Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

ELIMU YA ALLAH HAINA MWANZO WALA MWISHO

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
IMEANDIKWA NA NDUGU ZETU WA KIISLAMU

UFAFANUZI WA NENO ELIMU
ELIMU YA ALLAH HAINA MWANZO WALA MWISHO
Katika makala iliyopita ambayo inahusiana na elimu ya Mwenyeezi Mungu, tulielezea kuwa kuna njia mbili katika kufafanua elimu ya Mwenyeezi Mungu, makala hiyo ya mwanzo tulielezea njia moja, na katika makala hii no 2 tutaelezea njia nyengine, nayo ni hii ifuatayo:-
2- Elimu isiyo ya moja kwa moja, (Yaani kwa kupitia Mitume ya Mwenyeenzi Mungu wanaadamu hutunukiwa elimu hiyo).
Kama vile tunavyosoma ndani ya Qur-ani.

وَاللّهُ اَخْرَجَكُم مِّن بُطُونِ اُمَّهَاتِكُمْ لاَ تَعْلَمُونَ شَيْئاً وَجَعَلَ لَكُمُ الْسَّمْعَ وَالاَبْصَارَ وَالاَفْئِدَةَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ[1]
Na Mwenyezi Mungu amekutoeni matumboni mwa mama zenu, hali ya kuwa hamjui kitu, na amekujaalieni masikio na macho na nyoyo ili mpate kushukuru.
Maelezo kuhusiana na aya

Inatajwa Qudra ya Mwenyeenzi Mungu na uweza wake na neema zake, basi na zizingatiwe na zishukuriwe.
-Tofauti ya pili kuhusiana na upeo wa elimu ya Mwenyeenzi Mungu, ina maana ya kuwa elimu ya Mwenyeenzi Mungu haina mpaka fulani,(yaani Mwenyeenzi Mungu Mtukufu ana elimu ya kila kitu, na elimu yake haina mwanzo wala mwisho). Elimu ya Mwenyeenzi Mungu ni tofauti na elimu ya mwanaadamu, kwani elimu ya mwanaadamu ina kiwango fulani na hakuna mwanaadamu yoyote mwenye elimu ya vitu vyote duniani isipokuwa Allah (s.w).

Qur-ani karym inathibitisha kauli hiyo kutoka katika kauli za malaika wa Mwenyeenzi Mungu pale waliposema:-
قَالُواْ سُبْحَانَكَ لاَ عِلْمَ لَنَا إِلاَّ مَا عَلَّمْتَنَا إِنَّكَ اَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيم[2]
Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyo tufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hikima.
Vile vile kauli ya Mwenyeenzi Mungu juu ya Mtume wake hadharati Muhammad (s.a.w.w) anasema:-
قُل لاَّ اَمْلِكُ لِنَفْسِى نَفْعاً وَلاَ ضَرّاً إِلاَّ مَا شَاء اللّهُ وَلَوْ كُنتُ اَعْلَمُ الْغَيْبَ لاَسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ إِنْ اَنَاْ إِلاَّ نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ[3]
Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa ninayajua ya ghaibu ninge jizidishia mema mengi, wala ovu lisinge nigusa. Mimi si chochote ila ni mwonyaji na mbashiri kwa watu wanao amini.
Maelezo kuhusiana na ayaMakafiri wakimfanyia stihzai Mtume wakimwambia “tuangamize” basi Tufanyie hivi au Tufanyie hivi kama kweli wewe ni Mtume.
Basi ndiyo Mtume ameambiwa awajibu hapa kwamba hakuna Binaadamu yoyote anayeweza kujifanyia analolipenda au kuwafanyia wenziwe analolitaka, la nafuu wala la madhara. Wala hakuna anayejua ya ghaibu akapata kujivutia hili upesi au kujiepusha na hilo kwa haraka, yote haya ni yake mwenyewe Mwenyeenzi Mungu.
Na juu ya kuwa Mwenyeenzi Mungu amesema haya na akamwambia Mtume wake ajinasibishie haya; kuna watu wanaowaitakidia viumbe wenzao uweza wa haya.

Uislamu wa namna hiyo una hatari. Si Uislamu huo. Kumuitakidia kiumbe mwenzio uweza wa Mwenyeenzi Mungu na hali ya kuwa unamuona anataabishwa hata na kidudu chungu! Akili gani fupi hizo? Na akili gani potofu hizo!

Anasema Mwenyeenzi Mungu katika aya ya 24-25 ya Suratun-Najm,

اَمْ لِلْإِنسَانِ مَا تَمَنَّي. فَلِلَّهِ الآخِرَةُ وَالاُولَي[4]

Ati mtu anakipata kila anacho kitamani? Mwenyezi Mungu tu ndiye Mwenye dunia na Akhera.
Na anasema mara nyingi kabisa kuwa kujua ghaibu kumo katika mikono ya Mwenyeenzi Mungu peke yake. Hakuna anayejua ya Ghaibu ila Yeye,na huwapa baadhi ya Ghaibu hizo Mitume. Basi wasidanganywe watu, na wakakubali kudanganyika. Yakufuatwa ni haya yanayosemwa katika Qur-ani na hadithi sahihi za Mtume, siyo ya kufuatwa hayo yanayopigiwa ngoma tu na watu.

Mipaka ya elimu ya Mwenyeenzi Mungu
Tukizingatia kwa makini aya za qur-ani tutagundua kuwa kuna aya nyingi ambazo zinaelezea kuhusu elimu ya Mwenyeenzi Mungu isiyo na mwisho.
Aya hizo zinazoelezea kuhusu elimu ya Mwenyeezi Mungu zinatufahamisha na kutuelewesha sisi kuwa sifa zote njema anastahiki kusifiwa Mola wa viumbe vyote, na hakuna mja yeyote anayestahiki kusifiwa kwa sifa hizo isipokuwa Yeye Allah (s.w). Basi na tuangalie aya hizi mbili zifuatazo:-

وَلَوْ اَنَّمَا فِى الاَرْضِ مِن شَجَرَةٍ اَقْلاَمٌ وَالْبَحْرُ يَمُدُّهُ مِن بَعْدِهِ سَبْعَةُ اَبْحُرٍ مَّا نَفِدَتْ كَلِمَاتُ اللهِ إِنَّ اللهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ[5]
Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingeli kwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
وَمَا تَكُونُ فِى شَاْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلاَ تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلاَّ كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُوداً إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ وَمَا يَعْزُبُ عَن رَّبِّكَ مِن مِّثْقَالِ ذَرَّةٍ فِى الاَرْضِ وَلاَ فِى السَّمَاء وَلاَ اَصْغَرَ مِن ذٰلِكَ وَلا اَكْبَرَ إِلاَّ فِى كِتَابٍ مُّبِينٍ[6]
Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Qur'ani, wala hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnapo shughulika nayo. Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimo katika Kitabu kilicho wazi.
Maelezo kuhusiana na aya

Aya hii inaonyesha kuwa Mwenyeenzi Mungu, halimfichikii lolote; analijua kila jambo lililopita na lililoko na linalokuja…. Na Aya hii inaonyesha kuwa katika mambo yetu na mikutano yetu zitolewe stish-hadi za Qur-ani, watu wasikie ya Mungu. Na kama hawajui maana yake wafasiriwe.
Lakini yako wapi haya sasa kwetu sisi, sasa makasida tu yasiyofasiriwa. Na bora yasifasiriwe, lakini mengine yanaonyesha ukafiri dhahiri kama ile kasida inayosema:-
Waniimal Waali             Waaliyha
Na nyengine zinazoonyesha kuvunja heshima za Mitume kama ilivyobainishwa katika aya ya 253 ya Suratul-Baqarah.
تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلـٰي بَعْضٍ مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللّهُ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ وَآتَيْنَا عِيسَي ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَاَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ وَلَوْ شَاء اللّهُ مَا اقْتَتَلَ الَّذِينَ مِن بَعْدِهِم مِّن بَعْدِ مَا جَاءتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَلَـكِنِ اخْتَلَفُواْ فَمِنْهُم مَّنْ آمَنَ وَمِنْهُم مَّن كَفَرَ وَلَوْ شَاء اللّهُ مَا اقْتَتَلُواْ وَلَـكِنَّ اللّهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيد[7]
MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo. Katika wao wapo ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine akawapandisha vyeo. Na tukampa Isa mwana wa Mariyam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana walio kuwa baada yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo kati yao walio amini, na wengine kati yao walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo.
Maelezo kuhusiana na aya
Aya hii inaonyesha kuwa Mitume daraja zao ni mbali mbali kwa Mwenyeenzi mungu kama binaadamu wengine na Malaika na majini na vyenginevyo. Wanazidiana kwa fadhila za Mwenyeenzi Mungu na kwa amali zao walizozifanya ambazo si sawa sawa. Za wengine ni kubwa zaidi au nyingi zaidi kuliko za wenzao.
Na hapa Mwenyezi Mungu amewataja watatu katika hao Mitume wakubwa kabisa. Naye ni huyo aliyesemezwa na Mwenyeenzi Mungu. Naye ni nabii Musa, aliyepewa hoja zilizo wazi… naye ni Nabii isa. Na aliyepandishwa vyeo vikubwa kabisa. Naye ni Nabii Muhammad, na vile vile katika hao wakubwa kabisa ni nabii Ibrahimu na Nabii Nuhu kama ilivyofahamishwa katika Aya nyenginezo kama Aya ya saba ya Suratul-Ahzab inavyosema:

وَإِذْ اَخَذْنَا مِنَ النَّبِيِّينَ مِيثَاقَهُمْ وَمِنكَ وَمِن نُّوحٍ وَإِبْرَاهِيمَ وَمُوسَي وَعِيسَي ابْنِ مَرْيَمَ وَاَخَذْنَا مِنْهُم مِّيثَاقاً غَلِيظاً[8]
Na tulipo chukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na Ibrahim na Isa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu.

Na anayewekwa mbele katika hao ni:-
a) Nabii Muhammad (s.a.w.w).
b)Kisha Nabii Ibrahimu (a.s)
c) Tena nabii Musa.
d) Baadae Nabii Isa.
e) Na hatimae nabii Nuhu (a.s)
Na huyo Roho Mtakatifu ni Jibril anayewaletea Wahyi Mitume. Basi kwa Mitume wengine kateremka mara nyingi zaidi kuliko kwa Mitume wengine.
Na aliposema Mwenyeenzi Mungu . Na kama Mungu angalitaka…ni kuonyesha kuwa Mwenyeenzi Mungu hakuwaumba Wanaadamu umbo la Malaika. Na angetaka angewaumba hivyo (Kimalaika); wakawa wanakwenda mwendo ule ule waliowekewa, hawakhalifu hata kidogo, ikawa wanafanya mema tu. Lakini binaadamu kawaumba akawapa huria ya kufanya mema na mabaya. Na angalitaka kuwaumba Kimalaika asingeshindwa. Lakini Mwenyewe Mwenyeenzi Mungu katafautisha baina ya viumbe vyake- Malaika kawaumba wana akili na hawana matamanio,akawaumba wanyama kuwa wana matamanio lakini hawana akili (wana utambuzi mdogo tu). Na akawaumba wanaadamu na yote mawili. Wana matamanio na wana akili ya kupima baina ya jema na baya na baina ya jema na jema zaidi na baina ya baya na baya zaidi,- wafanye wanalolitaka bila kufungika kwa moja wapo. Na hayo Matamanio yao ndiyo yanayowapelekea kutowafikiana. Na angetaka Mwenyeenzi Mungu asingewaumba hivi. Basi Mwanaadamu akipigana na matamanio yake akafika katika utakatifu unaokurubia wa Kimalaika huwa bora kuliko hao Malaika, na akitawaliwa na matamanio yake anakuwa kama mnyama, na zaidi kuliko mnyama kwani yeye ana hatamu ya akili, naye hataki kuzuilia kasi zake kwa hatamu hizo.

[1] Surat Nahli aya ya 78

[2] Suratul-baqara aya ya 32

[3] Surat-Al-aaraf aya ya 188

[4] Suratun-Najm aya ya 24-25

[5] Surat Luqman aya ya 27

[6] Surat Yunus aya ya 61

[7] Suratul-Baqarah aya ya 253

[8] Suratul-Ahzaab aya ya 7


MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini