Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

DALILI YA UIMAM.

0 Voti 00.0 / 5

BSMILAHI AR-RAHMANI AR-RAHIIMI.

DALILI YA UIMAM.
Assalaam Alaikum warahmatullah wabarakatuh. Katika sehemu iliyotangulia kuhusu Uimamu tumegusia kuhusu Imani anayoimiliki kila Shia Ithnaashariy {yaani yule Shia (sio kila shia) ambaye anaamini kuwa Maimam (a.s) baada ya Mtume (s.a.w) ni kumi na wawili tu kama Mtume (s.a.w) alivyowataja katika hadithi yake tukufu,sio pungufu ya kumi na mbili wala zaidi ya kumi na mbili.hii ndio maana ya neno shia ithnaashariy}kuwa:

Washia (Wale ambao watu wakitofautiana kuhusu Mtume (s.a.w) huchukua kauli ya Imam Ali (a.s), na wakitofautiana kuhusu Imam Ali (a.s) huchukua kauli ya Imam Jaafar bin Muhammad -Al-swadiq- (a.s) ) huamini kuwa baada ya kifo cha Mtume (s.a.w) ni lazima Imam achaguliwe na Mwenyeezi Mungu(s.w) ili awe msimamizi na mlinzi wa mafundisho ya sheria za Kiislaam pamoja na kuwaongoza watu katika njia iliyonyooka.

Ama katika sehemu hii, baada ya kuliweka wazi suala la Uimam na kwamba Washia wana itikadi gani kuhusu Uimam, itakuwa ni vema baada ya utangulizi huo tukagusia kunako dalili ya Uimam.

Tunatambua wazi kwamba uzingatiaji na mapenzi aliyokuwa nayo Mwenyeezi Mungu (s.w) kwa viumbe wake unampelekea kukiongoza kila kiumbe kuelekea katika lengo maalum (ili kiweze kuufikia ukamilifu halisi na saada). Kwa mfano:Mtu unaotoa matunda huongozwa ili uweze kustawi,kukua na kutoa matunda.Kwa hiyo utakuta mfumo wa maisha ya mti huo unaotoa matunda unatofautiana na mfumo wa maisha ya ndege.Vile vile kila ndege huishi maisha yake kwa njia maalum na kufuata lengo mahsusi.Kwa njia hii tunagundua kuwa kila kiumbe huongozwa ili kulifikia lengo lake maalum na kufuata njia nyoofu tu.

Bila shaka Mwanadamu ni moja wapo ya viumbe vya Mwenyeezi Mungu (s.w),ikiwa hili litakuwa wazi kwa kila mtu kwamba mwanadamu naye ni kiumbe wa Mwenyeezi Mungu (s.w), basi hakutakuwa na ubishi juu ya kauli hii kwamba:(Naye analazimika kufuata nji hiyo hiyo ya kuongozwa ili kulifikia lengo maalum la kuumbwa kwake ambalo ni: Ukamilifu na saada.) Kwa kuwa Mwenyeezi Ndiye mwenye kumuongoza mwanadamu ili kuufikia ukamilifu huo na saada,ukamilifu huo mwanadamu ataweza kuufikia kupitia njia aliyoiweka Mwenyeezi Mungu (s.w) kuelekea ukamilifu wa mwanadamu na Saada hiyo.Hivyo yeye ndiye atakayechagua kiongozi wa kuwaongoza wanadamu,hakuna mtu atakuwa na jukumu hili la kumchagua kiongozi ili kuwaongoza wanadamu kwani njia ya kuufikia ukamilifu na saada haijui ispokuwa yule aliyemuumba mwanadamu na anayemjua mwanadamu kwa maana nzima ya kumjua.

Mfano Mwenyeezi Mungu (s.w) ndiye anayemchagua Nabii ili kuwaongoza wanadamu,hivyo hakuna mtu yeyote mwenye uwezo au mwenye jukumu la kumchagua Nabii ili awe kiongozi kwa wanadamu,bali jukumu hilo ni la yule aliyemuumba mwanadamu ambaye ndiye anayejua njia bora ambayo kwayo mwanadamu anaweza kuufikia ukamilifu na saada. Kwa mantiki hiyo,uongozi wa Mwenyeezi Mungu (s.w) kwa mwanadamu hasa,unapaswa kufikiwa kupitia mwito,ulinganiaji na mawasiliano ya dini na sheria zake kupitia Manabii ili mwanadamu asije kuwa na hoja yoyote dhidi ya mfumo huu wa Mwenyeezi Mungu (s.w), au kwa ibara nyingine:Ili mwanadamu asijekuwa na hoja mbele ya Mola wake na kusema:{Mimi nilitaka kuufikia ukamilifu na saada lakini sikupata wa kuniongoza kuelekea ukamilifu huo hivyo sikujua ni pitie njia ipi}. Allah (s.w) amesema kwamba:

*رسلا مبشرين ومنذرين لئلا يکون للناس على الله حجة بعد الرسل...*

"Mitume ,watoao habari nzurii (za watu wema) na waonyao (wabaya) ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyeezi Mungu baada ya (baada ya kuletwa hawa) Mitume.." Aya hii Tukufu inatoa dalili juu ya ulazima wa kuchaguliwa Manabii na kuanzishwa mfumo wa mwito wa kidini.Baada ya kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w) ambaye kailinda dini na kuwaongoza watu kwa Isma yake, ni muhimu kwa Mwenyeezi Mungu (s.w) kumchagua mtu ambaye ni sawa na Mtume (s.a.w) katika {Isma} na (sifa bora} ispokuwa (Wahyi na Utume) ili aichukue nafasi ya Mtume (s.a.w) na kuyalinda mafundisho na sheria tukufu za Dini ya kiislaam bila ya kasoro yoyote na kuwaongoza watu.

Kinyume na hilo, ratiba nzima ya mafunzo yote pamoja na sheria alizokuja nazo Mtume (s.a.w) baada ya Mwenyeezi Mungu (s.w) kumkabidhi jukumu la kuwaongoza watu itaharibika na ikisha haribika watu watakuwa na hoja dhidi ya mfomo wa uongozi wa Mwenyeezi Mungu (s.w).Na kwakuwa Mwenyeezi Mungu (s.w) kaisha kataa kuwa kamwe mwanadamu hatakuwa na hoja juu ya mfomo huo wa Mwenyeezi Mungu (s.w),hii ni dalili tosha kuwa baada ya Mtume (s.a.w) Mwenyeezi Mungu (s.w) hawezi kuacha ratiba nzima ya sheria zake ziharibike,hawezi kuacha mafundisho yote aliyoyafundisha Mtume (s.a.w) yaharibike, hawezi pia kumuacha mwanadamu pasina kiongozi wa kumuongoza katika njia iliyonyooka na ukamilifu na saada. Hivyo akili ya mwanadamu (pasina kuangalia Kitabu cha Mwenyeezi Mungu -s.w- kinasemaje,au Sunna tukufu za Mtume -s.a.w- zinasemaje) inahukumu kuwa ni muhimu kwa Mwenyeezi Mungu (s.w) kumchagua mtu anayemfanana Mtume (s.a.w) katika Isma na sifa zingine zote bora (Ispokuwa Wahyi na Unabii) ili Mtu huyo aichukue nafasi ya Mtume (s.a.w) na kuyalinda mafundisho yote na sheria za dini tukufu ya kiislaam bila ya kasoro yoyote ile na pia aweze kuwaongoza watu

UDHARURA(ULAZIMA) WA KUWEPO IMAM.

Mwanadamu kapewa akili ili akili yake imuongoze katika maisha yake ya duniani awe kujua hili ni halali na hili si halali,hili ni haki na hili si haki,hili linastahiki na hili halistahiki,njia hii ni sahihi na njia hii ni ya maangamizi na kadhalika.Lakini uwezo wa akili hii una mipaka kuna mambo akili inaweza ikatambua na kuna mambo inaweza kufanya makosa.ndio maana unakuta wanadamu hukosea kila mara wakati wana akili.Kukosea huku kunaonyesha kwamba akili ya Mwanadamu ina sifa ya kukosea,kama sio hivyo basi tungelikuwa tunamuona kila mwanadamu kila anachokifanya ni sahihi! Hili halijathibitika na halitathibitika kamwe,bali ukweli utarudi pale pale kuwa akili ya mwanadamu hajitoshelezi yenyewe katika kila kitu kumuongoza mwanadamu katika maisha yake. Kwa mantiki hiyo basi,kutokana na makosa yanayofanywa na akili za wanadamu,akili hizo haziwezi kutegemewa katika kuwaongoza wanadamu bila ya kuwepo Manabii wa Mwenyeezi Mungu (s.w).

Vile vile kuwepo Maulamaa katika Umma wa Kiislaam wakifanya ulinganio ndani ya umma huo hakutoshi kuwafanya watu kutokuwa na haja ya kuwepo Maimam {waliochaguliwa na Mwenyeezi Mungu -s.w-} kama tulivyofafanua juu ya hilo,suala la msingi hapa sio ati watu kufuata dini au kutoifuata,bali jambo linalojadiliwa hapa na ambalo ndilo la msingi ni kuwa ni lazima dini ya Mwenyeezi Mungu (s.w) iwafikie watu bila ya kasoro yoyote ile wala mabadiliko yoyote yale.

Ni jambo la wazi kuwa Maulamaa na Wanazuoni wa Umma wa Kiislaam sio Maasumina kutokana na makosa wala dhambi,sawa sawa wawe na imani ya hali ya juu na taqwa ya hali ya juu au ya kawaida,kwa vyovyote vile watakavyokuwa nayo.Hivyo kuna uwezekano kwa Maulamaa hao na Wanazuoni hao kuupoteza Umma na kuuangamiza Umma na kuyabadilisha mafundisho na sheria za Dini ya Kiislaam hata kama ni kwa kutojua.Mpaka leo hii hatujapa hata A'alimu au Mwanazuoni yeyote yule na katika zama zozote zile kuwa alidai kuwa yeye ni Maasum hafanyi kosa wala dhambi!! Na dalili nzuri kabisa kuhusiana na suala hili ni kuwepo kwa Madhehebu na vikundi vingi mbali mbali vilivyodhihiri katika Uislaam.Hii inaonyesha kwamba vikundi hivyo kila kikundi kina rai yake na mtazamo wake na itikadi yake tofauti na kikundi kingine au madh-hebu tofauti na hiyo.

Kwahiyo,kwa njia yoyote ile na kwa vyovyote vile,kuwepo Imam Maasum ni muhimu katika kulinda mafundisho na sheria halisi za Mwenyeezi Mungu (s.w),ili watu wapate kunufaika na uongozi wake wanapopata fursa ya kunufaika nao na ili waweze kuielekea njia ile itakayowafikisha kwenye lengo kuu ambalo ni (kupata au kuufikia ukamilifu na saada).

KAULI YA MTUME (S.A.W) KUHUSIANA NA WILAYA {UONGOZI}.

Usikose sehemu ya tatu ijayo kuhusiana na kauli ya Mtume (s.a.w) kuhusu uongozi,je ni kweli Mtume (s.a.w) aliuacha Umma huu pasina kuainisha nani atakuwa kiongozi baada yake? Na ikiwa ni jawabu ni ndio kama baadhi ya watu wanavyoitikadia na kuamini hivyo,je huku si ni kumdhalilisha Mtume (s.a.w) kwa kumfanya aonekane ni Mtume asiyejali Umma wake mpaka anaamua kuacha umma hivi hivi pasina kiongozi? Hayo yote tutayazungumzia katika sehemu ya tatu ijayo Inshaallah.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini