Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

AINA ZA DINI NO.2

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

AINA ZA DINI NO 2

Katika makala iliyopita, (makala namba moja) tulielezea aina mbili za dini, na tukaelezea natija zinazopatikana kuhusiana na maelezo tuliyoyaelezea katika makala hiyo, katika makala hii tutendelea kwa kuelezea natija nyengine zinazohusiana na dini.

miongoni mwa natija hizo ni hizi zifuatazo:-

A: Kuletwa taaluma na hukumu za Mwenyeezi Mungu kupitia lugha na tamaduni maalumu – lugha ya kiarabu – haina maana ya kuwa dini ya kweli na dini ya haki ilikuwa ni dini ya kiarabu inayofafanuliwa au kuelezewa kupitia mtindo wa tamaduni maalumu.

Bali dini na mapendeleo aliyonayo mwanaadamu ndani ya nafsi yake.mapendeleo ambayo yanaendana na matakwa ya dini ya Mwenyeezi Mungu.

Lugha ya kiarabu ni lugha tukufu iliyosifiwa na Mwenyeezi Mungu, Mitume na Ahlulbayt (a.s), na ndio Qur-ani ikateremshwa kwa lugha ya Kiarabu na kuwataka watu wanaposoma Qur-ani waisome kwa lugha ya kiarabu, lugha ya kiarabu ndio lugha kuu katika kubainisha hadafu na malengo ya dini, lakini ni lazima tuzingatie kuwa ni dini inayosawazisha lugha, kiasi ya kwamba wahyi – Qur-ani - ulibainishwa kwa mabainisho ya balagha ya hali ya juu kabisa, na hakuna mwanaadamu yoyote aliyeweza au anayeweza au atakayeweza kutoa balagha kama hiyo, basi Mwenyeezi Mungu Mtukufu ndipo alipowaambia:-

وَإِن كُنتُمْ فِى رَيْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلـٰي عَبْدِنَا فَاْتُواْ بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُواْ شُهَدَاءكُم مِّن دُونِ اللهِ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ[1]

Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.

Maelezo kuhusiana na Aya:

Makafiri walikuwa wakikanusha Qur-ani, na kudai kuwa ni maneno yake yeye Muhammad (s.a.w.w), si maneno ya Mwenyeezi Mungu, basi hapa Mwenyeezi Mungu anawatahayarisha, na kuwaambia kwamba Muhammad ni mwanaadamu kama nyinyi, basi kama yeye ameweza kutunga maneno kama haya, kwa nini nyinyi hamuwezi? Jaribuni na muwaite hao waungu wenu wakupeni msaada.

B: Tunaposoma Qur-ani tunatakiwa kutambua uhakika wa lafudhi za Qur-ani na yale yanayokusudiwa, sio mazungumzo ya lugha hiyo, kwa sababu ni lazima tuifahamu Qur-ani kupitia uhakika wa Qur-ani yenyewe, na Qur-ani yenyewe ndio inayoonyesha maana maalumu ya lafudhi hizo, kwa mfano, tunapotaka kufahamu maana ya neno dini ni lazima turejee katika Qur-ani, au vitabu vya dini, kwa sababu ndani ya vitabu hivyo au ndani ya Qur-ani tunaweza kufahamu maana halisi ya neno dini na uhakika wake.

C: Dini ni mkusanyiko na mjengeko wa elimu na hukumu za mambo mbali mbali, dini inatoa mabainisho ya elimu yanayohusiana na uongofu na saada ya wanaadamu katika maisha yake ya duniani na Akhera, na hukumu zinabainisha maamrisho na makatazo, -yaani- (yale yanayomlazimikia mwanaadamu kuyafanya, na yale yasiyomuwajibikia kuyafanya), ambayo yanaendana na haki na yenye thamani katika nyoyo za wanaadamu, kwa hiyo, dini sio desturi na tabia tu, bali mbali ya desturi, vile vile imekusanya mambo mengine ambayo humuongoza mwanaadamu katika njia ya uongofu na saada .

[1] Surat Albaqarah Aya 23.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini