Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

DALILI ZINAZOTHIBITISHA KWAMBA MOLA NI MMOJA

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

DALILI ZINAZOTHIBITISHA YA KWAMBA MOLA NI MMOJA NA WALA HANA MSHIRIKA.

Hapana shaka hakuna dalili yoyote inayothibitisha au kukubalika kuwepo kwa waungu zaidi ya mmoja, na kwa wale wenye itikadi hiyo hawana dalili yoyote ya kuthibitisha madai yao.

Miongoni mwa watu ambao wana itikadi hiyo ni “firauna” pale alipompa dasturi waziri wake na kumwambia:-

   وَقَالَ فِرْعَوْنُ يَا اَيُّهَا الْمَلاَ مَا عَلِمْتُ لَكُم مِّنْ إِلَهٍ غَيْرِى فَاَوْقِدْ لِى يَا هَامَانُ عَلـٰي الطِّينِ فَاجْعَل لِّى صَرْحاً لَّعَلِّى اَطَّلِعُ إِلَي إِلَهِ مُوسَي وَإِنِّى لاَظُنُّهُ مِنَ الْكَاذِبِينَ[1]

Na Firauni akasema: Enyi waheshimiwa! Sijui kama mnaye mungu asiye kuwa mimi. Ewe Haman! Niwashie moto unichomee udongo, unijengee mnara nipate kumchungulia mungu wa Musa. Na hakika mimi namwona yeye ni katika waongo.

Mwanaadamu yeyote mwenye akili na aliye huru katika kufikiri na kuzingatia anafahamu ya kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kuumba vitu vilivyomo ulimwenguni, kwa sababu hakuna mtu yoyote mwenye elimu kamili ya vitu hivyo, basi vipi inawezekana kutokea mtu ambaye hana elimu ya vitu hivyo lakini akaweza kuviumba? . Na ni kwa sababu hiyo basi Mitume (a.s) yote ya Mwenyeenzi Mungu imethibitisha na kusema kuwa kuwepo kwa Mwenyeenzi Mungu mmoja ni jambo lililowazi kabisa na lisilo na shaka yoyote.

Qur-ani tukufu inasema:-

قَالَتْ رُسُلُهُمْ اَفِى اللهِ شَكٌّ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالاَرْضِ يَدْعُوكُمْ لِيَغْفِرَ لَكُم مِّن ذُنُوبِكُمْ وَيُؤَخِّرَكُمْ إِلَي اَجَلٍ مُّسَـمًّى قَالُواْ إِنْ اَنتُمْ إِلاَّ بَشَرٌ مِّثْلُنَا تُرِيدُونَ اَن تَصُدُّونَا عَمَّا كَانَ يَعْبُدُ آبَآؤُنَا فَاْتُونَا بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ[2]

Mitume wao wakasema: Ati pana shaka na Mwenyezi Mungu, Muumba mbingu na ardhi? Yeye anakuiteni apate kukufutieni madhambi yenu, na akupeni muhula mpaka muda ulio wekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni wanaadamu kama sisi. Mnataka kutuzuilia na waliyo kuwa wakiabudu baba zetu. Basi tuleteeni hoja ilio wazi.

Wataalamu wenye akili na kutafakari wamethibitisha kuwa kila kitu duniani kina dalili zake, na kwa sababu watu hao ni wenye kutafakari basi huthibitisha kitu kwa kutumia dalili, watu hao huongokewa na kuwa pamoja na Mwenyeenzi Mungu, ama kwa wale ambao hawatafakari na kutafuta dalili ya kitu hupotokewa na kuwa mbali na Mwenyeenzi Mungu. Qur-ani inayathibitisha hayo kwa kusema:-

اَلا إِنَّ لِلّهِ مَن فِى السَّمَاوَات وَمَن فِى الاَرْضِ وَمَا يَتَّبِعُ الَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِ اللهِ شُرَكَاء إِن يَتَّبِعُونَ إِلاَّ الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلاَّ يَخْرُصُونَ[3]

Jueni kuwa ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na ardhini. Na wala hawawafuati hao wanao waomba badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ni washirika wake. Wao hawafuati ila dhana tu, na hawasemi ila uwongo.

Kutokana na kwamba kuwepo kwa Mwenyeenzi Mungu ni jambo la kweli na la haki, na akili yoyote ya mwanaadamu inakubali haki, basi pindi mwanaadamu atakapofikiri na kutafakari atakuwa na akida (itikadi) ya kuwepo Mwenyeenzi Mungu na wala hatokubali kumkufuru Mwenyeenzi Mungu, mwanaadamu huyo atamuamini na kumuabudu Mola wake kitabia na kimatendo. Mwenyeenzi Mungu anauelezea uhakika huo kutokana na

yale waliyosema watu wa motoni kwa kusema:-

وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ اَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِى اَصْحَابِ السَّعِيرِ[4]

Na watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na akili, tusingeli kuwa katika watu wa Motoni!

[1] Suratul-qasas aya ya 38

[2] Surat Ibrahiym aya ya 10

[3] Surat Yunus aya ya 66

[4] Suratul-Mulk aya ya 10

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini