Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

TAWHIYD NA NIDHAMU YA DUNIA

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI                                                                                                       KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

TAWHIYD NA NIDHAMU YA DUNIA

Hakuna shaka ya kuwa Mwenyeenzi Mungu Mtukufu ameviumba vitu vyote duniani vikiwa katika nidhamu maalum, kama anavyosema Allah(s.w):-

الَّذِى خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقاً مَّا تَرَي فِى خَلْقِ الرَّحْمَنِ مِن تَفَاوُتٍ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَي مِن فُطُورٍ[1]

Aliye umba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha nadhari! Unaona kosa lolote?

Nidhamu hiyo ya uumbaji inathibitisha kuwepo kwa Mola mmoja, na Mola huyo ndiye aliyeviumba vitu vyote duniani, na kasha akaviweka katika nidhamu maalumu. Kwani kama kuna mungu zaidi ya mmoja kusingelikuwa na nidhamu yoyote na kungelikuwa na hitilafu na tofauti baina ya muumba mmoja na mwengine, basi natuzingatie ayah ii inayothibitisha kauli hiyo.

 لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلاَّ اللهُ لَفَسَدَتَا فَسُبْحَانَ اللهِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ[2]

Lau wangeli kuwamo humo miungu wengine isipo kuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeli fisidika. Subahana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayo yazua.

Maelezo kuhusiana na aya

Hii ni kawaida isiyoanguka kuwa “ Mafahali wawili hawakai zizi Moja” Basi wangekuwako waungu wawili wangepigana daima hata mmoja amshinde mwenziwe au wauwane; udhia wishe. Na muda wote huo- wa kuzatiti vita mpaka kutiana mikononi- hawatashughulikia jengine ila hilo tu la kutafuta kushinda. Tena mambo atayaendesha nani?

Na wakiwa wengi zaidi kuliko wawili ndiyo vivyo hivyo- watapigana mpaka wamalizane. Au- tuseme wapatane. Na wakipatana basi watauparaganya tu mwenesho wa ufalme wao kwani kwa “Manahodha Wengi jahazi huzama.”

Basi Mwenyeenzi mungu ni mmoja tu. Wahadahu Laa Sharyka Lahuu. Na watu mambo yao ndiyo vivi hivi. Yakiwa yanaendeshwa na chungu ya wakubwa – na kila mmoja hakubali kumsikiliza mwenziwe – basi yataharibika tu. Ndiyo maana Mtume akihimiza kuwa sharti – katika kila mkusanyiko – apatikane mkubwa anayetiiwa na wote kwa anayoyasema yakaingia shariani; au akilini yakiwa hayahusu sheria. Akisema Mtume kuwa watu – wakishakuwa watatu – katika msafara wao – basi sharti wamfanye mmoja mkubwa wao kwani mambo hayatengenei yakiwa fujo, ovyo ovyo, hayana mkubwa. Inasemwa kwa kiarabu; Laa yasluhunaasu fawdhaa Laa saraatalahum. Yaani mambo hayatengenei yakiwa ovyo, hayana mkubwa au wakubwa wa kuyaendesha.Na sharti ya hao wakubwa – ilivyoweka uislamu – ni wawe na elimu nzuri na utambuzi kamili. Ikiwa si hivyo, si wakubwa hao, wala mambo hayataendelea . Inasemwa: Walaa saraata Idhaa Fuhhaaluhum saaduu

TAWHIYD ( KUAMINI MOLA MMOJA) NDANI YA SHERIA NA VITABU VYA MWENYEENZI MUNGU

Vitabu vyote alivyoviteremsha Mwenyeezi Mungu (s.w) vinathibitisha sheria moja , Nayo ni kuwa na imani ya Mola mmoja tu.Ijapokuwa “ tawhiyd” na kuamini Mola mmoja ni dalili moja wapo inayoonesha nidhamu ya dunia, lakini vile vile sheria ya vitabu vyote vya Mwenyeenzi Mungu yaani (Qur-ani, Tawrati, na Injili) vimekuja na sheria moja tu, nayo ni kuamini Mola mmoja.

Imamu Ali (a.s) katika wasia wake aliomuusia mwanawe Imam Hassan (a.s) anasema:-

[3]“واعلم یا بنی انه لو کان لربک شریک لاتتک رسله و لرایت اثار ملکه و سلطانه

”Ewe mwanangu elewa kuwa kama Mwenyeenzi Mungu angelikuwa na mshirika, Mitume yake ingelikuja kwako wewe, na ungeliona alama na uwezo wake Allah (s.w). Ijapokuwa sheria za vitabu vyote vya Mwenyeenzi Mungu zinawiana kifikra na kijamii miongoni mwa wanaadamu, na zinahitilafiana katika baadhi ya hukumu, ama katika nguzo za dini, akida (itikadi), na tawhiyd hakuna tofauti yoyote . Kama vile anavyosema Allah katika Qur-ani.:-

وَمَا اَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلاَّ نُوحِى إِلَيْهِ اَنَّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اَنَا فَاعْبُدُونِ[4]

Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu.

1- ATHARI YA TAWHIYD (KUAMINI MOLA MMOJA) NA UMOJA WA WANAADAMU KATIKA JAMII

Kuwa na imani ya Mola mmoja inaweza kuwa sababu ya kuwaweka wanaadamu na kuwa kitu kimoja,  na kuondosha hitilafu zao za kikabila,geografia, kaumu, rangi n.k.

Katika zama za kijahilia jamii ya kiarabu ilikuwa haina itikadi ya kumuamini Mola mmoja, bali kila kabila lilikuwa likiamini na kuabudu sanamu maalumu, na kutokana na sababu hiyo basi kulikuwa hakuna umoja wa mawafikiano yoyote katika jamii ya kiarabu, kila siku kulikuwa kuna vita baina ya kabila na kabila, lakini baada ya kudhuhuru (kuja) uislamu na kupinga kuabudu masanamu hali ilibadilika na waarabu wengi wakaiamini dini ya kiislamu, wakaijenga jamii yao na wote kuwa kitu kimoja, na katika kipindi kidogo tu baada ya kuja uislamu sio jamii ya kiarabu tu iliikubali dini ya kiilamu kwa shauku kubwa bali hata jamii mbili kongwe kabisa kihistoria yaani Irani na Rumu waliipokea na wakaukubali uislamu kwa mikono miwili.

Kwa upande mwengine sio kwa sababu tu makafiri walilinganiwa kuamini Mola mmoja na kuokoka na shirki ya kuamini miungu tofauti, bali kutokana na kuwa dini zote za mbinguni ambazo ni Masihi, Yahudi na Islamu dini zote hizo ni za Mwenyeezi Mungu, na dini zote hizo zinawalingania wanaadamu kuamini Mola mmoja tu, basi tutaona kwamba ijapokuwa katika dini kunahitilafiana katika mambo mbali mbali ama vile vile kuna ushirikiano wa mambo katika tawhid, yaani waislamu, wakiristo, na mayahudi wote wana itikadi ya kuamini Mola mmoja.

Mwenyeezi Mungu anampa desturi (amri) Mtume wake Muhammad (s.a.w.w) kwa kumwambia:-

“قُلْ يَا اَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْاْ إِلَي كَلَمَةٍ سَوَاء بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ اَلاَّ نَعْبُدَ إِلاَّ اللّهَ وَلاَ نُشْرِكَ بِهِ شَيْئاً وَلاَ يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضاً اَرْبَاباً مِّن دُونِ اللهِ فَإِن تَوَلَّوْاْ فَقُولُواْ اشْهَدُواْ بِاَنَّا مُسْلِمُونَ[5]

Sema: Enyi Watu wa Kitabu! (Mayahudi, na wakiristo) Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu. Na katika aya nyengine anasema:-

لاَ إِكْرَاهَ فِى الدِّينِ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ فَمَنْ يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَيَ لاَ انفِصَامَ لَهَا وَاللّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ[6]

Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

Maelezo kuhusiana na aya Baadhi ya Waarabu wa madina kabla hakwenda Nabii Muhammad huko walikuwa wanafuata dini ya kiyahudi. Lakini wengi wao wakiabudu masanamu. Ulipokuja Uislamu, takriba wote hao waliokuwa wakiabudu masanamu walisilimu. Ama katika wale waliokuwa na dini ya kiyahudi walisilimu kidogo tu, na wengine wakasaliana Mayahudi japo kuwa ni waarabu. Basi baba zao waliosilimu na ndugu zao na wakubwa wao, na waume zao, na bwana zao walitaka wawatie katika Uislamu kwa nguvu. Basi wakakatazwa hapa na Mwenyeenzi Mungu kuwa:

Hakuna ruhusa kukmkalifisha asiyetaka, kila mtu kapewa akili ya kutambua jema na baya. Basi akifuata upotofu hiari yake mwenyewe, na Mungu atamtesa Akhera huko si hapa.

Basi umefedheheka hapa uwongo wa wale wanaozua kuwa Uislamu unalazimisha watu kwa nguvu kuingia katika dini hiyo japo wenyewe hawataki. Basu Uislamu gani huo wanaousingizia hivyo? Na Uislamu ni huu uliyomo katika Qur-ani – mweupe hauna kificho chote, lakini anayetaka kukutukana hakuchagulii tusi.

Basi kuwa na imani ya kuwa mola ni mmoja tu kunasababisha kuondosha hitilafu ziliopo baina ya wanaadamu katika jamii, kwa sababu mwanaadamu aliye bora kwa wengine mbele ya Mwenyeenzi Mungu ni yule mwenye taquwa (mcha mungu) na mwenye kumuamini Mola wake kuwa ni mmoja, na Yeye ndiye anayepaswa kuabudiwa. Kama Qur-ani inavyosema:-

يَا اَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَاُنثَي وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوباً وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ اَكْرَمَكُمْ عِندَ اللهِ اَتْقَاكُمْ إِنَّ اللهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ[7]
Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.

[1] Surat Mulk aya ya 3

[2] Surat Anbiyaa aya ya 22

[3] Nahjulbalagha, barua ya 3

[4] Surat anbiyaa aya ya 25

[5] Surat Al-imrani aya ya 64

[6] Suratul-Baqara aya ya 256

[7] Surat Hujurati aya ya 13

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini