Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MA'AD {UFUFUO}

0 Voti 00.0 / 5

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

MA'AD {UFUFUO}

Assalaam Alaikum.

Ma'ad ni moja kati ya Nguzo Kuu tatu za dini tukufu ya kiislaam na mojawapo ya mambo muhimu katika dini hii tukufu.Tunatambua wazi kuwa kila Mtu anaweza kutofautisha kati ya vitendo vizuri na vibaya kwa kutumia maumbile aliyopewa na na eliyemuumba (yaani Mwenyeezi Mungu -s.w-).Utakuta kila mtu anauchukulia wema (hata kama yeye binafsi hafanyi wema) kuwa ni jambo zuri na lenye kupaswa kutekelezwa na kwamba vitendo vibaya na viovu (hata kama yeye binafsi ni mtenda maovu) ni jambo baya sana na linalopaswa kuachwa.

Bila shaka yoyote,ubaya na uzuri na wema pia,yote haya yanatokana na mitazamo ya matokeo na pia malipo ya sifa hizi mbili.Vile vile kila mtu atakubaliana na mimi katika kauli hii kwamba hakuna hata siku moja mtenda matendo mazuri akakosa kupata malipo ya matendo yake mazuri na mtenda matendo maovu akakosa kupata malipo ya matendo yake maovu.Lakini hapa mtu anaweza kuuliza swali hili:Mbona kila tukichunguza kwa jicho kali sana tunatakuta watenda mema huishi katika mashaka na matatizo na wakati huo huo watenda maovu na mabaya walio wengi ambao huhusika kikamilifu na uhalifu na ukatili na unyama pamoja na kuwa na tabia zote mbaya na khabithi wanaishi katika hali ya furaha na saada?.!

Jawabu la swali hili ni kama tulivyotangulia kusema kwamba hata kama mtu anatenda matendo maovu, lakini ukimuuliza je kutenda matendo maovu ni vizuri?atakujibu hapana! Hawezi kukujibu kinyume na jibu hilo kwa sababu maumbile ya mwanadamu hayatambui kuwa ni jambo zuri,bali huutambua ubaya kuwa ni jambo ovu lenye kupaswa kuachwa,nah ii ndio maana hata muovu huona uovu wa matendo yake na kamwe hawezi kuwa na matumaini ya kulipwa malipo mema kutokana na uovu wake bali katika nafsi yake anajua wazi mia kwa mia kuwa malipo ya matendo yangu haya mabaya ni malipo sawa sawa,kama anavyojua mtenda mema na mazuri kuwa malipo ya matendo yangu haya mazuri ni malipo sawa sawa hata kama itaonekana ataishi kwa mashaka na matatizo na Yule muovu akaishi kwa raha na furaha hali ya kuwa ni muovu.Kila mmoja (yaani mwema na muovu) katika nafsi zao anajua kuwa mimi ninastahiki kupata malipo mema kwa matendo yangu mema,na muovu anajua kuwa mimi ninapaswa kupata malipo maovu kama matendo yangu yalivyo.

Lakini kiufupi Muovu kuishi maisha ya furaha na mwema kuishi maisha ya tabu na mashaka,hii ni kwa kipindi kifupi tu kila mtu kuwa katika hali aliyokuwa nayo,hali hiyo haiwezi kuwa hivyo milele pasina kubadilika,bali mwema kuishi kwa raha na furaha na muovu kuishi kwa mashaka na tabu kutokana na uovu wake,hii ndio hali ambayo kila mtu anastahiki kuipata hata kama kwa sasa hivi kila mtu haijamfikia hali hiyo,ama wakati wake ukifika na ikamfikia kila mtu hali yake anayotakiwa kuwa nayo kulingana na matendo yake mazuri au mabaya,basi haibadiliki kamwe na kuwa vingenevyo bali milele ataishi (ikiwa alikuwa mwema) kwa saada kutokana na wema wake na ataishi (ikiwa alikuwa muovu) kwa tabu na mashaka na adhabu kali kutokana na uovu wake kama tutakavyogusia hivi punde katika suala hili.

SWALI
Swali ni kwanini Mtu anakuwa na hali kama hii au kwa ibara nyingine ni kwanini Mwanadamu anazingatia katika nafsi yake kulingana na maumbile ya kiuanadamu kuwa wema ni jambo lenye kustahiki kutekelezwa (hata kama hatendi wema yeye binafsi) na kuwa uovu ni jambo linalotakiwa kuachwa (hata kama yeye binafsi ni mtenda maovu)?

Jawabu la swali hili ni kama ifuatavyo:
Ni kwamaba katika Mustakbarli na katika Ulimwengu usio kuwa huu (wa duniani), kama kusingelikuwepo siku ya malipo au kama kusingelikuwepo siku ambayo imewekwa (rasmi) kwa ajili ya kuhukumu na kutoa malipo yanayofaa kwa vitendo vizuri na vitendo vibaya,basi uzingatiaji huu wa anaoumiliki kila mwanadamu (kuwa wema ni mzuri na ni muhimu na kwamba uovu ni mbaya) usingelikuwepo katika maumbile ya Mwanadamu.

Haipaswi (kabisaa) kudhaniwa kuwa malipo ya wema ambao mwanadamu huchukulia kuwa ni jambo zuri, huleta (yaani hayo malipo) mpangilio na utaratibu katika jamii na hatimaye watu kupata saada maishani na kuwa mtu mwema mwenyewe hupata sehemu flani ya wema alioufanya.Na vile vile haipaswi kudhaniwa kuwa mtu muovu huivuruga jamii kwa vitendo vyake viovu na kuwa yeye mwenyewe hukabiliwa na athari mbaya za vitedno hivyo.!

Ndio hata kama fikra ya aina hiyo ni sahihi kwa kiwango flani kwa wale wasiokuwa na mpangilio na wasiofaa,jambo hilo halihusiani na wale watu waliofikia kilele cha uwezo na ambao furaha na ushindi wao kamwee hauathiriwi na kuwepo au kutokuwepo mpangilio katika jamii.Kinyume cha hivi,wakati machafuko na ghasia zinapotokea katika jamii na wakati ambapo maisha ya watu huwa mabaya sana,watu hawa (yaani wale waliofikia kilele cha uwezo) huwa na furaha na kuhisi ushindi zaidi,yaani itakuwa ni vigumu sana kwa mtu yeyote yule kuwafanya watu hao wauone wema kuwa ni jambo zuri na uovu kuwa ni jambo baya!

Vile vile hata kama watu hawa huwa na saada katika kipindi kifupi cha maisha yao,haipaswi kuwa majina yao yatakuwa mabaya na kuchukiwa na watu milele kwa sababu ya vitendo vyao viovu.Hii ni kwa sababu dhihirisho la ubaya wa majina yao na kuhukumiwa vibaya na kizazi cha baadaye hutimia katika hali ambayo watu hao wanakuwa wameisha kufa tiyari na kutokuwa na athari yoyote katika maisha yao yaliyokuwa yamejaa furaha tele,raha pamoja na uchangamfu.

Kwa hiyo (Ikiwa hayo yote hayapaswi kudhaniwa kwa sababu tulizozitaja) hakutakuwepo haja ya mwanadamu kuuchukulia wema kuwa ni jambo zuri na hivyo kutaka kulitekeleza,wala uovu kuwa jambo baya na hivyo kutaka kuliepuka,natija itakayopatikana ni kulegea kwa itikadi tuliyoitaja katika Aqoid kuwa kila mtu anaitikadia kuwepo kwa Mwenyeezi Mungu (s.w) Muumba wa Mbingu na Ardhi na vyote vilivyomo, asiyekuwa na mshirika mwenye kustahiki kuabudiwa yeye tu.Kama kusingelikuwepo Ma'ad (Ufufuo), itikadi hii ingelikuwa itikadi isiyokuwa na msingi na natija hii tuliyoitaja hapa ingelitimia kirahisi tu.

Kwa hiyo kupitia maumbile haya safi ambayo tumepewa na Mwenyeezi Mungu (s.w) Muumba wa kila kitu, ni lazima tuelewe kuwa Mwenyeezi Mungu (s.w) atawafufua watu wote (au viumbe wake wote) baada ya kufa na kuvichunguza vitendo vya watu hao walivyovitenda katika maisha yao mafupi ya duniani.Mwenyeezi Mungu (s.w) atatoa Malipo mazuri na Baraka za milele kwa watenda mema kutokana na vitendo vyao vizuri,na kuwaadhibu waovu kwa vitendo vyao viovu.Siku hii ya kuvichunguza vitendo vya watu baada ya kuwafufua ili walipwe kulingana na walivyotenda huitwa:

YAUMUL-QIYAAMA,(yaani siku ya kiyama).

Na laiti kama isingelikuwepo siku hii (siku ya kiyama au Ma'ad),hakuna mwanadamu yeyote ambaye angelihisi kuwa wema unatakiwa kwa kuwa ni mzuri na ubaya hautakiwi kwa kuwa ni mbaya.Hivyo chanzo cha kuwa na hisia kama hizi na kuzingatia huku kunakopatikana kwa kila Mwanadamu yeyote yule (kuwa wema ni mzuri na uovu ni mbaya)si kingine bali ni kwa sababu ya kuwepo siku hii ambayo Muumba wa kila kitu kaiweka ili kuwalipa wale watenda wema malipo ya wema wao,na kuwalipa wale watenda maovu malipo ya maovu yao.Hivyo haipaswi kudhaniwa kuwa kuna chanzo kingine tofauti na hicho kuhusiana na suala hilo kama tulivyoashiria kunako hilo.

MA'AD ,DINI NA IMANI.
Dini zote ambazo huwaita watu katika kumwabudu Mwenyeezi Mungu (s.w) na kuwasihi wafanye mambo mema na kujizuia na mabaya, huamini Ma'an na maisha ya baadaye huko akhera ya milele.Utakuta watu hao hawana (wa dini hizo wenye kumuabudu Mwenyeezi Mungu (s.w)) shaka kuwa wema huwa na thamani unapokuwa na malipo mazuri, na kwa kuwa hatuyaoni malipo hayo mazuri humu duniani,basi bila shaka malipo hayo yapo na yataonekana huko akhera ambapo atayapata yule aliyetenda wema. Istoshe zile dalili na athari zinazoonekana katika makanisa ya kale yanayogunduliwa na wataalaam wa mambo ya kale zinaonyesha kuwa watu wa kale walikuwa na imani katika maisha ya baadaye au kwa ibara nyingine walikuwa na imani na maisha yatakayofuatia (ya milele) baada ya maisha haya mafupi ya duniani.Na kwa msingi wa itikadi yao enzi hizo,walikuwa wakifanya baadhi ya mambo katika desturi zao na kuwapa wafu vifaa (fulani fulani wanavyovijua wao) ili wafu hao wapate kuvitumia vifaa hivyo katika maisha yao ya baadaye (waliyoyaelekea baada ya kuachana na maisha ya duniani).Ndio, itikadi hii ni ya ajabu kidogo lazima mtu ushangae lakini kuna nukta ya kuzingatia kuwa watu hao walikiamini Ma'ad au walikiamini kuwa kuna maisha baada ya maisha ya duniani.

"MA'AD KATIKA QUR'AN
"MA'AD -UFUFUO" KAMA ILIVYO-(ULIVYO) KATIKA QUR'AN TUKUFU.
Mwiso wa sehemu ya kwanza. Somo hili litaendelea inshaallah. Usikose sehemu ijayo kuhusiana na ufufuo kama ulivyo katika Qur'an Tukufu ili ujue Qur'an inasemaje kuhusu watu kufufuliwa,je Mwenyeezi Mungu (s.w) aliyemuumba mwanadam kutoka kwenye manii,atashindwa kumfufua na kumrudishia uhai wake baada ya kuwa maiti?ni swali tutakalolijibu katika sehemu ijayo ya bahthi hii ya ufufuo au Ma'ad.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini