Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KUCHANGANYA SWALA

0 Voti 00.0 / 5

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI

KUCHANGANYA SWALA

Hata kama imeruhusiwa, kwa nini kufanya hivyo?
Hakuna anayesema kuwa kuna ubaya kuziswali Swala bila ya kuzikusanya. Swala za Dhuhr na `Asr, pia Maghrib na 'Isha' zinaweza kuswaliwa, aidha, kwa kukusanywa au kwa kutenganishwa. Hata hivyo, kukusanya Swala mbili kulikofanywa na Mtume (s.a.w.w.) kunaonyesha huruma ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ya kuwarahisishia ummah, na ziko sababu kwa nini imekuwa ni ada miongoni mwa Mashia, nazo ni:
" Watu mara nyingi wana shughuli na majukumu yao mengi, hususan katika nchi ambazo utaratibu wa nchi hizo wa kielimu na kikazi haukidhi mahitaji ya Waislamu ya kuweza kuswali Swala zao tano za kila siku. Baadhi ya kazi hufanywa kwa masaa mengi mfululizo, bila ya kuingiliwa. Kwa hivyo, ni vizuri, na ili kujiepusha na kukosa Swala ya pili, Shia huziswali mbili katika kipindi kimoja, iwe ni mapema au baadaye katika wakati wanaouchagua.

" Ni pale watu wanapokutana kutoka mbali ili kuswali mojawapo ya Swala hizo mbili; na kwa kuwa imeruhusiwa kukusanya zote mbili, wao huziswali zote mbili kwa jamaa, moja baada ya nyingine. Kwa njia hii wanakuwa wametekeleza yote, wajib na kuswali kwa jamaa (jama'ah) na hivyo kupata thawabu zaidi. Hebu mathalan angalia mfano wa Swala ya Ijumaa. Tumeona kwamba maelfu ya ndugu zetu wa kisunni huswali Swala za Ijumaa kwa wakati wake kabisa, lakini wengi wao hawapati kuswali Swala ya `Asr, wacha kuswali kwa jamaa. Kwa upande mwingine Mwislamu Mshia anayeswali Swala ya Ijumaa, ataweza kuiswali Swala ya `Asr kwa jama'ah.

" Kwa sababu sunnah hii haitekelezwi na ndugu zetu wa kisunni, ndio ikawa ni sababu nyingine ya Mashia kuhisi kwamba ni vyema waihuishe. Tungelipenda kuona watoto wetu na Waislamu wawe wanajua kwamba kukusanya Swala za Dhuhr na `Asr, pia Maghrib and 'Isha' kunaruhusiwa, na hivyo ni kunatokana na sunnah za Mtume (s.a.w.w.).

Hitimisho:
Kukusanya Swala za Dhuhr na `Asr, na kukusanya za Maghrib na 'Isha', kunajuzu kulingana na Qur'an na sunnah za Mtume Muhammad (s.a.w.w.), isitoshe kwafaa zaidi. Kutotekelezwa na ndugu zetu wa Sunni kwa Sunnah hii yenye ushahidi wa kutosha, hakuifanyi kwamba iwe haifai katika maisha yetu, kama Mwanachuoni mashuhuri mfafanuzi wa Sahih Muslim, Sheikh An-Nawawi alivyoandika:
Pindi Sunnah inapothibitishwa kuwa ni sahih, basi haiwezi kuachwa kwa sababu tu watu wengi hawaifanyi. [an-Nawawi, Sharh Sahih Muslim, (Beirut, 1392 A.H.), Juz. 8, Uk. 56] "Simamisha Swala Jua linapopinduka mpaka giza la usiku, na (kusoma) Qur'an ya Alfajiri. Hakika Qur'an katika Alfajiri ni yenye kushuhudiwa." (Qur'an: Sura: 17, Aya: 78)

Kwa nini Mashia wanakusanya Swala?
Mashia wanatekeleza Swala tano za kila siku za wajib. Hata hivyo aghlabu wao hukusanya ya Dhuhr na ya 'Asr kwa kuziswali kwenye kipindi kilichoelezwa kuwa kinaanzia mwanzo wa Dhuhr hadi mwisho wa 'Asr. Vilevile wanaonelea kuwa inajuzu vivyo hivyo kukusanya Swala za Maghrib na 'Isha. Kufanya hivi ni kwa uthibitisho kamili wa Qur'an na Hadith sahih za Mtume (s.a.w.w.).

Madhehebu ya Sunni ki-fiqh - sipokuwa ya Hanafi- yanaruhusu kukusanya Swala za wajib (al-jam` bayn al-swalatayn) kama kutakuwa na sababu ya mvua, safari, hofu, au dharura zozote. Lakini madhehebu ya Hanafi hayaruhusu kukusanya Swala za kila siku za wajib wakati wowote ule, isipokuwa Swala za Al-Muzdalifa wakati wa kuhiji. Ama madhehebu ya Maliki, Shafi'i, na Hanbali, wote wanakubaliana kujuzu kukusanya Swala pindi pale mtu anaposafiri, lakini wametofautiana kuhusu sababu zingine. Na madhehebu ya Shia Ja'fariyya yanasema kwamba mtu anaweza kukusanya Swala tano bila ya sababu yoyote.

Nyakati za Swala kulingana na Qur'an
Imam Fakhr al-Din al-Razi, mwanachuoni, mfasiri mashuhuri wa Qur'an wa Sunni, ameandika haya kuhusu Aya zilizonukuliwa (Sura 17, Aya 78): "Ikiwa kama tutafasiri giza (ghasaq) kwa maana ya pale giza linapoanza kuingia, basi neno ghasaq litakuwa na maana ya mwanzo wa Maghrib. Kwa msingi huu, nyakati tatu zimetajwa katika Aya hiyo: 'wakati wa mchana, wakati inapoanza kuingia Maghrib na wakati wa of Fajr'. Hii itakuwa kwamba mchana, ni wakati wa Dhuhr na `Asr, nyakati hizi huchanganywa kwa Swala hizi mbili (Dhuhri na Asr). Wakati inapoingia Maghrib ndio wakati wa Maghrib na 'Isha' kwa hivyo nyakati hizi pia huchanganywa kwa Swala hizi mbili. Hii inaruhusu kukusanya Swala ya Dhuhri na Asr. Na Maghrib and 'Isha' wakati wote. Hata hivyo, kuna ushahidi kwamba kukusanya wakati uko nyumbani bila ya udhuru wowote hakuruhusiwi. Hii yaashiria mtazamo kwamba kukusanya kunaruhusiwa wakati wa safari au kama kuna mvua, n.k.."
[Fakhr al-Din al-Razi, al-Tafsir al-Kabir, Juz. 5, Uk. 428]

Tutaonyesha kwa kifupi ushahidi usiopingika kwamba kukusanya Swala bila ya dharura yoyote kunajuzu. Hata hivyo ni wazi kwamba nyakati za Swala za wajib ni tatu pekee: 1) Wakati wa Swala mbili za faradhi, Dhuhr na `Asr, ambao unashirikishwa pamoja kwa mbili hizo. 2) Wakati wa Swala mbili za faradhi, Maghrib (jioni) na 'Isha' (usiku) ambao pia unashirikishwa pamoja kwa mbili hizo. 3) Wakati wa Swala ya Fajr (mapema alfajiri) ambao ni maalum pekee kwa hiyo.

Je Mtume (s.a.w.w.) alikusanya Swala?
" Amepokea Ibn 'Abbas kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (amani imshukie) aliswali Madina (rak'ah) saba na (rak'ah) nane, yaani (zimekusanywa) Swala za mchana (Dhuhr) na alasiri (`Asr) (rak'ah) nane; na Swala za jioni (Maghrib) na usiku ('Isha') (rak'ah) saba. [Sahih al-Bukhari (Tafsiri ya kiingereza), Juz. 1, Kitabu cha.10, Namba 537; Sahih Muslim (Tafsiri ya kiingereza), Kitab al-Salat, Kitabu 4, Sura 100 Combination of prayers when one is resident, Hadith Na. 1522]

" 'Amepokea Abdullah b. Shaqiq: Siku moja Ibn 'Abbas alituhutubia mchana (baada ya Swala ya mchana) mpaka jua likachwa na nyota zikaangaza, watu wakaanza kusema: Swala! Swala! Akaja bwana mmoja kutoka ukoo wa Banu Tamim akiwa ameshikilia kusema bila ya kugeuka: Swala! Swala! Ibn 'Abbas akakemea: "Mwana wa kukoswa na mamaye we! Wanifundisha mimi Sunna?" Kisha akasema: "Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) akikusanya Swala za Dhuhr na `Asr pia Swala za Maghrib na 'Isha' ." 'Abdullah b. Shaqiq amesema: "Nilikuwa na shaka kidogo akilini mwangu kuhusu jambo hilo, kwa hivyo nilikwenda kwa Abu Huraira na kumuuliza juu ya jambo hilo, naye alitoa ushahidi wa maelezo yake." [Sahih Muslim (Tafsiri ya kiingereza), Kitab al-Salat, Kitabu cha 4, Sura 100 Combination of prayers when one is resident, Hadith Na. 1523, 1524]

Lakini hiyo haikuwa kwa ajili ya safari, hofu, au mvua?
Hadith nyingi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) zaonyesha waziwazi kwamba yeye alikuwa akikusanya Swala bila ya udhuru wowote maalum. " Mtume (s.a.w.w.) aliswali akiwa mjini Madina, bila ya kuwa safarini, saba na nane (hii yaashiria Rakaa saba za Maghrib na 'Isha' zikiwa zimekusanywa, pia Rakaa nane za Dhuhr na `Asr zikiwa zimekusanywa).
[Ahmad ibn Hanbal, al-Musnad, Juz. 1, Uk. 221]
" Mtume (s.a.w.w.) aliswali Dhuhr na `Asr kwa kuzikusanya, pia Maghrib na 'Isha' kwa kuzikusanya pasi na kuwa na sababu ya hofu au safari.
[Malik ibn Anas, al-Muwatta', Juz 1, Uk. 161]

Kwa hakika hata twaambiwa na baadhi ya Hadith nini sababu ya Mtume (s.a.w.w.) kufanya hivyo. IIlikuwa ni kuwarahisishia ummah! " Ibn 'Abbas ameeleza kwa Mtume (s.a.w.w.) alichanganya Swala ya mchana na ya alasiri, pia ya Magharibi na ya 'Isha' akiwa Madina, bila ya kuwa katika hali ya hofu au mvua. Na katika Hadith iliyopokewa na Waki' (maneno yake ni): "Nilimwambia Ibn 'Abbas: Ni nini kilichomfanya yeye kufanya hivyo? Akasema: Ili umma huu (wa Mtume) usifanyiwe mambo kuwa mazito." [Sahih Muslim (Tasiri ya kiingereza), Kitab al-Salat, Kitabu cha 4, Sura 100 Combination of prayers when one is resident, Hadith Na. 1520; Sunan al-Tirmidhi, Juz 1, Uk. 26]

" Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) aliswali Swala za mchana na za alasiri pamoja akiwa Madina bila ya kuwa katika hali ya hofu au katika hali ya kusafiri. Abu Zubair amesema: "Nilimuuliza Sa'id (mmoja kati ya wapokezi) kwa nini yeye alifanya hivyo. Naye alisema: Nilimuuliza Ibn 'Abbas kama ulivyoniuliza wewe, naye alinijibu kwamba yeye (Mtume mtukufu) hakutaka mtu yeyote katika umma wake atiwe katika uzito." [Sahih Muslim, Tafsiri ya kiingereza, Kitab al-Salat, Kitabu cha 4, Sura 100 Combination of prayers when one is resident, hadith no. 1516]

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini