Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KHUTBA YA FATIMA ZAHRAA (A.S)

0 Voti 00.0 / 5

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

KHUTBA YA FATIMA ZAHRAA (A.S)

KHUTBA YA MBORA WA WANAWAKE ULIMWENGUNI FATIMA ZAHRAA (A.S).

Abdallah bin Hassan amepokea kwa sanadi yake kutoka kwa baba zake juu yao rehma na amani ya kuwa: Pindi Abubakar na Omar walipo kata shauri la kumzuilia na kumnyima mwana Fatima shamba lake la Fadak, na habari hizo kumfikia bibi huyo, alijifunika ushungi wake (alijifunga ushungi) kichwani na kuvaa buibui lake na kutoka akiwa katika kundi la wahudumu wake (walio kuwa kati ya watu watatu au zaidi) na akiwa na wanawake wa kabila lake, huku akitembea kwa utulivu na kwa mwendo wa hatua fupifupi mwendo ulio shabihiana na mwendo wa baba yake Mtume (s.a.w), hadi akafika na kuingia kwa Abubakar, nae akiwa katika kundi la Muhajirina na Answar na wengineo.

Akaikunja nguo yake ya kiunoni na kuketi chini kisha akatoa sauti ya mlio, sauti ambayo iliwafanya watu kulia kutokana na sauti hiyo ya kilio aliyo itoa, na majlisi (kikao) ile ikajawa na kelele za vilio, kisha akatulia kiasi hadi sauti za vilio za watu wale zikatulia, na hamasa pia huzuni zao zilipo tulia akaanza mazungumzo yake kwa kumsifia Mwenyezi Mungu kwa sifa njema na kumhimidi na kumtakia rehma Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w), kisha watu wakaangua tena kilio chao, na walipo nyamaza akaendelea na mazungumzo yake na kunena:

Sifa zote njema na himidi zote ni zake Mwenyezi Mungu juu ya yale aliyo waneemesha nayo viumbe, na shukrani ni zake Mwenyezi Mungu juu ya ilhamu aliyo wapatia waja wake watakasifu, ilhamu ya kufahamu tawhidi (upweke wa Allah) ya Mwenyezi Mungu, na sifa pia shukurani na himidi zote ni zake kwa yale aliyo wapatia waja kama vile kuwepo kwao wakiwa hai, na kutokana na neema zote alizo waneemesha nazo (kama akili, uwezo wa kuzungumza na mengineyo).

Na himidi zote ni zake kutokana na neema za ujumla na pana alizo mpatia mwanadamu kabla ya kumuumba (yaani alizo ziumba mwanzo kwa ajili ya mwanadamu kabla ya kuumbwa kwake).

Na kutokana na neema zisizo katika wala kumalizika alizo mpatia mwanadamu, na kutokana na neema kamili zisizo pungua wala kumalizika ambazo Mwenyezi Mungu aliwaneemesha nazo wanadamu bila ya masimbulizi.

Neema ambazo ni nyingi na zisizo hesabika, na kutokana na neema ambazo hakuna uwezekano wa kutoa malipo yake yalinganayo na neema hizo, na shukurani zenye kulingana na ukubwa na wingi wa neema hizo, neema ambazo hakuna uwezekano wa kudiriki (kuelewa) ukomo wake, na kuwahimiza pia kuwaita (kuwataka) kumshukuru yeye na kumuomba ili awaongezee na kuwazidishia neema hizo na kuendelea kwake bila kukoma.

Na akawataka viumbe kumhimidi na kumshukuru na kumtukuza ili neema ziendelee kuwafikia kwa wingi na kuwakamilishia neema hizo, na akawahimiza pia kuwahamasisha kufanya mambo mema na matendo mema yawafanyayo kupata thawabu na neema hizo (neema za dhahiri na batini) za duniani na akhera kama kutendeana wema.

Na ninashuhudia ya kuwa hapana mola wa haki na apasae kuabudiwa isipokiwa Mwenyezi Mungu wa pekee asie na mshirika. Neno ambalo (shahada) ikhlasi imefanywa kuwa ndio taawili na ufafanuzi wake. Na akazifanya nyoyo kuwa ndizo zibebazo matokea ya neno hilo (yaani zenye kubeba neno la tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu).

Mwenyezi Mungu ambae haonekani kwa macho (macho hayana uwezo wa kumuona yeye). Mwenyezi Mungu ambae hasifiwi kwa ndimi za watu (yaani mwanadamu hawezi kufikia ukamilifu na kikomo cha sifa zake). Mwenyezi Mungu ambae akili fikra na wahmu za watu hazina uwezo wa kumpatia namna, picha wala aina ya kuwa kwake na namna alivyo.

Ameviumba vitu kwa mara ya kwanza bila vitu hivyo kuwepo kabla ya kuumbwa kwake, na akavifanya viwepo (akaviumba) bila kuangalizia kwenye mfano wowote na kuvifananisha nao. Na akaviumba vitu vyote (akavifanya viwepo) kwa uwezo wake, na akaviumba na kuvifanya viwepo kwa utashi na irada yake na kwa hiyari yake, bila ya yeye kuwa na haja ya kuviumba kwake na kuvifanya viwepo, (bila ya yeye kuvihitajia viumbe hivyo).

Na bila ya kuwepo faida yeyote aipatayo kwa kuviumba kwake katika maumbile na sura au shakli tofauti, na aliviumba katika hali hiyo si kwa jambo jingine, bali ni kuthibitisha na kudhihirisha hekima yake, (ya kukiweka kila kitu mahala pake kinapostahili), na aliviumba hivyo na kuvipa maumbile tofauti ili kuwatanabahisha viumbe (wanadamu) juu ya Twaa (utiifu) yake.

Na ili kudhihirisha uwezo wake, na ili waja wake waweze kumuabudu yeye, na kwa ajili ya kuutukuza na kuueneza wito wake alio waitia watu, kisha akaweka thawabu kwa ajili ya wenye kumtii, (akaweka thawabu kwa kumtii kwake), na akaweka adhabu kwa wenye kumuasi yeye, ili kuwazuwia waja na kuwakinga kutokana na ghadhabu na adhabu yake, na kuwapeleka kwenye pepo yake.

Na ninashuhudia ya kuwa baba yangu Muhammad ni mja wake na Mtume wake, alimchagua na kumteua kabla haja mpatia ujumbe wa utume( alimchagua kabla hajampa utume), na kumuita jina (kumchagulia jina) kabla ya kumchagua na kumteua, alimchagua wakati viumbe hawafahamu mambo ya ghaibu na wakiwa wamesitiriwa kunako mambo ya ghaibu, na wakiwa ni wenye kuhifadhiwa na kukingwa na mambo yenye kuogopesha, na wakiwa ni wenye kuambatanishwa kumalizika na kutoweka kwao katika dunia hii, hali akiwa ni mwenye ujuzi na mwenye kufahamu (ujuzi utokao kwa Mwenyezi Mungu kuhusu) mwisho wa mambo yote, na akiwa ni mwenye ufahamu kamili wa matukio yatakayo tokea katika zama mbali mbali, na mwenye maarifa na kufahamu mambo yatakayo tokea na mahala (zama) yatakapo tokea na makadirio yake Mwenyezi Mungu, alimtuma kama Mtume ili kutimiza na kukamilisha amri yake na utashi wake, na kwa ajili ya kutekeleza au kuisimamisha hukumu yake aliyo iamuru kutekelezwa, na kutekeleza au kusimamisha makadirio ya rehma yake, akaukuta na akauona umma ukiwa ni wenye kutofautiana na kufarakana na ukiwa ni wenye kufuata dini tofauti, baadhi wakiwa wameketi na kuabudu moto, na wengine wakiabudu masanamu yao, wakimpinga Mwenyezi Mungu pamoja na kumfahamu kwa maumbile yake.

Mwenyezi Mungu akawaletea nuru kupitia kwa baba yangu Muhammad (s.a.w) wakati walipo kuwa vizazi vya upotovu na kuziondolea nyoyo zao matatizo yaliyo kuwa nazo, na kuyaondolea macho shubha na kiza kilicho kuwa kimetanda mbele yake na kutouona ukweli, na kuwasimamishia watu nguzo za uongofu (akasimama kati ya watu kwa uongofu) na kuwaokoa kutokana na upotovu, na kuwaonyesha njia ya haki na njia ya tawhiid na kuiacha njia ya upotovu, na akawaongoza kwenye dini ya sawa, na kuwalingania kwenye njia iliyo nyooka, kisha akamchukua roho yake uchukuaji wa upole na taratibu kwa hiyari na mapenzi na kwa kuridhiria.

Kwa hivyo Muhammad akahamia kwenye nyumba ya raha na mapumziko na kuihama nyumba yenye taabu na matatizo, huku akiwa amezungukwa na malaika wema, na akiwa amepata maridhio (ameridhiwa) ya Mola msamehevu, (mwingi wa kusamehe), na kuwa jirani (kuwa karibu) na mfalme alie jabbar, (rehma za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya baba yangu Mtume wake na mwaminifu juu ya ujumbe wake na wahyi wake, mteule wake na mbora wa viumbe wake na mteule wake, na amani iwe juu yake na rehma za Allah na baraka zake.

Kisha akawageukia wanakikao walio hudhuria kwenye majlisi na kusema:
Nyinyi enyi waja wa Mwenyezi Mungu ndio walengwa wa amri zake Mwenyezi Mungu na makatazo yake, na nyinyi ndio wabebaji wa dini yake na wahyi wake na kuwafikishia watu na nyumati na zama zijazo, na nyinyi ndio wabebaji wa amana ya Mwenyezi Mungu (Amana ya taklifu) katika nafsi zenu, (na nyinyi ndio waaminifu wa Mwenyezi Mungu kwa nafsi zenu) yaani amana ya nafsi zenu na amana ya kufikisha ujumbe wake, amri zake na makatazo yake, na nyinyi ndio wafikishaji wa Amana hiyo kwa nyumati na watu wajao, kiongozi wake wa haki yuko kati yenu na ahadi yake amekupeni nyinyi, au ameitoa kwenu, na akakuachieni usia wake na amana yake (akaacha kwenu na juu yenu amana yake, nayo ni ile aliyo isema Mtume (s.a.w):

Hakika mimi nimeacha kwenu vizito viwili kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu (familia yangu) ikiwa mtashikamana navyo hamtapotea kamwe kimojawapo ni kikubwa kuliko kingine, hakika kitabu cha Mwenyezi Mungu ni kamba ya Mwenyezi Mungu iliyo fungwa (nyooshwa) kutokea mbinguni hadi kwenu na ncha nyingine ya kamba hiyo iko kwa Mwenyezi Mungu na nyingine iko mikononi mwenu (iko kwenu) na akavifanya vitu viwili hivyo kuwa makhalifa wake juu yenu, navyo ndivyo vitakavyo bakia hadi siku ya kiama, kitabu cha Mwenyezi Mungu chenye kutamka, na Qur'ani yenye kusema kweli, na mwangaza (nuru) yenye kumeremeta) na yenye daraja ya juu kabisa, na ni mwanga wenye kuangaza, yenye dalili na ushahidi ulio wazi, yenye kubainisha siri na mambo yaliyo fichika na rehma za Mwenyezi Mungu zilizo ndogo sana na zilizo fichika, dhaahiri yake ikiwa wazi na yenye kuonekana, yenye kuwatakia mema waliyonayo wafuasi wake wenye kutii amri zake na kuacha makatazo yake, (wafuasi wake mema yao ni yenye kupendwa na kutamaniwa na watu wa dini nyingine.

Kutokana na kupata kwao daraja ya juu kwa Mwenyezi Mungu, yenye kuwaongoza wafuasi wake kwenye maridhio ya Mwenyezi Mungu, na yenye kuwafikisha kwenye uokovu kwa kuisikiliza kwa kutii amri zake na kufuata maelekezo yake na hukumu zake na makatazo yake.

Kwani Qur'ani humuongoza mtu kwenye uongofu na kuepukana na upotovu, na kumfikisha kwenye nyumba ya utukufu. Kutokana na Qur'an ndio mtu huzifikia hoja na dalili za Mwnyezi Mungu zilizo wazi na zenye nuru kwa ajili ya kuwashinda maadui, na kutokana na Qur'an ndio twaweza kuzifikia faradhi zake, (mambo yake aliyo yafaradhisha na kubainishwa kwa uwazi kabisa), na kutokana na Qur'an ndio twaweza kuyafahamu mambo aliyo yahadharisha na kuyaharamisha, na kutokana na Qur'an twaweza kufahamu mambo ya wazi aliyo yabainisha na kuyafafanua na kuyadhihirisha wazi wazi, na dalili zake zenye kutosheleza, na fadhila zake alizo zifanya kuwa sunna kama sala za sunna na sala za usiku (Tahajjud) na mambo mengine mengi ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, na kuwahimiza kuyafanya, na mambo mengine mengi aliyo kupeni na kukuruhusuni kuyafanya kama biashara na miamala mbali mbali, na sheria zake alizo ziweka na kuwafaradhishia kuzitekeleza na kuzifanya kuwa wajibu.

Na akaifanya Imani kuwa ndio kitu cha kuwatwahirisha na kuwatakasa kutokana na ushirikina, na akaifanya Sala kuwa ni kitu cha kuwatakasa nyinyi kutokana na kiburi, na akaifanya Zaka kuwa ndio kitu cha kuzitakasa nafsi na kiongezacho Riziki, na akaifanya funga kuwa ndio kiimarisho cha ikhlasi (kumtakasia nia Mwenyezi Mungu), na akaifanya Hija kuwa ndio kitu cha kuimarisha Dini, na akaufanya uadilifu kuwa ndio kitu kiwekacho nidhamu kati ya nyoyo mbali mbali, na akaifanya twaa yetu (kutu tii sisi) kuwa ndio sababu ya watu kuwa na nidhamu katika maisha yao, na Uimamu wetu akaufanya kuwa ndio amana ya kuto tofautiana, na akaifanya Jihadi kuwa ndio sababu ya izza na utukufu wa Uislaam, na akaifanya subira kuwa ndio sababu ya kupata malipo mazuri, na kuamrisha mema akakufanya kuwa ndio maslahi kwa watu wote, mtu mmoja mmoja na hata jamii.

Na kuwatendea mema wazazi wawili akakufanya kuwa ni kinga kutokana na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na kuunga udugu (kwa kuwafanyia upole na wema jamaa) akakufanya kuwa ni sababu ya kuongezeka kwa umri (umri kuwa mrefu), na kuongezeka kwa kizazi, na akakufanya kulipiza kisasi kuwa ni sababu ya kupata msamaha na maghfira ya Mwenyezi Mungu, na kukamilisha vipimo na mizani akakufanya kuwa ni kubadilika na kugeuka hali ya upungufu na kuondoa hali hiyo ya upungufu katika biashara, kwani kukamilisha vipimo na kuto punguza vipimo ni baraka katika riziki na ni sababu ya kuongezeka kwa mali na ni sababu ya kuhifadhi na kulinda haki za watu.

Na akakataza kunywa pombe (mvinyo) ili kuwaokoeni kutokana na mambo machafu na mabaya na najisi mbali mbali zitokanazo na tendo hilo, (kwani kunywa pombe ni sababu ya kuondokewa na akili, kuharibika kwa kizazi na mwili na humpa mtu ushupavu wa kutenda mambo ya haram, na kuto tekeleza majukumu ya kiutu na mengineyo, na kujiepusha kuwatuhumu watu kwa uovu wa uzinifu ni kinga ya kupata laana ya Mwenyezi Mungu, na kujiepusha na wizi ni sababu ya kupata ucha Mungu na ni sababu ya kujikinga na matumizi ya watu bila ya idhini ya kisheria, na hiyo ndio Iffa.

Na Mwenyezi Mungu ameharamisha na kuzuia kumshirikisha ili waja wamtakasie yeye nia ya uungu katika ibada zao, kwa hivyo basi mcheni Mwenyezi Mungu kama inavyostahili (ukweli wa kumcha) na msife isipokuwa nanyi mkiwa Waislaam, na mtiini Mwenyezi Mungu kwa yale aliyo kuamrisheni na kukukatazeni kuyafanya, kwani kwa hakika si jambo jingine wamchao zaidi Mwenyezi Mungu kati ya waja wake ni maulamaa.

Kisha akasema:
Enyi watu fahamuni ya kwamba mimi ni Fatima na baba yangu ni Muhammad rehma na amani za Allah ziwe juu yake, ninasema kauli yangu hii mwanzo na mwisho, na siyasemi niyasemayo kimakosa, na wala silifanyi nilifanyalo kidhulma na kwa ujeuri au kwa kuvuka mipaka na kinyume na haki, kwa hakika amekujieni Mtume atokanae na nyinyi waarabu na akiwa ni mtu kama nyinyi, mwenye kutaabishwa sana na mashaka na taabu kubwa inayo kupateni, kama madhara myapatayo na mtakayo yapata na yatakayo wafika kwa kuacha kwenu njia ya haki na imani ya Mwenyezi Mungu na kuangamia kwenu katika akhera, akiwa ni mwenye pupa na hima kubwa ya kuwaongozeni na akiwa ni mpole kwa waumini. (Suratut-tawbah).

Ikiwa mtaiangalia vema nasaba yake na kumfahamu mtamkuta kuwa ni baba yangu kinyume na wanawake wenu, na ni ndugu wa mtoto wa Ami yangu kinyume cha wanaume wenu, na ni mtu bora kabisa anae faa kunasibishwa nae mtu yeyote rehma na amani ziwe juu yake na Aali zake.

Alifikisha ujumbe wa Mola kwa kudhihirisha maonyo na vitisho (kwa njia iliyo bora, na kuonyesha vitisho vya siku ya kiama), huku akiwa ni mwenye kujiepusha na njia na mwendo wa washirikina, na huku akiwapiga wao (viongozi wao) kwa dalili na hoja zenye nguvu, na hali ya kuwa akiyashika makoo yao na midomo yao na wasiwe na jambo la kusema, na akiwaita na kuwalingania watu kwenye njia ya Mwenyezi Mungu kwa hekima na mawaidha mazuri, akivunja masanamu na kuyadondosha (kuyaangusha) kwa kuyasukuma vichwa (na kuangukia vichwa) vyao, hadi kikundi kikubwa kikakimbia na wengine kurudi nyuma (kuto endelea na mapambano) na majeshi yao kushindwa vibaya hadi usiku wa kiza ukatoweka kutokana na kudhihiri kwa mwanga wa Asubuhi, na haki halisi kudhihiri wazi wazi bila kificho, na kiongozi wa haki kutamka na kusema yaliyo ya haki, sauti za mafasidi na wanafiki zikawa hazitoki wakawa mabubu hawana la kusema na unafiki wao kuteketezwa na chuki za ukafiri na uovu kutoweka, na wafuasi wa unafiki na watumishi wake kutoweka, na kusambaratika makubaliano (wafuasi) ya kufru, tofauti na unafiki, na kuimarika mizizi ya Imani.

Na hapo mkatamka na kukiri neno la Ikhlas (yaani laa ilaha illa llah), kwa haraka na kutoka moja kwa moja kwenye hali ya njaa (kutoka kwenye hali ya uhaba wa chakula) (yaani kwa nyuso zenu kuwa nyeupe na kupata utukufu na kujilinda kwao na kuto kula mali za watu kwa batili. (na hii ni kinaya cha matendo yao kuwa ni matendo ya Ikhlas na nyoyo zao kuwa safi, na mlikuwa kama tone la maziwa lililo changanywa na maji kwa mnywaji, na mlikuwa kwenye fursa nzuri kwa wale walio kuwa wakikutilieni tama ya kukushambulieni (yaani mlikuwa ni wachache na madhalili), na mlikuwa kama kijinga cha moto akichukuacho mtu mwenye haraka, na mlikuwa ni watu wenye kukanyagwa kwa miguu kutokana na udhalili wenu, na mkinywa maji ya njiani yaliyo chezewa na ngamia na kukojolewa na ngamia hao, na mkiifanya ngozi isiyo dibagiwa kuwa ndio chakula chenu.

Au mkila nyama iliyo kaushwa kwa jua), hali mkiwa madhalili wa kutupa (mkiwa mbali na miji) na utamaduni, mkiogopa watu walio kuwa pembezoni mwenu (majirani zenu) wasikushambulieni na kuwatekeni) Mwenyezi Mungu alie takasika akakuokoeni kutoka kwenye hali hiyo kutokana na Muhammad rehma na amani ziwe juu yake na Aali zake baada ya matatizo makubwa na madogo au matatizo ya muda mrefu, na baada ya kupata majaribio na mitihani ya watu mabubu (yaani mashujaa wasio fahamu njia na namna ya kutumia ushujaa wao) wa kiarabu na walio kuwa na nguvu, na mbwa mwitu wa kiarabu kama wezi na majambazi waliokuwa wakipora mali za watu kama mbwa mwitu.

Na baada ya kujaribiwa kwa wapingaji na wakiukaji wa amri kati ya watu walio pewa kitabu (Ahlul-kitab) ambao walikuwa ni wanafiki na walio kuwa kama mashetani walio asi, waliokuwa wakitakabari na kuvuka mipaka na sharia za Mwenyezi Mungu (Mayahudi na Wakristo na Majusi), kila walipo kuwa wakiwasha moto wa vita katika nafsi zao Mwenyezi Mungu akiuzima moto huo, na kila walipo kuwa wakijitokeza na kuchomoza wafuasi wa shetani, na kila washirikina walipo fungua midomo yao kwa ajili ya fitina au kila walipo kuwa wakifungua upenyo wa fitina humtupia na kumtuma nduguye (Ali bin Abi Twalib) kwenye upenyo na midomo yao na makao yao, (kwa maana kuwa kila walipo anzisha fitina basi Mtume huivurumisha haki juu ya batili kama alivyo kuwa akimtuma nduguye katika moto wa vita na hakuwa akirudi wala kusimamisha vita mpaka ahakikishe amewadhalilisha na kuutuliza moto wa vita vile kwa upanga wake, na alikuwa harejei mpaka akanyage masiko yao kwa miguu yake, na kuuzima moto wenye kulindima kwa upanga wake, alie kuwa akitaabika katika dhati ya Mwenyezi Mungu, yaani akiitabisha nafsi yake tukufu katika kutekeleza amri za Mwenyezi Mungu na makatazo yake.

Na akifanya juhudi wake zote na kutoa uwezo wake wote na kila anacho kimiliki kwa ajili ya kuliinua neno la haki, akiwa ni mtu wa karibu wa Mtume (s.a.w). (kwani alikuwa ni mtoto wa Ami yake na mtu wa karibu sana kwake katika maarifa ya Mwenyezi Mungu na wasii wake na khalifa wake, na huo ni ukaribu wa Uimam kwa Utume.

Sayyid (bwana) wa mawalii wa Mwenyezi Mungu mtukufu, mwenye kuharakia na mwenye maandalizi wakati wote katika twaa'a ya Mwenyezi Mungu na mtoaji nasaha za kweli na za kimatendo kwa Mtume (s.a.w), mwenye kufanya juhudi kubwa na mwenye kufanya kazi bila kuchoka na mfanyaji wa saa'i wakati wote wa kuinusuru haki, alie kuwa akifanya kazi na kupigana na makafiri na kuto sitishwa au kuogopa lawama za mtu yeyote katika kupigania dini ya Mwenyezi Mungu, na nyinyi mkiwa katika maisha mazuri, maisha ya kifahari (katika vyakula vinywaji na kujishughulisha na mambo ya kimaisha) mkiwa mmekaa raha mstarehe bila matatizo yoyote na mkiwa kwenye neema (mkiwa mmeneemeka) na mkiwa ni wenye amani na utulivu, huku mkisubiria kushukiwa kwetu na mabalaa na mitihani ya kidunia na kutoweka kwa neema alizo tuneemesha nazo Mwenyezi Mungu, na mkitaraji kufikiwa na habari za mitihani yetu na kufikwa kwetu na matatizo, na mkirudi nyuma na kurejea na kutoshiriki kwenye vita na mapigano (kati ya waislaam na makafiri katika zama za Mtume (s.a.w).

Na pindi Mwenyezi Mungu alipo mchagulia Mtume wake nyumba ikaliwayo na mitume wake (yaani nyumba ya rehma na msamaha wake na pepo yake) na marejeo ya watawala wake, ikadhihiri ndani ya nyoyo zenu alama na hikidi (chuki) za unafiki, na vazi la dini kuzeeka na kuchanika chanika, na yule aliekuwa na ghadhabu zake ndani ya moyo wake, na kiongozi wa wapotovu akatamka aliyo yataka kutokana na ghadhabu hiyo huku akiwa kinyume na mwendo wa Mtume (s.a.w), na akadhihiri alie kuwa dhalili na dhaifu akiwa kati ya kaumu yake waliokuwa wachache na madhalili, na walio kuwa hawana hadhi yeyote na nafasi yoyote kwa watu, na kutamka maneno yake au kutoa sauti yake kwa kupiga kelele mfano wa ngamia, huku akitamka maneno ya batili na upotovu, na huku shetani akikokota mikia yake katika safu zenu na nafsi zenu na katika akili zenu, na shetani kujitokeza na kudhihiri kutoka mafichoni mwake aliko kuwa amejificha akiogopa haki, huku akikuiteni nyinyi kwa sauti kubwa na akakukuteni ni wenye kuitikia wito wake, na mkiwa ni wenye kutekeleza malengo yake (kwani alikuoneni mkiwa tayari kupokea wito wake) na alikuoneni ni wenye kuhadaika na kufuata mambo ya kidunia (kama utawala na kupenda uongozi na kumtupa mkono wasii wa Mtume) akakuiteni kufuata amri zake.

Kisha akakutakeni msimame na kumsaidia, akakukuteni mkiwa ni watu makhafifu (wepesi) wa kuitikia wito wake, na akakuhamasisheni na kukutakeni kufanya haraka, na akawatia ghadhabu ya kuichukia haki, na akakukuteni mkiwa ni wenye kuichukia haki pamoja nae, mkawatia alama ngamia wa wenzi wenu (hiki ni kinaya cha kuwa mkawaona watu wengine wakiwa ni wenye kufuata haki na nyinyi mkiwa ni wenye kufuata batili na upotovu) na mkanywa maji yasiyo kuwa yale aliyo kuandalieni Mwenyezi Mungu.

Mliyafanya hayo wakati ambapo ahadi zenu mlizo wekeana na Mtume muda wake ni mfupi sana tangu kuwekwa kwa ahadi hizo, nanyi kugeuka na kubadilisha ahadi hizo (kama usia wake Mtume (s.a.w) alio utoa akiashiria ukhalifa wa Ali bin Abi Twalib (a.s) na kwamba hiyo ilikuwa ni ahadi aliyo ifunga pamoja nanyi, nanyi mkaikhalifu ahadi hiyo kwa maslahi ya kidunia na matakwa binafsi, huku jeraha likiwa ni kubwa sana, nalo ni jeraha la kufiwa na Mtume (s.a.w), na hali ya kuwa jeraha hilo bado halija pona nyinyi mmetofautiana na kufarakana na kukiuka na kuvunja ahadi yake (kwa khalifa wake) alie mteua na kumsimamisha siku ya Ghadiir (pale alipo simama na kusema:

Je mimi si bora kwenu kuliko nafsi zenu wakajibu ndio akasema: Ewe Mwenyezi Mungu yule ambae mimi nilikuwa ni mtawalia mambo yake basi Ali ni mtawaliaji wa mambo yake ewe Mwenyezi Mungu mtawalishe mwenye kumtawalisha Ali (mpende), na mfanyie uadui mwenye kumfanyia uadui Ali, na mnusuru mwenye kumnusuru Ali, na muache (mtupe mkono) mwenye kumuacha Ali), na hali ya kuwa Mtume bado hajazikwa, mkaharakia kutoa madai ya kuchelea (kuogopa) fitina.

Ama kwa hakika walitumbukia ndani ya fitina hiyo, na kwa hakika jahannam ni yenye kuwazunguuka na kuwachoma makafiri, (wale ambao walikhalifu amri zake na amri za Mtume wake), ni umbali ulioje uliopo kati yenu na kati ya haki na ukweli wa kushuhudia ya kuwa hapana Mola illa Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na mna nini nyinyi kwa haya amliyo yafanya (imekuwaje mkayafanya haya mliyo yafanya) ikiwa mwadai kuwa ni waislaam na wafuasi halisi wa Uislaam.

Mnakwenda wapi, wakati ambapo kitabu chenye kubainisha mambo yote na chenye hoja na dalili zilizo wazi kipo, na mambo yake ya faradhi yakiwa dhahiri na wazi, na hukumu zake zikiwa bayana, na mafunzo yake yakiwa ni yenye kumeremeta na kudhihiri, na makatazo yake yakiwa wazi na bayana, na maamrisho yake yakiwa wazi na dhahiri, hayo yote kwa hakika mmeyaweka nyuma ya migongo yenu, je mwayachukia na kuyapa migongo yenu na kuchukua mengineyo, (imekuwaje kuyaacha maamrisho hayo na kuyaweka nyuma ya migongo yenu na kuto yafuata) na vipi mwahukumu kwa hukumu zingine zisizo kuwa hukumu za Qur'ani kutokana na matamanio yenu na matakwa yenu?.

Haya mliyo yafanya kuwa ni mbadala wa Qur'ani na hukumu zake ni mabaya zaidi kwa ajili ya madhalimu, na mwenye kufuata dini nyingine tofauti na Uislaam hakitakubaliwa kwake kitu chochote nae siku ya kiama (Akhera) atakuwa ni miongoni mwa watu walio pata hasara (walio hasirika).

Kisha hamkukaa (hamkubakia) isipokuwa muda mchache tu baada ya kuyafanya hayo mliyo yafanya (kwa kuchukua utawala na kuzua fitina na kwenda kinyume na njia iliyo nyooka njia ya Qur'ani) na kabla fitina hiyo haija tulia na kupoa, na wakati utawala na uongozi ulipo wawia mwepesi kuuchukua, kisha mkaanza kuuwasha moto wake kwa mara nyingine na kuuchochea moto huo, na mkazidi kuufanya uwe ni wenye kulindima zaidi na zaidi, na huku mkiitikia wito wa shetani alie mpotovu, na mkizima nuru ya dini ya Allah yenye kudhihiri kila mahala na isiyofichika, na kuzidharau pia kuzificha kuzizima zisionekane na kuto zijali sunna safi za Mtume (s.a.w), mkinywa maziwa taratibu huku mkijifanya mnakunywa mapovu na mabaki ya maziwa, (ni mfano kwa maana kuwa mwajifanya kuwa mwafanya juhudi kwa ajili ya dini wakati hakuna mkitakacho isipokuwa dunia na saa'i yenu na juhidi zenu ni kwa ajili ya dunia).

Mwalificha jambo wakati ambapo mwayafanya hayo na mwatembea kwa ajili ya shetani na Ahli zake shetani na watoto wake kwa kujisitiri na kwa taabu kubwa (hii kinaya ya wale wafanyao matendo ya kishetani huku wakijaribu kuyaficha hayo wayafanyayo na kuyasitiri kwa vazi la dini).

Na maumivu yatufikiayo kutoka kwenu au kutokana na vitendo vyenu mfano wake ni kama mfano wa mtu mwenye kukatwa mwili wake na kuchomwa mwili wake kwa sime, na kuchomwa kwa ncha ya mkuki. (hii ni ishara ya machungu na maumivu ya moyo wayapatayo na ambayo yamekuwa yakisongamana kwao Ahlul-baiti kutokana na matendo wayashuhudiayo ya kuzififiza na kupinga juhudi na kazi ya Mtume (s.a.w) na kuiweka dini yake hatarini kwa jina la Mwenyezi Mungu mtukufu na kwa jina la dini). Nanyi hivi sasa mwadai ya kuwa sisi hatuna urithi wowote, je mwaitaka hukumu ya kijahili (mwahukumu kulingana na hukumu ya zama za kijahili) ni hukumu gani iliyo nzuri kuliko hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini ya kukutana na Mola wao,? Je hamlifahamu hilo? Hakika mwalifahamu, ndio hakika jambo hilo limekuwieni wazi (mwalifahamu wazi) kama jua likiwa katika ya mchana ya kuwa mimi ni binti yake Mtume (s.a.w).

Enyi Waislaam, je mwaridhia ninyang'anywe urithi wangu hali ya kuwa mwasikia na kuona? Ewe mtoto wa Abi Quhafah! hivi kweli waridhia kwa mujibu wa hukumu ya kitabu cha Mwenyezi Mungu umrithi babako na mimi nisimrithi babangu? Hakika umekuja na jambo zito, na uzushi mkubwa na mbaya kabisa. Je ni makusudi kabisa mmeacha hukumu ya kitabu cha Mwenyezi Mungu na kukiweka nyuma ya migongo yenu kwani chasema:

وورث سليمان داود

(Na Sulaiman akamrithi Daud) suratul an-namli aya 16 na akasema katika kusimulia habari za Yahya bin Zakaria pindi alipo sema:

فهب لي من لد نك وليا يرثني ويرث من آل يعقوب

Basi nipe mimi walii atokae kwako ili anirithi mimi na awarithi Aali (jamaa) za Yaaqub). Suratu Maryam 19, na akasema:

واولوالارحام بعضهم أولي ببعض في كتاب الله

Na ndugu wao kwa wao ni bora zaidi (kurithiana) katika kitabu cha Mwenyezi Mungu). Na akasema pia:

يوصيكم الله في أولاد كم للذ كر مثل حظ الأنثيين

Mwenyezi Mungu anakuusieni ya kuwa mtoto wa kiume apawe mara mbili ya wanawake wawili). Suratun-nisaa'i. Na pia akasema:

إن ترك خير الوصية للوالد ين والأقربين بالمعروف حقا علي المتقين

Ni bora ikiwa ataacha usia kwa ajili ya wazazi wawili na ndugu wa karibu kwa wema ni haki juu ya wamchao Mwenyezi Mungu). Suratul-baqarah 180.
Na mkadai ya kuwa mimi sina hisa yoyote wala sina urithi wowote kutoka kwa baba yangu, na wala hakuna udugu kati yetu, je Mwenyezi Mungu alikuhusisheni nayo nyinyi tu aya aliyo iteremsha na kumtoa baba yangu kwenye aya hiyo? Je si nyinyi msemao ya kuwa watu wa milla mbili (dini mbili tofauti) hawarithiani? Je mimi na baba yangu si watu wa milla (dini) moja? Na je nyinyi ndio wajuzi zaidi wa aya zinazo zikhassisi aya zilizo Ammu kuliko baba yangu na mtoto wa Ami yangu (yaani Ali a.s)? (Al-khas wal-amu) Basi jambo hili ni lako (ewe Abubakar) na ukiwa ni mwenye kuliongoza na likiwa ni lenye kuandaliwa na kuwekewa makalio yake…….

Utakutana nalo siku ya kufufuliwa kwao, ni ubora ulioje wa hukumu ya Mwenyezi Mungu, na kiongozi akiwa ni Muhammad, na siku iliyo ahidiwa ya kukutana ni siku ya kiama, na siku ya kiama watu wa batili watapata hasara, na wakati huo hakutakunufaisheni kujuta (majuto) kwenu, na kila habari ina mahala pake na mtakuja kumfahamu atakae jiwa (atakae patwa) na Adhabu yenye kudhalilisha na kupatwa na Adhabu ya daima isiyo koma.
Kisha akawageukia Ma'answari na kusema (a.s): Enyi mashuhuda (mashahidi), enyi wateule na walinzi (wasaidizi) wa dini, na wenye kuihifadhi na kuulinda Uislaam, ni udhaifu gani huu mlio nao wa kuto itetea haki yangu na ni uzembe gani huu muufanyao katika dhuluma ninayo fanyiwa nanyi kuto jali? Je baba yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuwa akisema!

(Mtu huhifadhiwa katika kizazi chake)? Ni kwa kiasi gani mmekuwa wepesi na mmefanya haraka kuzua mambo, (ni kipi kilicho kufanyeni mfanye haraka na muwe wepesi kuzua mambo) na kuvunja ahadi, na ni kwa kiasi gani mmeachana na kumnusuru Mtume wenu pamoja na kuwa ni muda mchache tangu kutengana nae wakati mnao uwezo wa kufanya ninalo jaribu kulitekeleza (kutetea haki yake) na ni wenye uwezo na nguvu ya kulifanya nilikusudialo, mwasema ya kuwa Muhammad amekufa na kwamba hamta muona baada ya kifo chake.

Basi jambo hilo ni kubwa na limepanuka na kutangaa, na ufa wake umekuwa mkubwa, na ardhi imekuwa kiza kwa kutokuwepo kwake (kwa kutoweka kwake), jua na mwezi kushikamana (kupatwa) na nyota kutawanyika kutokana na msiba wake, na matarajio kukatika, na majabali kunyenyekea na kupatwa machungu kwa kufariki kwake, na himaya (uangalizi) ikapotezwa na kutoweka na heshima na utukufu kuondolewa wakati wa kufariki kwake, nina apa kwa jina la Mwenyezi Mungu hakika hilo ndio balaa kubwa na mtihani mkubwa kabisa, na msiba adhimu, hakuna balaa na msiba mkubwa kuliko huo, na hakuna balaa la haraka zaidi mfano wake, lilizungumziwa na Qur'ani kwa uwazi kabisa (na kitabu cha Mwenyezi Mungu alie takasika kwa uwazi kati ya majumba yenu. (nje ya majumba yenu)

Asubuhi na jioni, ikipiga kelele na kutoa wingwi pembezoni mwa majumba yenu, na kwa kuisoma kwa lugha fasaha na kwa lahaja ya waarabu, na kueleza yaliyo wafika Mitume walio kuwa kabla ya Mtume huyu, hukumu yenye kubainisha haki na batili, na hukumu isiyo teteleka pale alipo sema:
(Hakuwa Muhammad isipokuwa ni Mtume kwa hakika wamepita kabla yake mitume ikiwa atakufa au kuuwawa mtarudi nyuma ya visigino nyenu, na mwenye kurudi nyuma alikotoka hatomdhuru Mwenyezi Mungu kwa chochote na Mwenyezi Mungu atawalipa wenye kushukuru). Surat -al-imaran 144.

Ni umbali ulioje wa kutokea jambo hili (usaidizi). Enyi wana wa Qailaa (Awsi na Khazraji)? Hivi kweli urithi wa baba yangu waporwa na kuchukuliwa na kuliwa hali ya kuwa mnaona na kusikia?, na hali mkiwa katika vikao vya watu hao, (je kweli nadhulumiwa urithi wa baba yangu hali ya kuwa nyinyi mpo na mkiona na kusikia dhuluma na uadui ninaofanyiwa) kwa hakika wito wa ukweli unakuhusuni nyinyi na ubainifu huu na maonyaji haya niliyo yatoa pia ni yenye kuwahusu nyinyi.

Wakati nyinyi idadi yenu ni kubwa ya kutosha na ni wenye uwezo na maandalizi ya kuinusuru haki kutokana na wingi wenu na kutokana na nguvu mlizo nazo, pia ni wenye nyenzo na nguvu katika jamii ya kiislaam, na hali ya kuwa mnazo silaha za kuithibitisha haki na mnazo ngavu za kudhibiti uadui ufanywao.

Mnafikiwa na wito wa kuinusuru haki na hamuitikii wala kujibu wito huo, na mnafikiwa na wito wa watu wenye kudhulumiwa ambao mwafahamu fika kuwa ni wenye kudhulumiwa na hamtoi msaada wowote, hali ya kuwa nyinyi ni watu wenye kusifiwa kwa ushujaa na ujabari, na wenye kufahamika kwa itikadi nzuri na wenye matendo mema, na mkiwa ni chaguo zuri lililo chaguliwa kubeba ujumbe na kuutetea.

Mme wapiga vita waarabu kwa ajili ya dini na kustahmili matatizo na taabu na kuto tetereka katika vita, na mkiwa ni watu mlio chaguliwa kwa ajili ya kulinda dini na kwa ajili yetu Ahlul-baiti (a.s) na mkawapiga vita kaumu mbali mbali na kuwashinda na kupambana na mashujaa mbali mbali mkiwa si wenye kujali, nasi tukiwa si watu wenye kujali katika kutekeleza amri za Mtume na Ahlul-baiti wake (a.s) tukiwa amrisha nanyi kutii amri, hadi Uislaam ukatimia na kukamilika kutokana na sisi, na kheri za Uislaam kuenea na kutangaa (kama vile ukombozi wa nchi mbali mbali na kupatikana kwa ghanima (ngawira) zilizo patikana.

Na wito kuenea na matunda ya haki na uadilifu kudhihiri, na washirikina kusarenda na kusalim amri kutokana na ushindi wa Uislaam, na sauti za uongo na uzushi na vitimbwi kuzimika na kutoweka, na moto wa ukafiri kuzimika waliokuwa wakiuwasha dhidi ya Uislaam na waislaam, na wito wa batili na matatizo kutulia, na kuenea kwa nidhamu ya dini, sasa imekuaje baada ya kuifahamu haki na kufanya juhudi kubwa kuithibitisha na kuitetea haki mmekuwa ni wenye kutatizika na kutokuwa na misimamo madhubuti kuhusu mambo yenu, na imekuaje mmekuwa ni wenye kuficha ukweli mlio ufahamu baada ya kuwa mlikuwa mkiutangaza na kuto tatizika katika kuunusuru, imekuwaje mwarudi nyuma baada ya kuwa mlitangulia na kuwa mbele katika kuutetea, na imekuwaje mwamshirikisha Mwenyezi Mungu baada ya kuamini, ni ubaya ulioje wa watu walio kwenda kinyume na ahadi zao baada ya kuzifunga na kutoa ahadi hizo na wakaazimia kumtoa Mtume katika mji wa madina na hali ya kuwa wao walikuanzeni, je mwawaogopa wakati ambapo Mwenyezi Mungu ndie mwenye haki na anae paswa kuogopwa ikiwa kweli nyinyi ni waumini. (suratut-tawbah 13).

Ama kwa hakika ninaona baada ya kuisimamia na kuitetea haki ambayo mlikuwa mkiitekeleza na baa ya kustahmili shida na taabu kubwa kwa ajili yake mmekuwa ni watu wenye kupenda starehe na kuacha kuitetea haki, na mka mtenga na kumuweka kando mtu ambae alikuwa ndie mwenye haki zaidi ya kuitekeleza sheria na mwenye maarifa zaidi ya sehemu za kukunjua mkono na sehemu za kuukunja mkono huo, (yaani mwenye kufahamu sehemu za kutoa na zisizo stahili kutoa).

Na mkakaa kando mkistarehe peke yenu na kuyakimbia majukumu kutokana na mas'ulia yaliyomo kwenye majukumu hayo na kwenda kwenye raha za maisha na kutostahmili majukumu, na mkayatupilia mbali yale mliyo yafahamu na kuyahifadhi (yaani mkaitupilia mbali dini ambayo mlikuwa mmeihifadhi na kuwa chini ya bendera yake (deraya) kwa kufanya uadilifu wenu kuwa wapole na kuwa ndugu mkaiacha kando pale mlipo itika wito wa shetani) na mkavitapika vile vinywaji mlivyo vinywa kwa raha mstarehe, ikiwa nyinyi mtamkufuru Mwenyezi Mungu pamoja na wote waliomo ardhini hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kujitosheleza na mwenye kusifika kwa sifa njema.

Fahamuni ya kuwa nimeyasema haya niliyo yasema nikiwa ni mwenye maarifa kamili ya furaha mliyo nayo na iliyoko katika nafsi zenu na nikifahamu kamili uvunjaji wa ahadi ulio onyeshwa na kuwa nao nafsi zenu, lakini maneno haya ni kitu kilicho dhihirishwa na nafsi na ni matokeo ya ghadhabu na hasira, na ni kutokana na kushindwa kustahmili (ustahmilivu mchache) na ni kutokana na kudhikika kwa kifua na kuto weza kuyastahmili, na ni kwa ajili ya kusimamisha na kutimiza hoja juu yenu (si kwa kutaraji kupata msaidizi).

Basi uchukueni utawala huo na uchukueni kwa mabavu maadamu mmekataa kufuata njia iliyo nyooka na ya wazi, na uchukueni hali ya kuwa ni wenye kujeruhiwa (au hali ya kuwa ni wenye jeraha mgongoni mwake), na wenye miguu dhaifu (hapa ameufananisha Ukhalifa na farasi alie jeruhiwa mgongo wake na mwenye miguu dhaifu asie weza kutembea) na huku ukiwabebea aibu, na huku ukiwa umeambatana na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu daima na daima, na aibu isiyo kwisha, na ukiwa umeungana na moto wa Mwenyezi Mungu uwakao bila kukoma au kuzimika, moto ambao huvichoma vifua.

Na hayo myafanyayo mnayafanya huku yakionwa na Mwenyezi Mungu, na siku hiyo wataelewa wale walio dhulumu ni mrejeo gani watakayo rejea. Na mimi ni binti wa Muonyaji (Nadhiir) wenu mbele yangu kuna adhabu kali, fanyeni amali zenu hakika sisi ni wenye kufanya amali, na subirini matekeo ya amali zenu hakika sisi ni wenye kusubiri matendo ya amali zetu.

Abubakar Abdallah bin Othman akamjibu na kusema:
Ewe binti wa mtume wa Allah, kwa hakika babako alikuwa ni mpole na mkarimu na mwenye huruma na rahim kwa waumini, na juu ya makafiri kuna adhabu yenye kuumiza na adhabu kali, ikiwa tutamuangalia nasabu yake tunamkuta kuwa ni baba yako tofauti na wanawake wengine, na ni ndugu wa mumeo tofauti na ndugu wengine, alimsaidia na kujitolea kumuenzi kuliko kila rafiki mpenzi.

Na akamsaidia katika kila jambo zito, hakupendeni isipokuwa mtu mwema na hakuchukieni isipokuwa muovu alie mbali na uongofu, nyinyi ni kizazi chema cha Mtume wa Mwenyezi Mungu mlio teuliwa na kuchaguliwa, dalili zetu ni juu ya kheri na mwendo wetu ni kuelekea peponi, na wewe ewe mwanamke mteule na bora, na binti wa Mtume mteule, unasema kweli katika kauli yako, na hakuna shaka katika utimamu wa akili yako, si mwenye kutaradadi katika kudai haki yako, na si mwenye kuzuiliwa kupata haki yako, naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kamwe sijaacha na kukiuka na kwenda kinyuma na kauli na njia ya Mtume wa Allah, na kamwe sikufanya jambo lolote isipokuwa kutokana na ruhusa yake, na kiongozi kamwe hawaongopei raia zake.

Kwa hakika mimi nina shuhudia na namshuhudisha Mwenyezi Mungu na anatosha yeye Allah kuwa shahidi ya kuwa mimi nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema: (Sisi mitume haturithishi dhahabu wala Fedha wala nyumba wala shamba, bali sisi hurithisha kitabu na hekima, elimu na utume, na urithi wowote tulio kuwa nao ni wa Waliyul-amri (Mtawala wa mambo ya Waislaam) baada yetu, yeye ahukumu katika urithi huo kwa mujibu wa hukumu yake, kwa hakika Farasi na silaha nilizo zichukua nimeziweka ili Waislaam wazitumie kupigania vita na kupigana jihadi na makafiri, na wazitumie kupigana na waovu na waasi, na sikufanya hivyo isipokuwa ni kutokana na Ijmai ya Waislaam wote, sikujifanyia mimi peke yangu na wala sikulifanya hilo kwa uamuzi wangu pekee, na haya ndiyo mali yangu na hii ndio hali yangu, ichukue na iko mbele yako, hutanyang'anywa na hatuna akiba yoyote tuiwekayo tofauti nawe.

Hakika wewe ni Sayyidah (bibi) wa umma wa baba yako, na mti mwema wa wanao, na hatuipingi fadhila yoyote uliyo nayo na wala halipotolewi lolote katika tawi lako na asili yako, hukumu yako ni yenye kutekelezwa juu ya yale yaliyoko katika milki yangu, je wataraji niende kinyume na kumkiuka baba yako (s.a.w) katika hilo?

Fatima (a.s) akasema:
Utakasifu ni wake Mwenyezi Mungu baba yangu kamwe hakuwa ni mwenye kuacha kutekeleza amri za kitabu cha Mwenyezi Mungu, wala hakuwa ni mwenye kupinga wala kwenda kinyume na hukumu zake, bali alikuwa ni mwenye kufuatilia hatua kwa hatua athari na amri zake, na akifuata mipaka yake, je mwafanya Ijmai juu ya kufanya hadaa na kukhalifu ahadi kwa kumtolea sababu za uongo na za kuzua? (ili kuyapa uhalali matendo yenu) na haya mliyo yafanya baada ya kufariki kwake ni sawa na yale maovu aliyo tendewa katika zama za uhai wake!

Hiki hapa kitabu cha Mwenyezi Mungu chenye hukumu za uadilifu , na kitamkacho ubainifu, kinasema: (Atakae nirithi mimi na kuwarithi wana (Aali) wa Yaakub, na pia kinasema: (Na Sulaiman akamrithi Daud), na Mwenyezi Mungu alietakasika akabainisha mgawanyo wa hisa za urithi (vigao vya hisa), na akaweka sheria kwa kubainisha faradhi za urithi, na kudhihirisha hisa ya wanaume na wanawake, jambo lililo ondoa sababu na illa za wafuatao batili, na kuondoa dhanna na shubha za aina mbali mbali kwa watakao bakia, hapana, walikuwa wakiyafahamu haya, bali nafsi zenu zimekupendezeeni (na kukupambieni kulifanya jambo hilo, uvumilivu (subira) ni mwema na Mwenyezi Mungu ndie msaidizi kwa haya myasemayo.

Abubakar akasema:
Amesema kweli Mtume wa Mwenyezi Mungu, na amesema kweli binti yake, wewe ni madini ya hekima (chimbuko), na mahala pa uongofu na rehma, nguzo ya dini na hoja yenyewe, sioni kwamba ukombli na ukweli, (kwa hakika ni mwenye kusema kweli) na wala sipingi hotuba na maneno yako, hawa hapa Waislaam wakiwa mashahidi kati yangu mimi na wewe, basi jifungamanisheni na yale niliyo jifungamanisha nayo, na kwa kuwatii kwao, niliyo yachuku niliyachukua bila ya kujitweza (kufanya kiburi) wala kwa uamuzi wangu peke yangu, wala sikufanya uamuzi mimi binafsi na sikuyafanya yangu binafsi kwani wao ni mashahidi juu ya hayo.

Kisha Fatima (a.s) akawageukia watu na kusema:
Enyi Waislaam, wenye kuharakia kwenye maneno ya batili yasemwayo (yasemekanayo), wenye kuridhia matendo mabaya na ya hasara, je hamuizingatii (hamifanyii mazingatio) Qur'an au kwenye nyoyo zenu kuna makufuli? Hapana (si hivyo kawme bali yamekuwa mazuri kwenye nyoyo zenu yale maovu mliyo yafanya (matendo yenu maovu), kwa hivyo masikio yenu yakaziba na kuto sikia na macho yenu kuwa pofu, na ni ubaya (uovu) ulioje wa taawili (tafsiri) mlizo zifanya, na ni mabaya sana hayo mliyo yaashiria, na ni mabaya zaidi hayo mliyo yachukua kwa mabavu na kuyapora, naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu hakika mtayakuta ni mazito sana kuyabeba, na mwisho wake ukiwa ni mgumu, pindi (siku ambayo) pazia litakapo ondolewa machoni kwenu, na kudhihiri wazi wazi madhara makubwa nyuma yake, na kukudhihirikieni kutoka kwa Mola wenu ambayo hamkuwa mkiyatarajia, na hapo wenye kufuata batili kupata hasara.

Kisha akaligeukia kaburi la Mtume (s.a.w) na kusema: Kwa hakika baada yako kulikuwa na habari na mambo makubwa na mazito, lau kama unge yashuhudia usinge kuwa ni mwingi wa kutoa hotuba (kuzungumza).

Hakika sisi tumekukosa wewe na kwa kukukosa wewe ardhi imekosa mvua na kheri zake, na watu wako (kaumu yako) wameingiwa na kasoro, kwa hiyo shuhudia na usiwe kando nao.

Na kila mtu anacho cheo na ukaribu kwa Mwenyezi Mungu na ni mwenye kujikurubisha kwa sharifu (mtukufu). Ulipo ondoka watu wakadhihirisha waliyo kuwa nayo ndani ya vifua vyao na nyoyo zao na ardhi ikawa ni kizuizi cha kukufikia wewe. Watu walituelekea kwa nyuso zenye kukunjamana na ghadhabu na kutudhalilisha pindi tulipo kukosa, na ardhi yote imeporwa na kuchukuliwa kwa mabavu.

Wewe ulikuwa ni mbalamwezi na nuru waitegemeayo watu kupata mwanga, na juu yako ndio vilikuwa vikishuka vitabu kutoka kwa Mwenye utukufu. Na Jibrilu alikuwa akitulewaza kwa aya za Qur'an, kwa hivyo umetoweka na watu kukukosa pia na kheri zote zimezuilika (zimewekewa hijabu hazitufikii).

Laiti mauti yangetufikia sisi kabla yako pindi ulipo ondoka na kutoweka na udongo ukatuzuwia kukufikia wewe. Kisha Fatuma (a.s) akarejea na kumkuta Amiril-muuminiin akimsubiri na akitaraji kurudi kwake nyumbani na huku akiangali huku na kule kuona atatokea wapi, na alipo fika nyumbani na kutulia akamwambia Amiril-muuminiin (a.s):
Ewe mtoto wa Abi Twalib mbona umejifunika na kujifunga maguo kama mtoto mchanga, na mbona umeketi kwenye nyumba ya mwenye kutuhumiwa, ewe ulie fanya maamuzi makali na kupinga mambo mengine kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu, subiri khiyana ya watu kwa kupinga kwako nguvu ambayo mbwa mwitu na mbweha walisalenda kwa nguvu hiyo, na kukufanyia khiyana manyoya yaliyo dhalili, (hiki ni kinaya cha mtu alie acha vita na asie na silaha ya kupigania) (Yaani mtu alie weka chini silaha na kutotumia nguvu matokeo yake ni watu wote kumfanyia khiyana, watu walio zoea katika historia yao kuunga mkono nguvu, sawa iwe ya haki au ya batili).

Mwenye kuweka chini silaha kwa ajili ya maridhio ya Mwenyezi Mungu hapana budi asubiri upingaji wa watu wote hata mabaradhuli). Huyu hapa mwana wa Abi Quhafah akinipora urithi nilio pewa na baba yangu, (akiashiria shamba la Fadak) na chakula cha kuwatosheleza wanangu, ama kwa hakika amedhihirisha na kutangaza wazi kabisa dhuluma aliyo nifanyia na kudhihirisha uadui wake kwangu ulio mkubwa, na akanizuilia kupata usaidizi wa makabila mawili (Ausi na Khazraji), na usaidizi wa muhajirina, na watu kunipa nyongo na kujiepusha nami na kuto nisikiliza wala kunijali.

Hakuna mtetezi awezae kuitetea haki, wala hakuna awezae kuzuia nguvu ya maadui na wachokozi, nimetoka nikiwa ni mwenye kudhibiti hasira yangu na mwenye subira, na nimerejea ni kiwa ni mwenye kudhulumiwa na kunyimwa haki yangu, na nikiwa sina hoja yoyote ya kulishika jambo hilo, laiti mimi ningekufa kabla sijafikwa na udhalili kama huu wa kulazimika kuyanyamazia hayo wayafanyayo watu hawa, na laiti ningefikiwa na mauti kabla ya siku ya kufariki kwangu, naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu hakika yeye ndie mwenye kufahamu udhuru wangu kwa yale niliyo yazungumza nikikuhami na kukutetea wewe, kwani yeye ndie mwenye kufahamu niyasemayo na mwenye kukubali udhuru wa wasemao kweli.

Maumivu yangu na huzuni yangu ni kubwa kila lichomozapo jua na kila lizamapo (akiwa na maana kuwa kwa kufariki Mtume (s.a.w) hapana budi tusubiri watakayo yafanya watu hawa na tusitaraji isipokuwa kupambana na mambo mazito na kutokea kwa uzushi kwa jina la dini asubuhi na jioni (wakati wote).

Mwenye kutegemewa amefariki (yaani Mtume) na wasaidizi kuwa madhaifu (Ahlul-baiti) baada yake, kwa hivyo namshitakia baba yangu juu ya dhuluma niliyo fanyiwa, na namshitakia Mwenyezi Mungu juu ya uaduia niliofanyiwa, ewe Mwenyezi Mungu hakika wewe ni mwenye uwezo na nguvu sana kuliko wao, na mwenye nguvu na ghadhabu kali kwa madhalimu.

Amiril-muuminiin (a.s) akamjibu: Huna sababu ya kuhuzunika na kujuta kwani huzuni hanayo yule aliestahmili huzuni na mateso ya dunia yenye kumalizika, bali maumivu na huzuni na majuto ni ya yule alie iuza akhera yake kwa dunia yake, kwa hivyo akainunua huzuni ya milele na ghadhabu ya Jabbar, nao si wengine bali ni maadui wako.

Izuie nafsi yako kunako ghadhabu na huzuni (usihuzunike) ewe binti wa Mtume (s.a.w) na ishi kwa utulivu na raha na kuwa ni mwenye subira na mtoto wa Mtume wa pekee ulie bakia, naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu sijakuwa dhaifu wala kushindwa katika kutekeleza jukumu langu la kidini na wala sikukosea katika makadirio yangu ya kuitetea haki, ikiwa unataka matumizi ya kukutosheleza kuisimamisha haki basi fahamu ya kuwa riziki yako ni yenye kudhaminiwa, na msimamizi wako pia mlezi wako (ambae ni Mwenyezi Mungu) ni muaminifu juu ya usimamizi wake, kwani yeye ndie mwenye dhamana ya kutoa riziki za waja na hakhalifu wala kukiuka ahadi zake, na riziki uliyo ahidiwa na kuandaliwa na ya milele ni bora zaidi kuliko hiyo waliyo kupora na kukuzuilia. Basi matarajio yako na subira yako mtegemezee Mwenyezi Mungu. Fatuma akasema: Najitegemeza kwa Mwenyezi Mungu (yeye ndie nimtegemea. Na akanyamaza.

MWISHO

REJEA:

Al-ihtijaaj, juzu 1 98.

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini