Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HEKIMA YA ALLAH KATIKA NIDHAMU ISIYO YA KIMAUMBILE

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

HEKIMA YA ALLAH KATIKA NIDHAMU ISIYO YA KIMAUMBILE

Alama nyengine inayothibitisha na kuonesha hekima ya Mwenyeezi Mungu ni kwamba, Mwenyeezi Mungu hakumuacha mwanaadamu bila ya kumuonesha njia itakayomuongoza katika njia njema, na siku ya mwanzo alimuelewesha Nabii adam (a.s) uhakika wa dunia.

وَعَلَّمَ آدَمَ الاَسْمَاء كُلَّهَا ثُمَّ عَرَضَهُمْ عَلـٰي الْمَلاَئِكَةِ فَقَالَ اَنبِئُونِى بِاَسْمَاء هَـؤُلاء إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ[1]

Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya hivi ikiwa mnasema kweli.

Mwenyeezi Mungu amemchagua Nabii Adam (a.s) kuwa ni Mtume wa mwanzo duniani, na kwa kuendelea kuituma Mitume mengine alithibitisha hekima yake katika nidhamu isiyokuwa ya kimaumbile, kama tunavyomsikia Nabii Ibrahim (a.s) akisema:-

رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولاً مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ إِنَّكَ اَنتَ العَزِيزُ الحَكِيمُ[2]

Ewe Mola Mlezi wetu! Waletee Mtume anaye tokana na wao, awasomee Aya zako, na awafundishe Kitabu na hikima na awatakase.Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Mwenyeezi Mungu Mtukufu na Hakiym alituma sheria zake kupitia Mitume yake mitukufu kutokana na maendeleo ya wanaadamu,hadi zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambaye ni Mtume wa mwisho na dini yake ndiyo dini kamili aliyokuja nayo kutoka kwa Mola wake (s.w).

Qur-ani kariym inaelezea hekima ya Mwenyeezi Mungu katika nidhamu isiyo ya kimaumbile, pale aliposema:-

الَر كِتَابٌ اُحْكِمَتْ آيَاتُهُ ثُمَّ فُصِّلَتْ مِن لَّدُنْ حَكِيمٍ خَبِيرٍ[3]

Alif Lam Ra. Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa, kilicho toka kwa Mwenye Hikima na Mwenye Khabari.

Hekima ya Mwenyeezi Mungu katika nidhamu ya Akhera.

Imani na itikadi ya kuamini hekima ya Mwenyeezi Mungu katika nidhamu ya Akhera inamfanya mwanaadamu awe na hadafu na malengo katika maisha yake.

Qur-ani kariym baada ya kuelezea uumbaji wa ardhi, milima, kuteremshwa kwa upepo na mvua, nidhamu ya mauti na uhai,kukusanywa watu siku ya kiama na kulipwa kutokana na waliyoyatenda, inaonesha alama na hekima ya Mwenyeezi Mungu.

وَإِنَّ رَبَّكَ هُوَ يَحْشُرُهُمْ إِنَّهُ حَكِيمٌ عَلِيمٌ[4]

Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi.

Na kwa wale ambao hawana itikadi na imani ya siku ya kiama, na wana itikadi na kufasiri kuwa mauti ni mwisho wa maisha, watu hao wana hofu na wanaogopa maisha baada ya kufa, na wana madai kuwa madhumuni ya uumbaji wa dunia hayana uhakika. Basi Mwenyeezi Mungu anawambia watu hao kwa kusema:-

اَفَحَسِبْتُمْ اَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثاً وَاَنَّكُمْ إِلَيْنَا لاَ تُرْجَعُونَ[5]

Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?.

Maelezo kwa ufupi kuhusiana na somo lililopita.

* Tukisema kwamba Mwenyeezi Mungu ana hekima ina maana ya kwamba Mwenyeezi Mungu anafanya kila kitu kutokana na elimu isiyo mpaka aliyonayo, na anaiongoza dunia kutokana na program maalumu alizozipanga.

* Alama zinazothibitisha hekima za Mwenyeezi Mungu zinaonekana kwa uwazi kabisa katika viumbe vyote, kuanzia nidhamu za kimaumbile na zile zisizokuwa za kimaumbile.

* Kuzingatia hekima za Mwenyeezi Mungu kunamfanya mwanaadamu aikuze imani yake katika kumuamini Mwenyeezi Mungu na uhakika wa dunia.

Masuala.

1- Vipi tunaweza kukabiliana na tofauti au hitilafu zilizoko katika baadhi ya mambo baina ya mwanamke na mwanamme.

2- Fafanua maana ya neno hekima, na elezea mtu anayeitwa hakiym anatakiwa kuwa na sifa gani?.

3- Kwa nini nidhamu ya mauti na uhai ni moja katika hekima zake Allah (s.w)?.

4- Vipi tofauti za wanaadmu zinathibitisha hekima za Mwenyeezi Mungu?.

5- Vipi kuchaguliwa na kuteuliwa kwa Mitume (a.s) kunathibitisha hekima za Mwenyeezi Mungu?.

6- Vipi tunaweza kutoa dalili za kuthibitisha hekima ya Mwenyeezi Mungu kutokana na kuwepo kwa siku ya Kiama?.

[1] Suratul-Baqara Aya ya 31

[2] Suratul-Baqara Aya ya 129

[3] Surat Huud Aya ya 1

[4] Surat –Alhijr aya ya 25

[5] Surat Muuminuun Aya ya 115

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini