamini Mwenyezi Mungu S.W.T. ni kitu kingine. Kwahivyo Mwenyezi Mungu alimjibu Nabii Nuuh katika Surat Huud aya ya 45 na ya 46, "
وَنَادَى نُوحٌ رَبَّهُ فَقَالَ رَبِّ إِنَّ ابْنِي مِنْ أَهْلِي وَإِنَّ وَعْدَكَ الْحَقُّ وَأَنْتَ أَحْكَمُ الْحَاكِمِينَ * قَالَ يَا نُوحُ إِنَّهُ لَيْسَ مِنْ أَهْلِكَ إِنَّهُ عَمَلٌ غَيْرُ صَالِحٍ فَلَا تَسْأَلْنِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنِّي أَعِظُكَ أَنْ تَكُونَ مِنْ الْجَاهِلِينَ
Maana yake, "Na (Nabii) Nuuh alimuomba Mola wake (alipomkumbukia mwanawe ameangamia na watu makafiri) akasema "Ewe Mola wangu! Mwanangu ni katika watu wa nyumbani kwangu (mbona umemuangamiza)? Na hakika ahadi yako ni haki. Na Wewe ni Mwenye haki kuliko mahakimu (wote)." Akasema (Mwenyezi Mungu) "Ewe Nuuh! Huyu si katika watu wako. Mwendo wake si mwema. Basi usiniombe jambo usio na ujuzi nalo. Mimi nakunasihi usiwe miongoni mwa wajinga."
Mara Nabii Nuuh alitambua kwamba utiifu umeshinda huruma na hapo hapo akamuomba Mola wake amsamehe na kumrehemu kwa lile kosa kubwa alilolifanya bila yeye kujua kwamba haifai kumuombea mtu wa Motoni. Kama ilivyokuja katika Surat Huud aya ya 47,
"قَالَ رَبِّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ أَنْ أَسْأَلَكَ مَا لَيْسَ لِي بِهِ عِلْمٌ وَإِلا تَغْفِرْ لِي وَتَرْحَمْنِي أَكُنْ مِنْ الْخَاسِرِينَ
Maana yake, "(Nabii Nuuh) akasema "Ee Mola wangu! Mimi najikinga Kwako nisije kukuomba (tena) nisiyoyajua; na kama hunisamehe na ukanirehemu, nitakuwa miongoni mwa watakaopata khasara."
Na ndivyo hivyo inavyotambulikana kwamba mtoto wa Nuuh pamoja na mama yake walikuwa ni miongoni mwa watu makafiri, na kama inavyojulikana kuwa makafiri ni watu wa Motoni. Na hii inathibitisha Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na kutolewa na L-Bukhari na Muslim wakati Mtume S.A.W. alipokuwa akiwatahadharisha jamaa zake, "
''يَا مَعْشَرَ قُرَيْشٍ اشْتَرُوا أَنْفُسَكُمْ لاَ أُغْنِي عَنْكُمْ مِنَ اللَّهِ شَيْئًا ، يَا بَنِي عَبْدِ الْمُطَّلِبِ : لاَ أُغْنِي عَنْكُمْ مِنَ اللَّهِ شَيْئًا ، يَا عَبَّاسَ بْنَ عَبْدِ الْمُطَّلِبِ : لاَ أُغْنِي عَنْكَ مِنَ اللَّهِ شَيْئًا ، يَا صَفِيَّةُ عَمَّةَ رَسُولِ اللَّهِ : لاَ أُغْنِي عَنْكِ مِنَ اللَّهِ شَيْئًا ، يَا ): سَلِينِي مَا شِئْتِ من فَاطِمَةُ بِنْتَ رَسُولِ اللَّهِ (محمداً مالي لاَ أُغْنِي عَنْكِ مِنَ اللَّهِ شَيْئًا''
Maana yake, "Enyi kundi la Quraishi! Zinunueni nafsi zenu. Mimi sitawafaeni chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Enyi wana wa Abdul Muttalib! Sitawafaeni kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Ewe Abbas bin Abdul Muttalib! Sitakufaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Ewe Safia shangazi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.)! Sitakufaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Ewe Fatima bint ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Muhammad S.A.W.)! Niulize chochote utakacho katika mali yangu. Sitakufaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu."
MWISHO