Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

VIPENGELE VYA MIUJIZA YA QUR_ANI

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI 

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

VIPENGELE VYA MIUJIZA YA QUR-ANI (1) A.

Wanaelimu wamejadiliana maudhui mbali mbali yanayohusiana na miujiza ya Qur-ani, lakini vile vile wamehitilafiana nadhari kuhusiana na maudhui hayo, maulamaa wa zama zilizopita wametowa nadharia nyengine, na maulamaa wa zama hizi wametoa nadhari nyengine, ijapokuwa katika kauli zao wameongezea na zile nadharia za watu wa zama zilizopita.[1]

Wanaelimu wa zama hizi tulizonazo wameigawa miujiza ya Qur-ani katika nyanja tatu zifuatazo:-

Miujiza ya mabainisho, miujiza ya kielimu, na miujiza ya kisheria.

Katika somo hili tutakizungumzia nyanja hiyo ya mwanzo, yaani miujiza ya mabainisho, na katika somo linalofuata tutaelezea nyanja mbili zilizobakia.

 1- MIUJIZA YA MABAINISHO

Katika miujiza ya mabainisho, matamshi (lafdhi na nukta). yaliyotumika katika ibara yana balagha ndani yake, ijapokuwa matamshi hayo yanaleta maana asili kwa kuzingatia na yale yaliyomo.

Miujiza ya mabainisho katika Qur-ani imegawika katika sehemu tano zifuatazo:-

A. KUCHAGULIWA MANENO

Mjengeko wa maneno yaliyochaguliwa katika ibara za Qur-ani, ni mjengeko uliopangwa kwa nidhamu na utaratibu maalumu, hivyo kama kutaondolewa maneno katika ibara hizo na kuweka maneno mengine, zile sifa zote asili za maneno yaliyomo ndani ya ibara hiyo hazitawiana, na maana ya ibara hiyo pia itabadilika, kwa hiyo maneno yaliyotumika katika ibara za Qur-ani, ni maneno ambayo tayari yako katika mfumo na nidhamu maalumu iliyopangwa na Allah (s.w). Uchaguliwaji huo wa maneno ni kutokana na vipengele hivi vifuatavyo:-

 1. Mtiririko na mnasaba wa sauti, na mjengeko uliopo katika herufi na maneno yaliyomo ndani ya ibara za Qur-ani, katika hali ambayo herufi ya mwisho ya kila neno, na herufi ya mwanzo ya neno linalofuata linafanana na lenye uhusiano maalumu.

2. Mnasaba wa maneno yaliyomo ndani ya Qur-ani, kiasi ya kwamba ukizingatia maneno yaliyomo katika ibara hizo yanaleta ufahamu maalumu na yenye mfungamano wa kipekee.

3. Ibara zilizochaguliwa katika kuyapanga maneno hayo ya Qur-ani, zimezingatiwa ufasihi wake kwa kupitia sheria za kielimu, (elimu bayani).

Vipengele hivyo vitatu vimezingatiwa katika kila sifa ya neno, kwa ujumla mjengeko wa kila neno uko katika sehemu yake maalumu, na kila neno limewekwa kwa mjengeko ulio bora kabisa. Ili kuthibitisha hayo natushuhudie ushahidi maarufu katika Suratul-Qasas Aya ya 179, inayojulikana kwa jina la Aya kisasi. Allah (s.w) anasema:-

وَلَكُمْ فِى الْقِصَاصِ حَيَاةٌ يَاْ اُولِيْ الاَلْبَابِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ[2]

Maana ya Aya hiyo ni kama ifuatavyo:-

 Mtakuwa nao uhai (mzuri) katika kulipiza kisasi enyi wenye akili, ili msalimike.

Maelezo kuhusiana na Aya ya 179 ya suratul baqarah.

Watu watakuwa na uhai mzuri kwa sababu kila mtu atakaa kwa adabu yake kwani anajua kuwa akiuwa atauawa, na akidhuru na yeye atafikishiwa madhara. Katika kujikimbizia madhara nafsi yake yanakimbizika hayo madhara kwa watu wengine.

Hayo yalikuwa ni maelezo kuhusiana na Aya hiyo ya 179.

Watu wa jamii ya kiarabu katika kutafuta njia rahisi ya kuhifadhi kanuni zao za nchi, za kijamii na sheria za kimahakama za zama zile walikuwa wakitumia sentensi fupi ambazo zilikuwa na (garamer).

Na kwa sababu hiyo basi kwa ajili ya kutaka kuweka nidhamu katika sheria na kanuni zao za kisasi, walijisaidia kwa kutafuta wanafasihi mahiri wa lugha, na baada majadiliano mengi waliyokuwa nayo baina yao, waliwafikiana nadhari kuhusiana na ibara, au sentensi hii waliyoitunga isemayo (القتل انفی للقتل), yaani uuwaji ni njia moja ya kuzuia mauwaji, ama kama tutailinganisha ibara hiyo na Aya ya kisasi, itaeleweka kuwa watu hao wameghafilika kiasi fulani katika nadharia yao hiyo waliyowafikiana, kwa sababu:-

1. Katika lugha uuwaji bila ya kuwa na vigezo maalumu haiwezi kuwa ni njia ya kuzuia mauwaji.

2. Katika ibara hiyo kumetumika neno huru lisilo na sifa maalumu, yaani haikuelezewa ni uuwaji wa aina gani ilikuwa ni lazima waelezee sifa za uwaji wenyewe.

3. Aya ya Qur-ani imekuja kuthibitisha kitu, ama  ibara hiyo waliyotumia wao  imekuja katika mtindo wa kuzuia kitu – yaani aya ya Qur-ani inathibitisha kuwa mauwaji ya kisasi hupelekea maisha, yaani watu huishi katika salama, tofauti na mauwaji waliyofafanuwa wao yaani mauwaji yanazuia uuwaji, kwani mauwaji hupelekea kukithiri kwa mauwaji, na katika uzungumzaji wa maneno ibara inayothibitisha ni bora kuliko ibara nayokanusha.

4. Neno kisasi lililotumika katika Qur-ani linaleta maana ya uadilifu, katika hali ambayo neno katli amablo lina maana ya mauwaji walilotumia wao linaleta hofu katika nyoyo za wanaadamu.

5. Katika Aya ya Qur-ani kumetumika fani katika uchaguwaji wa maneno, kwani tukizingatia neno kisasi ambalo limefafanuliwa kwa maana ya mauwaji, vile vile limefafanuliwa kuwa linawaletea watu maisha ya salama, kwa hiyo Qur-ani imezingatia uchaguwaji wa maneno katika sharti mbili zilizo asili, nazo ni:-

1. Mtu awe ameimiliki lugha kwa ukamilifu, na awe anajuwa vyanzo vya maneno wapi hutumika neno kama hilo.

2. Akili yake daima iwe tayari kutumia maneno ambayo yanahitajika kutumika, asiwe ana yumba yumba kutafuta neno lenye kunasibiana, bali maneno yote ni lazima yaweko hadhiri akilini mwake na ajuwe vipi kuyatumia.

[1] (rejea Kitabu cha Elimu ya Qur-ani, ukurasa wa 356-367)

[2] Suratul-Baqara Aya ya 179,

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini