Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MAZAZI YA IMAMU MAHDY (A.J) 3

0 Voti 00.0 / 5

Kuzaliwà kwa IMAMU MÀHDI a.s 15 SHAABANI 255 HIJIRIA:- 3

Jina la Mama yake IMAMU MÀHDI a.s

Jina la Mama yake Imamu MÀHDI a.s hasa lilikuwa ni Narjiskhatun, majina yake mengine ni Malika, Sausan na Rayhana. Yeye ni mjukuu wa Mfalme wa utawala wa Uturuki. Historia ya kuvutia ya Narjiskhatun kufika Samarra ni kama ifuatavyo:

Imesimuliwa na Bashir bin Sulayman kuwa: "Niliitwa na Imamu Ally an Naqii (baba yake Imamu Hassan Askàriy a.s) Imamu wa kumi na kuambiwa: wewe ni katika kizazi cha wasaidizi wetu na marafiki zetu. Nitakupa shughuli muhimu kwa sababu mimi nina Imani na wewe: Mimi nilimwomba aniamrishe tu kwa sababu nilijiandaa kutimiza anachotaka. Akaniambia kwamba anahitaji kumnunua kijakazi.

Akaniamurisha niende Baghdad kwa ajili ya shughuli hiyo, na nitakapofika huko niende kwenye ukingo wa mto. Huko mimi nitaona majahazi mengi na mateka wa kike wakiuzwa. Mimi niende kwa mtu mmoja aitwaye Omar bin Yazeed ambaye atakuwa na mtekwa wa kike aliyevaa nguo mbili za hariri. Yeye (huyo mtekwa wa kike) atakataa kuuzwa kwa mnunuzi yoyote na atakuwa anazungumza lugha ya Kituruki. Imamu Ally Naqii akanipa Dinar 120  akaniambia kwamba muuzaji atakubali kumuuza huyo mtekwa kwa hiyo bei. Vilevile alinipa barua ya kumpa huyo mtekwa wa kike.

Mimi nilikwenda Baghdad kama nilivyoagizwa na kwa alama nilizoelezwa na Imamu Ally Naqii, nilimtambua huyo mtekwa na nikampa barua. Kusoma barua hiyo tu huyo bibi machozi yalimjaa machoni mwake na akamwambia Maliki wake kwamba hatakubali kununuliwa na mtu yeyote isipokuwa miye (Bashir bin Sulayman ).

Kwa hivyo nilirudi nyumbani huko Baghdad na huyo mtekwa ambaye aliiweka barua hiyo juu ya macho yake na kulia sana. Nilimuuliza kwa nini anabusu hiyo barua na kulia wakati yeye ni mgeni kutoka Uturuki na hamjui mwandishi wa barua hiyo. Yeye akasema, "Sikiliza, mimi ni mjukuu wa Kaisar, Mfalme wa Uturuki na jina langu ni Malika. Jina la baba yangu ni Yashua na jina la Mama yangu ni Shamunusafaa. Baba yangu aliandaa mipango niolewe na mpwa wake. Siku moja aliwaita mapadri wote , mawaziri viongozi na wafuasi wake, na kumkalisha mpwa wake juu ya kiti cha enzi ambacho kilipambwa na almasi na kumwomba padri afunge ndoa yetu. Padri alipoanza kufungua kitabu kutaka kufunga ndoa masanamu waliotundikwa ukutani waliporomoka na mwana Mfalme (mpwa wa baba yangu ) akazirai na kuanguka na kiti cha enzi kilivunjika vipande vipande. Mapadri walitetemeka na kumuomba msamaha baba yangu Mfalme, kwa sababu hawakutarajia kutokea balaa hiyo.

Mfalme alihuzunika sana. Akaona ndoa hiyo ilikuwa na nuksi na kwa hivyo aliagiza kiti kingine cha enzi na kutundikwa masanamu tena ukutani. Padri tena akaanza kufunga ndoa na tukio hilo hilo likatokea tena. Waliohudhuria wote walishituka sana na wakaondoka papo hapo. Baba yangu alifedhegeshwa sana na siku nyingi alikuwa hakutoka nje ya kasri.

Usiku huo huo nilimuona Nabii Issa katika ndoto. Yeye alikuwa pamoja na Maswahaba wake waliokuwa wamehudhuria sherehe ya ndoa yangu. Kiti kirefu cha enzi kiliwekwa pahali palipowekwa kiti cha mwana Mfalme (aliyetaka kunioa) na kilikaliwa na mtu mkubwa mwenye uso uliojaa NURU. Baada ya muda mfupi tu niliwaona watu wenye nyuso za NURU na hapo Nabii Issa alisimama kuwakaribisha na kuwapa nafasi karibu yake. Nilimuuliza mtu mmoja anijulushe hao waliokuja walikuwa nani? Nikaarifiwa kwamba hao ni Mtume wa Uislamu Muhammad pamoja na mrithi wake Ally a.s na Maimamu kumi na moja wanaotokana na dhuria yake.

Mtukufu Mtume Muhammad s.a.w.w akamwomba Nabii Issa kumchumbia Malika bint wa Shamunusafaa kwa mjukuu wake Imamu Hassan Askàriy ambaye uso wake uking'aa kwa NURU (ombi hilo lilifanywa kwa Nabii Issa kwa sababu Malika alitokana na kizazi cha Hadharat Shamoon mrithi wa Nabii Issa). Nabii Issa akamuomba Hadharat Shamoon atoe kibali chake na papo hapo Hadharat Shamoon akakubali kwa kuona hiyo ni heshima kuu. Kwa hiyo ndoa yangu ikafungwa na Imamu Hassan Askàriy a.s.

Mara macho yangu yakafunguka ghafla na mimi nilijawa na furaha. Nilikumbuka hiyo ndoto. Hata hivyo niliogopa sana sikumhadithia ndoto hiyo mtu yeyote. Hapo baadaye mimi nikaanza kuwa mgonjwa na Kumkumbuka Imamu Hassan Askàriy na hali yangu ikaanza kudhoofu. Safari moja nilimuona bint wa Mtume Muhammad s.a.w.w bi Fatumah a.s na katika ndoto mimi nilisimama kwa taadhima na nikamweleza hali yangu na kutomuona Imamu Hassan Askàriy a.s.

Bi Fatumah alimuamurisha nisome "SHAHADA" , nikawa Mwislamu na baadaye kila usiku nilimuona Imamu Hassan Askàriy katika ndoto akinituliza. Mara moja Imamu Hassan Askàriy aliniambia kwamba babu yangu atatuma jeshi kuivamia nchi ya Waislamu na mimi nibadilishe mavazi yangu niungane na jeshi kama mtumishi mmojawapo. Waislamu watashinda vita hivyo, na mimi nitatekwa na kwa hivyo niungane na mateka wengine, mpaka Baghdad."

Mimi (Bashir bin Sulayman) niliposikia hayo nilijawa na furaha na nilimleta Bibi Narjiskhatun hadi Samarra kwa Imamu Ally Naqii a.s. Imamu Ally Naqii a.s alimkaribisha na akamkabidhi kwa Dada yake Halima Khatun.

Baadaye Imamu Ally Naqii a.s alimuozesha Bibi Narjiskhatun na mwanae Imamu Hassan Askàriy a.s akawabashiria kwamba watampata mwana ambaye atakuwa Hujja (dalili) duniani wa kuthibitisha kuwepo kwa Mungu .wakati dunia itakapokuwa imeghariki katika ukandamizaji, uovu na ulaghai yeye Atakuja kutawala na kuleta uadilifu na usawa.

Imamu MÀHDI a.s alizaliwa Samarra, Iraq Alfajiri siku ya Ijumaa tarehe 15 Shaban 255 hijiria. Nyumbani kwa baba yake mtukufu. Alizaliwa Twahara na amekwishatahiriwa na uso wake uliojaa NURU ambayo ilipenya paa na kuelekea mbinguni. Alipozaliwa tu, kwanza alisujudu na huku kuonyesha kidole cha shahada kuelekea mbinguni na kuthibitisha Upweke wa Mungu na Unabii wa Mtume Muhammad s.a.w.w na UIMAMU wa Ally a.s pamoja na warithi wake kumi kuwa ni Maimamu (Makhalifa) wa kweli. Hapo baadaye akamwomba Mungu atimize ahadi yake.

Halima Khatun, bint wa Imamu wa tisa, Imamu Muhammad Taqiy a.s shangazi wa Hassan Askàriy a.s akamnyanyua mtoto aliyezaliwa na kumpa baba yake ambaye alimpakata.Imamu MÀHDI a.s papo hapo akamuamkia baba yake ambaye alimjibu na akamwambia aendelee kusema kwa amri ya Mungu. Hapo tena Imamu MÀHDI a s akarudia kuthibitisha Upweke wa Mungu, na Utume wa Mtume Muhammad s.a.w.w urithi wa Maimamu kumi na moja na kusoma aya ya Qur'an (akiwa na umri wa saa chache tangu kuzaliwà)

"Na tunataka kuwafadhili waliodhoofishwa katika ardhi na kuwafanya wawe ni viongozi na kuwafanya ni warithi. 28:5 Qur'an.

 Hapo baadaye Imamu Hassan Askàriy a.s akamrudisha huyo mwana kwa Bibi Halima Khatun na Halima Khatun akamrudisha mtoto kwa Mama yake. Mwana huyo alimuamkia mama yake vilevile.

Katika sherehe ya akika Imamu Hassan Askàriy a.s alimwamrisha wakili wake Othman Saidi Umri kuwagawia masikini nyama ya mbuzi 10,000 na mikate 10, 000 .

Tukio la kuzaliwà Imamu MÀHDI a.s limesimuliwa pia na wanazuoni wa Ahlisuna/Sunni kama:

Shekhul Islamu wa Istanbul, Shekh Sulayman Balkhi Kanduzi, katika Yanabiul Mawaddah.

Tarekh ibn Khaladun Jz 2 Uk 24.

Shawahidun Nubuwwat, Uk 247.

Tarekhul Islamu cha Dhahabi.

Na vingine vingi.

Fuatana nami sehemu ya Ishirini historia ya Imamu MÀHDI a.s

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini