Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MUASISI WA USTAARABU

0 Voti 00.0 / 5

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHII

MUASISI WA USTAARABU

MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W), MUASISI WA USTAARABU WA KIISLAMU

Ustaarabu wa Kiislamu umejadiliwa na kuchunguzwa na wanafikra katika pande mbalimbali na vitabu na makala nyingi na za aina mbalimbali zimeandikwa kujadili suala hilo. Hata hivyo suala lililopuuzwa na kufumbiwa macho kwa kiasi kikubwa katika medani hiyo ni nafasi ya kimsingi na isiyo na kifani ya Mtume Muhammad amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake katika kuweka jiwe na msingi na kuasisi ustaarabu huo adhimu.

Mche wa mti huo mkubwa ulipandikizwa kwa mikono mitukufu ya Nabii Muhammad (saw) na misingi yake ikaimarishwa kwa hijra na kuhamia mtukufu huyo katika mji wa Yathrib. Makala hii inachunguza misingi muhimu ya ustaarabu katika mtazamo wa wasomi na nafasi ya Nabii Muhammad (saw) katika kuleta amani na utulivu, mshikamano wa kitaifa, ushirikiano na muawana, maadili bora, subira na ustahamilivu, umoja na mshikamano na hali bora ya wastani ya kimaisha ambavyo vyote ni miongoni mwa sababu za kujitokeza ustaarabu na kustawi kwake.

Dibaji
Ustaarabu wa Kiislamu umechunguzwa na kufanyiwa utafiti na wasomi mbalimbali katika pande mbalimbali. Ustaarabu huo wenyewe umebuni mbinu na utaratibu wa mfumo mkubwa zaidi wa kisayansi na kuitunuku dunia shakhsia kubwa za kielimu katika nyanja mbalimbali za sayansi. Kwa hakika maendeleo na ustawi wa haraka, adhama, ukamilifu na upana wa ustaarabu wa Kiislamu na vilevile kushiriki kwa matabaka mbalimbali ya mataifa na kaumu tofauti katika kujenga na kustawisha ustarabu huo ni miongoni mwa mambo yaliyowastaajabisha wengi. Mambo hayo yamewalazimisha wanafikra wengi hususan wa Kimagharibi kuinua juu mikono pale wanapozungumzia na kuchunguza historia ya ustaarabu wa Kiislamu.

Pamoja na hayo inatupasa kutambua kwamba, kipindi bora na cha dhahabu cha Uislamu katika upande wa ustawi na uhai wa kidini na kiroho na kufikiwa malengo na thamani zake kilikuwa kipindi cha zama za uhai wa Mtume Muhammad (saw) na siku za kuasisiwa dola la Kiislamu mjini Madina. Kipindi hicho kilikuwa zama za kupandikiza mbegu iliyoota na kuwa mti mkubwa na kupata lishe ya kutosha kutoka kwenye ardhi safi na yenye rutuba. Mti wa ustaarabu wa Kiislamu ulizaa matunda yake karne kadhaa baada ya kupandwa kwa mikono mitukufu ya Mtume wa Uislamu na matunda yake yalidhihiri katika nyanja mbalimbali za utamaduni, sanaa, sayansi, teolojia, falsafa, fasihi na kadhalika.

Kuhusiana na ustawi na kukua ustaarabu wa Kiislamu, Dakta Hussain Nasr anaamini kwamba: "Ni katika kipindi cha baada ya kustawi jamii ya Kiislamu na baada ya kuonekana waziwazi athari za wahyi na ufunuo wa Kiislamu ndipo ustaarabu mpya wa Kiislamu ulipopata rangi na sura yake maalumu ya Kiislamu na elimu, fasihi na falsafa ilipofikia kileleni…" (Sayyid Hussein Nasr : Wanafalsafa Watatu wa Kiislamu) Ustaarabu wa Kiislamu ulifikia daraja ya juu ya ukamilifu na ustawi kutokana na wahyi na hatua zilizochukuliwa na Mtume Muhammad (saw) kwa kadiri kwamba msomi wa Kiswisi Adam Metz ameiita karne ya nne Hijria kuwa ilikuwa zama za nuru za ustawi na ustaarabu wa Kiislamu. (Adam Metz: Ustaarabu wa Kiislamu katika Karne ya Tatu Hijria) Bibi Zigrid Honkeh anasema kuwa ustawi wa ustaarabu wa Kiislamu ulizidi ule wa Ugiriki mara dufu. Bibi Honkeh anaamini kwamba Waislamu waliuathiri zaidi ulimwengu wa Magharibi kwa njia ya moja kwa moja na kwa pande kadhaa kuliko Wagiriki. (Zegrid Honkeh: Utamaduni wa Uislamu Barani Ulaya)

Kama tulivyosema, ustaarabu wa Kiislamu umejadiliwa na kuchunguzwa katika pande mbalimbali. Hata hivyo inasikitisha kwamba mijadala mingi kuhusu ustaarabu wa Kiislamu imepuuza nafasi na mchango mkubwa usiokuwa na kifani wa Nabii Muhammad (saw) katika kuweka misingi na kuasisi ustaarabu huo. Katika makala hii tutajaribu kwa muhtasari na kutazama nafasi ya mtukufu huyo katika ustaarabu wa Kiislamu kwa kutilia maanani nguzo na sababu muhimu zinazoathiri katika kustawisha ustaarabu wa mwanadamu.

Maana ya ustaarabu
a- Maana ya Kilugha
Neno "Tamaddun" linalomaanisha ustaarabu katika lugha ya Kiarabu linatokana na neno "madana" linalomaanisha kukaa na kuishi sehemu, kuwa na maadili na tabia za wakazi wa mjini. Neno hilo linashabihiana na lile la "civil" la kilatini linalotokana na "Civilization". (Louis Maaluf: al Munjid) Wagiriki wa kale walitumia neno hilo kuonyesha kuwa mji ni majmui ya taasisi na uhusiano wa kijamii ambao ndio maisha bora zaidi. (Muhammad Ridha Batini: Farhange Muaser) Katika kamusi za lugha ya Kifarsi pia neno "tamaddun" lililotumiwa kwa maana ya ustaarabu linamaanisha kuishi mjini, kuwa na tabia na maaadili ya wakazi wa mjini, kushirikiana watu wa jamii katika masuala ya kijamii, kiuchumi, kidini, kisiasa na kadhalika. Japokuwa katika lugha za Mashariki na zile za kilatini kuishi mijini kumetajwa kuwa ndio kigezo cha ustaarabu, lakini tunapaswa kuelewa kwamba, mara zote ustaarabu haumaanishi kuishi mjini, bali mstaarabu ni mtu aliyeingia katika daraja ya maisha ya mjini. Si hayo tu, bali kwa hakika kuishi mjini ni matokeo na matunda ya ustaarabu na si sababu yake. John Bernard anasema: Mji ni sehemu ya ustaarabu na si kweli kwamba kuishi mijini ndio sababu ya ustaarabu. (Jean Bernard: Elimu ya Historia) Will Durant anaamini kwamba ni ustaarabu pekee ndio uliomfanya mwanadamu afikirie suala la kuanzisha mji.

b- Maana ya Kiistilahi
Kumetolewa maana mbalimbali za kiistilahi za ustaarabu. Kabla ya kuanza kutazama maana hizo tunapaswa kusema kwamba "ustaarabu" ni mafhumi na maana mpya kwa kiasi fulani (Will Durant: Historia ya Ustaarabu) na imekuwa na mabadiliko mengi katika miongo kadhaa ya hivi karibuni. Kwa kutilia maanani ukweli huo, tutachunguza ustaarabu katika mtazamo wa baadhi ya wanafikra wa Kimagharibi na Kiislamu.

Will Durant anaarifisha ustaarabu kwa kusema: Ustaarabu ni mfumo wa kijamii unaopelekea kuharakishwa mafanikio ya kiutamaduni na unaofanya ubunifu kwa shabaha ya kutumia fikra, mila na desturi na sanaa. Ni mfumo wa kisiasa ambao unalindwa na maadili na sheria; na ni mfumo wa kichumi ambao unadumu kwa kuendelezwa uzalishaji. Samuel Huntington anasema: Ustaarabu ni ngazi ya juu kabisa na utamaduni na utambulisho mpana zaidi wa kiutamaduni. (12) Henry Lucas anasema: Ustaarabu ni jambo lililoshikamana barabara linalojumuisha masuala yote ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na hata sanaa na fasihi. (Samwell Huntington: Nadharia ya Mgongano kati ya Tamaduni Mbalimbali)

Ustaarabu katika mtazamo wa Arnold Twinby ni matokeo ya akili na watu wachache wenye uvumbuzi na hodari. (Henry Lucas: Historia ya Ustaarabu) Kwa maana kwamba katika jamii kuna tabaka la watu hodari wenye vipawa vya ubunifu na uvumbuzi na ustaarabu hutokea katika jamii kutokana na mabadiliko na mwelekeo wa jamii hiyo kuelekea kwenye ukamilifu. Wanafikra wa Kiislamu pia wametoa maana zao makhsusi kuhusu ustaarabu. Ibn Khaldun anasema kuwa ustaarabu ni hali ya kijamii ya mwanadamu. (Ibn Khaldoun: Muqaddima)

Kwa mtazamo wa mwanafikra huyo wa Kiislamu, jamii yenye nidhamu makhsusi kutokana na kuanzisha utawala na kuwa na vyeo na taasisi za serikali kwa shabaha ya kulinda nidhamu na kusimamia uendeshaji wa utawala huo na ikatoka katika hali ya maisha ya kibinafsi na kuelekea kwenye maisha ya kimjini, ikatayarisha mazingira ya kuenea maadini mema za sifa aali za kinafsi kama elimu na sanaa, huwa imestaarabika.

Allamah Muhammad Taqi Ja'fari anaarifisha ustaarabu kama ifuatavyo: 'Ustaarabu ni muundo wenye uwiano wa mwanadamu katika maisha yanayokubalika kiakili, wenye uhusiano wa kiadilifu na unaowashirikisha watu na makundi yote ya jamii katika kupeleka mbele malengo ya kimaada na kiroho ya mwanadamu katika nyanja zote chanya. (Allamah Muhammad Taqi Ja'fari: Tafsiri ya Nahjul Balagha) Kutokana na jumla ya yaliyosemwa na wanafikra kuhusu ustaarabu tunaweza kusema kuwa: Ustaarabu ni daraja ya juu ya utamaduni na nidhamu ya kijamii. Ni kutoka katika maisha ya jangwani na kuingia katika njia ya kuasisi asasi imara za kijamii au kwa mujibu wa kauli ya Ibn Khaldun, ni kupata ustawi na maendeleo (Ali Akbar Wilayati: Ustawi wa Ustaarabu wa Uislamu na Iran)

Sababu Zinazochangia katika Kuasisi na Kustawi Ustaarabu
Kuna mambo mengi yanayoathiri na kuchangia katika kuasisi na kustawisha ustaarabu. Kwa mtazamo wa Will Durant, kuna nguzo nne muhimu zinazochangia katika kuanzisha ustaarabu ambazo ni: Kuona mbali na kufanya hadhari katika masuala ya kijamii, kuwa na taasisi ya kisiasa, desturi na kanuni za kimaadili na kufanya bidii katika njia ya kupata maarifa na kueneza sanaa. (Will Durant: Historia ya Ustaarabu) Will Durant anaamini kwamba ustaarabu hudhihiri wakati ghasia na ukosefu wa nishamu unapotoweka, kwani ni wakati wa kuondoka woga na hofu ndipo hisi ya udadisi na haja na kuvumbua na kubuni inapopata fursa na kujitokeza. Wakati huo mwanadamu hujisalimisha kwa hisi inayomuongoza kimaumbile katika njia ya kutafuta elimu na maarifa na kutayarisha zana za kuboresha maisha yake.

Ibn Khaldun anasema kuwa kuna mambo saba yanayochangia katika kuasisi ustaarabu. 1- Serikali na kiongozi. 2- Sheria za kidini au za kimila. 3- Akhlaki na maadili mema. 4- Kazi. 5- Viwanda. 6- Jamii na 7 ni mali. Ibn Khaldun anaona kuwa mambo matatu ya kwanza yaani serikali na uongozi, sheria za kidini na maadili mema, yanaweza kutambuliwa kuwa ndiyo nguzo muhimu zaidi za ustaarabu kuliko manne yanayofuatia. (Izzatullah Radmanesh: Itikadi za Ibn Khaldoun) Kwa kutilia maanani mitazamo na maoni tofauti tunaweza kuashiria mambo kadhaa yafuatilia kama nguzo muhimu zinazochangia katika kuasisi ustaarabu.

Utulivu na Usalama
Mshikamano wa kitaifa anaoashiria Ibn Khaldoun katika kitabu cha Muqaddima, ndio roho ya kila ustaarabu. Suala hilo huwapa watu wa jamii ari na azma, moyo wa ushirikiano na lengo makhsusi. (Will Durant: Historia ya Ustaarabu) Ushirikiano na muawana akhlaki na maadili bora, subira na ustahamilivu mkabala wa fikra tofauti, kwa maana ya kustahamili na kuwaelewa vyema wale unaotofautiana nao na si kupuuza na kutojali, kulinda umoja na mshikamano na kutotengana, dini na kadhalika.

A- Mtume Muhammad (saw) na suala la Usalama na Utulivu
Ustaarabu wa Kiislamu ulianza sambamba na ulinganiaji wa dini hiyo mjini Makka na kukita mizizi baada ya kuasisiwa serikali ya Bwana Mtume mjini Madina. Wakati huo serikali ya Kiislamu ilikwenda sambamba na kuanishwa maisha ya mjini. Katika miaka ambayo Waislamu walikuwa Makka, Makuraishi walifanya kila wawezalo kuwazuia watu kuingia katika dini ya Kiislamu na washirikina wa Makka waliwaudhi na kuwatesa mno Waislamu.

Mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Bani Hashim katika pango la Abu Twalib, vifo vya Bibi Khadija mke wa Mtume (swa) na Abu Twalib ami yake ambao wote wawili walikuwa nguzo imara iliyokuwa ikimhami na kumsaidia Mtume na Waislamu, viliwanyima amani na usalama wafuasi wa dini hiyo. Hii ni katika hali ambayo Mtume Muhammad (saw) alikuwa na haja kubwa ya mahala penye amani na usalama kwa shabaha ya kuweka jiwe la msingi la ustaarabu mkubwa wa Kiislamu. Kwa sababu hiyo, Mtume alielekea Twaif kwa shabaha ya kutayarisha mazingira bora ya yenye utulivu na amani kwa ajili ya Waislamu. Hata hivyo safari hiyo ya Twaif haikuwa na matunda mazuri kwani wakuu wa mji huo hawakukubali wito wa mtukufu huyo, na kinyume chake walichochea makundi ya wahuni, watu waovu na watoto ili wamshambulie Mtume na kumfukuza katika mji huo.

Katika mwaka huo kulipatikana mazingira mazuri ya kukutana Nabii Muhammad (saw) na kundi la watu wa Yathrib. Mtume Muhammad (saw) alikuwa na tabia ya kuyaendea makabila mbalimbali yaliyokwenda kuzuru nyumba ya Mwenyezi Mungu katika msimu wa Hija na kuyalingania dini ya Kiislamu. Alifanikiwa kukutana na watu sita wa kabila la Khazraj na kuwalingania ujumbe wake. Watu hao wa kabila la Khazraj waliitikia wito na ujumbe wa Mtume ambao waliutambua kwamba unatoa bishara ya suluhu, amani na ucha-Mungu. Walimwambia: Tuanaenda kwa watu wa kabila letu na kuwafikishia ujumbe wa dini yako, asaa kwa baraka zako vita na mapigano ya muda mrefu yakamalizika katika mji wetu. Iwapo utafanikiwa kukomesha vita na mapigano na kutuunganisha tena utakuwa mtu azizi na bora zaidi kwetu sisi. (Sayyid Ja'far Shahidi: Historia ya Uislamu) Makabila ya Aus na Khazraj yalikuwa katika vita kwa miaka mingi kabla ya kudhihiri dini ya Kiislamu katika bara Arabu.

Miaka miwili baadaye yaani mwaka wa 13 baada ya kubaathiwa Mtume, wawakilishi wa watu wa Yathrib (Madina) walimpa Mtume Muhammad (saw) mkono wa utiifu katika msimu wa ibada ya Hija na kuahidi kupigana dhidi ya maadui wa Mtume na Waislamu na kuungana na kila atakayeungana na kuwa na urafiki na Waislamu. Waliahidi pia kupigana vita na yeyote atakayewashambulia Waislamu. Ni baada ya baia' na makubaliano hayo ndipo Mtume alipowaruhusu Waislamu kuhamia Yathrib. Kwa utaratibu huo juhudi za bwana Mtume amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake za kutayarisha mazingira ya amani na utulivu kwa ajili ya Waislamu zilizaa matunda. Mazingira hayo ya amani mjini Yathrib (Madina) yalimtayarishia Mtume (saw) hali nzuri zaidi ya kuimarisha misingi na nguzo za utawala wa Kiislamu.

B- Mtume Muhammad (saw) na Mshikamano wa Kitaifa
Hatua iliyofuatia ya Mtume katika kutayarisha uwanja mzuri wa kuasisi ustaarabu wa Kiislamu ilikuwa kujenga umoja na mshikamano. Tangu alipoingia Yathrib, Mtume Mtukufu alitayarisha mazingira ya kujenga umoja na mshikamano katika jamii mpya ya Kiislamu. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na mtukufu huyo ni:
Kutayarisha mkataba wa kwanza kabisa katika Uislamu Katika miezi ya mwanzoni mwa kuwepo kwake Yathrib (Madina) Mtume wa Mwenyezi Mungu aliandika mkataba kati ya Muhajirina na Ansar kwa upande mmoja na Mayahudi wa Madina kwa upande mwingine. Katika mkataba huo Mtume aliahidi kwamba dini na mali za Mayahudi zitaheshima kwa masharti maalumu. Mkataba huo ulionyesha jinsi Mtume Muhammad (saw) alivyoheshimu misingi ya uhuru, nidhamu na uadilifu katika maisha ya kijamii. Vilevile mkataba huo uliunda kambi moja ya watu wa Madina dhidi ya uvamizi na mshambulizi yoyote kutoka nje. (Ja'far Subhani: Sayyidul Mursalin) Vipengee muhimu vya mkataba huo ambao umenukuliwa na Ibn Is'haq ni hivi vifuatavyo:
a- Waislamu na Wayahudi wataishi mjini Madina kama taifa moja.
b- Waislamu naWayahudi watakuwa huru katika kutekeleza ibada zao za kidini.
c- Iwapo vitatokea vita, kila moja kati ya makundi hayo mawili limtamsaidia mwenzake dhidi ya adui iwapo halitakuwa mchokozi.
d- Pande zote mbili zitashirikiana kuulinda mji wa Madina iwapo utashambuliwa na adui.
e- Mkataba wowote ule wa suluhu na adui utatiwa saini baada ya mashauriano ya pande mbili.
f- Kwa kuwa Madina ni mji mtakatifu, unapaswa kuheshimiwa na pande zote mbili na ni haramu kufanya umwagaji damu wa aina yoyote katika mji huo.
g- Iwapo kutatokea hitilafu na ugomvi, basi mwamuzi wa mwisho wa hitilafu hizo atakuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).> (Muhammad Ibrahim Ayini: Historia ya Mtume wa Uislamu)

Mkataba wa udugu kati ya Muhajirina na Ansar
Miezi nane baada ya hijra na kuhamia Madina, Mtume Muhammad (saw) alifunga mkataba wa udugu baina ya Muhajirina (Waislamu waliohama kutoka Makka) na Ansar (wenyeji wa Madina) wa kusaidiana katika njia ya haki na kurithiana baada ya mmoja wa Waislamu waliofunga mkataba wa udugu kufariki dunia. Kwa hatua hiyo Mtume (saw) alijenga umoja na mshikamano wa pande zote kati ya Muhajirina na Ansar. Kazi ya kuweka usawa na udugu kati ya Waislamu ilifikia kiwango cha juu kiasi kwamba kila Muislamu alikuwa akimtanguliza na kumpa kipaumbele Muislamu mwenzake. Imepokelewa kwamba siku ya kugawa ngawira za vita vya Bani Nadhir Mtume aliwaambia Ansar kwamba: Iwapo mnataka tutawashirikisha Muhajirina katika kugawa ngawira hizi, la sivyo zichukueni zote. Ansar walijibu kwa kusema: Tunatoa ngawira zote hizi kwa ndugu zetu Muhajirina na tutawashirikisha pia katika mali na nyumba zetu. (Sayyid Ja'far Shahidi: Historia ya Uislamu)

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa hukumu ya kurithiana kwa kutumia mkataba huo wa udugu ilifutwa baada ya vita vya Badr baada ya kuteremshwa aya ya 75 ya suratul Anfal inayosema:

وَأُوْلُواْ الأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَى بِبَعْض فِي كِتَابِ اللّهِ

Na jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Kwa vyovyote vile, juhudi kubwa za mtukufu Mtume za kujenga mshikamano na udugu katika jamii ya Kiislamu zilikuwa na taathira kubwa kiasi kwamba katika miaka ya awali ya kuasisiwa serikali ya Kiislamu, wazee na watu wazima walikuwa wakipaka hina ndeve zao na kuenda kwenye medani za vita vya jihadi wakionekana kama vijana.

C- Mtume Mtukufu na Juhudi za Kuleta Moyo wa Muawana na Ushirikiano
Katika hatua zilizofuatia baadaye, Mtume (saw) alihuisha moyo wa muawana na ushirikiano katika jamii changa ya Kiislamu. Suala hilo la kusaidiana na kushirikiana ni miongoni mwa mambo yaliyotiliwa mkazo mno katika aya za Qur'ani Tukufu. Aya ya suratul Maida inasema: Na saidianeni katika mambo ya kheri na takwa na msisaidiane katika kutenda dhambi na uadui. Al Maida …. Ushirikiano uliotajwa katika aya hiyo kuhusu ni kanuni kuu inayotawala masuala yote ya kijamii, kisheria, kimaadili na kisiasa. Kwa mujibu wa kanuni hiyo, Waislamu wote wanawajibika kushirikiana katika kazi nzuri na kujiepusha kabisa kushiriki katika kazi zenye malengo batili na maovu, dhulma na uonevu, japokuwa mtendaji kazi hizo atakuwa ndugu, rafiki na jamaa wa karibu.

(Ayatullah Makarim Shirazi: Tafsirul Amthal) Moja ya hatua za awali kabisa za Mtume Muhammad (saw) baada ya kuhamia Madina ilikuwa ni kujenga msikiti. Mapokezi makubwa ya watu wa Madina kwa mtukufu huyo yalimfanya achukue hatua ya kujenga kituo cha Waislamu kabla ya jambo lolote lile kilichopewa jina la msikiti. Msikiti huo ulitumiwa kwa ajili ya masuala ya elimu na malezi, siasa, kukata kesi na masuala mengine ya kijamii ya Waislamu. Kituo hicho yaani msikiti wa kwanza kujengwa Madina, kilijengwa katika ardhi ambako ngamia wa Mtume alipiga magoti baada ya kununuliwa kwa dinari kumi. Waislamu wote walishiriki katika ujenzi wa msikiti huo. Hata mtukufu Mtume (saw) alishiriki katika ujenzi huo akibeba mawe na vifaa vya ujenzi sawa na Waislamu wengine. Imenukuliwa kwamba Usaid bin Hudhair alimwendea mtukufu huyo aliyekuwa akibeba mawe na vifaa vya ujenzi na kumwambia: Ya Rasullah! Niruhusu mimi nibebe jiwe hilo. Mtume alimwambia: Nenda ubebe jiwe jingine. (34)

Kushauriana katika masuala mbalimbali ni moja ya sababu za kuimarisha moyo wa muawana na ushirikiano. Qur'ani Tukufu imezungumzia suala la kushauriana katika aya zake kadhaa. Zaidi ya yote ni kuwa, kitabu hicho kitakatifu kina sura iliyopewa jina la Shura kwa maana ya mashauriano, ambayo inasisitiza na kutilia mkazo suala la kushauriana. Sura hiyo pia imelitaja suala la mashauriano sambamba na masuala mengine muhimu kama Sala na kutoa mali katika njia ya Mwenyezi Mungu. Aya za 37 na 38 za suratu Shura zinasema:

وَالَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ وَإِذَا مَا غَضِبُوا هُمْ يَغْفِرُون َ* وَالَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَمْرُهُمْ شُورَى بَيْنَهُمْ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ*

Na wanaoepuka madhambi makubwa na mambo machafu, na wanapokasirika wao husamehe * Na wanaomwitikia Mola wao Mlezi, na wakashika Sala, na mambo yao yakawa ni kwa kushauriana baina yao, na kutokana na tulichowaruzuku wakawa wanatoa. Vilevile aya ya 159 ya suratu Aal Imran baada ya kutangaza msamaha kwa wote, inamuamuru Mtume (saw) kushauriana na Waislamu na kusikiliza maoni yao kwa ajili ya kuhuisha shakhsia na maisha yao ya kifikra na kiroho.

Mbali na wahyi na ufunuo, Mtume Muhammad (saw) mwenyewe alikuwa na upeo mkubwa wa kifikra kiasi kwamba hakuhitajia kufanya mashauriano na watu wengine. Hata hivyo alikuwa akiitisha vikao vya mashauriano kuhusu masuala yanayohusiana na utekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu na si utungaji wa sheria, hususan kati ya watu wenye uwezo mkubwa wa kutafakari kwa ajili ya kuwaelimisha Waislamu umuhimu wa kufanya mashauriano katika masuala ya kisiasa na kimaisha kwa upande mmoja, na kukuza vipawa vya kifikra kati ya watu kwa upande wa pili. Mtume alihimiza mno juu ya umuhimu wa kufanya mashauriano kwa kadiri kwamba mara nyingine alikuwa akiweka kando rai na mtazamo wake kwa ajili ya kuonesha heshima kwa mitazamo ya watu wengine. (Ayatullah Makarim Shirazi: Tafsirul Amthal)

Imam Ali bin Mussa Ridhaa ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume (saw) anasema kuhusiana na jinsi mtukufu huyo alivyokuwa akichukua maamuzi kwamba: Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akishauriana na masahaba zake na kisha anachukua maamuzi kuhusu jambo analotaka. (Mustafa Delshad: Sira ya Mtume) Tunajifunza kutokana na hadithi hii kwamba kufanya mashauriano ilikuwa ni sehemu ya sira na mwenendo wa Mtume Muhammad (saw) na kwamba mtukufu huyo alikuwa akihimiza na kushikamana vilivyo na sera hiyo. Historia imenukuu kesi nyingi za kipindi cha maisha ya Mtume au wakati wa utawla wake ambako alikuwa akiitisha vikao vya mashauriano na masahaba zake kwa ajili ya kuchukua maamuzi kuhusu masuala mbalimbali. Hapa tunaashiria baadhi ya kesi hizo: - Katika vita vya Badr, Mtume Muhammad (saw) alishauriana na masahaba zake kuhusu suala la vita vyenyewe, kuainisha eneo la vita na kuhusu mateka wa vita hivyo.

- Katika vita vya Uhud Mtume wa Mwenyezi Mungu aliitisha kikao cha mashauriano na kushauriana na masahaba zake kuhusu utaratibu wa kukabiliana na jeshi la Makuraish na kisha akachukua uamuzi. - Mtume Mtukufu (saw) aliliweka suala la vita vya Ahzab (Khandaq) katika kikao cha mashauriano na kujadiliana na masahaba zake kuhusu njia za kukabiliana na jeshi kubwa la washirikiana kisha akachukua uamuzi kwa mujibu wa mashauriano hayo. - Vilevile alishauriana na masahaba kuhusu jinsi ya kukabiliana na Mayahudi wa Madina katika vita vya Bani Nadhir na Bani Quraidha.

- Baada ya washirikina wa Makka kuzuia msafara wa Waislamu kuelekea Makka kwa ajili ya kuzuru nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mtume Muhammad (saw) aliitisha kikao cha kushauriana na masahaba zake kuhusu suala hilo. - Mtume Muhammad (saw) pia alishauriana na masahaba zake kuhusu kadhia ya kuendeleza mzingiro dhidi ya washirikina katika vita vya Twaif, wakati wa vita vya Tabuk na wakati wa kukombolewa Makka. (Mustafa Delshad: Sira ya Mtume) Katika mashauriano hayo yote mtukufu Mtume alilenga kuimarisha moyo wa mshikamano, muawana na ushirikiano katika jamii ya Kiislamu. Aliona kuwa jamii ya kibinadamu na jumuiya isiyokuwa na mashauriano ndani yake ni majmui maiti na isiyokuwa na uhai na haistahili kuendelea kuwapo. (Murtadhaa Farid: Mwongozo wa Mwanadamu)

D- Mtume Mtukufu na Maadili
Moja ya sifa za ustaarabu wa Kiislamu ni kueneza maadili mema ambayo Mtume anasema: Nimetumwa kuja kukamilisha maadili mema. (Mulla Mahdi Naraqi: Jamiul Sa'adati) Utafiti katika maneno ya Mwenyezi Mungu unaonesha wazi umuhimu mkubwa wa sifa hiyo katika jamii ya Kiislamu. Tunapotazama mfumo wa kimaadili wa Uislamu na Mtume mwenyewe ambaye ndiye kigezo na kielelezo halisi cha mfumo huo kwa mujibu wa aya ya 21 ya suratul Ahzab inayosema: (Bila shaka mnacho kigezo kizuri (ruwaza njema) kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu..), tunapata masuala mawili muhimu:
1- Mfumo wa elimu ya malezi na maadili wa Kiislamu ni mpana mno kwa kadiri kwamba ni vigumu sana kutoa faharasa yake kamili. Ukweli huo unadhihiri wazi zaidi kwa kutupia jicho hadithi nyingi za mtukufu Mtume na mafundisho yake ya kimaadili. Katika uwanja huu pia tunaweza kusema kuwa Mtume Muhammad (saw) hakuacha kuzungumzia chochote kile hata suala dogo mno linalohusiana na mwenendo na maadili ya Kiislamu. Mtukufu huyo alibainisha nukta zote kubwa na ndogo za malezi ya kiroho na kimaadili kupitia sentensi fupi, nyepesi kufahamika na zinazotoa mwongozi wa kimatendo.

2- Mafunzo ya kimaadili ya Mtume (saw) ambayo yametolewa kwenye Qur'ani Tukufu yamepangika katika utaratibu ambao watu wa tabaka na daraja mbalimbali za kifikra, kiroho na kimaanawi wanaweza kufaidika na mafundisho hayo kulingana na uwezo wao wa kufahamu na kuelewa mambo. Kwa maana nyingine ni kuwa, kila mtu anaweza kuchota katika mto huo wenye maji safi kulingana ukubwa au udogo wa chombo na gudulia lake mwenyewe.

Kimsingi tunapaswa kuashiria hapa kuwa mafunzo ya kimalezi na kimaadili katika kila jamii hayapaswi kuhusu tabaka moja makhsusi na kuzuiwa kwa matabaka mengine. Mfumo bora wa maadili na malezi unapaswa kuwa na sifa inayowawezesha watu wa matabaka yote kufaidika nao kulingana na uwezo wa kila mtu. (Muhammad Ali Sadat: Maadili ya Kiislamu) Mafundisho ya kimalezi na kimaadili ya Mtume yaligusa nyanja mbalimbali za maisha kama madili ya siasa, maisha, jinsi ya kuamiliana na watu, maadili ya maingiliano ya ndani ya ndoa, maadili ya utawala, maadili ya mijadala na mazungumzo na kadhalika.
E- Mtume Mtukufu na Kuimarisha Moyo wa Subira na Uvumilivu
Moja ya sifa makhsusi zilizotajwa kwa ajili ya kustawi na kunawiri ustaarabu ni moyo wa subira na uvumilivu. Subira ni miongoni mwa mambo yaliyosisitizwa mno ndani ya Qur'ani Tukufu. Neno hilo na minyambuliko yake limetajwa zaidi ya mara mia moja katika aya mbalimbali za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Katika aya mbalimbali za kitabu hicho Mtume Muhammad (saw) anaamrishwa kuwa na subira na uvumilivu katika masuala mbalimbali. Miongoni mwa aya hizo ni ile ya 35 ya suratul Ahqaf inayosema:

فَاصْبِرْ كَمَا صَبَرَ أُوْلُوا الْعَزْمِ مِنَ الرُّسُلِ وَلا تَسْتَعْجِل لَّهُمْ

"Basi subiri, kama walivyosubiri Mitume wenye stahamala kubwa, wala usiwafanyie haraka.." Vilevile aya ya saba ya suratul Muddathir inasema:

وَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ

"Na kwa ajili ya Mola wako Mlezi, subiri." Aya ya 17 ya suratu Swad pia inasema:
اصْبِرْ عَلَى مَا يَقُولُون

"Subiri kwa hayo wayasemayo.." Aya ya 48 ya Suratul Qalam inamwambia Mtume mtukufu kwamba :

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلا تَكُن كَصَاحِبِ الْحُوت

"Basi ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi, wala usiwe kama mmezwa na samaki.." , na aya ya 77 ya suratu Ghafir inasema:

فَاصْبِرْ إِنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَق

"Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli". Mtume Muhammad (saw) alikuwa mvumilivu na mwenye subira kubwa mno katika kuendesha masuala ya nchi na kuongoza watu. Mwanahistoria Ibn Shahrashub ameandika kuwa Mtume Muhammad (saw) alikuwa na subira na uvumilivu kuliko mwanadamu yeyote yule. (Mustafa Delshad: Sira ya Mtume) Mtume mwenyewe anasema: Nimetumwa kuwa kituo kikuu cha subira na uvumilivu na mgodi wa elimu na maarifa.." (Mustafa Delshad: Sira ya Mtume) .

Mifano ya Subira na Uvumilivu wa Mtume Muhammad (saw)
Mwanzoni mwa utawala wa serikali yake mjini Madina, Mtume (saw) aliwaheshimu na kuwaenzi wasiokuwa Waislamu waliokuwa wakiishi katika mji huo kama Mayahudi. Si hayo tu, bali alifunga nao mikataba mbalimbali na kuamiliana nao kwa wema maadamu wanaheshimu mikataba na makubaliano hayo. Baada ya vita vya Uhud, baadhi ya masahaba walimtaka Mtume wa rehma na amani awalaani Makuraish na washirikina. Mtume aliwajibu kwa kusema: "Sikutumwa kuja kulaani na kuapiza watu, bali nimetumwa kwa ajili ya kuwalingania haki na rehema. Ewe Mola Mlezi! Waongoze watu wa kaumu yangu, hakika wao hawaelewi". (Mustafa Delshad: Sira ya Mtume) Subira na Uvumilivu wa Mtume Mbele ya Maudhi ya Mayahudi Dakta Twaha Hussein anasema: Baada ya kuhamia Madina na kuanza kuishi na masahaba zake wa Ansar na Muhajirina, Mtume hakuwafanyia uadui wa aina yoyote Mayahudi wala kuwaonyesha kinyongo na roho mbaya. Aliamiliana nao kwa subira na ustahamilivu na alitaka kujenga uhusiano wa ujirani mwema nao na kusaidiana katika hali zote za shida na raha. (Twaha Hussein: Dini ya Kiislamu)

Uvumilivu wa Mtume Mbele ya Maudhi ya Wanafiki
Licha ya kwamba wanafiki waliendeleza maudhi na kukwamisha harakati za Uislamu hususan kiongozi wao Abdullah bin Ubay bin Salul ambaye aliendeleza mwenendo huo hadi alipofariki dunia mwaka wa tisa Hijria, lakini Mtume alionyesha uvumilivu mkubwa na kuamiliana nao kwa subira na ustahamilivu kiasi kwamba imenukuliwa kuwa alisalia hata maiti ya kiongozi wa kundi hilo la wanafiki. (Twaha Hussein: Dini ya Kiislamu)
F- Mtume Muhammad (saw) na Juhudi za Kujenga Umoja na Mshikamano
Sifa nyingine ambayo inaweza kuwa na taathira kubwa katika ustawi wa ustaarabu ni umoja na mshikamano ambao ulipewa umuhimu mkubwa tangu mwanzoni mwa harakati za Mtume Mtukufu. Qur'ani inawahimiza mno Waislamu kuwa na umoja na mashikamano katika aya zake nyingi kupitia imani ya tauhidi na Mungu Mmoja. Historia pia imethibitisha kwamba mtukufu huyo alifanikiwa kujenga umoja na mshikamano kati ya Waislamu na kuimarisha udugu na upendo baina ya wafuasi wa dini hiyo katika kipindi kifupi. Mtume aliunganisha pamoja makabila yaliyokuwa katika vita na mapigano kwa zaidi ya miaka mia moja na kuanzisha udugu na upendo baina yao.

Mwandishi mashuhuri wa Kiingereza John Davin Port ameandika kuwa: Muhammad, Mwaraabu wa kawaida aliweza kubadili makabila yaliyokuwa yametengana na madogo madogo, yasiyokuwa na mavazi wala chakula wa nchi yake na kutengeneza jamii yenye umoja na nidhamu. Aliyaarifisha makabila hayo katika mataifa mengine na kuyadhihiridha kama jamii yenye sifa njema za kimaadili na kuyawezesha kuyashinda madola makubwa ya Kirumi na Kifarsi katika kipindi cha chini ya miaka 30. Makabila hayo yaliweza kudhibiti maeneo ya Misopatimia na Misri na kueneza mamlaka yao katika ardhi iliyoanzia pwani mwa Antlantiki hadi Asia ya mbali.

G- Mtume Muhammad na Dini Yenye Kujenga Ustaarabu
Dini imeweza kupata nafasi yake makhsusi na ya juu kabisa katika jamii mbalimbali. Hii leo imethibitika kuwa hakuna utamaduni au ustaarabu unaouweza kupatikana bila ya dini kuwa na mchango mkubwa katika kuunda na kuasisi utamaduni na ustaarabu huo. Baadhi ya wataalamu wanasema kuwa dini ndio batini ya ustaarabu na kwamba dini ni mithili ya roho katika kiwiliwili cha jamii. Nafasi na mchango wa dini katika ustaarabu inaweza kuchunguzwa katika pande mbili. Kwanza ni kuwa uongofu unaotoka kwa Mwenyezi Mungu unastawi na kuchanua zaidi kupitia vipawa vya kimaumbile vya wanadamu na kuondoa ada na desturi zilizopitwa na wakati na zinazomtia minyororo mwanadamu kwa kufanya mabadiliko makubwa ndani ya fikra na roho za watu. Ni katika kivuli cha mabadiliko hayo ndipo maisha ya kiuchumi ya mwanadamu yanapostawi na vipawa vya elimu, sanaa, fasihi na kadhalika vinapopata kuchanua.

Katika upande mwingine dini inatayarisha mazingira mazuri ya umoja na mashikamano bali baadhi ya wataalamu wa mauala ya jamii kama Ibn Khaldun wanasema kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya dini na mshikamano wa jamii.

Natija
Tunaweza kusema hapa kuwa jamii iliyoundwa na Mtume Muhammad mjini Madina ilikuwa na sifa zote zinazohitajika kwa ajili ya kuanza harakati mpya ya ustaarabu. Kwa msingi huo kuhamia Madina kwa Mtume Muhammad (saw) na kuunda serikali kunapaswa kutambuliwa kuwa ilikuwa ni hatua nyingine muhimu ya mtukufu huyo baada ya kupewa utume na kutangaza ujumbe wake kwa ajili ya kuaisisi ustaarabu mpya wa Kiislamu. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ambaye alipokelewa vyema na watu wa Yathrib (baadaye Madina) aliweka jiwe la kwanza la msingi wa ustaarabu wa jamii yake juu ya masuala kadhaa kama uvumilivu na subira, maelewano, kupinga na kupambana na udikteta na siasa za kiimla, upole na upendo, ujirani mwema na kadhalika. Nafasi isiyokuwa na kifani ya Mtukufu huyo katika kuaasisi na kustawisha ustaarabu wa Kiislamu inapaswa kuchunguzwa na kufanyiwa utafiti wa kina zaidi.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini