Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

AINA ZA DINI NO. 1

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

AINA ZA DINI

Dini zimegawika katika sehemu mbili:-

1.Dini zinazotokana na kizazi cha Nabii Ibrahimu (a.s), dini hizo ndizo dini za Allah (s.w).

2. Dini zinazotokana na tamaduni maalumu za watu, dini hizo sio dini sahihi.

Dini ya Wahyi ni dini ya Nabii Ibrahimu (a.s) na ndio dini iliyoletwa kutoka kwa Mwenyeezi Mungu Mtukufu. ni bayana maalumu inayowafunga watu wote katika mfumo mmoja, na katika mwenendo maalumu, na inawalazimu wao kuitii dini hiyo.

Wahyi wa dini ni wenye kukubalika na kufahamika katika tamaduni zote, hii ni kwa sababu wahyi huo unawiana na kuwendana na matakwa ya dini, matakwa ya dini ni matakwa ya wanaadamu wote, ikiwa dini inakubalika na kufahamika na wanaadamu wote, na ikiwa dini ina uwezo wa kufuta, na kuondoa mambo yanayoleta madhara na yasiyo na faida yoyote katika maisha ya mwanaadamu, au inaweza kuweka na kuwaletea wanaadamu maadili mema yaliyo na faida katika maisha yao, na yanayowaletea saada ya duniani na Akhera, hii ni kwa sababu lugha ya dini ni lugha iliyomo ndani ya nafsi za wanaadamu wote , na ni lugha inayofahamika na kila mmoja wetu, na ni lugha inayowaletea wanaadamu athari nzuri katika maisha yao.

Lugha mahasusi na maalumu ya dini ni lugha ya kiarabu, lugha ya nafsi, na ni lugha asili iliyojaaliwa kutokana na mambo yote yaliyo dhahiri na yaliyo jificha, mambo ambayo yana uhusiano na ulimwengu wa wanaadamu.

Dini haifuti yale yaliyorithiwa kutoka kwa Mitume ya Mwenyeezi Mungu na Ahlulbayt (a.s), na wala haipingi suna, fikra, na maadili yanayoendana na nafsi za wanaadamu, kwa sababu akili na fikra salama ya mwanaadamu inafanya mambo kupitia miongozo ya dini na miongozo ya Mitume ya Mwenyeezi Mungu na Ahlulbayt (a.s), baadhi ya wakati dini inachukua yale mambo yanayoleta faida katika maisha ya wanaadamu, mambo ambayo yanaleta maslahi na yanaweza kupatikana ndani ya tamaduni njema, kwa upande mwengine dini inapinga na kuondoa mambo ambayo yanaleta madhara kwa wanaadamu, na baadhi ya wakati huthibitisha mambo ambayo yamo katika tamaduni za watu lakini ni yenye kukubalika kiakili , kinafsi, na kimoyo. Kwa maelezo hayo tunapata natija hizi zifuatazo:-

A: Kuletwa taaluma na hukumu za Mwenyeezi Mungu kupitia lugha na tamaduni maalumu – lugha ya kiarabu – haina maana ya kuwa dini ya kweli na dini ya haki ilikuwa ni dini ya kiarabu inayofafanuliwa au kuelezewa kupitia mtindo wa tamaduni maalumu.

Bali dini na mapendeleo aliyonayo mwanaadamu ndani ya nafsi yake.mapendeleo ambayo yanaendana na matakwa ya dini ya Mwenyeezi Mungu.Lugha ya kiarabu ni lugha tukufu iliyosifiwa na Mwenyeezi Mungu, Mitume na Ahlulbayt (a.s), na ndio Qur-ani ikateremshwa kwa lugha ya Kiarabu na kuwataka watu wanaposoma Qur-ani waisome kwa lugha ya kiarabu, lugha ya kiarabu ndio lugha kuu katika kubainisha hadafu na malengo ya dini, lakini ni lazima tuzingatie kuwa ni dini inayosawazisha lugha, kiasi ya kwamba wahyi – Qur-ani - ulibainishwa kwa mabainisho ya balagha ya hali ya juu kabisa, na hakuna mwanaadamu yoyote aliyeweza au anayeweza au atakayeweza kutoa balagha kama hiyo, basi Mwenyeezi Mungu Mtukufu ndipo alipowaambia:-

وَإِن كُنتُمْ فِى رَيْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلـٰي عَبْدِنَا فَاْتُواْ بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُواْ شُهَدَاءكُم مِّن دُونِ اللهِ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ[1]

Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.

Maelezo kuhusiana na Aya:

Makafiri walikuwa wakikanusha Qur-ani, na kudai kuwa ni maneno yake yeye Muhammad (s.a.w.w), si maneno ya Mwenyeezi Mungu, basi hapa Mwenyeezi Mungu anawatahayarisha, na kuwaambia kwamba Muhammad ni mwanaadamu kama nyinyi, basi kama yeye ameweza kutunga maneno kama haya, kwa nini nyinyi hamuwezi? Jaribuni na muwaite hao waungu wenu wakupeni msaada. Katika makala ijayo tutaelezea natija nyengine tunazozipata kuhusiana na maelezo hayo ya dini.

[1] Surat Albaqarah Aya 23.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini